Kitabu cha Nabii Hosea MAZINGIRA Hosea aliishi wakati wa historia ya Israeli taifa hilo la kale lilipogawanyika kuwa falme mbili. Israeli ilikuwa ufalme wa kaskazini na Yuda ufalme wa kusini. Huduma ya Hosea ilianza katika enzi ya mfalme Yeroboamu II katika Israeli na mfalme Uzia (au Azaria) wa Yuda, ikaendelea kupitia enzi za wafalme waliofuata (Hosea 1:1). Wakati wa mafanikio Wafalme Yeroboamu wa pili na Uzia (au Azaria) wa Yuda walitawazwa karibu wakati mmoja, yaani katika mwanzo wa karne ya nane k.K. Wote wawili walitawala muda mrefu na utawala wao ulikuwa na mafanikio. Wakati ule nchi za Israeli na Yuda zilikuwa imara sana. Haikuwa hivyo tangu enzi ya mfalme Daudi, wala mafanikio ya kibiashara hayakuwa na mfano wake katika historia ya Israeli. Hali hiyo kwa sehemu iliwezekana kwa sababu hali ya kisiasa katika maeneo yale ilikuwa njema kwa Israeli na Yuda. Shamu iliyokuwa na mamlaka makubwa awali, ilizidi kurudi nyuma, na Uashuru ulioinuka kuwa na mamlaka zaidi, ulishughulika na kupigana vita na maadui wa kaskazini mwake, na hivyo kwa muda wa miaka 40 haukujali habari za Israeli na Yuda. Katika hali hiyo, Yeroboamu II aliweza kupanua ufalme wake katika eneo la Hamathi sehemu za kaskazini hadi Bahari ya Chumvi kusini, kama ilivyotabiriwa na nabii Yona. Jambo hili lilimpa mamlaka juu ya barabara nyingi za biashara zenye maana kubwa, na hivyo nguvu ya Israeli iliongezeka sana. Lakini kuhusu mambo ya dini, mfalme huyo hakufaa kabisa (2Fal 14:23-29). Wakati huo Uzia (au Azaria) alipanua ufalme wake. Alieneza utawala wake upande wa magharibi kupitia nchi ya Wafilisti mpaka Bahari ya Kati, upande wa mashariki kupita nchi ya Amoni, na kusini alitawala nchi yote hadi Bahari ya Shamu na Misri. Aliimarisha Yerusalemu kwa ngome za kujitetea kivita, aliboresha maendeleo ya kilimo na ufugaji katika nchi yote, alikuwa na jeshi kubwa naye aliwapa askari zake silaha mpya kabisa. Kosa lake kuu lilikuwa kwamba, alifikiri angeweza kuwa mkuu wa dini ya taifa kama vile alivyokuwa mkuu wa siasa na serikali, na kwa ajili ya lengo hilo la kinyume Mungu alimwadhibu vikali (2Fal 15:1-7; 2Nya 26: 6-23). Hali ya maendeleo ya jamii Maendeleo ya kibiashara katika karne ya nane pia yalisababisha tamaa ya mali na uharibifu kwa habari za magendo na rushwa kiasi ambacho hakikuonekana katika Israeli na Yuda mpaka wakati huo. Lakini watu waliofaidi kutokana na maendeleo na mafanikio hayo hawakuwa watu wa kawaida (kama vile wakulima waliokuwa raia wengi zaidi), bali maafisa na wafanya biashara. Watu hao walikuwa na mamlaka na ushawishi. Waliwanyanyasa maskini bila kujali kitu, wakijua kwamba, kutokana na desturi ya kutoa rushwa mahakamani, maskini hawakuwa na njia yo yote ya kujitetea. Watu waliomcha Mungu walianza kuona kwamba desturi kama hizo baada ya muda zingeleta hukumu ya Mungu na uharibifu wa taifa zima. Nabii wa kwanza wa wakati ule ambaye maandiko yake tunayo mpaka sasa alikuwa Amosi. Aliwalaumu sana watu wa hali ya juu waliokuwa na udhalimu mwingi katika ufalme wa kaskazini. (Kwa habari zaidi kuhusu hali ya udhalimu katika jumuia ya wakati ule, taz. maelezo yanayotangulia uchunguzi wa kitabu cha Amosi.) Mambo ambayo Hosea alikabiliana nayo Ingawa Amosi alilaumu na kuonya sana, hali ya maadili ya jumuia ya Israeli ilizidi kuwa mbaya. Mambo haya yanaonekana wazi katika maandiko ya Hosea. Kama vile Amosi, hata Hosea alishughulika zaidi katika ufalme wa kaskazini, yaani Israeli, ingawa mara nyingine alitaja ufalme wa kusini. Si matajiri na wenye mamlaka tu waliowanyanyasa maskini, bali pia makuhani. Wakati huo dini ilikuwa imechafuka vibaya, na ilikuwa hali hiyo ya dini ambayo Hosea aliishambulia sana. Aliona hali hiyo kuwa sababu ya uovu wote wa Israeli. Ibada ya Mabaali pamoja na sherehe zake za kuongeza uzaaji wa hali yo yote pamoja na uasherati wa kidini (taz. 'Ibada ya Mabaali' hapo chini), ilienea zaidi wakati ule kuliko ilivyokuwa siku za Amosi. Waisraeli kwa jumla hawakujua neno kuhusu tabia ya BWANA (YAHWEH) (Hos 4:1-6,17-19; 5:4; 6:6-10; 7:14-16; 8:5-6; 13:6; taz.Amo 2:7-8). Kwa kuwa uhusiano wa agano baina ya Israeli na BWANA ulifananishwa na uhusiano wa ndoa, ushirika wa Israeli na miungu mingine kwa kweli ulikuwa zinaa ya kiroho. Hosea alijulishwa mambo hayo katika maisha yake mwenyewe kwa mfano hai wa mke wake, Gomeri, alipofanya zinaa. Gomeri alimwacha Hosea akawafuata wapenzi wengine. Lakini maisha yake matamu hayakuchukua muda mrefu naye aliuzwa kuwa mjakazi. Wakati huo wote Hosea aliendelea kuwa mwaminifu kwa ndoa yake, naye alikuwa bado akimpenda mke wake aliyepotea. Alipomwona hivi katika utumwa wake alimkomboa tena. Upendo wa Hosea kwa mkewe ulikuwa mfano wa upendo wa agano la Mungu kwa watu wake waliokuwa wamemwasi. Wao pia wangepelekwa kifungoni, lakini baada ya kusafishwa uchafu wa ushirika wao na miungu ya Kikanaani, wangerudishwa tena katika nchi yao. Ibada ya Mabaali Miungu ya Kikanaani ilijulikana kuwa Mabaali (wingi wa Baali, maana yake Bwana, Mwenyewe au Mume). Miungu ya kike ilijulikana kwa jina la Ashtarothi au Maasheri (wingi wa Ashera). Miungu hiyo iliaminiwa kuwa miungu ya hali ya ulimwengu. Watu walifikiri kwamba ilikuwa na uwezo wa kuongeza uzazi kwa wanadamu, wanyama na ustawi wa ukulima. Tangu siku za kwanza za kuishi kwao Kanaani, Waisraeli walikuwa na hatari ya kupotezwa na dini za Wakanaani. Waliona mambo yaliyofanana baina ya ibada ya YAHWEH (BWANA) na ibada ya miungu ya nchi hiyo, na baada ya muda walichanganya mambo hayo. Kwa kweli, walifikiri kwamba YAHWEH alikuwa Mungu wa ulimwengu, naye alikuwa mume na Bwana wa Israeli (Kiebrania = baal). Wakanaani pia waliabudu katika madhabahu za milimani (zilizoitwa 'mahali pa juu'), sawa sawa na Waisraeli wa kale walivyofanya. Baadhi ya alama za mahali pa ibada ya Baali zilikuwa bustani takatifu na nguzo za mawe au miti, na nguzo hizo ziliitwa Asherimu (wingi wa Ashera, mungu wa kike). Katika mahali pale pa juu malaya wa kiume na wa kike walipatikana, na pamoja nao waabudu waliweza kuendeshea sherehe za kuongeza uzazi. Sherehe zile zilikuwa za kushirikiana kimwili kama sehemu ya ibada ya kidini ambamo watu waliamini kwamba wangewashawishi miungu ili waongeze familia, ufugaji na nafaka ya mashambani. Waisraeli walipomwacha YAHWEH (BWANA) na kufuata Mabaali, walipata hatia ya zinaa ya kiroho na hata ya kimwili (Hos 2:5,8; 4:10-13; 7:14-16; 9:1-2). Kurudi nyuma kwa hali ya siasa katika Israeli na Yuda Uovu wa kijamii na wa kidini ulioongezeka katika enzi za Yeroboamu II na Uzia nao ukaendelea katika enzi za wafalme waliofuata. Zaidi ya hayo, matatizo makubwa ya siasa yalitokea. Katika Israeli enzi ya Yeroboamu ilikuwa imara sana kwa muda mrefu, hata alipokufa hakuwepo mtu aliyeweza kutawala nchi kama yeye. Taifa lote liliingia katika machafuko ya kisiasa, watu wenye tamaa ya utawala walipopata mamlaka juu ya nchi. Matokeo yake yalikuwa mfululizo wa mauaji, mapinduzi na mabadiliko ya serikali yaliyogeuza taifa imara kuwa dhaifu (2Fal 15:8-26). Baada ya muda mfupi Waashuri walianza kuonyesha hamu ya kuingiza Israeli katika ufalme wao ulioongezeka upesi. Wafalme mbalimbali wa Israeli walipobadili badili siasa yao ya kupenda au kuchukia Uashuru, Waashuri walizidi kujiingiza katika mambo ya Israeli (2Fal 15:19-29; 17:3-4). Hatimaye, katika mwaka wa 722 k.K., Waashuri waliteka Israeli na kuwapeleka watu wake kifungoni (2Fal 17:5-6). Hali ya siasa katika Yuda kwa muda fulani ilikuwa imara kuliko ile ya Israeli. Hayo yalikuwa hivyo kwa sababu Yothamu, mwana wa Uzia, aliendelea na siasa ya baba yake (2Fal 15:32-36). Lakini mfalme aliyefuata, yaani Ahazi, alikuwa na utawala wa taabu kabisa. Alikuwa dhaifu kwa upande wa siasa, akipeleka Yuda katika ushirika na Uashuru, na kwa mambo ya mwungano huo nusura uhuru wa Yuda uishe. Kwa upande wa dini hakufaa kabisa (2Fal 16:1-20). Mfalme aliyefuata, yaani Hezekia, alikuwa na shida sana kurekebisha uhuru wa Yuda na kuleta marekebisho ya kidini (2Fal 18:1-19:37). (Kwa habari zaidi kuhusu utawala wa Yothamu, Ahazi na Hezekia, taz. maelezo ya mazingira ya kitabu cha Mika, katika kipengele cha 'Matukio ya siasa'.) MUHTASARI 1:1-3:5 Maisha ya kifamilia ya Hosea na mafundisho yake 4:1-8:14 Kuharibika kwa maadili katika Israeli 9:1-13:16 Adhabu ya Israeli 14:1-9 Upendo wa Mungu wa kusamehe