MAELEZO KUHUSU INJILI YA YOHANA Mshiriki wa Yesu Mapokeo ya karne ya kwanza pamoja na maandiko ya Biblia yanadokeza kwamba 'Mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda' alikuwa Yohana mwana wa Zebedayo, na Yohana huyo alikuwa mwandishi wa Injili ya Yohana (Yn 21:20,24). Ingawa waandishi wa Injili nyingine wanamtaja Yohana mara nyingi, jina lake halionekani katika Injili ya Yohana. Kwa kufanya hivi, bila shaka mwandishi alifuata desturi ya wengi ya kudokeza jina lake tu, lakini watu walifahamu maana yake ya kweli (Yn 13:23; 19:26; 27:7). Kwa kutumia jina lake hivyo, labda vile vile alitaka kuonyesha shukrani yake kwa Yesu kwa yote aliyomfanyia. Familia ya Yohana iliishi pwani ya Ziwa Galilaya. Yeye na kaka yake Yakobo walishirikiana na baba yao Zebedayo katika kazi ya uvuvi pamoja na Petro na Andrea waliokuwa ndugu wawili wa familia nyingine ya kijiji chao (Mt 4:18-21; Lk 5:10). Mama yake, Salome anaonekana kuwa umbu lake Mariamu, mama yake Yesu (Mt 27:56 Mk 15:40; Yn 19:25). Inaonekana kama ndugu wale wawili wawili, yaani Yohana na Yakobo na Petro na Andrea, waliitikia mahubiri ya Yohana Mbatizaji nao walimtazamia Mwokozi aliyeahidiwa. Yesu alipofika, wao walikuwa miongoni mwa watu wa kwanza waliomfuata (Mt 4:22; Yn 1:35-40). Baadaye wote wanne walikuwemo katika kundi la Mitume 12 (Mt 10:12), na Petro, Yakobo na Yohana baadaye walikuwa karibu zaidi na Bwana (Mk 5:37; 9:2; 14:33). Yesu aliwaita Yakobo na Yohana 'Wana wa ngurumo', labda kwa sababu mara nyingine walikuwa na juhudi zaidi wasiweze kuitawala bidii yao (Mk 3:17; Lk 9:49-56). Petro alipoendelea kupata sifa zaidi miongoni mwa wanafunzi, Yakobo na Yohana walijaribu kumrudisha nyuma kidogo kwa njia ya kumwomba Yesu awape wao wawili vyeo vikuu katika ufalme. Ahadi ya pekee ambayo Yesu aliwapa ilikuwa ya adha iliyowakabili (Mt 20:20-28). Wakati wa kupaa kwake Yesu, Petro na Yohana walionekana wazi kuwa Mitume wawili walioongoza (Lk 22:8; Yn 19: 26-27; 20:2-9; 21:20). Kiongozi wa Ekklesia Katika Ekklesia la kwanza Petro na Yohana walikuwa katika uongozi maalumu nao walipata adha kali (Mdo 1:13; 3:1-11; 4:13-20; 5:40). Walikuwa miongoni mwa watu wa kwanza walioonyesha kwamba Ekklesia lazima lipokee watu wasio Wayahudi sawa sawa na Wayahudi (Mdo 8:14-17,25) nao walitoa changamoto kwa kazi ya kueneza Injili kwa Mataifa (Gal 2:9). Biblia haisemi mengi kuhusu huduma nyingine za Yohana. Maandiko yasiyo ya Biblia yanadokeza kwamba alipata umri mkubwa sana (taz.Yn 21:20-23), na miaka yake ya mwisho aliishi Efeso na jirani yake, na kutoka huko aliandika Injili yake na barua zake. Alijulikana kuwa ni 'Mzee' (2Yoh 1; 3Yoh 1), na kufuatana na mapokeo ya kale, alikuwa mwandishi wa kitabu cha Ufunuo. Ikiwa hivyo, labda miaka yake ya mwisho alikuwa mfungwa katika kisiwa cha Patmo, si mbali kutoka pwani ya Efeso (Ufu 1:9). Mapambano na walimu wa uongo MaEkklesia ya maeneo ya Efeso kwa muda mrefu yalihangaishwa na mafundisho ya kinyume (taz.Mdo 20:17,29-30; Ufu 2:2). Mafundisho yenyewe yalikuwa ya aina ya Unostiki ulivyotokea wakati wake wa kwanza, yaani mafundisho ya kinyume yaliyoleta shida kubwa katika maEkklesia ya karne ya pili. Wanostiki walijaribu kueleza baadhi ya siri za ulimwengu - kama vile uhusiano baina ya wema na uovu, roho na mwili, Mungu na wanadamu -wakiunganisha imani ya Kikristo na falsafa ya kipagani. Walikanusha kwamba kunaweza kuwa mwungano wa mambo yanayoonekana kama hayalingani, kwa hiyo baadhi yao walikanusha kwamba Yesu alikuwa mwanadamu kamili, na wengine walikanusha kwamba alikuwa Mungu kamili. Yohana alipinga kabisa makosa hayo yote. Lakini maandiko yake yalikuwa zaidi kuliko upinzani wa mafundisho ya kinyume. Yeye alikuwa na makusudi ya kuwajenga na kuwaongoza Wakristo katika imani thabiti katika Kristo, ili waweze kuwa washiriki kamili wa uzima wa milele unaotolewa na Yesu Kristo (Yn 20:31; taz.i:4; 3:15; 4:14; 5:24; 6:27; 8:12; 10:10; 11:25; 14:6; 17:3; taz.pia lYoh 1:1-3; 5:13). (Kuhusu uhusiano wa Yohana na Injili nyingine, taz. kipengele kilichotangulia cha 'Uandishi wa Injili nne'.) Upekee wa Bwana Yesu Tangu mwanzo wa Injili yake, Yohana aliweka wazi kwamba Yesu alikuwa Mungu (Yn 1:1) naye alikuwa mwanadamu (Yn 1:14). Alikuwa wa milele (Yn 1:2), aliumba vitu vyote (Yn 1:3) naye alitoka mbinguni ili kumdhihirisha Mungu kwa wanadamu (Yn 1:18; 3:13; 5:18-19; 6:62; 8:23,26; 14:9,11). Pia alikuwa mwanadamu kamili. Alikuwa na mwili wa binadamu pamoja na viungo vyote (Yn 4:6-7; 9:6; 12:3; 19:34), naye alikuwa na hisia za kawaida za wanadamu (Yn 11:35; 12:27; 19:26-27). Kama Wanostiki wenye mafundisho ya uasi wa mwongo wa tisa wa karne ya kwanza walikuwa na shida ya kumkubali Yesu katika upekee wake, hata Wayahudi walioshika mapokeo wa mwongo wa tatu walikuwa na shida hiyo. Mtindo wa kuwafundisha watu waliohangaishwa katika maeneo ya Efeso ulikuwa kukariri habari na mafundisho ya Yesu. Alikumbuka habari nyingi sana za Yesu (Yn 21:25), lakini alichagua chache tu. Hakusimulia matukio ya maisha ya Yesu tu, bali alionyesha maana ya matukio hayo. Kwa sababu hiyo aliyaita 'ishara' (Yn 20:30; taz.2:ll; 4:54; 6:14; 7:31; 12:18,37). Ishara za Yesu, licha ya kuonyesha kwamba alikuwa Masihi, pia zilionyesha kwamba alikuwa Mwana wa Mungu (Yn 20:31). Wayahudi walifikiri kwamba Yesu alikufuru alipojidai kuwa Mungu aliyekulia miongoni mwao (Yn 6:42; 8:53-59; 10:33; 19:7). Matokeo yake, ishara za Yesu mara nyingi zilisababisha mahojiano marefu sana na Wayahudi (k.mf.mwujiza wa Yn 5:1-15 ulisababisha mahojiano ya 5:16-47; mwujiza wa Yn 9:1-12 ulisababisha mahojiano ya 9:13-10:38). Mahojiano hayo na mengine ambayo Yesu na Wayahudi walikuwa nayo yalimpa Yohana mambo mengi ya kufundisha. Alitumia maneno yale yale ya Yesu kwa kuwafundisha Wakristo ukweli (Yn 7:1-39; 8:12-58). Kama Yohana na mwandishi wa Injili nyingine walisimulia habari za mwujiza mmoja, walitumia habari zake kwa njia tofauti. Kama mwandishi mwingine hakuandika mengi zaidi kuliko kusimulia habari yenyewe, Yohana aliongeza kusimulia mafundisho mengi yaliyotokana nayo (ling.Mt 14:13-21 na Yn 6:1-14 na mafundisho yaliyofuata katika Yn 6:26-65). Yohana alitaka kuonyesha maana na umuhimu wa matukio, kwa hiyo alisimulia baadhi ya mazungumzo na watu fulani kwa kirefu sana (k.mf. na Nikodemo katika Yn 3:1-15, na mwanamke wa Samaria katika Yn 4:1-26). Hali kadhalika alitumia masimulizi ya karamu ya mwisho, ambayo waandishi wengine waliyaeleza kifupi tu, ili kuandika mafungu manne ya mafundisho juu ya elimu ya msingi wa Kikristo. Hapo vile vile mafundisho yalikuja moja kwa moja kutoka katika midomo ya Yesu (Yn 13:1-16:33). Jiji la Yerusalemu lilikuwa makao makuu ya upinzani wa Yesu, kwa hiyo mahojiano yake mengi na Wayahudi yalitokea huko. Yohana alitumia mahojiano mengi ya namna hiyo kwa mafundisho yake, kwa hiyo habari nyingi katika Injili yake zilitokea Yerusalemu (Yn 2:13; 5:1; 7:14,25; 8:20; 10:22-23; 11:1). Habari hii ni tofauti sana na Injili nyingine zinazohusika zaidi na Galilaya na kutaja Yerusalemu kwa kifupi tu, isipokuwa siku chache karibu na kusulibiwa kwake.