Kitabu cha Nabii Habakuki MAZINGIRA Ingawa Habakuki hakutaja wafalme wa Yuda wa wakati wake, ujumbe wa kitabu chake unadokeza wakati wa kutabiri kwake. Alitangaza ujumbe wake wakati wa miaka ya mwisho wa ufalme wa Yuda Babeli ilipoinuka kuwa ufalme mkuu wa ulimwengu, nao ulitishia kuteka Yuda. Nabii na Wababeli Baada ya kuteka Uashuru mwaka wa 612 k.K., Wababeli walipata mamlaka makuu katika maeneo ya Mesopotamia na Palestina. Halafu mwaka wa 605 k.K. walishinda Misri sehemu za Karkemishi katika Mto Frati (taz. ramani katika maelezo ya Nahumu). Hapo awali Wamisri waliteka Yuda, na hivyo baada ya kushindwa, Wababeli walipata utawala juu ya Yuda(2Fal 23:33-35; 24:7; Dan 1:1-4). Wayuda walipowaasi Wababeli, majeshi yao yaliteka Yerusalemu, wakawachukua wenyeji wengi wa hali ya juu katika kifungo cha Babeli, wakamweka mfalme mpya juu ya wale waliobaki jijini (mwaka wa 597 k.K.; 2Fal 24:10-17). Baada ya miaka michache, mfalme mpya alipowaasi vile vile, Wababeli hawakuvumilia zaidi. Walibomoa Yerusalemu na kupeleka wenyeji wengi zaidi waliobaki katika kifungo cha Babeli. Huo ulikuwa mwisho wa ufalme wa Yuda (587 k.K.; 2Fal 25: 1-12). Nabii Habakuki aliishi wakati wa kwanza Wababeli walipoimarisha utawala wao juu ya Yuda. Kitabu chake kinaeleza jinsi alivyojadiliana na Mungu baada ya kupata habari kwamba Mungu alikuwa akiwaandaa Wababeli kuwa chombo chake cha kuadhibu Yuda. Habakuki alihangaika, labda alikasirika, kwa sababu alijua kwamba Wababeli walikuwa wenye dhambi waovu kuliko Wayuda. Mungu alimhakikishia Habakuki kwamba, watu wo wote wa Yuda ambao wangeendelea kuwa waaminifu kwake hawangekuwa na haja ya kuogopa. Ingawa taifa la Yuda kwa ujumla lingeangamizwa, waaminifu wangefurahia baraka yake. Mungu alikuwa na ujumbe kwa Wababeli vile vile. Hawakuwa na sababu ya kujivuna. Walionyesha kiburi kisichovumilika walipowashinda watu wa Mungu, kwa hiyo wao pia wangeadhibiwa katika hukumu ya Mungu. Imani ya Habakuki iliimarishwa alipoongea na Mungu. Labda hakupata maelezo ya kinaganaga aliyoyatazamia kwa Mungu, lakini alipata ufunuo wa mamlaka na hekima ya Mungu, na hivyo alipata ufahamu zaidi wa Mungu, naye aliamua kuendelea na uaminifu wake. MUHTASARI 1:1-2:5 Habakuki analalamika, na Mungu anamjibu 2:6-20 Dhambi za Wababeli 3:1-19 Habakuki anategemea hukumu ya Mungu