Edomu na kubomolewa kwa Yerusalemu Majeshi ya Babeli yalipobomoa ukuta wa Yerusalemu na jiji lote, Waedomu walijiunga nayo, wakifurahi katika uovu wao kusaidia kazi ya kufutilia mbali alama za mwisho wa taifa la Yuda (Zab 137:7; Eze 35:5,12,15). Nabii Obadia, aliyeandika ujumbe wake muda fulani baada ya mambo hayo, alitangaza hukumu ya Mungu juu ya Waedomu, kwa sababu walijishirikisha katika uadui ule dhidi ya taifa la udugu wao, ambalo afadhali wangalilisaidia. (Waisraeli walitokana na Yakobo, na Waedomu walitokana na kaka yake, yaani Esau; taz.Mwa 25:23-26; 32:28; 36:1,8-9. Kwa habari za mifarakano iliyokuwepo, kwanza baina ya ndugu wale wawili na baadaye baina ya mataifa yale mawili yaliyotokana nao, taz.Mwa 27:36,39-45; Hes 20:14-21; 2Sam 8:13-14; 2Fal 8:20-22; 14:7; 16:6; 2Nya 25:11-12; 28:17.) Nchi ya Edomu ilikuwa kusini ya Yuda, kati ya Bahari ya Chumvi na Ghuba ya Akaba, mwisho wa mkono wa kaskazini mashariki wa Bahari ya Shamu. (taz. ramani katika maelezo ya Hesabu na Hosea.) Ilikuwa nchi yenye milima mingi na miamba iliyowapa watu wake nafasi nzuri ya kujitetea dhidi ya mashambulio ya maadui. Mlima mkuu katika ile uliitwa Seiri, na kwa jina hilo nchi yote mara nyingine ilitajwa (Mwa 32:3; 36:8-9; Kum 2:1-5). Miji yake mikubwa ilikuwa Sela (Petra), Bozra na Temani katikati ya nchi na Ezion-geberi katika ghuba ya Akaba. Waedomu, na hasa wale wa eneo la Temani, walikuwa na sifa kuhusu hekima na hila yao (Ayu 2:11; Yer 49:7), lakini kiasi cho chote cha werevu au ujanja usingeweza kuwaokoa na hukumu ya Mungu iliyowakabili. Sawa sawa na unabii wa Obadia, taifa la Edomu liliangamizwa baadaye, na nchi yake iliwekwa ukiwa na maadui zake (Mai 1:1-4). UJUMBE WA OBADIA Dhambi ya Edomu (1-14) Waedomu walifikiri kwamba nchi yao isingeweza kutekwa na maadui kwa sababu ya mifumo yao ya kujitetea waliyoweka katika milima yao yenye miamba. Obadia anawaonya Waedomu kwamba, haidhuru wangekwea milima yao mpaka wapi au wangeimarisha ngome zao kiasi gani, hakuna jambo liwezalo kuwaokoa na maafa ya uangamizi ujao. Majeshi ya maadui yamekwisha anza kujiandaa kwa kuwashambulia (1-4). Mwizi avunjaye nyumba anaiba vitu vile tu anavyovitaka, akiacha vingine katika nyumba; mfanyakazi katika shamba la mizabibu anachuma zabibu zile tu zilizokomaa na kuacha nyingine; lakini askari wa maadui zao watakapoteka nyara katika Edomu watachukua kila kitu. Hata vitu vya thamani vilivyofichwa katika mapango ya milima vitachukuliwa (5-6). Waedomu walijivunia ujanja wao wa kisiasa na kijeshi. Viongozi wao walifikiri kwamba walikuwa na akili zaidi kuliko mataifa ya nchi za jirani, na mara nyingi walitumia ujanja wao kwa kuwadanganya washiriki wao. Kwa hiyo aibu yao ya kushindwa itakuwa kubwa zaidi, watakapoona kwamba baadhi ya majirani wale, ambao walidhania kwamba ni washiriki wao, waliwadanganya na hivyo wanasaidia kuwaangusha (7-9). Sasa Obadia anatoa sababu za hukumu ya Mungu juu ya Edomu. Wababeli waliposhambulia na kuteka Yerusalemu, Waedomu hawakufanya jambo lo lote ili kusaidia taifa la udugu wao. Vibaya zaidi, waliwasaidia washambulizi (10-11). Walifurahi kuona jiji la Yerusalemu likitekwa nyara, na hasa walijiunga katika utekaji huo. Pia waliwasaidia Wababeli kuwakamata Wayuda kwa njia ya kuzuia njia kwa wale waliojaribu kukimbia (12-14). SikuyaBwana (15-21) Katika siku ya BWANA, Mungu atajiingiza katika mambo ya wanadamu na kuwaadhibu wenye dhambi kadiri ya dhambi zao. Waedomu walisherehekea utekaji wa Yerusalemu kwa kufanya karamu kubwa yenye ulevi katika magofu ya hekalu la Wayahudi juu ya Mlima Sayuni. Sawa sawa na maadui wengine wa Yuda, wao wakati huo watalewa kwa namna nyingine: yaani watanyweshwa kikombe cha hasira ya Mungu (15-16). Baada ya kuwaadhibu maadui wa Israeli, Mungu atawaokoa watu wake kutoka kifungoni na kuwarudisha katika nchi yao. Atarudisha utakatifu wa Sayuni, lakini atatuma hukumu ya kufaa juu ya Edomu. Atawaangamiza Waedomu kama vile moto unavyoteketeza makonde yenye nyasi kavu (17-18). Kutoka Yerusalemu, taifa la Israeli litakalokuwa limeimarishwa upya, litaenea kuelekea kusini katika nchi ya Edomu, magharibi katika nchi ya Wafilisti, kaskazini katika nchi yao wenyewe ambayo Wafilisti walikuwa wameiteka, na mashariki kuvuka Mto Yordani na kuteka upya nchi yao ya zamani ya upande huo (19; taz.Amo 9:12). Wafungwa watafunguliwa kutoka makambi yao ya nchi za kigeni na kupewa makazi mapya katika sehemu mbalimbali za nchi yao, kuanzia Foinike (Sarepta) kaskazini hadi Negebu kusini (20). Wakati huo Waisraeli watawatawala maadui zao wa zamani, wakionyesha wazi mbele ya mataifa yote kwamba Mungu anatawala historia. Utawala mkuu ndio kazi yake (21).