MAELEZO KUHUSU INJILI YA MARKO Mwandishi Sawa sawa na Injili nyingine tatu, mwandishi mwenyewe hakutajwa. Lakini tangu karne ya kwanza ilieleweka kila mahali kwamba mwandishi wake alikuwa Yohana Marko wa Yerusalemu, na Injili yake inaonyesha maelezo ya Petro kuhusu huduma ya Yesu. Marko alitokana na familia yenye heshima katika Ekklezia la kwanza jijini Yerusalemu. Wazazi wake walikuwa na nyumba kubwa nao waliweza kuajiri watumishi (Mdo 12:12-13), na angalau jamaa yake mmoja wa karibu, Barnaba, alikuwa na shamba la maana (Mdo 4:36-37; Kol 4:10). Kufuatana na mapokeo ya kale inaaminiwa kwamba, katika nyumba ya familia ya Marko Yesu alikula Pasaka ya mwisho pamoja na wanafunzi wake, na wanafunzi walikutana katika nyumba hiyo siku za kwanza za Ekklezia (Lk 22:11-13; Mdo 1:13). Huduma ya Marko katika Injili Labda habari za kwanza kuhusu Marko tunazipata katika habari za kijana aliyewafuata Yesu na marafiki zake katika bustani ya Gethsemane, lakini alikimbia maadui walipotaka kumkamata. Habari hizo zimeandikwa katika Injili ya Marko tu (Mk 14:51-52). Kufuatana na desturi ya kawaida, mwandishi aliweza kusimulia habari zake binafsi bila ya kutaja jina lake moja kwa moja (Yn 13:23; 2Kor 12:2). Kwa kuwa viongozi wa Ekklezia la kwanza walikutana katika nyumba ya familia ya Marko, Marko aliwajua Petro na viongozi wengine wa Wakristo wa wakati ule (Mdo 12:12-14). Paulo na Bamaba waliridhika naye hata wakamchukua kutoka Yerusalemu hadi Antiokia ya Shamu, na kutoka huko mpaka Kipro na Asia Ndogo katika safari yao ya kwanza ya kueneza Injili (Mdo 12:25; 13:1-5). Baada ya muda mfupi tu, Markb aliwaacha Paulo na Barnaba akarudi Yerusalemu (Mdo 13:13). Paulo alifikiri jambo hilo lilionyesha udhaifu katika tabia ya Marko, akakataa kumchukua katika safari yake ya pili. Paulo na Barnaba walipobishana juu ya jambo hilo na kuachana, Barnaba alimchukua Marko katika safari ya kutembelea Kipro tena (Mdo 15:36-41). Biblia haisemi neno kuhusu kazi ya Marko katika miaka kumi iliyofuata. Lakini habari nyingine za karne ya kwanza zinathibitisha kwamba kwa muda fulani alikuwa pamoja na Petro aliyeeneza Injili katika maeneo ya kaskazini mwa Asia Ndogo (siku hizi Uturuki kaskazini). Alishirikiana sana na Petro, hata Petro akamwita mwanawe (IPet 5:13). Baada ya muda, hao wawili walitembelea Rumi ambapo Petro alilisaidia Ekklezia kwa njia ya mafundisho yake kuhusu maisha na huduma ya Yesu. Petro alipoondoka Rumi, Marko alibaki huko, na kwa sababu ya shida za Wakristo wa huko aliandika habari za Yesu jinsi alivyokuwa amemsikia Petro akizisimulia. Matokeo yake ni Injili ya Marko. Paulo alipofika Rumi alimkuta Marko huko akamsifu katika barua yake kama mtu aliyeweza kuwasaidia Wakristo wachanga (Kol 4:10). Baada ya miaka kadhaa, Paulo alipongojea hukumu yake ya kifo, aliomba Marko awe pamoja naye katika siku zake za mwisho (2Tim 4:10). Alama maalumu katika Injili ya Marko Katika Injili ya Marko kuna alama nyingi zinazoonyesha makusudi na tabia ya Petro. Licha ya matukio yanayohusiana na kifo na ufufuo wa Yesu, habari nyingi zaidi za huduma yake zilizoelezwa katika Injili ya Marko zilitokea Galilaya, ambapo mji wa nyumbani kwa Petro, Kapernaumu, unaonekana kuwa makao ya Yesu kwa muda mwingi zaidi. Kwa kweli, makao yake hasa yaliweza kuwa katika nyumba ya Petro (Mk 1:21,29; 2:1; 9:33). Maelezo ya Marko yanaonyesha tabia ya harakati ya Petro, tunapoona haraka katika masimulizi kutoka tukio moja hadi lingine. Lugha yake kwa kawaida ni ya moja kwa moja kuliko ilivyo katika mifano ya Injili nyingine. Taarifa zake huwa fupi na moja kwa moja, na habari za kinaga naga zinaonekana dhahiri zaidi. Haya yanaonekana wazi zaidi katika masimulizi ya matendo na michomo ya moyo ya Yesu (Mk 1:41; 3:5; 4:38; 6:6; 10:14,16,21,32). Uhalisi wa Petro unaonekana pale ambapo udhaifu au makosa ya Petro yameonyeshwa kwa wazi zaidi kuliko katika Injili nyingine (Mk 9:5-6; 14:66-72, ambapo matukio ambayo yangeweza kumletea sifa hayakutajwa (taz.Mt 14: 16:17). Habari zote za Yesu zilitokea Palestina, kwa hiyo watu wa Mataifa walioishi Rumi walihitaji kuelezwa mambo kadhaa. Kwa sababu hiyo Marko alitafsiri maneno ya Kiebrania au ya Kiaramu katika Kiyunani (Mk 3:17; 5:41; 7:11,34; 15:22,34) na kueleza imani na desturi za Kiyahudi (Mk 7:3-4; 12:18,42; 14:12; 15:42). Adha ya Wakristo Wakati wa mwongo wa sita wa karne ya kwanza serikali ilizidisha adha dhidi ya Wakristo, na hasa baada ya Kaisari Nero kuwalaumu Wakristo kwamba eti wao waliwasha moto mkubwa jijini Rumi mwaka wa 64 b.K. Muda mfupi kabla ya hayo Petro alikuwa ameandika barua kutoka Rumi (akiliita jiji hilo kwa jina la fumbo 'Babeli'; IPet 5:13). Katika barua hiyo aliwaonya Wakristo wa kaskazini mwa Asia Ndogo kwamba, ingawa walikwisha udhiwa, wangekabiliwa na mabaya zaidi. Aliwatia moyo wavumilie adha yao kama jambo la kuimarisha imani yao, na hivyo watazamie wakati wa ushindi mkubwa (IPet 1:6; 2:20-23; 3:14-17; 4:12-16). Muda mfupi baada ya hayo, Petro mwenyewe aliuawa na Warumi (2Pet 1:14; taz.Yn 21:18-19). Injili ya Marko, sawa sawa na waraka wa kwanza wa Petro, iliandikwa katika mwanzo wa wakati ule wa kuongezeka adha. Iliwakumbusha Wakristo wa Rumi (kutokana na uzoefu wa Petro kuhusu maisha na mafundisho ya Yesu) kwamba wangehitaji nguvu na uthabiti kwa kuvumilia kueleweka vibaya, kulaumiwa kwa uongo, kuudhiwa au hata kusalitiwa (Mk 3:21,30; 4:17; 8:34-38; 10:30; 13:9,13; 14:41,71-72; 15:15,19,32). Jinsi Marko alivyomwona Yesu Injili ya Marko inasimulia matendo zaidi kuliko Injili nyingine, lakini mafundisho ya Yesu yamepungua. Kusudi la msingi la mafunsisho yake linadokezwa katika mstari wa kwanza wa Injili, yaani kuonyesha kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu (Mk 1:1). Katika ubatizo wa Yesu katika mwanzo wa huduma yake ya hadharani, tangazo la Mungu kuhusu Yesu lilionyesha mambo maalumu ya huduma yake ya pekee. Tangazo hilo liliunganisha madondoo ya Agano la Kale kuhusu Masihi wa mbari ya Daudi na Mtumishi wa Mungu, likionyesha kwamba njia ya Yesu kuelekea utukufu wa ufalme ingekuwa njia ya Mtumishi ateswaye (Mk 1:11; taz.Zab 2:7; Isa 42:1). Yesu alikuwa Mwana wa Adamu wa mbinguni aliyeahidiwa na Mungu ufalme wa ulimwengu wote udumuo hata milele. Lakini angepokea ufalme huo kwa njia ya mateso ya msalabani tu Mk 8:29-31,38; 10:45; 14:62; taz.Dan 7:13-14). Tunavyoweza kutazamia, kifo cha Yesu ni kilele cha Injili ya Marko, lakini Marko anataka kuonyesha kwamba ushuhuda wa Yesu ulisababisha kifo chake. Marko peke yake anasimulia kwamba, wakuu wa Sanhedrin walipomwuliza Yesu kama alikuwa ndiye Masihi, Mwana wa Mungu, Yesu alijibu wazi, 'Mimi ndiye'. Kisha Yesu alipanua jibu lake ili kuonyesha kwamba alikuwa Masihi, Mwana wa Mungu na pia Mwana wa Adamu wa mbinguni, naye alikuwa njiani kuelekea utukufu wake wa ufalme mbinguni (Mk 14:61-64). Katika Injili yake yote Marko anatia mkazo katika ukweli wa lazima kwamba Yesu alikuwa ndiye Mwana wa Mungu. Wanafunzi wake walitambua jambo hilo (Mk 8:29), na Baba yake wa mbinguni alilithibitisha siku ya kubadilika sura yake (Mk 9:7). Yesu mwenyewe alisema jambo hilo wazi mbele ya wanafunzi wake na mbele ya maadui zake (Mk 13:32; 14:61-62), na hata akida wa jeshi la Kirumi alilazimika kukiri habari hiyo (Mk 15:39).