3:1-21 HUKUMU YA MWISHO NA BARAKA Mpaka wakati huo Yoeli alitia mkazo katika mambo ya siku ya BWANA ambayo hayakujulikana vizuri, kwa mfano, hukumu ya wenye dhambi wote, pamoja na Israeli na Yuda, na baraka kwa waaminifu wote bila ya kujali umri, wanawake au wanaume au hali katika jumuia. Wakati huo Yoeli anashughulika na mambo yaliyojulikana zaidi, yaani wokovu wa watu wa Mungu na hukumu juu ya maadui zao. Lakini anataka wasomaji wake waelewe mambo hayo katika nuru ya yale aliyokwisha waambia kuhusu wokovu wa Mungu na hukumu yake juu ya ulimwengu wote. Watu wa Mungu wanaweza kuwa na uhakika wa wokovu wao binafsi kama wametubu dhambi zao kwanza, na maadui juu ya hukumu yao (taz. 2:32; Mdo 2:37-39; 17:30-31). Hukumu ya mataifa ya maadui (3:1-15) Yoeli anatoa mfano wa mataifa yakikutana kwa mashambulio ya mwisho dhidi ya Yerusalemu. Lakini mataifa hayo hayatambui kwamba ni Mungu aliyeyakutanisha. Wakati huo atatimiza hukumu yake juu yao kwa sababu ya makosa yao juu ya taifa la Yuda. Hatia kuu katika mashtaka yao ni kwamba yaliteka maeneo ya nchi ya Yuda na kuwafukuza wenyeji wake katika nchi nyingine au kuwauza kuwa watumwa (3:1-3). Mataifa ya Tiro, Sidoni na Ufilisti yanatajwa kama mifano ya mataifa yale yaliyopigana vita na Yuda na kujilipiza kisasi kwa njia ya kuteka nyara katika hekalu na kuwauza watu wake kuwa watumwa. Wakati huo Mungu atayatendea mataifa hayo sawa sawa na yalivyowatendea Wayuda (4-8; taz.2Nya 21:16-17). Nabii akirudia tena mfano wa mataifa yaliyokutana kwa ajili ya kupiga vita katika bonde la nje ya Yerusalemu, anawachokoza maadui kwa maneno ya kinyume, akiwahamasisha waandae majeshi yao vizuri kwa mashambulio yao. Kisha anamwita Mungu, ili Yeye ashushe majeshi yake ya malaika (mashujaa wake; mst.llb), wawe tayari kutekeleza hukumu yake juu ya maadui (9-12). Wakati wa uamuzi wa Mungu utawadia, naye atatangaza neno lake la hukumu juu ya mataifa. Mataifa yana hatia, uovu wao ni mkubwa, kwa hiyo hayana budi kufa. Watafyekwa na kukatwa kama zabibu katika mizabibu yake; damu yao itatiririka kama vile juisi ya zabibu inavyofurika katika shinikizo yake. Bonde la hukumu ya Mungu litajaa mizoga ya askari waliokufa vitani (13-15). Baraka za watu wa Mungu (3:16-21) Wakati wa hukumu ya Mungu juu ya maadui zake pia ni wakati wa wokovu wake wa Yerusalemu. Atawalinda watu wake wasipate adhabu, atawasafisha na uchafu wao na kuwapa amani na mafanikio (16-18). Baada ya kuwaadhibu maadui zake (inayoonyeshwa kwa mfano wa Misri na Edomu), Mungu ataishi miongoni mwa watu wake milele. Watesi watapokea hukumu yao ya haki, lakini wenye haki wataingia katika uzima wa milele (19-21). Siku ya Bwana Katika kitabu chake Yoeli anaonyesha jinsi matukio ya maafa ya nzige yalivyokuwa mfano na utabiri wa matukio makubwa zaidi yatakayotokea baadaye. Alionyesha jinsi siku ya BWANA itakavyoleta hukumu na wokovu. Kuhusu mlingano wa hukumu ya siku ya BWANA ya siku za Yoeli (yaani maafa ya nzige) na hukumu ya siku ile kuu ya mwisho ya BWANA, linganisha 2:3 na 2:30; 2:10a na 3:16a; 2:10b na 3:15; 2:11a na 3:11b. Kuhusu mlingano wa baraka ya watu wa Mungu baada ya maafa ya nzige na ile ya baada ya hatua kuu ya mwisho ya Mungu dhidi ya mambo ya wanadamu, linganisha 2:23-24 na 3:18; 2:26-27 na3:16b-17.