Kitabu cha Matendo ya Mitume UTANGULIZI Kitabu cha Matendo ya Mitume ni kitabu cha maana sana kwa ufahamu wetu kuhusu chanzo cha Ekklesia na ukuaji wake wakati wa kwanza. Jina lake refu, yaani Matendo ya Mitume, linadokeza kazi nyingi zaidi ya Mitume Yohana na Petro katika siku za kwanza za Ekklesia na kazi kubwa ya Mtume Paulo katika maendeleo na uenezi wa Ekklesia katika ulimwengu wa Mataifa. Kitabu hiki pia kina maana kubwa kwa kuelewa Maandiko ya Agano Jipya kwa ujumla wake. Barua za kwanza za Paulo ziliandikwa wakati wa Matendo ya Mitume, na wasomaji wa siku hizi wataelewa hata nyaraka nyingine za Agano Jipya vizuri zaidi wakijua kitabu cha Matendo ya Mitume. Mwandishi wa Matendo ya Mitume Maelezo ya wakati wa kwanza wa Ukristo, pamoja na Maandiko mengine ya Biblia yenyewe yanadokeza kwamba Luka aliandika kitabu cha Matendo ya Mitume. Kitabu hicho kilikuwa cha pili kati ya vitabu viwili vilivyoandikwa na Luka, yaani cha kwanza kilikuwa Injili ya Luka. Luka alimwandikia mtu mwenye heshima aliyeitwa Theofilo, ili kumpatia maelezo ya kuaminika kuhusu Ukristo tangu wakati wa kuzaliwa kwa mwanzilishi wake mpaka Mtume wake mkuu alipofika Rumi (Lk 1:1-4; Mdo 1:1-2). Kwa utaalamu wa fani yake Luka alikuwa mganga (Kol 4:14), lakini pia alikuwa mwandishi wa historia mwenye uwezo sana. Wataalamu wa historia wasio Wakristo wanamtambua kuwa mwandishi aliyeaminika, na masimulizi yake ni kitabu cha marejeo kwa uchunguzi wa wakati ule uliobadilisha mkondo wa historia ya ulimwengu. Kwa uangalifu sana alitaja tarehe za mwanzo wa masimulizi yake akizilinganisha na matukio ya historia isiyohusika na dini (Lk 1:5; 2:1-2; 3:1-2), na vitu vilivyogunduliwa na ajiolojia vinathibitisha usawa kabisa wa maneno ya teknolojia aliyoyatumia kuhusu mahali na maafisa wakuu (Mdo 13:7; 16:12,35; 18:12,16; 19:31,35). Sehemu nyingine za Matendo ya Mitume ni masimulizi ya ushahidi wa Luka mwenyewe, nazo zinaonekana pale alipotumia neno 'sisi'. Katika safari mbili za Paulo za kueneza Injili, kwa sehemu alisafiri pamoja na Paulo (Mdo 16:10-12; 20:5-6,13; 21:1,7,17), kisha alifuatana naye katika safari yake ya kwenda Rumi iliyoelezwa katika mwisho wa kitabu chake (Mdo 27:1-3; 28:16; taz.Flm 23-24). Kutokana na cheo ambacho Luka alikitumia kwa kumtaja Theofilo, inaonekana kama Theofilo alikuwa afisa mkuu wa serikali ya Kirumi (Lk 1:3; taz.Mdo 23:26; 26:25). Kama ilikuwa hivyo au sivyo, ni wazi kwamba wakati Luka alipoandika (yaani katika mwanzo wa mwongo wa sita b.K.), serikali ya Kirumi iliangalia sana Ukristo. Kwa hiyo Luka alijitahidi kuonyesha kwamba Ukristo haukupinga utawala wa Kirumi kwa njia yo yote wala haukuwa hatari kuhusu sheria ya serikali. Ili kuelewa sababu ya kutetea Ukristo namna hiyo, inafaa tukiangalia hali ya ufalme wa Kirumi ambamo Wakristo waliishi. Ibada ya Kaisari Katika karne ya mwisho kabla ya Ukristo, Warumi walieneza mamlaka yao mbali sana, lakini jambo hili halikujenga ufalme wa Kirumi moja kwa moja kama tunavyoujua katika Agano Jipya. Baada ya kuuawa kwa Julius Caesar mwaka wa 44 k.K., Rumi ilipitia muda wa taabu sana wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, machafuko ya kisiasa na shida nyingi za jumuia. Maelfu ya watu walikuwa maskini na pasipo kazi, wala watu hawakujali haki na sheria. Rushwa ilitawala, hasa kwa maafisa wa serikali, na wakuu wa jeshi walijaribu kujipatia mamlaka zaidi kwa njia ya hila na njama mbalimbali. Halafu, mwaka wa 27 k.K., mkuu mmoja alitokea aliyeweza kutawala vizuri na hata kuondoa machafuko nchini. Mtu huyo alikuwa mtawala wa kwanza wa ufalme ule mkubwa tunaouita Milki au Dola ya Kirumi, naye alichukua jina lake Kaisari Augusto (Caesar Augustus)(Lk 2:1). Alisifiwa na kuheshimiwa sana na watu, hata wafalme wote waliomfuata katika kiti cha enzi cha Rumi walichukua jina hilo la Kaisari kuwa ni cheo maalumu cha utawala wao (Lk 3:1; 20:22; Mdo 25:11,25). Watu walimshukuru sana Augusto kwa amani na sheria aliyoleta, hata wakamtukuza katika lugha ambayo kwa kawaida ilitumiwa kwa kusifu miungu yao. Kutokana na hayo, ibada ya Kaisari ilianzishwa ambayo baadaye ilikuwa dini rasmi ya kitaifa. Dini nyingine ziliruhusiwa, lakini ilibidi ziandikishwe (au kusajiliwa) kwanza serikalini. Hata hivyo, watu wote walipaswa kuisujudu na kuiabudu sanamu ya Kaisari, ingawa waliweza kuwa na dini nyingine zilizosajiliwa na serikaii. Wayahudi tu hawakulazimishwa kutii sheria hiyo, kwa sababu Warumi walijua kwamba Wayahudi kamwe wasingeinama mbele ya sanamu yo yote. Wakati wote Warumi walipoamini kwamba Ukristo ni dhehebu la dini ya Kiyahudi, hawakuchukua hatua yo yote dhidi ya Wakristo. Lakini mara walipotambua kwamba Ukristo ni dini mpya tofauti na Uyahudi, na hivyo ilikuwa nje ya sheria ile ya pekee, Warumi waliwaudhi Wakristo kwa kuwafanyia ukatili sana. Uraia wa Kirumi Hapo mwanzo raia wa Kirumi alikuwa mwenyeji wa jiji la Rumi tu aliyepewa haki na upendeleo wa aina mbalimbali wa pekee uliotolewa na Kaisari. Baadaye serikaii ilipanua uraia ule hata kwa watu wa miji na mikoa mingine, au kwa watu waliojitoa zaidi kwa ajili ya ufalme. Watu wengine waliweza kuununua uraia huo. Uraia huo uliweza kutolewa kwa watu wasiokuwa na damu ya Kirumi, na watoto wao waliurithi kutoka kwa wazazi wao (Mdo 22:28). Raia wa Kirumi hakuweza kufungwa au kupigwa na hakimu au afisa wa mahali fulani wala hakuweza kuuawa bila hukumu maalumu ya baraza la wazee waliohusika. Raia aliweza kujitetea mbele ya mahakama, na kama hakuridhika na hukumu ya baraza hilo, aliweza kukata rufaa mpaka kufikia kwa Kaisari (Mdo 16:37; 22:25-29; 25:11). Mawasiliano Kati ya miji na majimbo ya ufalme wa Kirumi kulikuwa na usafiri na biashara nyingi. Maafisa wa serikaii, wafanyabiashara na askari walisafiri katika nchi zote za madola, ili waendeshe biashara na kulinda sheria na amani. Kwa kawaida waliishi katika miji maalumu iliyoitwa Makoloni. Katika miji hiyo iliyoimarishwa na kujengwa kwa mtindo wa Kirumi, maisha na mila ya Kirumi viliendeshwa, ingawa watu walikuwa mbali sana na jiji lao kuu. Raia wa miji hiyo walipewa madaraka ya kutawala miji yao, nao walipewa upendeleo wa aina nyingi wa uraia wa Kirumi. Baadhi ya miji hiyo iliyoitwa makoloni ilikuwa Antiokia ya Galatia, Listra, Troa, Korintho na Filipi (Mdo 16:12). Miji hiyo pamoja na mingine iliyokuwa ya maana iliunganishwa na Rumi kwa mabarabara makubwa na imara yaliyojengwa na Warumi katika ufalme wao wote. Wamisionari wa kwanza walichagua miji ile kwa kazi yao ya kueneza Injili na kuanzisha maEkklesia. Kama maEkklesia hayo yaliimarika vizuri, Injili iliweza kuenea upesi katika maeneo yote yaliyokuwa karibu. Lugha ya Kiyunani iliyoenea katika nchi zote wakati wa utawala wa Wayunani, iliendelea kuwa lugha kuu iliyotumika katika nchi zote za Dola ya Kirumi. Jambo hili lilisaidia sana kueneza Injili upesi kwa watu wa mataifa mengi. Lugha nyingine zilitumika katika mikoa mbalimbali (kwa mfano katika Palestina lugha ya Kiaramu iliyofanana na Kiebrania ilitumika), lakini kwa kawaida lugha ya Kiyunani ilitumika (taz. Mk5:41; 15:34; Yn 19:20; Mdo 14:11; 22:2). Lugha hiyo ya Kiyunani pia ilitumika karibu sehemu zote kwa kusoma na kuandika. Agano Jipya liliandikwa katika lugha hiyo, lakini siyo katika Kiyunani cha kale cha wasomi, bali katika lugha iliyotumiwa na watu wote. Hata hivyo, ilikuwa lugha tajiri kwa maneno na yenye nguvu ya ufafanuzi wa tofauti ndogo ndogo za maana na mawazo. Kwa sababu hii lugha hiyo ilifaa zaidi kuwa lugha ya asili ya Agano Jipya, ili Mungu awajulishe watu lengo lake kuu la wokovu wa ulimwengu. Wayahudi katika nchi za Madola ya Kirumi Kwa muda wa karne kadhaa Wayahudi walitawanyika katika nchi zote za Madola ya Kirumi. Baadhi yao walikuwa wamehamia kutafuta nafasi nzuri kwa ajili ya biashara, na wengine walikuwa wamekimbia nchi yao wakati wa shida na vita. Pia walikuwepo wale ambao wazazi wao zamani walichukuliwa mateka na mataifa ya kigeni, kama vile Waashuri na Wababeli waliokuwa wamevamia Israeli, kisha walihamia sehemu nyingine baada ya kupewa ruhusa na wakuu wao. Wayahudi wale waliitwa 'Wayahudi wa Utawanyiko', 'Waliotawanyika' au 'Wayahudi wa Diaspora' (Yn 7:35; IPet 1:1; Yak 1:1; 2Fal 15:29; 17:6; 24:14-15; 25:11; Ezra 1:1-4). Wayahudi walikuwa wameishi katika nchi za kigeni kwa miaka mingi, kwa hiyo wengi wao walijua lugha ya Kiyunani tu, wala hawakujua lugha ya Palestina, kama vile Kiebrania au Kiaramu. Hata hivyo, walihifadhi umoja wa Kiyahudi kwa njia ya kudumisha dini ya mababu zao. Po pote walipoishi, walijenga masinagogi kama vituo vya ibada, mafundisho na hifadhi ya mila na mambo ya Kiyahudi (Lk 4:16-17,31,33; 12:11; Mdo 13:14; 17:1; 18:7-8). Walifuata mapokeo ya torati ya Musa, na kama waliweza walikwenda Yerusalemu kwa kuazimisha sikukuu mbalimbali za kidini (Yn 5:1; 7:1-3). Wapagani wengi walivutiwa na hali ya juu na maadili ya dini ya Kiyahudi, na mara nyingi walihudhuria ibada za masinagogi. Baadhi yao walikubali hata kutahiriwa na kubatizwa kama Wayahudi, na hivyo walijulikana kuwa waongofu wa Wayahudi au 'proselitV (Mdo 2:10-11; 6:5). Lakini wengi wao hawakukubali haya yote. Walihudhuria ibada za masinagogi tu na kushika baadhi ya sheria za Sabato na chakula, ili wapate usafi zaidi na utakatifu katika maisha yao. Hao waliitwa ' Wachaji wa Mungu' au 'Watauwa' (Mdo 10:1-2; 16:14). Wengi wa watu wale wa kitaifa waliokwisha mjua na kumwabudu Mungu wa Wayahudi, walipenda kuwa Wakristo baada ya kusikia Injili ya Yesu Kristo (Mdo 13:43; 14:1; 17:4). Watu halisi wa Mungu Katika kitabu chake chote kwa Theofilo, Luka alionyesha wazi kwamba Wakristo, wala siyo wafuasi wa Uyahudi, walikuwa watu halisi wa Mungu. Ukristo haukuwa dini ya kinyume, bali ni mfululizo hasa wa mipango ya kidini ya Ibrahimu, iliyoendelezwa na Musa, Daudi na taifa la Israeli (Mdo 2:31-33; 15:15-18; 26:22-23; 28:23). Maendeleo hayo kutoka wakati wa kale hadi wakati mpya, yaani kutoka wakati wa Uyahudi mpaka ule wa Ukristo, yalisababishwa na Yesu Kristo. Yeye alikuwa Mwokozi wa Mungu kwa ulimwengu, yaani Masihi ambaye dini ya Kiyahudi ilimtaja, na kwa ajili yake dini hiyo iliandaa njia (Mdo 2:36; 3:18; 9:22; 17:3; 18:5,28). Wakristo waliwasaidia watu wengine. Walitoa misaada na uponyaji kwa wale waliokuwa wagonjwa, wenye shida na maskini (Mdo 3:2-6; 5:15-16; 9:32.41; 11:28-29; 14:8-10; 28:7-9). Maranyingine waliweza kuingizwa katika machafuko ya jamii, lakini Luka alionyesha wazi kwa mifano mbalimbali kwamba kamwe hawakuwa waanzilishi wa machafuko yo yote. Daima mamlaka ya Kirumi yalithibitisha kwamba Wakristo hawakuwa na hatia (Mdo 16:37-39; 18:12-16; 19:31,37; 23:20; 25:18; 26:31-32; 28:30-31). Karibu kila mara matatizo yalipotokea yaliyowahusu Wakristo, Wayahudi walistahili kupata lawama yake (Mdo 9:23,29; 13:50; 14:2,5,19; 17:5,13; 18:12-17; 21:27). Masimulizi yote ya Luka yalisisitiza ushindi wa Injili ya Kikristo na baraka yenye kutoa uzima iliyoletwa kwa watu wote bila ya kujali ukabila wao, na kuonyesha jinsi ambavyo kwa muda wa miaka 20 tu Ukristo uliongezeka kutokana na waamini wachache sanajijini Yerusalemu mpaka jumuia kubwa iliyoleta uzima mpya na matumaini katika Asia Ndogo, Ulaya ya mashariki na hata Rumi yenyewe (Mdo 28:31). MUHTASARI 1:1-2:47 Kuzaliwa kwa Ekklesia 3:1-5:42 Kukua kwa haraka na kupata sifa kwa watu. 6:1 -8:3 Mabadiliko Yerusalemu 8:4-9:31 Katika Palestina na nje yake 9:32-12:25 Yerusalemu na Mataifa 13:1-14:28 Kuingia Asia Ndogo 15:1-35 Tatizo kubwa la kwanza la Ekklesia 15:36-18:22 Kuingia Ulaya 18:23-21:16 Katika Asia Ndogo na Ulaya tena 21:17-23:35 Mwisho Yerusalemu yakataa Injili 24:1-28:31 Paulo aondoka mashariki na kwenda Rumi