Kitabu cha Nabii Yoeli MAZINGIRA Miongoni mwa manabii wa Agano la Kale, Yoeli anatofautiana na wengi wao, kwa sababu hakutaja wakati alipohubiri. Pendekezo mojawapo ni kwamba alitabiri katika Yuda muda wa miaka 835 hadi 830 k.K. hivi, yaani wakati wa mwanzo wa utawala wa mfalme-kijana Yoashi. Jambo hili lingeeleza kwa nini mambo ya Shamu, Uashuru na Babeli hayakutajwa katika kitabu chake. Mataifa yale yalikuwa maadui wakuu wa Israeli wakati wa ufalme wa mgawanyiko, yaani wakati ule mataifa hayo yalikuwa hayajajiingiza katika mambo ya Yuda. Pia lingeeleza kwa nini mfalme aliyetawala wakati ule hakutajwa, kwa sababu wakati ule utawala wa Yuda kwa jumla ulikuwa mkononi mwa kuhani Yehoyada (2Fal 11:1-21; 12:1-2). Sifa na mamlaka makuu ya Yehoyada labda pia yalikuwa sababu mojawapo ya mvuto wa Yoeli katika hekalu na ibada yake (Yoel:9,13; 2:12,15-17). Pendekezo lingine au uwezekano mwingine ungekuwa kwamba, kitabu chake kimeandikwa baada ya kurudi kutoka kifungo cha Babeli. Hivyo wakati wa kuandikwa kwake ungekuwa aidha miaka ya 520-510 k.K. (yaani baada ya huduma za Hagai na Zekaria na kujengwa upya kwa hekalu), au karibu na mwaka wa 400 k.K. (yaani wakati wa kizazi kimoja baada ya matengenezo ya Ezra na Nehemia). Kufuatana na mapendekezo haya, Yoeli ni mmojawao wa manabii wa kwanza au wa mwisho walioandika unabii wao. Makusudi ya kitabu Ingawa hatuna tarehe maalumu ya kuandikwa kwa kitabu cha Yoeli, msomaji wa siku hizi asiwe na shida ya kuelewa ujumbe wake. Sababu yake ni kwamba, tukio moja kubwa lililo msingi wa kitabu halihusu mambo ya siasa ya Yuda wala ya mataifa mengine. Tukio lake ni maafa makubwa ya nzige yaliyoleta uharibifu jijini Yerusalemu na katika mkoa wake. Maafa yale yalileta hasara kubwa ya kilimo, na watu wa eneo kubwa walipata shida kubwa. Hasara yake ilizidishwa tena kwa sababu maafa yalitokea katika kilele cha wakati wa ukame ulioleta shida sana nchini. Yoeli alitafsiri matukio hayo kuwa hukumu ya Mungu juu ya nchi ya Yuda kwa sababu ya dhambi za watu wake. Aliwaahidi watu kwamba, kama wangetubu, Mungu angewabariki upya na kuwapa nafaka tele na ufahamu zaidi wa nafsi yake. Aliona matukio hayo kuwa ni mfano wa hukumu za Mungu za wakati ujao juu ya maadui wote na baraka yake kwa watu wake. MUHTASARI 1:1-2:11 Maafa makuu ya nzige 2:12-32 Huruma ya Mungu kwa watu watubuo 3:1-21 Hukumu ya mwisho na baraka