7:1-9:10 MAONO YA HUKUMU Uvumilivu wa Mungu kabla ya hukumu (7:1-9) Wakulima walilipa kodi zao kwa njia ya kumpa mfalme mavuno yao ya kwanza. Baada ya hayo mavuno ya pili yalipatikana ambayo ni mavuno makuu ya watu wote. Katika maono ya Amosi, mavuno hayo ya pili yalikuwa na hatari ya kuharibiwa katika maafa ya nzige. Iwapo Mungu angewaadhibu Waisraeli kwa njia hii, labda wasingepata nguvu tena. Amosi alipowaombea Waisraeli kwa jambo hilo, Mungu aliitikia na kuwahurumia (7:1-3). Baadaye Mungu alijibu maombi yaliyofanana na hayo baada ya kutisha kwamba angeunguza nchi kwa ukame mkali (4-6). Lakini Amosi alipoona kwamba watu wengi zaidi waliendelea na dhambi zao, alijua wazi kwamba hukumu haikuweza kuzuiwa zaidi. Kama vile mjenzi apimavyo ukuta kwa timazi ili aone kama umenyooka, ndivyo Mungu apimavyo taifa la Israeli kadiri ya timazi yake kamili ili aone kama lina unyofu wa maadili yake. Ameona kwamba taifa lote limepotoka (limepindika) bila ya uwezekano wa kutengenezwa, kwa hiyo halina budi kuangamizwa. Dini iliyoharibika kwa utawala mwovu ni sababu ya ukosefu wa nchi, na kwa sababu ya mambo hayo hukumu lazima ije juu yake kwa ukali wote (7-9). Amosi na Amazia (7:10-17) Kuhani Amazia alisikia mahubiri ya Amosi huko Betheli akakasirika sana, kwa sababu Amosi alikuwa amelaumu desturi za dini ya Israeli kwa ujasiri wa namna hiyo. Alifanya mbinu ya kumwondoa nabii asiyependwa kwa njia ya kumshtaki kwa hatia ya usaliti, kwa sababu ya matangazo yake ya hukumu juu ya makao ya mfalme (10-11; taz.mst.9). Inaonekana kama mfalme hakujali mashtaka ya kuhani, na hivyo Amazia alijaribu kumwomba Amosi arudi kwenda katika nchi ya Yuda ambapo unabii wake dhidi ya Israeli ungekubaliwa vizuri zaidi na kumletea mapato mazuri (12-13). Amosi anajibu kwamba yeye si nabii wa kuajiriwa wala hakusomea kazi hiyo katika chuo. Yeye ni mkulima na mfugaji ambaye Mungu amemwita ili atangaze ujumbe wake kwa Israeli (14-15). Zaidi ya hayo, ana ujumbe kwa Amazia: Wakati nchi ya Israeli itakapotekwa na maadui, mke wake Amazia atakuwa kahaba kwa askari wa maadui, watoto wake watauawa, na mashamba yake yatagawanywa na washindi (14-17). Taifa la Israeli linakaribia mwisho wake (8:1-14) Kama vile msimu wa mavuno unavyofikia mwisho wake na matunda yanakusanywa katika vikapu, ndivyo taifa la Israeli litakavyofikia mwisho wake nalo litaadhibiwa. Sherehe za furaha zitageuzwa kuwa maombolezo, na badala ya kuwa na matumaini watu watakata tamaa. Maadui watakaposhambulia mauaji yatakuwa makubwa mno, hata mizoga ya watu italala mitaani na mashambani bila ya kuzikwa kwa muda mrefu (8:1-3). Amosi anarudia hali mbaya zilizopo katika IsĀ­raeli, ili aonyeshe sababu za kuangamizwa kwa taifa hilo. Watu wa hali ya juu huwanyonya watu wa hali ya chini (4). Wafanya biashara wenye uchoyo, wanaokasirika kwamba wanapaswa kuacha kazi yao mara kwa mara kwa ajili ya sikukuu za dini, huona shida kungoja sikukuu zipite, ili warudie shughuli zao za kufanya biashara yenye maslahi. Hawana kanuni za uaminifu. Wakiuza nafaka hutumia vipimo vidogo kuliko kawaida, na wakipima malipo ya wateja wao katika mizani hutumia vipimo vizito zaidi. Wanauza hata takataka za nafaka zinazobaki ambazo kwa kawaida maskini hupewa bure au wanyama wa kufugwa hulishwa (4-6). Hukumu itakayokuja juu yao itawaponda kama tetemeko la nchi na kuwapindua kama mafuriko ya maji (7-8). Si giza la kawaida tu litakalofunika taifa, bali giza la kiroho, isiwepo hata nuru kidogo ambayo siku hizi inapatikana kwa ajili ya kazi ya manabii. Katika uchungu na maombolezo yao, watu ghafla watapata njaa ya Neno la Mungu, lakini hawataliona, hata wakilitafuta sana (9-12). Si nguvu ya ujana wala miungu ya kigeni waliyoiabudu vitaweza kuwaokoa hukumu ya mwisho itakapowapata (13-14). Hakuna njia ya kutoroka (9:1-10) Katika maono ya mwisho, Mungu anasababisha majengo makubwa ya madhabahu yaanguke juu ya vichwa vya waabudu, akitoa mfano wa hukumu yake juu ya watu wa Israeli kwa sababu ya dini yao ya kinyume (9:1). Hakuna mtu atakayeweza kuepuka hukumu yake; hakuna mahali ambapo Mungu hawezi kufikia (2-4). Yeye ni Mungu wa ulimwengu wote naye ni mtawala wake. Ana uwezo wa kutimiza makusudi yake (5-6). Waisraeli wengine wanaweza kujitetea wakisema kwamba wao ni wateule wa Mungu. Aliwaleta kutoka Misri, kwa hiyo hangewapeleka katika utumwa wa nchi nyingine tena. Amosi anasisitiza kwamba baraka za wakati uliopita haziwezi kuwa dhamana au uhakika wa usalama kwa wakati ujao. Mungu aliongoza maendeleo na mambo ya mataifa mengine wala siyo ya Israeli tu, lakini watu wakiishi katika dhambi, Yeye atawaadhibu bila kujali ni wa taifa gani. Katika jambo hili Waisraeli hawana upendeleo kuliko mataifa mengine, kama vile Wakushi, Wafilisti na Washami. Mungu ataangamiza taifa la Israeli, lakini atawahifadhi watu wachache katika taifa hilo watakaoendelea kuwa waaminifu kwake. Kwa njia ya waaminifu hao atatimiza makusudi yake (7-8). Amosi anatoa mfano wa mwisho kuhusu uhakika wa hukumu itakayokuja juu ya Waisraeli wenye dhambi. Kama vile katika kupepeta ngano hakuna chembe ndogo inayoanguka chini, vivyo hivyo hakuna mwenye dhambi atakayeepukana na hukumu ya Mungu. Watu wakidhania kwamba, kwa kuwa ni watu wa Israeli hawatapata hukumu ya Mungu, wanajidanganya tu (9-10).