Kitabu cha Nabii Yona MAZINGIRA Kinyume cha vitabu vingine vya manabii, kitabu cha Yona hakitaji jina la mwandishi wake. Kitabu chake kimepata jina lake kutokana na mtu maalumu wa habari zake, yaani nabii ambaye wakati fulani alitabiri kwa usahihi kuongezeka kwa ufalme wa kaskazini wa Israeli wakati wa enzi ya Yeroboamu II (taz.2Fal: 14:23,25 na ramani ya sehemu hiyo). Habari nyingine iliyotofautiana na vitabu vingine vya manabii ni kwamba, kitabu hiki hakina mahubiri mengi ya nabii mwenyewe. Sehemu kubwa ya kitabu ni masimulizi, na tofauti nyingine, sehemu kubwa ni maandiko ya nathari. Makusudi ya kitabu Wakati wa enzi ya Yeroboamu II (miaka ya 793-753 k.K.) taifa la Israeli lilifurahia maendeleo mazuri na mafanikio kiasi kwamba watu kwa urahisi walijenga tabia ya kiburi juu ya taifa lao. (Kwa habari za hali ya wakati ule, taz. maelezo ya mazingira katika kitabu cha Hosea.) Hata nabii wa Mungu, Yona, alitekwa na roho ile ya kiburi cha utaifa. Bila shaka Yona alifurahi kuona utimizaji wa unabii wake kuhusu ushindi wa Yeroboamu, naye angeridhika zaidi angeweza kuona kuangamizwa kwa Uashuru, kwa sababu kuongezeka kwa mamlaka ya taifa hilo kulitisha uhuru wa Israeli. Mji mkuu wa Uashuru, Ninawi, ulikwisha tishwa na adui fulani kutoka kaskazini. Kwa hiyo Yona alishtuka Mungu alipomwambia aende na kuwaonya watu wa Ninawi kuhusu mashambulio yaliyowakabili. Aliagizwa awahamasishe watu wale watubu uovu wao, kusudi yamkini wangezuia hukumu ile ya kubomolewa kwa mji wao (Yon 3:4-5,10). Jibu la kwanza la Yona lilikuwa kukataa kwenda huko, kwa sababu angependa zaidi kuona Ninawi iangamizwe kuliko kuepushwa na hukumu namna hiyo. Yona alipaswa kujifunza kwamba Mungu ndiye mtawala wa mataifa yote, naye angeonyesha huruma yake kwa watu wo wote aliotaka kuwasaidia, hata wangekuwa watu waovu kama Waninawi. Watu wa Mungu walioona upendo na huruma ya Mungu mara nyingi, wangepaswa kuonyesha upendo wa namna hiyo kwa watu wengine. Mungu hakufurahi kuwaangamiza watu, na watu wake wanatakiwa kuwa na tabia iyo hiyo. Kama vile Mungu alivyopenda watu watubu na kusamehewa makosa yao, hata watu wake wanatakiwa kuwa na hamu hiyo (Yon 4:11; taz.Mdo 11:18; Rum 3:29; 9:15). MUHTASARI 1:1-17 Uasi wa Yona na matokeo yake 2:1-10 Zaburi ya kutoa shukrani 3:1-4:11 Toba ya watu wa Ninawi