3:1-19 HABAKUKI ANATEGEMEA HUKUMU YA MUNGU Zaburi ya fungu la tatu haina uhusiano wa moja kwa moja na Yuda na Babeli. Hata hivyo inahusika na maneno ambayo Habakuki aliyaandika sasa hivi, ikieleza kwamba Mungu anatokea katika kazi yake ya kuhukumu mataifa na kuwaokoa watu wake, Zaburi inaanza kwa maneno yanayoonekana kama jina la sauti iliyofaa kuimbiwa kwa wimbo huo (3:1). Habakuki anakumbusha matendo makuu ya Mungu aliyowatendea watu wake awali, naye anamwomba Mungu aendelee kushughulika kwa niaba yao tena. Lakini anajua kwamba, ghadhabu ya Mungu ikichokozwa dhidi ya wenye dhambi, maadui wa Israeli labda ha watakuwa watu wa pekee wa kupata shida. Watu wa Mungu pia wana dhambi, kwa hiyo nabii anaomba awahurumie atakaposhughulika nao (2). Hukumu ya Mungu inaonyeshwa katika mifano mbalimbali, na baadhi yake inaonekana kama imetolewa katika habari za kuokolewa kwa Waisraeli kutoka Misri na safari yao ya kwenda Kanaani wakiwa chini ya uongozi wa Musa. Inafanana na upepo mkali wa umeme wa radi unaoonekana ukikaribia katika vilele vya milima ya kusini (3-4); kama vile tauni ambayo hakuna mtu awezaye kuepuka nayo (5); kama tetemeko la nchi linalotisha mataifa na kutikisa milima (6); kama upepo mkali wa jangwani unaong'oa na kuangusha mahema ya Waarabu (7); kama mapinduzi ya maadui katika vita, ikiwa ni kwa njia ya majeshi au kwa njia ya nguvu za asili ya ulimwengu (8-9); kama mafuriko ya maji yanayochukua kila kitu (10); kama kupatwa jua na giza linalofunika nchi (11); kama ushindi wa mashujaa wa vita wanaowaua maadui na kuwaokoa watu wao 12-15). Nabii anatetemeka anapozingatia hukumu hiyo kali. Matumaini yake ya pekee ni kutegemea uangalifu wa haki na neema ya Mungu (16). Mashamba na mifugo vinaweza kuangamizwa, lakini yeye anaendelea kumtegemea Mungu. Nabii anatulia katika ujuzi kwamba, Mungu wa hekima na mamlaka visivyo na kikomo, anajua anachofanya, na mapenzi yake yana ukamilifu. Imani kubwa namna hiyo ndiyo jibu la maswali, mashaka na malalamiko aliyoyaonyesha awali (17-19).