3:9-20 WOKOVU KWA WATU WATUBUO Baada ya kuangamizwa wenye dhambi wote, wanyenyekevu walioacha dhambi zao (taz.2:l-3), watafurahia maisha mapya yenye amani na baraka. Katikati ya hukumu kuna huruma kwa watu watubuo. Wenye dhambi waliosafishwa kutoka mataifa yote watamwabudu na kumtumikia Mungu kwa mioyo safi (9-10). Dhambi za uasi, kiburi, udanganyifu na kutokuwa na uaminifu ambazo ni alama za wenyeji wa Yerusalemu wa siku za Sefania, zitaondolewa kutoka jumuia ya watu wa Mungu (11-13). Ingawa watu wa Mungu walipata huzuni kwa sababu ya adhabu yake juu yao, wakati huo huzuni zao zitabadilishwa kuwa furaha. Wataishi pamoja na Mungu aliye mfalme wao bila hofu ya hukumu tena (14-15). Wakitazamia ahadi hizo kwa wakati ujao, wasiwe wavivu wala wasikate tamaa, bali wachangamke na kuwa na matumaini. Kushindwa kwao kutabadilika kuwa ushindi. Mungu ataondoa aibu yao, na upendo wake utawapa uzima mpya (16-18). Wafungwa watakusanywa kutoka nchi za vifungo vyao, wakajengwa upya katika nchi yao wenyewe. Chini ya utawala wa Mungu watashirikiana naye wakipokea sifa kutoka kwa watu wote duniani (19-20).