2:1-3:19 KUBOMOLEWA KWA NINAWI Kubomolewa kwa sababu ya ukatili (2:1-13) Mafungu ya pili na tatu yana mashairi mawili yenye maana moja, yaani kubomolewa kwa Ninawi na sababu zake. Nahumu anaanza kuchora maelezo yake ya mashambulio dhidi ya Ninawi akiwaita walinzi wa ukuta wa mji, ili wawaonye wenyeji kwamba maadui wanakaribia. Wakati huo Mungu atawaangamiza watu wale walioangamiza Israeli na kunyanyasa Yuda (2:1-2). Nabii anatoa mfano wa askari waliovaa nguo za rangi ya kung'aa, magari ya vita yanayong'aa na farasi wanaocheza cheza, majeshi ya adui yanapokaribia ukuta wa mji. Maafisa wanaoongoza mashambulio wanatamani kupiga vita, hata wanajikwaa katika haraka yao (3-5). Askari wa adui wanavunja lango la kuzuia maji, wakifurisha maji katika mji na kuwahangaisha wenyeji wake. Baadhi ya askari wanamkamata malkia na masuria wa mfalme ambapo wengine wanateka nyara mjini (6-9). Waninawi walikuwa wakatili mno katika kuwaonea watu wa mataifa mengine, hata wanafananishwa na simba wanaoshambulia wanyama wasioweza kujitetea na kuwaburuta katika makao yao. Wakati huo simba wale wamekufa na makao yao yamekuwa ukiwa na tupu. Waninawi wachache wanaosalia wanatazama mji wao uliobomolewa wakitishwa sana na vitisho vyake (10-13). Kubomolewa kwa sababu ya uchoyo (3:1-19) Waashuri hawakuwa wakatili tu, bali pia walikuwa na uchoyo na tamaa. Mara nyingi waliteka mataifa mengine kwa ajili ya kuteka nyara tu. Kama vile kahaba, walitamani pesa na kujifurahisha tu, pasipo wazo lo lote kuhusu maadili mema. Nahumu anatoa mfano mwingine wa vita mjini Ninawi ambapo Mungu anachukua hatua kali ya hukumu dhidi ya watu wenye hatia (3:1-4). Kama vile kahaba, wenyeji wa Ninawi walijipamba kwa nguo za kuvutia na kuishi katika fahari na anasa, wakijaribu kuwadanganya wengine. Fahari yao itabadilishwa kuwa aibu. Mji wote utafanana na kahaba aliyeaibishwa kwa kuvuliwa nguo zake na kulazimishwa atembee uchi mitaani. Watu wale waliodanganywa na kuibiwa na Waninawi, wakati huo watawacheka (5-7). Nahumu anawakumbusha Waninawi mambo yaliyotokea katika mji wa No-amoni (au Thebes) wa Misri. Ulilindwa na boma bora nao ulikuwa na marafiki wenye nguvu, lakini ulitekwa, na watu wake walipelekwa kifungoni (8-10). Mambo yale yale yatatokea Ninawi. Ngome zake imara za nje ya mji zitabomolewa kwa urahisi kama vile tini mbivu zinavyotikiswa na kuangushwa kutoka katika miti yake. Askari wakaao mjini wakisikia habari hizo watakata tamaa, na mji utatekwa kwa urahisi na maadui (11-13). Wanaweza kuweka akiba ya maji kwa wakati wa kuzingirwa na maadui na kuimarisha kuta za mji ili kuwazuia maadui na vyombo vyao vya kubomolea, lakini mambo hayo hayatawaokoa. Mji wote utateketezwa kwa moto nao utaachwa ukiwa kama shamba lililoliwa na nzige (14-15a). Wafanya biashara, maafisa na wengine waliohusika na biashara ya Ninawi wanafananishwa na kundi la nzige. Lakini kama vile nzige wanavyoruka na kuondoka wakati wa jua kali, ndivyo hata wale watakavyotoroka wakati wa kushambuliwa Ninawi (15b-17). Viongozi wa Uashuru watauawa, wakiwaacha raia zao bila uongozi katika shida na kuwa mateka ya urahisi kwa washambulizi. Uashuru utaanguka wala hautainuka tena. Watu wale walioteswa na Waashuri wakati huo watafurahi (18-19).