Kitabu cha Nabii Hagai MAZINGIRA Hagai na Zekaria walifanya kazi pamoja jijini Yerusalemu baada ya Wayahudi kurudi kutoka kifungo cha Babeli. Kabla ya miaka 200 ufalme wa kaskazini, yaani Israeli ulishindwa na Waashuri na watu wake walipelekwa kifungoni katika nchi za kigeni (mwaka wa 722 k.K.; 2Fal 17:1-6). Baada ya muda watu wa ufalme wa kusini, yaani Yuda walipata shida hiyo hiyo waliposhindwa na kupelekwa kifungoni Babeli (miaka ya 605-587 k.K.; 2Fal 24:1-25:12). Watu wengi zaidi wa ufalme wa kaskazini walichangamana na mataifa walipoishi wakapotewa na ufahamu wa utaifa wao. Lakini sivyo watu wa ufalme wa kusini. Wao walihifadhi ufahamu wa utaifa wao, na hao ndio waliorudi na kujenga taifa la Israeli ya kale upya. Ingawa matengano baina ya watu wa kaskazini na wale wa kusini hayakuendelea, wengi wao waliorudi walikuwa watu wa ufalme wa kusini wa zamani, yaani wa Yuda. Zamani waliitwa Wayuda, lakini baadaye waliitwa Wayahudi, na jina hilo liliendelea kuwa jina la Waisraeli wote. Matukio yaliyowawezesha Wayahudi warudi katika nchi yao yalitokea mwaka wa 539 k.K. Waajemi walipowashinda Wababeli. Mfalme mpya wa Uajemi, Koreshi, alipotoa ruhusa kwa wafungwa warudi katika nchi zao, kundi kubwa la Wayahudi lilirudi Yemsalemu. Ingawa Wayahudi wale walikuwa chini ya utawala mkuu wa Uajemi, waliruhusiwa kuwa na utawala wao Yerusalemu. Viongozi wao wa kwanza walikuwa mtawala wa kiraia, Zerubabeli, na kuhani mkuu, Yoshua (au Yeshua). Hao wawili bado walitawala Hagai na Zekaria walipoanza huduma zao (Ezra 2:1-2; 5:1-2). Mahubiri ya Hagai na Zekaria Muda mfupi baada ya kufika Yerusalemu, Wayahudi walionyesha hamu yao ya kujenga hekalu upya katika Mlima Sayuni. Walijenga madhabahu ya kutolea sadaka, na katika mwaka wa pili walianza kuweka msingi wa hekalu (Ezra 3:1-3,8-10). Lakini watu wengine walioishi huko waliwapinga wajenzi, na matokeo yake, kazi ya ujenzi ilisimamishwa (Ezra 4:1-5,24). Kwa muda wa miaka 16 hivi kazi ya ujenzi katika hekalu ililala. Kwa sababu ya shida hiyo, Mungu aliwaita manabii Hagai na Zekaria ili wafanye kazi yao miongoni mwa watu wake. Walianza kuhubiri mwaka wa 520 k.K.. Kazi yao ilikuwa kuwaamsha watu na kuwatia moyo ili waendelee na kazi yao wala wasiiache tena kabla ya kuimaliza (Ezra 5:1-2; Hag 1:1; Zek 1:1). Watu walijitetea wakisema kwamba upinzani kutoka maadui wa eneo lao na ugumu wa wakati wa njaa kuwa ndiyo sababu za kutojenga. Manabii waliona kwamba mambo hayo hayakuwa sababu zake. Sababu hasa zilitokana na watu wenyewe. Hawakuwa tayari kufanya kazi kwa ajili ya Mungu, ingawa walifanya bidii sana kwa ajili ya kazi zao binafsi. Tatizo lenyewe lilikuwa la kiroho, wala si la kisiasa au shida ya kutokuwa na mali yo yote (Hag 1:2-4,9-10). Maneno hayo ya manabii yalithibitishwa kuwa kweli baada ya muda mfupi, kwa sababu watu walipoanza kazi ya hekalu tena, na upinzani ulipoanza upya, mfalme wa Uajemi aliwatia Wayahudi moyo. Aliandika hata amri rasmi ya pili ili kuthibitisha ile ya kwanza ya mfalme wa awali, yaani ya Koreshi, naye alitoa msaada wa pesa ili kuhakikisha kwamba kazi ikamilishwe vizuri (Ezra 5:3; 6:6-12). Mahubiri ya kwanza ya Hagai na Zekaria yaliwahamasisha Wayahudi kuanza kazi tena nayo yaliwatia moyo kuvumilia matatizo ya mwanzo yaliyochukua muda wa karibu miezi sita. Biblia yetu ina hotuba nne za ujumbe kutoka kwa Hagai na mbili kutoka kwa Zekaria zilizotolewa wakati huo. Baada ya miaka miwili Zekaria alitoa ujumbe wa tatu. Hotuba nyingine mbili za Zekaria zinaonekana kama zilitolewa baada ya kupita muda mrefu katika maisha ya nabii. Alama maalumu za vitabu vile viwili Mahubiri ya Hagai yalikuwa ya moja kwa moja nayo yalieleweka kwa urahisi, lakini yale ya Zekaria yana maono mbalimbali na ujumbe wa namna ya hadithi aliyopewa na Mungu. Matokeo yake, mahubiri yake yaliibua mawazo na maswali mengi kwa wasikilizaji wake. Aina ile ya mahubiri au ya maandiko ilijulikana kuwa ya wakati wa mwisho kabisa wa historia ya ulimwengu (au ya apocalyptic. Kuhusu alama za maandiko ya apocalyptic, taz. maelezo ya mazingira ya kitabu cha Danieli.) Hagai alishughulika zaidi na kuwaamsha watu watoke katika uvivu wao na kuwahamasisha waanze kazi yao ya kujenga hekalu upya. Zekaria alimsaidia Hagai katika huduma hiyo muhimu, lakini baadaye aliendelea na kutoa mafundisho mengine. Alitaka kuona mabadiliko ya kiroho yadumuyo katika maisha na makusudi ya watu, ili waweze kumtumikia Mungu vizuri zaidi wakati ujao. Kwa njia ya Zekaria Mungu aliwaandaa watu wake kwa kazi yao aliyowachagulia. Makusudi hayo yangepata utimilifu wake katika kuja kwake Masihi, kwa kuimarisha ufalme wake na wokovu wa watu ulimwenguni kote. Nusu ya pili ya kitabu cha Zekaria (yaani hotuba au matangazo ambayo labda yalitolewa muda wa baadaye katika maisha ya nabii) inaonyesha kwamba kazi hiyo isingekuwa rahisi. Yangetokea matatizo makubwa na nguvu na uwezo wa Mwovu, lakini mwisho ufalme wa Mungu ungeshinda. Muhtasari wa ujumbe na matukio mbalimbali Utaratibu wa ujumbe na matukio yaliyoelezwa katika vitabu vya manabii Hagai na Zekaria. k.K. Mwezi siku ujumbe/tukio kifungu 521 Dario kuwa mfalme 520 6 1 Ujumbe wa 1 wa Hag. Hag 1:1-11 6 24 Kuanzishwa hekalu Hag 1:12-15 7 21 Ujumbe wa 2 wa Hag. Hag 2:1-9 8 Ujumbe wa 1 wa Zek. Zek 1:1-6 9 24 Ujumbe wa 3 wa Hag. Hag 2:10-19 9 24 Ujumbe wa 4 wa Hag. Hag 2:20-23 11 24 Ujumbe wa 2 wa Zek. Zek 1:7-6:15 518 9 4 Ujumbe wa 3 wa Zek. Zek 7:1-8:23 516 12 3 Kumalizika hekalu Ezr 6:14-15 baada ya miaka Maono ya 1 ya Zek. Zek 9:1-11:17 ktk. uzee wake Maono ya 2 ya Zek. Zek 12:114:21