_____________________ NI KWELI YESU KRISTO ALISHUKA KUTOKA MBINGUNI? Did Jesus Christ really come down from heaven? _____________________ NI KWELI YESU KRISTO ALISHUKA KUTOKA MBINGUNI? Kabla hatujaanza, ni muhimu kuliweka jambo moja bayana. Bwana Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu. Yeye ni kiumbe mkuu katika ulimwengu wote, isipokuwa Mungu Mwenyewe. Lengo la kijitabu hiki ni kumtukuza Bwana Yesu, kwa namna anavyostahili kutukuzwa. Kwa bahati mbaya mafundisho ya Biblia kumhusu Bwana Yesu mara nyingi yamekuwa hayaeleweki ipasavyo. Kwa nia njema ya kumtukuza Bwana Yesu, lakini katika namna iliyopotoshwa, makanisa mengi hufundisha mambo kumhusu yeye ambayo hayatokani na Biblia. Kijitabu hiki kinalenga kusahihisha dhana hizi potofu. Sio kwa nia ya kuikosoa dini ya mtu yeyote, bali ni kuonyesha tu yale ambayo Biblia kwa usahihi inafundisha kumhusu Yesu, Mwana wa Mungu. Ni pale tu tutakapokuwa tumeyaelewa mafundisho hayo, ndipo tutakapoweza kumpa Bwana utukufu anaoustahili. "Nilishuka Kutoka Mbinguni" Jina la kijitabu hiki ni swali: ni kweli Yesu Kristo alishuka kutoka mbinguni? Kwenye sura ya 6 ya Injili ya Yohana kuna mstari unaoonekana kulijibu swali hilo. Yesu alisema: "Kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapanzi yangu bali mapenzi yake aliyenipeleka." (mstari 38) Lakini tusikurupuke kufikia hitimisho. Somo hili sio rahisi hivyo kama linavyoweza kuonekana. Utata unajitokeza kwa sababu kuna aina mbili za lugha zilizotofautiana sana, ile yenye maana ya moja kwa moja na ile ya kitamathali. Aina zote mbili zinatumiwa na Yesu katika sura hii tunayoitafakari. Katika mstari wa 64 alisema, "Lakini kuna wengine miongoni mwenu wasioamini." Hii ni lugha yenye maana ya moja kwa moja. Inamaanisha kitu kile kile inachokiongelea. Hata mtoto mdogo hawezi kukosea kuielewa maana yake. Lakini mistari mingine mingi haiko kama huu. Chukua kwa mfano, mstari wa 55 na 54. Hapa Yesu anasema: (1) "Nawaambieni, msipoula mwili wake mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu; aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele." Hii ni lugha ya kitamathali, haimaanishi kile ambacho inaonekana kukisema; badala yake, inabeba maana nzito zaidi. Huna budi kufikiri kwa uangalifu sana ili kuigundua maana yake halisi. Hivyo, kama hatuwi waangalifu, tunaweza kushindwa kirahisi kuielewa. Ukweli ni kwamba Wayahudi ambao hawakuwa wakiamini walishindwa kuielewa lugha hii na misemo iliyofanana na hiyo ya Yesu. Walisema, "Mtu huyu atawezaje kutupa mwili wake tuule?" Pengine walidhani Yesu alikuwa akihubiri juu ya watu kulana wao kwa wao. Vyovyote walivyofikiri, walikuwa wamekosea sana. Je, kuhusu kauli hii, "nilishuka kutoka mbinguni, "ni ya maana ya moja kwa moja au ya kitamathali? Kuna sababu nzuri ya kufikiri ilikuwa ya kitamathali. Katika mstari wa 31 wa sura hiyo hiyo kuna kitu kinatajwa ambacho Agano la Kale liliiita 'mana'. Hii ilikuwa mfano wa mkate ambao Mungu aliutoa, kwa miujiza, ili watu wake waweze kula walipokuwa nyikani. Maneno ya mstari wa 31 ni, "Aliwapa (Mungu) chakula cha mbinguni ili wale. Hii ni wazi kabisa kuwa ni lugha ya kitamathali. Mkate huu wa kimiujiza haukuokwa mbinguni kisha kudondoshwa duniani. Kauli kuwa ulitoka mbinguni inatujulisha kuwa Mungu wa Mbinguni aliutengeneza hapa duniani. Kuna utenzi maarufu watu wauimbao wakati wa mavuno. Kibwagizo kinaanza hivi, "Karama zote njema zinazotuzunguka hutumwa kutoka juu mbinguni." Maneno haya yamechukuliwa moja kwa moja kutoka kwenye Agano Jipya, kutoka katika Waraka wa Yakobo 1:17, ambao unasema kwamba kila kutoa kuliko kwema "hushuka kutoka juu, hushuka kwa Baba. Wakulima wanapouimba utenzi huo, hawapigi taswira kuwa mazao yao moja kwa moja hushuka "kutoka juu mbinguni." Wanamaanisha tu kuwa Mungu hutupa sisi mavuno yetu. Lugha Zaidi ya Kitamathali Biblia inatumia aina hii ya lugha ya kitamathali kuwahusu watu na pia vitu. Inatuambia kuwa "palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana." (Yohana 1:6.) Lakini Yohana hakuwahi kukaa mbinguni. "Ametumwa kutoka kwa Mungu" ni kauli inayoonyesha tu kwamba Mungu alimpa kazi maalum ya kuifanya. (2) Lakini maelezo haya yanaweza tu kuhusishwa na mistari ile ambayo kwa hakika inaelezea "kushuka" kwa Yesu kutoka mbinguni. Kuna mistari kadhaa mingine inayoelekea kuonyesha, kwa njia moja ama nyingine, kuwa kuna wakati Yesu aliwahi kuishi mbinguni, siku nyingi kabla hajaonekana duniani. Ufuatoa ni mmoja kati ya mistari hiyo: "Baba (alisema Yesu), unitukuze mimi pamoja nawe, kwa utukufu ule niliokuwa nao pamoja nawe kabla ya ulimwengu kuwako." (Yohana 17:5.) Mistari kama hiyo tutaichukuliaje? Ni ya kuchukuliwa kama ilivyo, au ni ya kitamathali? Je, ni kweli Yesu aliishi na Mungu mbinguni kabla ulimwengu haujaumbwa? Au maneno hayo yana maana nyingine nzito zaidi ya hiyo? Lengo la kijitabu hiki ni kuiacha Biblia ijisemee yenyewe na kutujibia maswali hayo. Mitazamo Mitatu Kumhusu Yesu Watu wasioiamini Biblia husema kwamba Yesu alikuwa ni mtu wa kawaida tu. Wanakosea. Yesu alikuwa ni Mwana wa Mungu. Hatuna haja ya kupoteza muda kujaribu kufikiria misingi ya dhana zao. Lakini tutaitafakari mitazamo mitatu tofauti kumhusu Yesu ambayo inafuatwa na Wakristo wanaoiamini Biblia. Mtazamo wa kwanza ndio hasa unaofuatwa na waumini wengi. Huu unaonyesha kwamba Yesu ni Mungu Mwenyezi katika hali ya ubinadamu. Wale wanaoamini katika mtazamo huu wanamtaja Yesu kama "Nafsi ya Pili katika Utatu," japokuwa inakuwa vigumu kidogo kugundua ni kipi wanamaanisha kwa kirai hicho. Kwa mujibu wa mtazamo huu, Yesu aliishi mbinguni milele na milele kabla hajatokea hapa duniani. Mtazamo wa pili unafundishwa na watu katika kundi linalojiita "Mashahidi wa Yehova," na pia madhehebu mengine madogo madogo. Wanasema kwamba Yesu sio Mungu, isipokuwa ni malaika mkuu aliyeumbwa na Mungu hapo zamani sana. Wao, pia, wanaamini kuwa Yesu aliishi kwa kipindi kirefu mbinguni kabla hajaja kuishi hapa duniani. Watu wanaoshikilia mojawapo ya mitazamo hii, bila shaka, wanaichukilia mistari hiyo kama ilivyo kwamba inaongelea habari za Yesu kushuka kutoka mbinguni. Mtazamo wa tatu unashikiliwa na Wakristadelfiani na baadhi ya watu wengine. Kwa mujibu wa mtazamo huu, Yesu hakuishi kama nafsi mbinguni kabla ya kuzaliwa hapa ulimwenguni, na mistari inayoongelea asili yake ya mbinguni haina budi kueleweka kwa lugha ya kitamathali. (3) Huu ndio mtazamo ambao utaongelewa kwenye kijitabu hiki. Iwapo utashangazwa na dhana hii, tafadhali vuta subira na endelea kukisoma. Kuna ushahidi wenye uzito mkubwa kwenye Biblia ambao unauthibitisha mtazamo huu. Yesu Alikuwa ni Mwanadamu Halisi Yesu hakuwa mwanadamu wa kawaida, mwenye kutenda dhambi. Kwa hilo tusikosee hata kidogo. Alikuwa ni mwanadamu wa pekee. Alikuwa ni Mwana wa Mungu. Lakini kwa maana halisi alikuwa ni mwanadamu na sio Mungu Mwenyezi. Hii haimaanishi aliacha kuwa mwanadamu mara tu alipopaa mbinguni kimwili. Biblia inatufundisha kumfikiria yeye kama mwanadamu, hata wakati huu. Siku nyingi baada ya Yesu kufufuka kutoka kwa wafu na kupaa mbinguni, Agano Jipya lilikuwa likitoa kauli kama hizi: "Zaidi sana neema ya Mungu, na kipawa kilicho katika neema yake mwanadamu mmoja Yesu Kristo kimezidi kwa ajili ya wale wengi… zaidi sana wao wapokeao wingi wa neema, na kile kipawa cha haki, watatawala katika uzima kwa yule mmoja, Yesu Kristo… kadhalika kwa kutii kwake mtu mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki." (Warumi 5:15-19.) "Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu." (1 Timotheo 2:5.) Hivyo Yesu kwa hakika ni mwanadamu. Haya ni mafundisho yasiyotiliwa shaka ya Agano Jipya. Sasa linganisha mafundisho hayo na maneno ya Askofu wa zamani wa Woolwich, Dk. Robinson, katika kitabu chake, "Mwaminifu kwa Mungu," kwenye kifungu cha maneno ambapo anaeleza jinsi Wakristo wengi wanavyomwona Yesu: "Yesu hakuwa mwanadamu aliyezaliwa na kulelewa, alikuwa ni Mungu kwa kipindi fulani katika jinsi ya fumbo. Alifanana na mwanadamu, lakini ndani alikuwa ni Mungu aliyejivika uanadamu - kama Baba Krismasi." Waumini wengi wanakiona kitendo cha askofu huyo kumfananisha Mungu na Baba Krismasi kuwa cha kukirihisha. Lakini licha ya hayo, wanakubali hiyo ndiyo kauli muafaka ya mafundisho ya kanisa. Iwapo Yesu alikuwa ni Mungu kweli, au hata malaika mkuu ambaye aliwahi kuishi mbinguni, basi kamwe hakuwa mtu halisi, bali Nafsi ya Uungu iliyojivika mwili wa kibinadamu. Lakini Agano Jipya linakataa. Linamwelezea Yesu kama mwanadamu. (4) Hii ndiyo sababu inayotufanya tufikiri kuwa mtazamo wa kawaida kumhusu Yesu umepotoshwa. Kuzaliwa kwa Yesu Kuzaliwa kwa Yesu Kristo kulikuwa ni matokeo ya muujiza mkuu. Mama yake alikuwa mwanamwali aliyekuwa hajaolewa bado na mwenye tabia nzuri. Alikuwa bikira. Hivi ndivyo ilivyotokea: "Malaika akamwambia, 'Usiogope Mariamu kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu…' Mariamu akamwambia malaika, 'Litakuwaje neno hili, maana sijui mume?'" "Malaika akajibu akamwambia, 'Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu za Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.'"(Luka 1:30-35) Yachunguze maneno hayo kwa makini zaidi. Kuna mengi ya kujifunza kutokana nayo. Mtoto angekuwa wa Mariamu mwenyewe. Malaika hakusema, "Mariamu, utazaa mwili wa nyama kwa ajili ya Nafsi ya Uungu kuja na kuishi ndani yake." Alisema, "Utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume." Maneno haya bila shaka yalikusudiwa yaeleweke kama yalivyo. Yanaelezea kuanza kwa maisha mapya ya mwanadamu - na sio kuja ulimwenguni kwa Nafsi ya Uungu. Pia, iwapo Yesu alikuwa ni Nafsi ya Uungu, mwenye umri wa mamilioni ya miaka kumzidi Mariamu, angeweza, katika hali yoyote halisi, kuwa mtoto wake? Lakini alikuwa mtoto wake, na sio tu aina fulani ya ajabu ya mtoto wa kambo. Katika injili zote Mariamu anatajwa kama mama yake, na kamwe sio mama yake wa kambo. Kwa upande mwingine, japokuwa mwanadamu Yusufu, ambayo baadaye alimwoa mama yake Yesu, wakati mwingine anaitwa baba yake, hatujaachwa kwenye mashaka yoyote kuhusu ukweli halisi. Luka anamwongelea Yesu kama "mwana, aliyedhaniwa kuwa wa Yusufu." (Luka 3:23.) Hivyo Yesu alikuwa kweli mwana wa Mariamu, sio Nafsi ya Uungu aliyekuwa akijifanya mwana wa Mariamu. Kama watoto walivyo, alifanana na mama yake katika njia nyingi. Hilo ndilo lililomfanya Yesu awe kweli ni mwanadamu. Wanadamu halisi hawaishi mbinguni kabla ya kuzaliwa, wala mtu huyu hakuwahi kuishi huko kabla. Kuchukuliwa kwake mimba kwa muujiza na kuzaliwa kwake kulikuwa ndiyo mwanzo halisi wa kuwepo kwake kama mwanadamu. (5) Mwanadamu ana asili ya udhaifu, ambayo imejaa majaribu mengi. Kama tutakavyoona baadaye, Yesu alirithi udhaifu wa asili wa mwanadamu kutoka kwa mama yake. Lakini hiyo ni sehemu ndogo tu ya hadithi. Malaika alisema wazi kuwa mtoto wa Mariamu angekuwa pia Mwana wa Mungu. "Nguvu za Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu," alisema malaika. (Luka 1:35.) Yesu pia alirithi mambo mengi kutoka kwa mzazi wake mwingine. Mungu alikuwa ndiye baba yake, na kutoka kwa Mungu alirithi utashi wa kufanya yale yaliyo mema, mara zote. Lilikuwa ni jambo hilo lililomsaidia kuushinda udhaifu wa asili wa mwanadamu - kupigana na majaribu na kuyashinda. Wakati wa Utoto wa Yesu Tunaambiwa machache sana kuhusu maisha ya utotoni ya Yesu. Kitu kimoja tunachoambiwa ni muhimu sana. Luka anaelezea jinsi Yesu alivyokuwa akikua kama ifuatavyo: "Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu." (Luka 2:52.) Wale ambao wanaamini kwamba Yesu alikuwa ni Mungu kweli, wanakanganywa na mstari huu. Ni vipi Mungu angeongezeka hekima na kujipendeza Mwenyewe? Wazo hilo linachekesha. Ni wazi Luka hakuamini kuwa Yesu alikuwa Mungu, akikaa kwa muda kwenye mwili wa mtoto mvulana. Vipi kuhusu dhana nyingine, kwamba Yesu alikuwa na malaika mwenye nguvu kutoka mbinguni, akikaa kwenye mwili wa mtoto mvulana anayekua? Dhana hii vile vile sio bora zaidi. Malaika kama huyo sharti alikuwa amekamilika, siku nyingi kabla ya kuja ulimwenguni. Malaika ndani ya mwili wa mtoto mvulana asingeweza "kuendelea katika hekima na … kumpendeza Mungu." Tunavyoona, mstari huu unaelezea kukua kwa mtoto mvulana halisi. Mwili wake ukiongezeka kimo. Kiwango chake cha hekima kikiendelea kupanuka. Na tabia yake ikawa nzuri mno hata Baba yake akapendezwa naye sana. (6) Ushindi Wake Dhidi ya Majaribu Inasemekana kuwa mabondia au wana mieleka wa kulipwa wakati fulani, kabla ya kupambana, hukutana faragha na kufikia makubaliano fulani. Wanakubaliana wasiumizane, japokuwa kwa nia ya kuwafurahisha watazamaji watalifanya pambano lao lionekane linapiganwa kwa nguvu na ujuzi wote. Huamua hata mtu wa kushinda pambano hilo la dhihaka, na kwa kweli hukubaliana kugawana hata fedha za tuzo la ushindi. Pambano la udanganyifu wa aina hii hitwa pambano la mteremko. Kwenye Biblia Yesu anaelezwa kama aliyepigana vita kuu dhidi ya majaribu ya kibinadamu. Alishindana na majaribu kila siku; na mara zote alishinda. Sote tunaelewa majaribu ni nini. Kama Yesu alikuwa mwanadamu halisi, basi tunaweza kuelewa kazi kubwa aliyokuwa nayo kuyashinda majaribu hayo. Lakini kama Yesu alikuwa ni kiumbe wa mbinguni aliyejivika mwili wa kibinadamu, basi hakuwa katika mapambano halisi - yalikuwa sawa na pambano la mteremko! Kwa sababu hakuna uwezekano wa Mungu au malaika kujaribiwa kama tunavyojaribiwa sisi. Biblia inasema, "Mungu hawezi kujaribiwa na maovu." (Yakobo 1:13.) Bado tunelezwa yafuatayo kuhusu Yesu: "Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana na sisi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi." (Waebrania 4:15.) Wakati mmoja Yesu alipokuwa akipambana na majaribu alimwambia Mungu, "Walakini sio mapenzi yangu, bali yako yatendeke." (Luka 22:42.) Ni dhahiri Yesu alikuwa na mapenzi yake mwenyewe ambayo yalipaswa yapondwepondwe, ili kwamba mapenzi ya Mungu yatendeke badala yake. Iwapo alikuwa ni mwanadamu kweli, tunaweza kuuelewa mstari huu. Lakini hauleti maana yoyote iwapo Yesu kweli alikuwa Mungu, au malaika katika umbile la mwanadamu. Jinsi Yesu Alivyopata Ukamilifu Kuna namna mbili zilizotofautiana sana ambapo kitu kinaweza kikawa kimepungua katika ukamilifu. Ni muhimu tukazingatia tofauti za namna hizo mbili. (7) Nyumba ya zamani inayokaribia kuporomoka haijawa kamilifu. Hii ni kwa sababu imechakaa. Mambo mengi yanakuwa yamepungua kwenye nyumba hiyo. Nyumba mpya ambyo ni nusu yake tu iliyojengwa nayo pia sio kamilifu.Lakini hii ni aina tofauti ya kutokukamilika wa kitu. Hakuna kilichoharibika katika nyumba hiyo, iliyojengwa nusu. Ni nzuri tu, kadiri inavyoendelea kujengwa. Lakini haijafikia ule ukamilifu. Yesu kamwe hakuwa amekamilika kwa maana ile ya mfano wa kwanza. Hakukuwa na kitu kilichokuwa kimeenda kombo kwake. Hakuwahi kutenda dhambi, hata mara moja. Lakini, tabia yake ilihitaji kuendelezwa hatua kwa hatu, kama nyumba inayojengwa, mpaka ilipokuja kukamilika. Kwa maana hii, alipaswa kuwa mkamilifu, kama nukuu za Biblia zifuatazo zinavyoonyesha: “Ingawa ni Mwana, alijifunza kutii wa mateso hayo yaliyompata; naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele.” (Waebrania 5:8,9). “Kwa kuwa ilimpasa yeye, ambaye kwa ajili yake na kwa njia yake vitu vyote vimekuwepo, akileta wana wengi waufikilie utukufu, kumkamilisha kiongozi mkuu wa wokovu wao kwa njia ya mateso.” (Waebrania 2:10) Kwa mara nyingine tena, ni wazi kuwa kuna kitu kilichoenda mrama katika dhana iliyozoeleka, kuwa Yesu alikuwa ni Nafsi ya Uungu aliyejivika mwili wa mwanadamu. Ni taswira gani unayoipata kwa Kiumbe kama huyo kulazimika kujifunza utii kwa njia ya mateso aliyoyapata? Unaweza kuelewa kweli ni vipi Nafsi ya Uungu kama huyo akamilishwe kwa njia ya mateso? Bila shaka huwezi. Tuna maelezo hapa ya mwanadamu halisi aliyejenga tabia ya ukamilifu tabaka juu ya tabaka. Ikiwa Yesu alikuwa Mungu Mwenyewe, au malaika mkuu, basi atakuwa alikwisha kamilishwa siku nyingi kabla hajaja wenye ulimwengu huu. Lakini hii haikuwa hivyo. Yesu, tunaelezwa wazi, alikuja kukamilishwa tu kwa njia ya mateso hapa ulimwenguni. (8) Kifo Chake Msalabani Kifo cha Bwana Yesu pia kinaleta matatizo kwa wale wanaoshikilia dhana zilizozoeleka sana kuhusu asili yake. Mungu hawezi kufa, Biblia inatuambia. (Danieli 12:7; 1 Timotheo 6:16). Wala Malaika hawafi (Mathayo 22:30.). Lakini, kama kila mtu anavyojua, Yesu alikufa msalabani. Watu wengine hufikiri wanalo jibu kwa jambo hili. Husema, “Ndiyo, lakini ulikuwa ni mwili wake tu uliokufa. Roho ndani ya mwili wake iliendelea kuishi. Fikra hizi sio sahihi. Biblia haisemi kwamba ulikuwa ni mwili wake tu uliokufa. Tunaambiwa kwamba, “kwa sababu alimwaga nafsi yake hata kufa.” (Isaya 53:12). Aidha, Biblia inatuonyesha kwamba Yesu alikiogopa kifo kama nasi tunavyokiogopa. Kifo kilikuwa ni majaribu ya kuogofya wake, kama kilivyo kwetu. “Yeye, siku hizo za mwili wake, alimtolea yule awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu.” (Waebrania 5:7.) Huu pia ni ushahidi wa kutosha kwamba Yesu hakuwa Mungu au malaika katika hali ya kibinadamu. Kiumbe kama huyo angehuzunika kiasi hicho kwa sababu ya kuupoteza mwili wake wa kibinadamu kwa muda mfupi tu? Hakika, ni mwanadamu halisi, ambaye alikuwa anakaribia kufa kweli, ndiye angeweza kuwa na hofu kama hiyo kuhusu kifo. Kwa Nini Yesu Yuko Mkono wa Kuume wa Mungu Kwa wakati huu Yesu ameketi upande wa kuume wa Mungu (Zaburi 110:1; Waebrania 1:13.) Katika maneno haya na kwa njia nyingine mbali mbali Biblia inatusimulia ni jinsi gani Yesu alivyo mkuu. Yeye ni mtu aliye mkuu katika uumbaji wote, wa pili tu kutoka kwa Mungu Mwenyewe. Hebu tuchukulie kwamba tulipaswa kuuliza swali hili, “Kwa nini iwe hivi? Kwa nini Yesu ni mkuu hivyo? Kwa nini Mungu amempa mahali pa juu hivyo? Wale wanaoamini kwamba Yesu ni Mungu au malaika wana jibu la mkato. Wanasema, “Kwa sababu daima alikuwa mkuu. Yeye alikuwa ni Roho kuu huko mbinguni kabla ya kuja duniani. Baadaye alirudi mbinguni ambako ndiko makao yake. Alirudi mahali pa juu ambako ndiko alikotoka.” (9) Lakini hili silo jibu la Biblia. Binlia inasema kuwa Yesu alikuja kupata ukuu baada ya maisha yake hapa ulimwenguni. Inasema kuwa alikuja kuwa mkuu baadaye kwa sababu Mungu alimfanya mkuu. Na inatuambia, mara zote, kwamba Mungu alimfanya mkuu kwa sababu alistahili kutokana na yale aliyoyatenda duniani. “Kwa sababu ya maumivu ya mauti, amevikwa taji ya utukufu na heshima.” (Waebrania 2:9.) “Kwa kuwa amekaza (Yesu) kunipenda (Mungu), nitamwokoa; na kumweka palipo juu, kwa kuwa amelijua jina langu.” (Zaburi 91:14.) “Umeipenda (Yesu) haki; umeichukia dhuluma, kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekupaka mafuta, mafuta ya furaha kuliko wenzako. (Zaburi 45:7.) “Aliyejinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo Mungu alimwadhimisha mno.” (Wafilipi 2:8,9.) Huu, kwa hakika, ni ushahidi wa mwisho wenye kuthibitisha kuwa Yesu alikuwa ni mwanadamu halisi. Yeye ni mwanadamu pekee aliyeweza kuyashinda majaribu ya kibinadamu kabisa. Hii ndiyo sababu sasa ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Kuyaangalia Mambo Katika Mtazamo wa Mungu Kwenye ukurasa wa kwanza na wa pili tuliyaangalia maneno ya Yesu, “Nilishuka kutoka mbinguni.” Tukiyakumbuka maneno ya utenzi ulionukuu maneno kutoka kwenye Biblia, “Karama zote njema zinazotuzunguka hutumwa kutoka juu mbinguni, “ tuliona kuwa maneno haya ya Yesu kwa namna rahisi yangeweza kuwa ni lugha ya kitamathali, na sio yeye maana ya maneno yenyewe. Sasa tunaweza kufikia hitimisho lililo wazi zaidi. Kwa kuzingatia mafundisho dhahiri tuliyoyaangalia, tunaweza kuwa na uhakika kuwa Yesu alikuwa mwanadamu halisi. Basi ikiwa ni hivyo, maneno yake kuhusu “kushuka kutoka mbinguni,” ni lazima yalikuwa ya kitamathali tu. Tunaweza kuwa na uhakika na hilo sasa. Ni dhahiri alimaanisha maisha yake yalianza wakati ule Mungu alipoushukia ulimwengu na kutenda muujiza mkuu kwa mama yake, Mariamu. Lakini hili bado linaacha baadhi ya mistari ikiendelea kutatiza. Kwa mfano, kuna maneno kutoka Yohana 17:5, ambapo Yesu anauongelea utukufu ambao “alikuwa nao pamoja na Mungu kabla ya ulimwengu kuwako,” na maneno mengine machache ambapo misemo kama hiyo inajitokeza. Msemo huo nao unaweza kuwa ni lugha ya kitamathali? (10) Ndiyo, unaweza kabisa. Lakini, ili tuiafiki maana ya misemo kama hiyo, hatuna budi kufanya jitihada maalumu kuyaangalia mambo katika mtazamo wa Mungu. Kuna tofauti nyingi baina yetu na Mungu. Tofauti moja inayotushughulisha sisi kwa sasa ni hii. Kwetu sisi wakati ujao ni muhali kuujua: tunaweza kukisia kinachoweza kutokea kesho. Lakini Mungu anajua mambo ya wakati ujao; kwake yeye kesho ni dhahiri kama ilivyo leo kwetu. Hii ndiyo maana unabii wa Biblia mara zote hutokea kuwa kweli. Paulo aliuzungumzia ukweli huu katika Warumi 4:17. Alisisitiza kuwa Mungu alikuwa amemwambia Ibrahimu katika Kitabu cha Mwanzo, “Nimekuweka kuwa baba wa mataifa mengi.” Angalia neno hili, “nime”. Siyo, “Nitakuweka,”, bali, “Nimekuweka”. Kwa wakati huo Ibrahimu alikuwa na mtoto mmoja tu. Lakini Mungu anapoahidi kitu, ahadi hiyo huwa ya uhakika. Huwa ni kama iliyokwishatimizwa tayari. Mwanadamu anapoahidi ahadi kwa kawaida husema, “Nitafanya kitu hiki na hiki”. Lakini Mungu, kupitia manabii Wake, mara kwa mara huongea hivi kuhusu wakati ujao. “Nimefanya kitu hiki na hiki,” wakati Anapomaanisha kuwa Atakitenda kweli kitu hicho. Katika sehemu iliyobaki ya Warumi 4:17 Paulo alipata fundisho kama hili hili kama hapo juu. Alisema kwamba Mungu “huyataja yale yasiyokuwako ana kwamba yamekuwako.” Wakati Ujao ni Jambo la Uhakika kwa Mungu. Kwa msaada kidogo kutoka kwa mtume Paulo tumweza sasa kuisimika kanuni moja muhimu. Kwetu sisi, ni wakati uliopita na huu tulionao tu ndio vitu halisi. Wakati ujao umefichika kutoka kwenye macho yetu. Mungu ni tofauti. Anaweza kuyaona ya wakati ujao kwa ukamilifu. Mambo ya wakati ujao ni ya uhakika kwa Mungu kama vile yalivyo yale ya wakati huu kwetu sisi wanadamu. Vile vile Mungu huweza kuongelea mambo ya wakati ujao kama kwamba yalikuwa yamekwisha tokea tayari. Kuna mifano mingi kwenye Biblia ambapo Mungu amefanya hivyo. Hapa kuna mifano mitatu kati ya hiyo. (11) (1) “Neno la Bwana likanijia kusema, “Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni nalikutakasa’.” (Yeremia 1:4,5.) Kumbe Mungu alimjua Yeremia kabla mtu huyo hajazaliwa! Ni wazi, hii ni lugha ya kitamathali. Haimaanishi kuwa ni kweli Yeremia alikuwako kabla ya kuzaliwa kwake. Inamaanisha kuwa Mungu aliweza kuona mbele ya wakati na kumwona Yeremia kabla hajazaliwa. Kwa maneno mengine, kabla Yeremia hajazaliwa, alikuwako katika fikra za Mungu. (2) “Kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika upendo. Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo sawasawa na uradhi wa mapenzi yake.” (Waefeso 1:4,5.) Hivyo haikuwa ni Yeremia peke yake; Mungu pia aliwajua watu wa kanisa lake kabla ya kuzaliwa kwao! Hii pia ni lugha ya kitamathali, iliyotegemezwa kwenye hekima ya Mungu ya kujua mambo ya wakati ujao. Katika sentensi ya pili ya dondoo hiyo, Paulo alisema kile ambacho alimaanisha, katika lugha yeye maana iliyo wazi: “Mungu alikuwa amekwisha amua kwamba angetufanya tuwe wanawe.” (3) “Naye (Yesu) amejulikana kweli tangu zamani, kabla haijawekwa misingi ya dunia; lakini alifunuliwa mwisho wa zamani kwa ajili yenu.” (1 Petro 1:20.) Katika nukuu hiyo, maneno “amejulikana tangu zamani” yanatushughulisha kidogo. Ni tafsiri ya neno la Kiyunani lenye kumaanisha “kufahamika mapema.” Hili ni aina ya neno la Kiyunani ambalo kwalo limepatikana neno la Kiingereza “prognosis”. Prognosis maana yake ni ubashiri. Ubashiri ni neno litumiwalo sana na madaktari. Kama lilivyo neno la Kiyunani linalofanana nalo, linamaanisha “utambuzi wa mapema.” Daktari anaweza kusema, kwa mfano, “Mtu huyu ana kansa ya tumbo. Ubashiri wangu ni kuwa kuvuja damu kutaendelea, na atakuwa amekufa ndani ya mwezi mmoja.” Madaktari, bila shaka, huweza kufanya makosa. Wanakubali kuwa ubashiri wao, kama ulivyo utabiri wa hali ya hewa, mara nyingi hutokea kuwa sio kweli. Mungu ni tofauti. Yeye kwa hakika hutambua mapema. Ubashiri wa Mungu ni wa uhakika kabisa. Hivyo mstari ulionukuliwa juu, unatuambia kuwa Mungu alijua yote kuhusu Yesu kabla hajaumba ulimwengu. Hili pekee ndilo tunalopaswa tulitarajie. Tumeona kwenye nukuu ya mwanzo kuwa Mungu alijua yote kuhusu Wakristo wa mwanzo kabla ulimwengu haujaanza. Yeremia, kanisa la mwanzo, na Bwana Yesu Kristo. Wote walikuwapo, kwenye fikra za Mungu, tangu mwanzo wa nyakati. (12) Hivyo haishangazi kwamba Yesu alikuwa amesema kwa Baba yake mbinguni, “Unitukuze mimi pamoja nawe, kwa utukufu ule niliokuwa nao pamoja nawe kabla ya ulimwengu kuwako.” (Yohana 17:5.) Tunajua sasa alikuwa ana maana gani kwa kauli hii. Mungu Mpangaji Mkuu Wakati wowote wanadamu wanapokusudia kufanya jambo lolote muhimu wanaanza kwa kuandaa mpango wa jinsi watakavyolitekeleza jambo hilo. Kabla ya kuanzisha vita, kamanda wa jeshi anatayarisha mpango wa vita, na kuwaonyesha majenerali wake. Kabla jengo lolote kubwa halijasimikwa, msanifu wa majengo hupewa jukumu la kuchora ramani ya jengo hilo. Mipango ya wanadamu mara nyingi inakwama. Adui anaweza kusonga mbele kwa kushitukiza na kuwafanya majenerali washindwe kuanzisha shambulizi lao kama lilivyopangwa. Mteja wa ujenzi huweza kuishiwa fedha na hivyo kumwamuru msanifu majengo kuchana chana michoro yake. Lakini hakuna kinachoweza kumzuia Mungu kutekeleza mipango yake kwa ulimwengu huu. Kama tulivyokwisha ona, Alianza kusema kama vile mipango yake ilikuwa tayari imekwishakamilishwa, hata kabla hajaanza kufanya lolote. Agano la Kale lilikuwa na neno kwa mpango wa Mungu. Liliuita “Hekima” ya Mungu. Kamusi Mpya ya Biblia (iliyoandikwa na watu wa makanisa, sio na Wakristadelfiani) inasema kuwa neno hekima katika Agano la Kale lina maana ya “utekelezaji wa Mungu usiozuilika wa yale aliyonayo katika fikra zake.” Hiyo ni fasili nzuri. Inaendana vizuri na maneno yafuatayo ya Agano la Kale. “Je! Hekima halii? Ufahamu hautoi sauti yake? … mahali pa kuyaingilia malango anapiga kelele: … Bwana alikuwa nami (hekima) katika mwanzo wa njia yake, kabla ya matendo yake ya kale. Nalitukuka tokea milele, tangu awali, kabla haijawako dunia.” (Mithali 8:1-23.) Kwa maneno mengine, kabla Mungu hajaanza kazi yake kwa dunia hii, aliandaa mpango wake – Hekima, kama Wayahudi walivyouita. Wayunani, ambao waliamini katika mungu au miungu, ingawaje sio Mungu wa kwenye Biblia, walikuwa na jina tofauti. Mpango wa Mungu waliuita “Neno” la Mungu. Kamusi hiyo hiyo ya Biblia inasema kuwa neno la Kiyunani kwa “neno” linamaanisha “mpango wa Mungu na pia nguvu za Mungu za uumbaji.” (13) Hii inatoa msaada mkubwa kwa sababu inatuwezesha kuielewa sura ya kwanza ya Injili ya Yohana. Inaelekea Yohana alichanganya dhana ya Kiyunani ya Neno la Mungu na dhana ya Kiyahudi ya Hekima ya Mungu. Injili yake inaanza hivi, “Hapo mwanzo kulikuwako Neno.” Watu wengine hawawezi kupata maana yoyote kutoka katika maneno hayo. Wengine hudhani wanaweza, lakini wanapata maana isiyo sahihi kutoka kwenye maneno hayo, kwa sababu wanafikiri Neno ni kiumbe anayeishi. (Kwa hali hiyo, ndiyo maana wafasili katika maneno haya wanalitaja Neno kama “naye” katika Biblia yetu ya Kiswahili. Neno la Kiyunyni kwa “naye” pia lina maana hiyo hiyo kwa “nalo”, na ndiyo inavyopaswa itafsiriwe hivyo hapa.) Sasa iwapo tutafikiri juu ya “Mpango” wa Mungu badala ya “Neno” Lake, na tukaliona kuwa ni “nalo” na sio “naye”, hiki ndicho tunachojifunza kutoka Yohana 1: “Hapo mwanzo kulikuwako Mpango, nao Mpango ulikuwako kwa Mungu, na Mpango ulikuwa Mungu. Mpango ulikuwako kwa Mungu toka mwanzo; vitu vyote vilifanyika kupitia Mpango, wala pasipo huo hakikufanyika chochote kilichefanyika … Nao Mpango ulifanyika mwili, ukakaa kwetu, nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.” (Yohana 1:1-14.) Maneno haya ya Yohana yanatoa muhtasari wa mafundisho ya Biblia vizuri sana. Yesu alikuwako mbinguni toka mwanzo, lakini sio kama nafsi. Alikuwako kama wazo kuu katika fikra za Mungu, kama kitovu kikuu cha Mpango wa Mungu. Hakuwako kama nafsi mpaka alipozaliwa Bethlehemu. Hivyo, kwa maneno ya Yohana, “nao Mpango ulifanyika mwili. Kumtukuza Yesu Kwa kuwa sasa tumekwisha ona yale Biblia inayofundisha kumhusu Yesu, tunaweza kuanza kumtukuza yeye kama ambavyo. Pengine, hatujawahi kufanya kabla. Utaweza kuona kwa nini hivi ndivyo iwapo utapiga taswira nyuma juu ya yale tuliyokwisha yajadili. Tuliona kwamba kuna aina mbili za lugha kwenye Biblia. Kuna lugha ya maana ya moja kwa moja, ambayo inamaanisha yale inayoyaongelea kama yalivyo. Na kuna lugha ya kitamathali, yenye kubeba maana nzito zaidi. Wakati ule Yesu aliposema alishuka kutoka mbinguni hakuwa amewahi kukaa huko mbinguni yeye binafsi. Hivyo maneno yake yasingeweza, kwa lugha ya maneno yeye maana ya moja kwa moja, kuwa kweli, bali ni lazima yalikuwa na maana ya kitamathali. (14) Kwa sababu Mungu anajua kila kitu Anaweza kuona yote ya wakati ujao. Mungu Mwenyezi anapoamua kutenda kitu huwa tayari ni kama kilichokwisha fanyika. Hivyo kabla hajauumba ulimwengu Mungu alitayarisha mpango au ramani ya kufuatwa wakati wa utekelezaji. Yesu alikuwa ni mwanzo wa mpango huu, na alikuwa sehemu muhimu sana ya mpango huo. Wafuasi wa Yesu, nao pia, wote walikuwemo kwenye mpango huo. Wote hao pamoja na Yesu, Bwana wao, wanatajwa kuwa walikuwako kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu. Si yeye wala wao walikuwa wakiishi wakati huo, bila shaka. Walikuwako tu katika fikra za Mungu kama sehemu ya mpango Wake. Katika maana hii ya kitamathali walikuwako wote mbinguni tangu mwanzo wa uumbaji. Lakini maisha halisi ya Bwana Yesu Kristo yalianza tu pale alipozaliwa mjini Bethlehemu. Kuzaliwa kwake kulikuwa kwa muujiza. Mungu alikuwa baba yake, na Mariamu, mama yake, alikuwa bikira. Alikuwa ni mama yake halisi, naye alikuwa ni mwana wake kabisa kama alivyokuwa mwana wa Mungu. Kwa sababu hiyo alikuwa ni mwanadamu halisi. Hii ilimaanisha kuwa alipatwa na majaribu yale yale ya kutenda dhambi kama mwanadamu mwingine yeyote. Lakini aliyashinda majaribu, kabisa. Aliishi maisha yasiyokuwa na dhambi, na akapata ukamilifu wa tabia. Kama tuzo kwa hilo Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, na kumfanya kiumbe mkuu ulimwenguni baada ya Mungu Mwenyewe. Iwapo ilimpendeza Mungu kumtukuza Yesu namna hiyo, nasi pia hatuna budi kumtukuza na kusema kwa Mungu: “Baba Yetu wa Mbinguni, mwanao alilazimika kupambana na majaribu, kama mimi ninavyolazimika kupambana nayo. Hivyo anafahamu jinsi ninavyojisikia.” “Lakini alishinda kila vita aliyopigana dhidi ya majaribu, wakati mimi mara kwa mara nashindwa katika vita ninayopigana. Bwana, naustaajabia ushindi wake mkuu na ninatamani ningeweza kufuata mfano wake kwa ukamilifu zaidi kuliko ninavyofanya.” “Lakini mimi ni dhaifu. Bwana nihurumie na unisaidie. Nisaidie niweze kufananna zaidi na Mwanao. Nisaidie niweze kujaribu kwa moyo wangu wote kumfuata yeye. Nisaidie niweza kumpenda, kumtukuza na kumtii.” “Mwenyezi Mungu, Mwanao amepitia maisha haya ya mateso na mauti yeye binafsi. Kwa sababu ninafahamu ananijua mimi, Bwana, naomba kupitia kwake msaada wako. Na ninajua kuwa utanisikia.” (15) Nukuu za Maandiko katika chapisho hili ni kutoka The Holy Bible in Kiswahili, Union Version, published as Maandiko Matakatifu yeye haki miliki za Chama cha Biblia Tanzania, 1994 na Chama cha Biblia Kenya, 1994. (16) Tena: 1 902059 00 - X Matayarisho ya Ubatizo 1 902059 01 - 8 Masomo ya Biblia kwa njia ya posta ya Wakristadelphian 1-4 1 902059 02 - 6 Ukimwi 1 902059 03 - 4 Mshitaki Wenu Ibilisi 1 902059 04 - 2 Masomo ya Biblia kwa njia ya posta ya Wakristadelphian 5-8 1 902059 05 - 0 Masomo ya Biblia kwa njia ya posta ya Wakristadelphian 9-11 1 902059 06 - 9 Masomo ya Biblia kwa njia ya posta ya Wakristadelphian 12-15 1 902059 07 - 7 Masomo ya Biblia kwa njia ya posta ya Wakristadelphian 16-19 1 902059 08 - 5 Masomo ya Biblia kwa njia ya posta ya Wakristadelphian 20-23 1 902059 09 - 3 Masomo ya Biblia kwa njia ya posta ya Wakristadelphian 24-27 1 902059 10 - 7 Masomo ya Biblia kwa njia ya posta ya Wakristadelphian 28-31 1 902059 11 - 5 Masomo ya Biblia kwa njia ya posta ya Wakristadelphian 32-36 1 902059 12 - 3 Masomo ya Biblia kwa njia ya posta ya Wakristadelphian 37-40 1 902059 13 - 1 Ufunuo mlango wa kwanza - Maelezo ya maneno ya mstari kwa mstari 1 902059 14 – X Ni Kweli Yesu Kristo Alishuka Kutoka Mbinguni? Kama unataka kujifunza zaidi njia ya Mkristo wa kweli anavyopaswa kuishi, basi ni lazima ujifunze Biblia. Ili kukusaidia; Kanise la Christadelphian Bible Mission limechapisha kijitabu kuhusu mafunzo ya Biblia kaitka somo hili muhimu. Lina itwa Kuishi katika Ukweli. Unaweza kupata nakala kutoka Kanisa la Christadelphian, au kutoka anuani iliyoandikwa katika kijitabu hiki. CBM Publishing 32 Blenheim Road, Far Cotton Northampton, England. NN4 8NW ISBN 1 902059 14 - X Registered Charity Number: 248979 / 1020558 Company Number: 2796412 Telephone +44 (0) 1604 463578 Facsimile +44 (0) 1604 765068 Email: CarlHinton@hotmail.com Web: http:\\www.CBM-Tz.org