UNABIIWA HAGAI Maonyo ya Hagai na matokeo yake (1:1-15) Wayahudi walitumia upinzani wa nje na hali ngumu ya maisha yao kwa kujitetea kwamba hawakuendelea kujenga hekalu lao upya. Walidai kwamba wakati wa kuanza kazi haujawadia (1:1-2). Lakini waliweza kujenga nyumba zao binafsi. Kwa kweli, walikuwa wametumia mbao nyingi zilizokuwepo kwa kupamba nyumba zao, ingawa mbao hizo zilipatikana kwa shida nazo zilitakiwa kwa hekalu (3-4). Kwa sababu ya ubinafsi wao, Mungu alikuwa amewaadhibu kwa njaa na umaskini (5-6). Watu walilalamika kwamba hawakuweza kujenga hekalu, kwa sababu walikuwa maskini. Nabii alijibu kwamba walikuwa maskini kwa sababu hawakutaka kujenga hekalu. Walikuwa na ubinafsi walipofikiri mahitaji yao tu, wala hawakufikiri mahitaji ya kazi ya Mungu. Kwa hiyo waliambiwa waende msituni na kupasua mbao kwa ajili ya kujenga hekalu (7-11). Mahubiri ya Hagai ya moja kwa moja yalileta matokeo mazuri kwa muda mfupi. Watu walitambua ukweli wa mashtaka yake wakaitikia wito wake, na baada ya muda wa majuma matatu tu walianza kazi ya hekalu tena. Walipomtii na kumcha BWANA, Yeye aliwaahidi kuwa pamoja nao (12-15). Ujumbe wa kutia moyo (2:1-9) Ingawa msingi wa hekalu ulikuwa umewekwa kabla ya miaka 16, bila shaka uliharibika kidogo tena wakati ule wote wa kuachwa ukiwa. Kazi nyingi zilitakiwa kabla ya kuanza ujenzi wa nyumba yenyewe. Baada ya kazi ya mwezi mmoja, watu waliweza kuona vya kutosha juu ya msingi uliorekebishwa, ili wapate ramani iliyowaonyesha ukubwa wa hekalu jipya. Baadhi ya wazee sana waliokumbuka ukuu na utukufu wa hekalu la Sulemani, labda walisema kwamba hekalu hili jipya halikupendeza likilinganishwa na lile la kwanza. Hagai aliona kwamba maneno hayo yangewakatisha wajenzi tamaa, kwa hiyo aliwaletea ujumbe wa kuwatia moyo (2:1-3). Akiwa msemaji wa Mungu, Hagai aliwapa uhakika wa Mungu kwamba, Yeye alikuwa pamoja nao kama vile alivyokuwa pamoja na watu wake hapo zamani alipowatoa Misri (4-5). Kama vile Mungu alivyotetemesha nchi wakati alipotoa sheria ya Musa katika Mlima Sinai, ndivyo kwa njia ya hekalu hilo 'angetikisa' mbingu na nchi katika maana kubwa zaidi. Kwa njia ya kujenga hekalu hilo, Mungu alikuwa akijenga upya sehemu kuu ya dini ya taifa la Uyahudi, kwa sababu kutoka taifa hilo Masihi wake angetokea. Hekalu la Israeli lingepewa utukufu na heshima zaidi kuliko wajenzi waliokata tamaa walivyoweza kuhisi. Mungu ambaye mali yote ya ulimwengu ni yake, angewasababisha watawala wa mataifa mengine walete hazina zao za dhahabu na fedha ili kupamba nyumba hiyo (6-8; taz.Ezra 6:8-12). Lakini utukufu mkubwa zaidi ungekuja kwa njia ya umati wa watu wa mataifa mengi ambao wangejiunga na Waisraeli katika hekalu halisi. Makao ya kweli ya Masihi yangekuwa miongoni mwa watu waliookolewa katika hekalu hai ambalo Yeye angelijenga ulimwenguni kwa utukufu. Hali ngumu ya muda ya wajenzi wa Kiyahudi ingeonekana kuwa si kitu ikilinganishwa na mafanikio na ukuu wa siku hiyo (9). Ahadi za baraka (2:10-19) Baada ya kupita miezi mitatu, kazi yote ya msingi ilikwisha (taz.l: 14-15; 2:18). Zekaria alikuwa amefaulu kuwahamasisha watu watubu (Zek 1:1-6), na wakati huo Hagai alitia mkazo tena kwamba, kusafishwa kiroho namna hiyo kulikuwa njia ya pekee ya kufurahia baraka za Mungu (10). Hagai aliwakumbusha watu kwamba tabia yao mbaya ya wakati uliopita ilikuwa sababu ya matatizo yao yote. Alitoa mfano wa kuonyesha kwamba, mtu akijishirikisha na vitu vichafu, vitu vile vinamfanya kuwa najisi, lakini akijishirikisha na vitu vitakatifu, vitu vile vinamfanya kuwa mtakatifu. Wakati wote walipokuwa wamedharau hekalu na kuliacha kama magofu au kama 'kitu kilichokufa' katikati yao, walikuwa najisi, na hivyo hawakuweza kukubaliwa na Mungu. Juhudi zao zote za kidini hazikuwafanya kuwa watakatifu, haidhuru kiasi gani walivyojishirikisha na vitu vitakatifu (11-14). Ubinafsi na uasi wa watu uliwaletea hukumu ya Mungu kwa njia ya kuharibiwa mavuno yao na upungufu wa chakula. Wakati huo walipoacha njia zao za ubinafsi na kumtii Mungu kwa njia ya kufanya kazi yake, wanahakikishiwa kwamba Yeye angebadili hali ile mbaya ya kilimo na kuwabariki kwa mavuno mazuri tena (15-17). Ahadi yake ya baraka ingeanza kutimizwa kuanzia siku ile ile, yaani siku ile walipohakikisha kwamba utii wao ulikuwa wa kweli, kwa sababu wakati huo walikuwa wamemaliza kazi za maandalizi katika msingi wa hekalu. Walikuwa wamethibitisha utii wao kwa matendo (18-19). Ujumbe wa binafsi kwa Zerubabeli (2:20-23) Halafu katika siku ile ile, Hagai alitoa ujumbe mwingine wa kutia moyo. Wakati huo ulikuwa ujumbe wa binafsi kwa mtawala mkuu, Zerubabeli (20). Zerubabeli alikuwa mzao wa Daudi wa mbari ya wafalme waliokuwa wametawala Yerusalemu, naye angalikuwa na haki ya kurithi kiti cha enzi cha Israeli (Mt 1:6-12). Lakini kwa kuwa taifa la Israeli lilikuwa bado chini ya utawala mkuu wa Uajemi, aliruhusiwa kuwa liwali tu. Ingawa mambo hayo yote yalikuwa na vizuio hivyo, Hagai alimtia Zerubabeli moyo, akimhakikishia kwamba, hata hivyo alikuwa mjumbe mteule wa Mungu. Kwa njia yake yeye, licha ya kujenga upya taifa lake la Israeli, Mungu pia angepindua mataifa yote na kujenga ufalme wake katika ulimwengu wote. Kwa kweli, Zerubabeli hakuishi ili aweze kuona ukamilifu wa matimizo ya maneno ya Hagai, lakini ahadi ilikwenda mbali kwa mzao mkuu wa Zerubabeli, yaani kwa Yesu aliye Masihi, ambaye katika Yeye unabii huo ungepata utimilifu wa maana yake (21-23; taz.Mt 1:12-16).