14:1-9 UPENDOWA MUNGU WA KUSAMEHE Mungu anaipenda Israeli, ingawa ina dhambi na uasi, naye bado anangojea toba ya watu kuliko uharibifu wao. Anawafundisha hata maneno yenyewe ya kukiri na kuomba msamaha wake. Katika sala hiyo wanakiri dhambi yao na kuahidi kwamba wataacha kutafuta misaada ya mataifa ya kigeni. Waache kuabudu miungu iliyochongwa na wanadamu; wasitegemee kitu cho chote isipokuwa Mungu na huruma yake (14:1-3). Iwapo wanatubu, Mungu katika upendo wake atawapa roho ya uaminifu itakayowekwa mahali pa roho ya uasi wa wakati huo. Atawabariki kwa kiburudisho, kwa uzuri, kwa nguvu na uwezo wa kutoa matunda mema (4-7). Mungu anawahakikishia watu wake kwamba Yeye anapenda kuwapa kwa fadhili zake baraka kubwa kuliko wao walivyoweza kutazamia, lakini hawakuweza kuzipata kutokana na ibada zao za Mabaali na tamaa yao ya mafanikio (8). Nabii anamaliza kitabu chake kwa maneno ya mashairi ya hekima, ili awakumbushe wasomaji wake kwamba, wakitia maanani ujumbe wake, watapata baraka, lakini wakiudharau, ujumbe huo utaleta maangamizi (9). Sisi tunajua kutokana na historia kwamba watu hawakuitikia onyo la Mungu. Taifa la Israeli (yaani ufalme wa kaskazini) lilitegwa na Waashuri mwaka wa 722 k.K., miji yake ilibomolewa na watu wake walipelekwa kifungoni (2Fal 17:1-6).