3:1-4:11 TOBA YA WATU WA NINAWI Mahubiri ya Yona Ninawi (3:1-10) Mungu alirudia agizo lake kwa Yona ili aende na kuhubiri Ninawi, na wakati huo Yona alitii (3:1-3). Ujumbe wa Mungu ulikuwa kwamba, baada ya siku 40 mji wa Ninawi ungepinduliwa kwa sababu ya uovu wake. Watu wote pamoja na mfalme wao walichomwa mioyo na maonyo hayo wakamrudia Mungu kwa kutubu (4-5). Hata mfalme alitoa amri iliyoagiza marekebisho ya maadili katika mji mziraa (6-9). Kwa matokeo ya toba ya watu wa Ninawi, Mungu alighairi vitisho vyake vya kuangamiza mji (10). Mafundisho kuhusu huruma (4:1-11) Wakati huo ilikuwa wazi kwa sababu gani Yona hakupenda kuhubiri Ninawi. Alitaka Waninawi waangamizwe wala si kuhifadhiwa; alitaka waadhibiwe wala si kusamehewa. Alijua kwamba Mungu alikuwa na huruma kwa wenye dhambi watubuo, lakini alitaka baraka hiyo itunzwe kwa ajili ya Waisraeli tu. Angalikubali kufa kuliko kuwaona Mataifa wale kusamehewa sawa sawa na Waisraeli (4:1-3). Mungu alijaribu kumfundisha Yona ili aone kwamba hakuwa na haki ya kukasirika, lakini Yona alikataa kusikiliza. Inaonekana kama bado alifikiri kwamba Mungu angebadili mawazo yake na kuangamiza Ninawi, na hivyo alikwenda nje ya mji, akajijengea kijibanda cha kujihifadhi, akangojea huko ili aone mambo ambayo yangetokea katika mwisho wa siku zile 40 (4-5). Yona hakuitikia maonyo ya kwanza ya Mungu, kwa hiyo wakati huo Mungu alimfundisha somo la huruma kwa kutumia mafunzo ya mfano hai. Kijibanda au kingo la Yona lilipoonekana kuwa halikutosha kumhifadhi joto kali la jua, Mungu aliumba mmea mkubwa wenye majani mengi ulioota usiku ili kumpaYona kivuli. Matokeo yake, Yona alifurahi sana. Kisha Mungu alisababisha mmea ule ufe, na Yona akae katika jua kali na upepo wa joto. Matokeo yake, Yona alikasirika tena (6-8). Yona hakutaka mmea ufe, wala Mungu hakutaka watu wa Ninawi wafe. Yona aliusikitikia mmea asiouumba, uliodumu siku moja tu. Si zaidi sana Mungu awahurumie watu wa Ninawi aliowaumba, ambao katika ujinga wao, wangaliangamia kabisa (9-11)?