Kitabu cha Nabii Mika MAZINGIRA Katika karne ya nane k.K. maendeleo ya ajabu ya kisiasa na ya maisha ya jamii yalionekana katika maeneo ya Palestina. Maendeleo hayo yalionekana sana katika ufalme wa Israeli kaskazini na katika ufalme wa Yuda kusini. Ukulima na biashara vilistawi katika nchi nzima, lakini pamoja na maendeleo ya kuongezeka mali kwa haraka, pia majaribu ya kawaida ya uchoyo, rushwa, magendo, udhalimu na maadili mabaya yaliongezeka. Mambo hayo tena yalisababisha maonyo na lawama kutoka kwa wajumbe wa Mungu, yaani manabii. Mika alikuwa nabii wa mwisho kati ya wanne wa wakati ule ambao maandiko yao yamehifadhiwa katika Biblia. Amosi na Hosea, manabii wa kwanza wa kundi hilo, walipeleka ujumbe wa Mungu hasa katika ufalme wa kaskazini, yaani Israeli. Wengine wawili, yaani Isaya na Mika, walishughulika zaidi na ufalme wa kusini, nao walitabiri wakati ule ule (Isa 1:1; Mik 1:1). Wote wawili walihusisha ujumbe wao hasa katika dhambi za jiji kuu la Yerusalemu. Mambo mengi ya vitabu vyao yanafanana, na walimu wengine walihisi kwamba Mika alikuwa mwanafunzi wa Isaya (Isa 8:16). Hali ya jamii Maendeleo na mafanikio hayakuwa manufaa ya jumuia yote. Waliofaidi zaidi kutokana na uchumi bora walikuwa wafanya biashara, maafisa na wenyeji wengine wa hali ya juu. Utajiri wao hasa ulitokana na kuwanyanyasa watu wa hali ya chini, kama vile wakulima na wafugaji, na pamoja na utajiri wao walipata mamlaka zaidi katika jumuia. Kwa njia ya mambo ya magendo na rushwa mahakamani, waliweza kupata cho chote walichokitaka, na matokeo yake, matajiri walizidi kutajirika ambapo maskini walizidi kupata shida. (taz.pia maelezo ya mazingira katika Amosi na Hosea.) Udhalimu ule wa ukatili ulimchukiza Mungu naye aliwaamsha manabii mbalimbali ili wawaonye watu kuhusu hukumu yake ambayo angeleta juu ya taifa lote kama watu wasingebadili maisha na tabia yao. Isaya alikuwa mtu mwenye ushawishi na sifa jijini Yerusalemu. Alikuwa mshauri wa mfalme aliyetumia daraja lake la juu ili kujaribu kujenga ufahamu mkubwa zaidi kuhusu mapenzi ya Mungu katika serikali ya taifa. Mika alitoka katika kijiji kidogo cha wakulima naye alishughulika zaidi na shida za wakulima wa hali ya chini. Yeye alilaumu uchoyo na tamaa ya matajiri wa mijini akawatetea wale waliopata shida kutokana na unyanyasaji wao. Tatizo moja kubwa la wakulima lilitokana na mbano wa biashara uliowekwa juu yao na watu wenye mamlaka na ushawishi. Kwa sababu ya tabia mbaya ya maafisa na wafanya biashara, wakulima walilazimishwa kukopa kwa matajiri ili waweze kuendelea na kazi yao. Matajiri walikopesha fedha kwa riba kubwa kiasi kwamba wakulima walishindwa kulipa madeni yao. Hivyo matajiri walichukua mali ya wakulima kama malipo, kwanza nguo na vyombo vya nyumbani (Mik 2:8) na baadaye, kama vitu vile havikutosha, nyumba za wakulima pamoja na mashamba yao (Mik 2:1-3,9). Mwisho we wakulima wakawa wapangaji wa ardhi waliolazimishwa kukodi mashamba yao kutoka kwa matajiri wao, na hivyo mizigo yao ilizidi kuwa mizito. Hali hiyo yote ya kusikitisha haikuonyesha wazo la haki ya watu wote wala ufahamu wa hali ya dini ya kweli wala ujuzi wa tabia ya Mungu. Mika aliwaambia watu kwamba, kama wangeendelea na maisha yenye tabia hiyo wasingeweza kumpendeza Mungu, haidhuru mara ngapi wangetokea na kumwabudu katika sherehe za kidini (Mik 6:6-8). Watu wasingeacha matendo yao yenye dhambi, taifa la Yuda lingeelekea hukumu ya Mungu (Mik 3:12; 6:16). Matukio ya kisiasa Mika alitabiri katika enzi za wafalme Yothamu, Ahazi na Hezekia wa Yuda. (Muda wote wa enzi hizo tatu ulikuwa katika miaka ya 740 hadi 687 k.K.) Hali ya siasa ilikuwa imara wakati wa enzi ya Yothamu, lakini ilikuwa na wasi wasi katika enzi ya Ahazi. Ahazi alihatarisha uhuru wa Yuda na kuharibu hali ya biashara kwa njia ya kununua ulinzi wa Waashuri dhidi ya maadui wengine. Siasa hiyo ililaumiwa sana nalsaya (2Fal 16:1-9; Isa 7:1-9; 8:5-8). (Ramani zinazosaidia kuelewa wakati huo ziko katika maelezo ya Hosea.) Mfalme aliyefuata, Hezekia, alirekebisha dini katika Yuda naye alifanya mikakati ya kukomesha ushawishi wa Uashuru katika Yuda. Bila shaka katika marekebisho yake Hezekia aliguswa na mahubiri ya Mika (Yer 26:18-19). Pia alishawishiwa na Isaya. Lakini alipotegemea msaada wa kijeshi kutoka Misri na mataifa mengine ili ajitetee dhidi ya Waashuri badala ya kumtegemea Mungu, Isaya alimpinga (2Fal 18:1-7; Isa 30:1-3,15). Siku moja Yerusalemu iliokolewa na hatari ya mazingira ya kivita ya Waashuri kwa njia ya mwujiza wa Mungu tu (2Fal 18:13-19:37). Wakati wa huduma ya Mika ufalme wa kaskazini, yaani Israeli, ulitekwa na Waashuri na watu wake walipelekwa kifungoni (mwaka wa 722 k.K.; taz.2Fal 18:9-12). Kuanzia wakati huo, ufalme wa kusini, yaani Yuda ulikuwa wote uliobaki katika ufalme ule mkubwa wa zamani uliotawaliwa na-Daudi. Wakati wa mgawanyiko wa ufalme, ufalme wa kaskazini uliitwa Israeli na ule wa kusini uliitwa Yuda, lakini Mika mara nyingi hatofautishi kati ya Waisraeli na Wayuda, naye anatumia majina ya 'IsĀ­raeli' na 'Yakobo' yakihusika kwa watu wa kila ufalme. Maelezo ya kitabu cha Mika yanayofuata yatafuata matumizi ya Mika ya majina haya, ingawa tunakumbuka kwamba sehemu nyingi zaidi za kitabu chake zinahusu ufalme wa kusini. MUHTASARI 1:1-3:12 Samaria na Yerusalemu tayari kwa hukumu 4:1-5:15 Ufalme bora 6:1-7:20 Mungu anashtaki na watu wanaitikia