Kitabu cha Nabii Danieli MAZINGIRA Kitabu cha Danieli kilipoandikwa, Wayahudi walikuwa katika kifungo cha Babeli. Katika wakati huo sehemu ya mwisho wa historia ya Israeli katika Agano la Kale ilianzishwa, na sehemu hiyo ya historia ilielekea katika wakati mpya ambao chanzo chake kilikuwa kuja kwake Yesu Kristo. Kutokana na Agano Jipya ni wazi kwamba kitabu cha Danieli kilikuwa na ushawishi mkubwa kwa vizazi vya baadaye. Jina ambalo Bwana Yesu mara nyingi alilitumia kama jina lake mwenyewe, yaani Mwana wa Adamu, lilitoka katika maono ya Danieli kuhusu mfalme wa ulimwengu wote aliyetumwa na Mungu (Dan 7:13-14; Mk 2:28; 14:62). Bwana Yesu alitaja maono ya Danieli katika maonyo yake kwa Wayahudi kuhusu nyakati za dhiki zilizowakabili (Mt 24:15), na Yohana katika kitabu cha Ufunuo alitaja maono ambamo mambo mengi yanatokana na kitabu cha Danieli (ling.Dan 2; 7 na 8 na Ufu 11; 12; 13 na 17). Mwandishi wa waraka kwa Waebrania anamtaja nabii Danieli kama mtu mwenye imani thabiti (Ebr 11:33). Mwendo mrefu wa Danieli Danieli alikuwa mmojawao wa wenyeji wa kwanza wa Yerusalemu waliopelekwa kifungoni Babeli wakati nchi ya Yuda ilipoanguka kuwa chini ya mamlaka ya Wababeli mwaka wa 605 k.K. Wakati huo ulikuwa mwaka wa nne wa utawala wa Yehoyakimu kadiri ya hesabu ya Yuda, lakini mwaka wa tatu kadiri ya hesabu ya Wababeli. Ilikuwa karibu na mwisho wa ufalme wa Yuda (2Fal 24:1a; Yer 25:1; Dan 1:1-6). (Kwahabari zaidi kuhusu historia ya wakati ule, taz. maelezo ya utangulizi wa kitabu cha Ezekieli.) Wakati wa kupelekwa kwake Babeli, Danieli alikuwa hajapata umri wa miaka 20. Alikuwa mmojawao wa kundi teule la vijana wenye akili na elimu ambao Wababeli waliwachagua kutoka nyumba na familia za kifalme na za hali ya juu huko Yerusalemu. Wababeli walikuwa wamefanya hivyo kwa makusudi ya kuwafundisha vijana wale, ili wawe maafisa katika makao ya mfalme wa Babeli (Dan 1:4). Katika muda wote wa njia yake ndefu, Danieli alishika baadhi ya madaraka ya juu kabisa katika serikali ya Babeli. Aliishi kupita wakati wa ufalme wa Babeli, naye alikuwa bado yu hai hata mwaka wa tatu wa mfalme wa Uajemi, Koreshi, aliyepindua ufalme wa Babeli mwaka wa 539 k.K. (Dan 10:1). Kwa hiyo aliishi hata kuwaona wafungwa wa kwanza wa Yuda wakirudi Yerusalemu na kujenga taifa lao upya (Ezra 1:1-4). Kitabu kwa ajili ya nyakati Mambo ya Kiyahudi yaliingiliwa sana na mabadiliko na matatizo yaliyotokea katika wakati wote unaoguswa na kitabu cha Danieli. Lakini watu wa Mungu walitiwa moyo wasije wakaacha kumtumaini Yeye. Jambo mojawapo lililo kuu katika kitabu cha Danieli ni mamlaka makuu ya Mungu. Kitabu chake kinaonyesha kwamba Mungu anatawala mambo ya wanadamu, yakiwa ni mambo ya maisha ya kila siku ya watu wake au mambo makuu kuhusu kuinuka na kuanguka kwa mataifa. Katika nusu ya kwanza ya kitabu, habari mbalimbali za Danieli na marafiki zake ziliandikwa zinazoonyesha utawala na utunzaji mkuu wa Mungu katika maisha ya watu walio waaminifu kwake. Katika nusu ya pili ya kitabu, kwa njia ya mfululizo wa maono ya ajabu, inaonyeshwa jinsi ambavyo Mungu angeendelea na utawala wake katika mambo ya watu wake wakati wa matukio makuu ya wakati wa usoni. Mafunuo yale yalihusu zaidi wakati mrefu wa machafuko na matatizo yaliyofuata baada ya enzi ya Waajemi. Kilele cha mambo hayo kilionekana katika matukio ya wakati wa Agano Jipya. Waandishi wa Agano Jipya, kwa upande wao tena, walichukua sehemu mbalimbali za mafunuo yale ya Danieli na kuyaunganisha na matukio makuu yatakayofuatana na kurudi kwake Yesu Kristo na mwisho kabisa wa dahari. Baadhi ya alama kuu za kitabu hiki Kutokana na kipawa chake cha kuelewa na kufundisha mapenzi ya Mungu, tangu wakati wa Agano Jipya Danieli anatambuliwa kuwa nabii (Mt 24:15). Haikuwa hivyo katika Agano la Kale. Wayahudi waliopanga vitabu katika kanuni ya vitabu vya Biblia ya Kiebrania (sawa sawa na Agano letu la Kale), hawakumtambua Danieli kuwa nabii. Hawakuingiza kitabu chake katika mpango wa vitabu vya manabii, bali walikiweka katika utaratibu wa vitabu vingine, yaani karibu na vitabu vya Esta, Ezra na Nehemia. Labda walifanya hivyo kwa sababu walimwona Danieli kuwa mkuu wa serikali katika makao ya mfalme wa Babeli kuliko kuwa mhubiri aliyetangaza Neno la Mungu kwa watu wake. Hata hivyo, Danieli alikuwa nabii ambaye kwa njia yake Mungu alidhihirisha makusudi yake, naye kwa kawaida alifanya hivyo kwa njia ya kumpa maono. Matokeo yake, kitabu cha Danieli kina alama nyingi za aina ile ya vitabu vinavyoitwa vya ufunuo wa mwisho (Kiyunani: apokalupto, maana yake 'kudhihirisha au kufunua'). Labda tungeweza kusema kwamba kitabu cha Danieli ni Ufunuo wa Agano la Kale. Katika maandiko ya mafunuo ya mwisho, maono yake mara nyingi yanashangaza au yanapita mifano ya ulimwengu wa kawaida, yakiwa na mifano ya kutisha ambayo mara nyingine ina wanyama wakali na hesabu za siri. Maono yanatolewa na Mungu, yanatafsiriwa na malaika, na kwa kawaida yanahusu matatizo makubwa ambayo Mungu na watu wake wanatokea kuwa washindi wake. Ingawa maana kuu ya maono inaweza kuwa wazi, mambo ya kinaganaga yanaweza kuonekana kuwa magumu. Kwa kutafuta kuelewa maono kama hayo, msomaji wa siku hizi hana budi kukumbuka kwamba, maelezo ya aina yo yote ya maono hayo hayakosi kuwa na sehemu fulani isiyoeleweka mpaka mwisho wake. MUHTASARI 1:1-6:28 Habari zinazomhusu Danieli na marafiki zake 7:1-12:13 Maono ya Danieli