Kitabu cha Nabii Sefania MAZINGIRA Kutokana na ujuzi tunaopata katika maandiko ya Biblia, inaonekana kama Sefania alikuwa nabii wa kwanza katika Yuda baada ya Isaya na Mika kumaliza huduma zao kabla ya miaka sabini. Mahubiri yake yalionyesha mwanzo wa wakati mpya wa kazi ya manabii katika Yuda, lakini pia ulikuwa wakati wa kubomolewa kwa Yerusalemu na mwisho wa ufalme wa Yuda. Nabii jijini Yerusalemu Katika muda mrefu wa miaka sabini kabla ya Sefania, mfalme wa Yuda alikuwa mfalme mwovu Manase. Wakati wa miaka yake 55 katika kiti cha enzi cha Yuda Manase aliwarudisha Waisraeli katika hali ya kiroho iliyokuwa mbaya kuliko ya Wakanaani walioangamizwa nao. Ukatili, mauaji na desturi za dini za kigeni vilikuwa alama kuu za utawala wake navyo viliharibu Yuda vibaya kiasi kwamba uharibifu wake haukuweza kurekebishwa tena na mfalme awaye yote aliyetawala baada yake, na matokeo yake yalikuwa uangamizi wa Yuda (2Fal 21:1-18; 23:26-27). Mwanawe Manase, Amoni, alifuata mfano wa siasa ya baba yake, lakini baada ya utawala mfupi wa miaka miwili tu aliuawa. Wakati huo watu walichoka na ukatili ulioendelea na mauaji yake, na hivyo waliwaua wauaji wa Amoni wakamweka mwanawe Yosia mwenye umri wa miaka minane tu juu ya kiti cha enzi (640 k.K.). Kwa njia hii madaraka ya utawala yalikuwa juu ya washauri wa mfalme, ambao wakati huo waliweza kujenga siasa ya taifa yenye amani na haki (2Fal 21:19-22:2). Yosia alipopata umri wa miaka 20, aliamua siasa yake mwenyewe naye alikuwa ameanza marekebisho ya dini yaliyodumu muda mrefu (2Nya 34:3-4). (Kwa habari zaidi ya marekebisho yake, taz.2Fal 22:3-23:25 na 2Nya 34:1-35:27). Inawezekana kwamba huduma ya nabii Sefania ilimhamasisha mfalme kuingiza marekebisho yake. Sefania alikuwa kijana ambaye labda hakumzidi sana mfalme kwa umri, naye pia alikuwa jamaa yake (wote wawili walikuwa wazao wa Hezekia; taz.l:l; 2Fal 20:21; 21:18,24). Sefania aliishi Yerusalemu alipoona na kulaumu maovu yale yale ambayo Isaya na Mika waliyalaumu kama miaka 100 iliyopita. Mahubiri yake bila shaka yaliwasababisha watu wengi wabadili maisha yao na kumsaidia Yosia katika marekebisho yake. Pia inawezekana kwamba alisaidia kuanzisha huduma mpya ya unabii katika Yuda. Manabii wengine wa wakati wa Sefania walikuwa Yeremia, Nahumu na Habakuki, na baada yao na baada ya kubomolewa kwa Yerusalemu walifuata Obadia na Ezekieli. MUHTASARI 1:1-3:8 Adhabu ya wenye dhambi 3:9-20 Wokovu kwa watu watubuo