Kitabu cha Nabii Nahumu MAZINGIRA Sehemu kubwa ya kitabu kifupi cha Nahumu inahusu hukumu ya Mungu juu ya Uashuru, na hasa kubomolewa kwa mji wake mkuu Ninawi. Waashuri walikuwa maadui wakatili wa Israeli na Yuda, lakini Nahumu aliona siku ya hukumu yao ikikaribia. Unyanyasi wa Waashuri Uashuru uliinuka kupata mamlaka makubwa katika ulimwengu wakati wa karne ya nane k.K., iliyokuwa zaidi ya karne moja kabla ya wakati wa Nahumu. Kuanzia katika makao yake makuu ya Mesopotamia uliimarisha ufalme ulioenea haraka katika mataifa yaliyokuwa katika maeneo ya Palestina. Mwaka wa 732 k.K. Waashuri waliteka Shamu, na mwaka wa 722 k.K. waliteka Israeli (yaani sehemu ya kaskazini katika ufalme uliogawanyika) na kuwapeleka wenyeji wake kifungoni (2Fal 15:29; 16:9; 17:3-6). Baada ya kuanguka kwa Israeli, ufalme wa kusini ulikuwa wazi kwa mashambulio ya Waashuri, na katika miaka mia iliyofuata, ufalme huo wa Yuda ulikuwa na shida ya kutetea uhuru wake dhidi ya Waashuri. Mara nyingine Yuda ilikuwa chini ya mamlaka ya Waashuri ikapaswa kuwalipa kodi nyingi, mara nyingine iliweza kuwaasi na kujipatia uhuru wake tena, lakini wakati wote kulikuwa na hali ya uadui mkali, au hata hali ya vita baina ya mataifa hayo (2Fal 16:7-20; 18:7-19:37; 2Nya 28:16,20,21; 30:6; 33:11). Wakati wa mfalme Yosia, aliyeanza utawala wake juu ya Yuda mwaka wa 640 k.K., Waashuri walikuwa dhaifu, na hali hiyo ilimwezesha Yosia kutekeleza marekebisho mengi ya kidini na kisiasa yaliyohitajika sana, bila ya kuingiliwa na Waashuri. Wakati wa enzi yake kulikuwa na uamsho wa kazi ya manabii katika Yuda, yaani wakati wake manabii Sefania, Yeremia, Nahumu na Habakuki walianza kazi yao. (Kwa habari za maana kuu ya marekebisho ya Yosia na uhusiano wake na kazi za manabii wale, taz. maelezo yanayotangulia kitabu cha Sefania.) Nguvu za Waashuri zilipopungua na Wababeli walipozidi kupata nguvu na mamlaka, Nahumu alitabiri mambo ambayo Wayuda waliyatazamia kwa muda wa miaka 100 hivi, yaani mwisho wa mamlaka ya Waashuri. Matangazo yake ya hukumu yalihusika zaidi na kubomolewa kwa mji mkuu wa Uashuru, Ninawi. Nahumu alieleza kupinduliwa kwake kwa mifano hai na kwa kuguswa mwenyewe, akifurahi kwamba mwisho hukumu ya Mungu ya kufaa ingekuwa juu ya taifa hilo lenye ukatili na ujeuri wake uliolifanya kuwa taifa la kishenzi kabisa katika historia yote ya wanadamu. Mwaka wa 612 k.K. mji wa Ninawi ulitekwa na majeshi ya Wababeli, kama Nahumu alivyokuwa ametabiri. MUHTASARI 1:1-15 Mamlaka ya Mungu 2:1-3:19 Kubomolewa kwa Ninawi