Kitabu cha Nabii Amosi MAZINGIRA Amosi alikuwa wa kwanza kati ya manabii wanne waliotabiri wakati wa karne ya nane k.K., wengine wakiwa Hosea, Isaya na Mika. Wakati ule Israeli iligawanyika katika falme mbili, na kila mmoja wa waandishi wale alitaja tarehe ya kuandika kwake kadiri ya wafalme wa Israeli na Yuda waliotawala wakati wa utabiri wao. Hivyo msomaji wa siku hizi anaweza kuelewa habari za hali ya mazingira ya huduma za manabii hao. Maelezo ya mazingira ya Hosea yanatoa muhtasari wa hali ya jumuia, ya dini na siasa katika Israeli na Yuda wakati wa manabii wa mwanzo wa karne ya nane k.K. Msomaji akisoma maelezo yale atapata ujuzi mzuri juu ya utangulizi wa maelezo haya ya kitabu cha Amosi. Mafanikio zaidi huleta uovu katika jamii Amosi alipoanza kuhubiri, Yeroboamu II alikuwa mfalme wa ufalme wa kaskazini, yaani Israeli, na Azaria (au Uzia) alitawala katika ufalme wa kusini, yaani Yuda. Katika enzi za wafalme hao mataifa yote mawili yalifurahia maendeleo mazuri na mafanikio, lakini pamoja na mafanikio hayo mabadiliko yaliingia yaliyoharibu dini, jumuia na maadili. Kuinuka kwa jamii ya wafanya biashara, iliyoanza kabla ya miaka 200 wakati wa enzi ya Sulemani, ilipata kilele chake wakati wa Yeroboamu II na Uzia. Wakati huo jumuia haikujengwa juu ya maisha ya kawaida ya ukulima na ufugaji. Kutokana na kukua kwa haraka kwa mambo ya biashara, maisha ya mijini yalipata maana mpya kabisa, na pamoja nayo uovu wa hali ya juu ulienea kwa jinsi ambavyo haujaonekana katika nchi. Kuinuka kwa haraka kwa watu wengine kulikuwa na maana ya kuzidi kuwa maskini kwa wengine. Kwa kadiri watu wa hali ya juu walivyozidi kuwa na mali na mamlaka, ndivyo walivyowanyanyasa watu wa hali ya chini. Mambo ya rushwa na magendo yalienea hata katika mahakama ya kawaida, na hivyo watu wa hali ya chini waliachwa bila njia au mbinu za kujipatia haki yao. Mahubiri ya moto ya Amosi Kwa mashambulio yake makali na yenye ushujaa dhidi ya wafanya biashara tajiri na watawala wasiokuwa na haki katika Israeli, Amosi alikuwa nabii wa kwanza aliyewatetea watu wa hali ya chini. Alikuwa mfugaji wa kondoo aliyeishi katika kijiji cha mbali karibu na mpaka wa kaskazini mwa Yuda, lakini mashambulio yake mengi yanaelekea Israeli. Labda ilikuwa hivi kwa sababu alipopeleka manyoya ya kondoo zake katika soko la ng'ambo ya mpaka huko Betheli na miji mingine, aliona udhalimu uliotawala katika maisha ya miji ya Israeli. Kwa kweli, Amosi mwenyewe alipata uzoefu na ujuzi wa hali hiyo, kwa sababu bila shaka alipaswa kushughulika na wafanya biashara wajeuri na maafisa waliokula rushwa. Katika mahubiri yake makali, Amosi alilaumu uchoyo ule uliochukiza na fahari iliyozidi kwa matajiri, kwa sababu alijua kwamba utajiri wao ulipatikana kwa njia ya udanganyifu, dhuluma na uvunjaji wa sheria tu (2:6-7; 3:10,15; 5:10-12; 6:4-6; 8:4-6). Walitimiza kanuni za dini na kushika sikukuu kwa bidii sana, walilipa zaka zao (yaani sehemu ya kumi ya mapato yao) na kutoa sadaka nyingi, lakini mambo yale yote yalikuwa bure machoni pa Mungu, kama waabudu waliendelea katika dhuluma yao ya kijamii (5:21-24; 8:3,10). Amosi aliona wazi mambo ambayo watu wa hali ya juu hawakuyaona, yaani taifa lote lilielekea hukumu kali ya Mungu (7:11). MUHTASARI 1:1-2:16 Hukumu juu ya mataifa mbalimbali 3:1-6:14 Sababu za adhabu ya Israeli 7:1-9:10 Maono ya hukumu 9:11-15 Matumaini kwa wakati uj ao