6:1-7:20 MUNGU ANASHTAKI NA WATU WANAITIKIA Mambo ambayo Mungu anayapenda (6:1-16) Mika akirudi tena katika siku zake, anatoa mfano wa mahakamani ambapo, mbingu na dunia zikiwa mashahidi, Mungu anawashtaki watu wake kuwa wameasi uaminifu wake (6:1-2). Mungu anakumbusha mambo makuu aliyoyafanya kwa ajili yao, kana kwamba anawauliza sababu ya kuitikia upendo wake kwa matendo mabaya namna hiyo (3-5). Jibu la watu linaonyesha jinsi walivyoelewa swali la Mungu vibaya. Wanauliza ni aina gani ya ibada anayotaka Mungu: Je, anataka sadaka zilizo sawa sawa na maagizo ya maneno ya sheria? Au anataka nyongeza ya idadi ya sadaka? Au sadaka ziwe bora zaidi? Au anataka sadaka za kipagani? Mungu awaambie tu anachotaka, nao wangejaribu kumpendeza (6-7). Mungu anawajibu kwamba amekwisha waonyesha (kwa njia ya Amosi, Hosea na Isaya, na kwa sheria yote) anachotaka, yaani haki na upendo kwa watu wenzao, na uaminifu na unyenyekevu kwa Mungu. Sadaka sahihi na bidii ya matendo ya dini havina maana wala thamani visipokuwa na tabia safi na maisha ya haki (8). Mika anaonya kwamba Mungu anawaona wafanya biashara tajiri katika miji yote ya Yuda, naye anakumbuka sana mbinu zao za ujeuri za kufanya biashara. Wakiuza nafaka hutumia vipimo vya mizani vilivyopungua, na wakimpimia mnunuzi pesa za malipo yake, hutumia vipimo vizito sana. Wanatajirika kwa kutumia ujeuri, uongo na hila (9-12). Mungu atahakikisha kwamba wadanganyifu wale hawatafurahia vitu vile walivyojipatia. Kwa njia ya ukame, njaa na mashambulio ya maadui, ataharibu mali yao waliyojipatia kwa njia ya dhuluma, na mwisho atawaangamiza wenyewe (13-16). Dhambi, toba na msamaha (7:1-20) Mika akisema kama mmojawapo wa waaminifu wa kweli katika Israeli, anakiri kwamba mashtaka ya Mungu ni sawa. Hawezi kuona kitu cho chote cha kumridhisha katika maisha ya watu kwa ujumla wake. Israeli yote ni taifa lisilomtolea Mungu matunda wala halimfai (7:1).