40:1-48:35 WAKATI MPYA Katika sehemu hii ya mwisho wa kitabu chake, Ezekieli anaongeza maelezo katika mfano aliokwisha toa kuhusu matengenezo ya Israeli katika nchi yao na wakati bora na wa baraka kuu utakaofuata. Amekwisha eleza kirefu habari za kurudi katika nchi ya ahadi, na sasa anashugulika na hekalu na jiji takatifu. Ingawa baraka zilizoonyeshwa na Ezekieli zilikusudiwa kwa Israeli baada ya matengenezo yake, taifa hilo, baada ya kurudi katika nchi yake, lilikosa baraka hizo, watu wake walipomwacha Mungu kama walivyomwacha siku za awali. Lakini walikuwepo watu wachache walioendelea kuwa waaminifu kwa Mungu, na yalikuwa mabaki ya waaminifu hao wa Israeli ya kale waliokuwa kiini au chanzo cha watu wapya wa Mungu, yaani Kanisa la Kristo. Yerusalemu mpya ni ushirika wa kiroho wa watu wa mataifa yote ambao 'wamezaliwa kutoka juu' (Gal 3:26-29; 4:26-28). Ushirika huo mpya unaweza kujifunza kutokana na mafundisho ya Ezekieli sawa sawa na watu wa siku za Ezekieli walivyoweza kujifunza. Lakini hata ushirika huo mpya labda kwa wakati huo haujaweza kupata baraka zote zinazoonyeshwa na Ezekieli. Inaonekana kama maono ya Ezekieli yanaona mbele zaidi, yaani yanaonyesha wakati ambapo ufalme wa Yesu1 Kristo utaimarishwa katika ukamilifu wa utukufu wake. Matazamio makuu ya watu wa Mungu ni wakati mpya utakaokuja Mungu atakapoishi daima katikati ya watu wake aliowaokoa kwa kanuni ya maisha ambayo haijaonekana wakati wo wote. Mifano na lugha Mungu alipodhihirisha baadhi ya alama kuu za maisha katika ufalme wake wa milele, alitumia maneno na mifano ambayo watu wa siku za Ezekieli waliweza kuelewa. Kwa kuwa matumaini ya wakati ule ya watu wale yalikuwa kurudi katika nchi yao na kuijenga upya pamoja na hekalu lake, Mungu alitumia matumaini ya wakati huo kwa kuwafundisha makusudi yake makuu. Matengenezo ya Israeli yalikuwa kama kivuli cha mfano tu wa mambo makubwa zaidi ya wakati wa usoni. Ezekieli alikuwa kuhani naye alielewa vizuri sana maisha bora ya watu wa Mungu yanayohusu kanuni bora za dini yao. Aliona hekalu ambamo Mungu aliishi kati ya watu wake, akiabudiwa nao katika kanuni za dini zilizokamilika katika kila hali (taz.43:10-12). Aliona taifa ambalo maisha yake bora yaliwezekana kwa njia moja tu, yaani kwa sababu kila jambo lilipangwa kwa mpango safi katika eneo lote la makao ya Mungu (taz.48:8,20,35). Kama vile manabii wengine, Ezekieli alitafuta sana ukweli na uhalisi wa kiroho kuliko mambo ya kidunia. Lakini alipaswa kutumia mifano ya vitu vya kidunia vinavyoonekana kwa kusudi la kueleza mambo ya kiroho, kwa sababu vitu vya dunia vilikuwa vya pekee ambavyo yeye na wasikilizaji wake waliweza kuvielewa. Hivyo anaweza kufananishwa na nabii Yohana aliyeandika kitabu cha Ufunuo. Kama vile Ezekieli alivyotumia mfano wa hekalu, Yohana alitumia mfano wa jiji la Yerusalemu. Wote wawili walitaka sana kuwaeleza wasomaji wao habari za ubora wa maisha utakaopatikana kwa ukamilifu wake katika wakati ujao tu. Hekalu: nyua zake za nje na za ndani (40:1-47) Ezekieli alipopata maono kuhusu hekalu jipya, miaka 25 ilikuwa imepita tangu alipopelekwa Babeli, na miaka 14 tangu Yerusalemu ilipobomolewa. Siku moja alipata maono ambapo yeye mwenyewe alijisikia kuwa katika nchi ya Israeli, na kutoka katika mlima mrefu aliona hekalu kubwa sana. Hi kuelewa ukubwa wake na vitu mbalimbali, alisaidiwa na mjumbe wa mbinguni aliyekuwa na uzi wa kitani kwa ajili ya kupima urefu mkubwa na mwanzi (ambao urefu wake ulizidi meta tatu kidogo), kwa ajili ya kupima sehemu fupi. Uhalisi wa vipimo bila shaka ulidokeza kwamba Mungu anafanya kila jambo kwa uhalisi na ukamilifu (40:1-4). Kitu cha kwanza ambacho Ezekieli alikiona kilikuwa ukuta uliozunguka eneo lote la hekalu (5). Eneo lile lilikuwa la mraba nalo liliingiliwa kwa njia ya lango kubwa lililofanana na pango katika ukuta wa upande wa mashariki. Kwa kuingia katika lango hilo, mtu alipaswa kukwea ngazi fulani, apite kizingiti kikubwa (6), kisha apite njia ya katikati (ambayo katika kila upande wake kulikuwa na vyumba vidogo vitatu kwa ajili ya walinzi wa hekalu). Halafu apite kizingiti kingine, kisha apite katika ukumbi na kuingia ua wa nje ya hekalu (7-9). Vipimo vya vyumba mbalimbali vya njia ya lango vinatajwa (10-15). Vyumba vyote vilikuwa na madirisha madogo kwa ajili ya kuingizia nuru na hewa, na katika viimo vyake kulikuwa na nakshi za kuchongwa mitende (16). Katika upande wa ndani ya ukuta wa nje vyumba 30 vilijengwa (labda kwa kutumiwa na waabudu) ambavyo milango yake ilikuwa upande wa ua wa nje (17-19). Kulikuwa na malango katika upande wa kaskazini na kusini ya ukuta mkuu yaliyofanana na lango lile la upande wa mashariki lililoelezwa hapo juu (20-27). Ndani ya ua wa nje kulikuwa na ua mdogo wa ndani. Ua ule wa ndani ulikuwa sakafu iliyoinuliwa kuliko ua wa nje (taz.40:18), nao uliweza kuingiliwa kutoka upande wa kusini, mashariki au wa kaskazini kwa njia ya kukwea ngazi nne na kupitia lango lililofanana na malango ya ukuta wa nje (28- 37). Ukumbi wa kila lango la kuingilia ua wa ndani ulikuwa na meza nane za kuchinjia wanyama wa sadaka (38-41), na meza nne kwa ajili ya kutunzia vifaa mbalimbali vilivyotumiwa kwa ajili ya kutolea sadaka (42-43). Upande wa ndani ya ukuta uliozunguka ua wa ndani kulikuwa na vyumba kwa ajili ya makuhani. Vyumba vya upande wa kaskazini vilikuwa kwa ajili ya makuhani wale waliohudumia hekaluni kila siku, vyumba vya upande wa kusini kwa ajili ya makuhani walioshughulika na sadaka. Madhabahu ya sadaka za kuteketezwa ilikuwa katikati ya ua wa ndani (44-47). Hekalu maalumu (40:48-41:26) Njia iliyoingia katika hekalu maalumu kutoka ua wa ndani ilipanda tena ngazi au madaraja upande wa magharibi ya ua, katikati ya nguzo mbili zilizokuwa juu ya ngazi hizo na kuingia katika ukumbi au chumba cha kuingilia (48-49). Kutoka ukumbini kulikuwa na mlango wa kuingilia mahali pakubwa pa hekalu, yaani maskani au Patakatifu, na kutoka Patakatifu pa nje mlango mwingine mwembamba uliingia katika Patakatifu pa Patakatifu (au Patakatifu pa ndani) (41:1-4). Katika upande wa nje wa kila ubavu na nyuma ya hekalu maalumu kulikuwa na ghorofa tatu za vyumba vilivyotumiwa kama ghala, labda kwa ajili ya kutunzia vitu vilivyotolewa na watu kuwa zaka, yaani sehemu ya kumi ya mapato. Kuta za kila ubavu na nyuma ya jengo kuu zilipunguzwa unene wake katika kila ghorofa. Kwa njia hii 'ngazi' au kingo zilipatikana katika kuta kuu, ambamo maboriti ya dari za katikati na juu yaliweza kulalia (5-7). Milango miwili ilikuwa katika ghorofa ya chini ya vyumba vile vya ghala, mmoja upande wa kaskazini na mmoja upande wa kusini. Ilifunguliwa katika sakafu iliyoinuliwa ambayo juu yake hekalu limejengwa (8-11). Ubavuni na nyuma katika sakafu hiyo kulikuwa na eneo lililozungukwa na ukuta nalo liliitwa ua wa hekalu. Upande wa nyuma kabisa ya ua huo, kukabiliana na ukuta wa nje wa magharibi, kulikuwa na jengo lingine, labda ghala nyingine tena (12). Vipimo mbalimbali vya hekalu na maeneo yake ya karibu sana vinaonyesha uhalisi na ukamilifu wa mambo yote. Kila kitu kilibuniwa kwa uangalifu, pasipo nafasi ya matokeo ya bahati tu (13-15a). Madirisha yaliwekwa sehemu za juu katika kuta za ubavuni mwa hekalu kama vile kwa kufunguka juu ya paa ya vyumba vya ghorofa iliyoegama katika kuta za ndani ya hekalu. Katika kuta zile za ndani, kuanzia chini, kupita mlango mkuu hadi upande wa chini ya madirisha yale ya juu, mapambo mengi ya miti iliyochongwa vizuri yaliwekwa (15b-2O). Milango ya mahali Patakatifu na Patakatifu pa Patakatifu ilikuwa nusu mbili mbili, kila mmoja uliweza kukujwa. Mbele ya milango iliyoingia katika Patakatifu pa Patakatifu kulikuwa na chombo ambacho kwa sehemu kilionekana kama madhabahu na kwa sehemu kama meza (21-26). Vyumba vya makuhani (42:1-20) Hapa Ezekieli anatoa maelezo mengine kuhusu vyumba vya makuhani vilivyopo katika ua wa ndani (taz.40:44-47). Kulikuwa na majengo mawili kwa ajili ya makuhani, moja upande wa kaskazini mwa hekalu na moja upande wa kusini. Kwanza jengo la upande wa kaskazini linaelezwa. Lilikwenda juu kiasi cha ghorofa tatu, pia liligawanywa katikati kwa ajili ya njia ya kupitia watu. Upande wake wa ua wa hekalu kwa njia hiyo kulikuwa na ghorofa tatu zenye chumba kimoja kirefu na chembamba kila ghorofa. Upande wake wa nje kulikuwa na ghorofa tatu za vyumba vya ghala. Katika ghorofa ya pili kulikuwa na roshani au baraza kila upande, na ghorofa ya tatu ilikuwa na baraza pana zaidi. Maana yake ilikuwa kwamba, vyumba vya kila ghorofa vilikuwa vyembamba zaidi kuliko vile vya ghorofa ya chini yake, na hivyo jengo lenyewe lilionekana kama ngazi (42:1-6). Eneo la vyumba vilivyokabiliana na ua wa nje katika njia yake lilichukua nusu tu ya eneo la vyumba vya upande wa hekalu maalumu. Nusu ya pili ya eneo la kukabili ua wa nje ilitenganishwa na njia hiyo kwa ukuta uliokuwa wazi katika mwisho wake, na hivyo eneo la namna ya paa juu ya njia ya kuingia ghorofa ya chini ilipatikana (7-9). Jengo la makuhani lililokuwa upande wa kusini mwa hekalu maalumu lilikuwa na muundo ule ule wa lile la kaskazini (10-12). Vyumba mbalimbali vya majengo yale vilitumiwa na makuhani kwa ajili ya kubadili nguo zao au kwa kulia chakula cha sadaka za watu (13-14). Kisha mjumbe wa mbinguni aliyemwongoza na kumwonyesha Ezekieli mambo yote aliondoka katika ua wa ndani, akapita ua wa nje kupitia lango la ukuta wa nje na kuondoka kabisa katika eneo la hekalu. Alipima eneo lote la hekalu akaona kwamba eneo lote lilikuwa mraba kamili. Ukuta mrefu uliozunguka eneo lote lilikuwa kwa ajili ya kulinda vitu vitakatifu vya Mungu visije vikatiwa unajisi na mambo ya maisha ya kila siku ya nje (15-20). Mungu anarudi hekaluni (43:1-12) Kabla ya miaka 19, Ezekieli alikuwa amepata maono. Alikuwa amemwona Mungu akiondoka hekaluni na Yerusalemu akatulia katika mlima wa karibu, kisha akaangamiza jiji na wenyeji wake (taz.8:l; 9:1-11; 10:19; 11:22-24). Wakati huo, baada ya kumalizika hekalu jipya, anamwona Mungu akirudi kwa njia ile ile, akiingia katika hekalu lake na kulijaza utukufu wake (43:1-5). Kisha Mungu alimwambia Ezekieli kwamba hekalu hilo lilikuwa makao yake ya hapa duniani. Lilikuwa takatifu na watu wake wajihadhari wasije wakalitia unajisi kama wazee wao walivyochafua hekalu la kwanza kwa njia ya kuabudu sanamu za miungu na kuwazika wafalme wao huko (6-9). Ezekieli aliamriwa kuwaeleza wafungwa habari za hekalu hilo na kuwafundisha kanuni zake. Makusudi yake yalikuwa waelewe zaidi utakatifu wa Mungu, ili waweze kuishi katika utii na kuepukana na makosa (10-12). Madhabahu ya kutolea sadaka (43:13-27) Katikati ya ua wa ndani kulikuwa na madhabahu ya sadaka za kuteketezwa. Kwa maumbile yake ilionekana kama masanduku makubwa matatu ya mraba yaliyopangwa moja juu ya lingine, lililo dogo likiwa juu na kubwa likiwa chini, madhabahu hiyo ikionekana kama ina ngazi za kuizunguka kila upande. Muundo wote wa madhabahu ulikuwa juu ya msingi uliojengwa katika sakafu. Ilikuwa kubwa sana, hata ilipaswa kuwa na ngazi pembeni, ili makuhani waweze kukwea na kufikia sehemu ya juu ambapo sadaka zenyewe zilitolewa (13-17). Madhabahu ilipaswa kuwekwa wakfu kwa huduma takatifu ya Mungu kwa njia ya sherehe iliyokuwa na sadaka za dhambi (kwa kudokeza utakaso) na sadaka za kuteketezwa (kwa kudokeza kujitoa kwa Mungu). Makuhani wale tu waliokuwa wa mbari ya Sadoki waliruhusiwa kutekeleza kazi yenyewe ya kutoa sadaka madhabahuni (18-24). Sherehe ya kuweka madhabahu wakfu ilitakiwa ichukue muda wa juma moja. Baada ya hayo, madhabahu iliweza kutumiwa kwa kutolea sadaka za kawaida (25-27). Huduma ya hekaluni (44:1-31) Utukufu wa Mungu ulikuwa umeingia hekaluni kupitia lango la mashariki la ua wa nje, kwa hiyo hakuna mwanadamu aliyeonekana kuwa amestahili kupitia lango hilo. Hivyo lango hilo lilifungwa siku zote bila kufunguliwa (44:1-2). Lakini mfalme (Yesu Kristo), baada ya kuingia lango la kaskazini au la kusini, aliweza kula chakula cha sadaka yake katika ukumbi uliokuwa karibu na lango la mashariki (3). Uwepo wa utukufu wa Mungu hekaluni ulikuwa na maana kwamba kulikuwa na kizuizi kwa mtu ye yote ambaye labda angeweza kuingiza desturi za kipagani katika eneo hilo (4-5). Kwa hiyo watu wa agano la Mungu tu waliruhusiwa kuingia hekaluni. Wageni hawakuruhusiwa hata kuajiriwa na watumishi wa hekalu (6-9; taz.Yos 9:23, 27; 2Fal 11:4-8). Huduma za kila siku za hekaluni, kama vile kulinda malango na kusaidia kuandaa mambo ya sadaka, zilipaswa kutimizwa na Walawi pamoja na makuhani wale wasiokuwa wa ukoo au mbari ya Sadoki. Makuhani hao wasiokuwa wa Sadoki walitengwa na kazi za madaraka ya juu zaidi kwa sababu ya ibada zao za sanamu hapo awali (10-14). Makuhani wa mbari ya Sadoki, waliokuwa na madaraka kamili ya kikuhani, walipaswa kutimiza sheria zote kuhusu makuhani. Walikatazwa kuruhusu kitu cho chote kilichounganika na Patakatifu kitiliwe unajisi kwa kuguswa na watu au kitu kutoka ulimwengu mchafu wa nje. Kizuizi hiki kilihusu hata nguo walizovaa wakati wa huduma yao ndani ya hekalu (15-19; taz.42:14). Katika kuonekana kwao, tabia yao, maisha yao ya kifamilia, usafi na unyofu walipaswa kuwa vielelezo kwa watu kuhusu maana ya kweli ya utakatifu (20-24). Iwapo kwa sababu yo yote walipata kuwa najisi kidini, walipaswa kutimiza sherehe zote za kutakaswa upya (25-27). Kama ilivyokuwa siku za awali, makuhani hawakuruhusiwa kuwa na urithi maalumu wa nchi. Mapato yao na riziki yao ya chakula vilitakiwa vitokane na vitu mbalimbali vilivyotolewa na watu (28- 31). Eneo la ardhi kwa makuhani, Walawi na mfalme (45:1-12) Kugawanya nchi kama alivyofanya Ezekieli, kulidokeza jambo la maana sana. Kufuatana na kanuni iliyotumiwa katika kutoa zaka na malimbuko kwa Mungu, kabla ya yote, sehemu ya nchi iliwekwa kando kuwa sehemu ya Mungu. Kwa njia hii ilikubaliwa kwamba nchi yote kwa kweli ni mali yake. Katika sehemu hiyo hekalu lilikuwemo, nalo lilizungukwa na eneo wazi lisilo mali ya mtu ye yote kwa kusisitiza kwamba vitu vitakatifu vya Mungu vilitengwa na vitu vya kawaida vya maisha ya kila siku vya nje vilivyokuwa najisi. Makuhani na Walawi walipewa nafasi ya kwanza katika mipango ya makazi mapya katika nchi, yaani wao walitakiwa wawe karibu na hekalu. Sehemu ya nchi ambayo hekalu lilikuwa ndani yake, walipewa makuhani, na eneo la ukubwa ule ule lililounganika na eneo hilo walipewa Walawi (45:1-5). Katika upande wa pili wa eneo la makuhani kulikuwa na eneo kwa ajili ya jiji (6). Eneo lililoelekea Bahari ya Kati upande wa magharibi na lililoelekea Mto Yordani upande wa mashariki lilikuwa la mfalme. Mfalme alipaswa kuridhika na sehemu kubwa aliyopewa wala asijichukulie ardhi ya watu wa kawaida sehemu nyingine nchini (7-8). Ezekieli akiwa na maelezo kuhusu kujipatia faida kwa njia ya kuwanyanyasa watu wengine, anaongeza maonyo mengine. Watawala wanakatazwa kutumia hali yao ya cheo au mamlaka ya juu kwa faida yao binafsi, wala wafanya biashara hawana ruhusa kuwadanganya wateja wao. Vipimo vyote vinapaswa kuwa sahihi (9-12). Sadaka na sikukuu (45:13-46:15) Watu wote walikuwa na sehemu yao katika mpango wa kutoa sadaka kwa ajili ya sikukuu za kitaifa na za dini. Sadaka zilikusanywa na mfalme ambaye baadaye alizitoa kwa niaba ya watu wake (13-17). Katika mwanzo na mwisho wa juma la kwanza la mwaka mpya, sadaka zilitolewa kwa ajili ya kutakasa hekalu (18-20). Sikukuu mbili za maana zaidi zilizotakiwa kusherehekewa hekaluni zilikuwa sikukuu ya Pasaka na Mkate Usiotiwa Chachu katika mwanzo wa mwaka (21-24), na sikukuu ya Vibanda katikati ya mwaka (25; taz-.Law 23:34-36). Bahari ya Kati Lango la mashariki kutoka ua wa nje kwenda katika ua wa ndani lilifungwa kila siku isipokuwa siku ya Sabato ya kila juma na kila siku ya mwezi mpya, ambapo mfalme alitoa sadaka kwa niaba ya taifa. Katika siku hizo mfalme, yaani mfalme peke yake, aliweza kuingia katika ukumbi wa lango hilo na kuwatazama makuhani wakitimiza huduma ya kutoa sadaka mle ndani, lakini hakuruhusiwa kupita katika lango hilo (46:1-2; taz.mst.8. Makuhani na Walawi tu waliruhusiwa kuwa katika ua wa ndani). Watu wa kawaida walipaswa kukutana katika ua wa nje mbele ya lango (3). Sadaka za kila juma na za kila mwezi zilipaswa kutolewa kadiri ya sheria iliyokwisha wekwa (4-8). Kulikuwa na kanuni maalumu kwa ajili ya kutunza utaratibu safi watu walipokutana kwa wingi sana katika ua wa nje wakati wa sikukuu za kila mwaka. Baada ya kupita katika lango moja, watu walipaswa kusogea kuelekea sehemu moja tu na kuondoka katika lango la upande mwingine (9-10). Mfalme alipotoa sadaka ya hiari yake, aliweza kutazama sherehe yake ikiendeshwa na makuhani, yeye mwenyewe akisimama karibu na lango la mashariki, kama ilivyokwisha elezwa (11-12). Licha ya sadaka za taifa za kila juma na mwezi na za sikukuu za mwaka, kulikuwa na sadaka ya kila siku (13- 15). Maelezo mengine kuhusu ardhi na hekalu (46:16-24) Iwapo mfalme aliweka alama sehemu ya eneo la ardhi yake na kumpa mmojawao wa wanawe, eneo lile liliendelea kuwa mali ya mwana huyo. Lakini kama mfalme alitoa zawadi ya namna hiyo kwa mmojawao wa watumishi wake, eneo lile lilipaswa kurudishwa kwa mfalme mwaka wa Yubile. (Kuhusu sheria ya mwaka wa Yubile, taz.Law 25:8-34). Kwa njia hii ilihakikishwa kwamba eneo la mfalme liliendelea kuwa mali ya ukoo wake, pia mfalme hakujaribiwa kujitwalia ardhi ya watu wengine, ili kufidia eneo lile alilotoa zawadi (16-18). Akirudia maelezo yake kuhusu hekalu, Ezekieli anaongeza kusema kwamba kulikuwepo na majiko katika ua wa ndani uliozungushwa na ukuta. Majiko hayo yaliwekwa ili makuhani waliotoa sadaka (yaani makuhani wa mbari ya Sadoki; taz.44:15-16) waweze kupika sehemu zao za chakula walichopewa kutokana na sadaka takatifu, bila ya kuwa na haja ya kwenda nje ya eneo takatifu (19- 20). Pia kulikuwa na majiko katika pembe nne za ua wa nje, ambapo watumishi wa hekalu (yaani Walawi na makuhani wasio wa mbari ya Sadoki; taz.40:10-14) walipika sehemu zao za chakula cha sadaka zilizokuwa za watu wa kawaida (21-24). Mto wa uzima (47:1-12) Katika kumaliza maelezo yake kuhusu hekalu na sherehe zake, Ezekieli anaonyesha kilele cha ajabu cha maono yake. Aliona maji yakitiririka kutoka chini ya lango la hekalu yaliyopita katika ua wa nje na chini ya ukuta wa nje (karibu sana na lango la mashariki upande wa kusini) (47:1-2). Kijito kile kilielekea mashariki, kikiongezeka upesi kuwa mto mpana na baada ya kuendelea kidogo, ulikuwa mto mkubwa sana (3-6a). Jambo la kwanza ambalo Ezekieli aliligundua katika mto huo wa ajabu lilikuwa miti mingi iliyositawi kila upande wa ukingo wake (6b-7). Kisha alielewa kwamba mto ulielekea mashariki na kuingia katika Bahari ya Chumvi, na katika njia yake yote humo baharini ulisababisha maisha mapya ndani ya maji ambayo mpaka wakati huo yalikuwa machungu na bila uhai (ingawa sehemu fulani za chumvi ziliachwa kwa ajili ya matumizi ya watu). Miti iliyoota ukingoni, licha ya kutoa matunda yenye chakula bora kila wakati, pia ilikuwa na dawa kwa ajili ya wagonjwa. Mto ulikuwa mfano wa baraka ya uponyaji, chakula bora na uzima tele uliotoka katika makao ya Mungu na kuwafikia watu wake (8- 12; taz.Ufu 22:1-2). Mipaka ya nchi (47:13-23) Nchi ambayo taifa la Israeli baada ya matengenezo yake liliweza kuimiliki ilipaswa kugawanywa katika maeneo sawa kwa makabila 12. Kabila la Lawi halikuwa na urithi wa ardhi, lakini Yusufu, aliyepokea baraka za mzaliwa wa kwanza, alipata sehemu mbili, yaani kwa Efraimu na Manase (13-14; taz.Mwa 48:5; lNya5:l). Mipaka mikuu ya nchi yote inaelezwa. Mpaka wa kaskazini ulikwenda kutoka sehemu fulani karibu na Tiro ya pwani ya Bahari ya Kati hadi eneo la chemchemi ya Mto Yordani. Mpaka wa mashariki ulifuata Mto Yordani hadi kusini, mwisho wa Bahari ya Chumvi. Mpaka wa kusini ulikwenda kutoka huko hadi Mto wa Misri ambapo uliufuata mto huo hadi pwani ya Bahari ya Kati. Mpaka wa magharibi ulifuata pwani ya Bahari ya Kati (15-20). Kuhusu ugawaji wa nchi, wageni walioishi miongoni mwa Waisraeli, walikuwa na haki sawa na wao. Walipaswa kupewa mashamba yao katika maeneo ya kabila lile ambamo waliishi (21-23). Ugawaji wa nchi (48:1-29) Nchi iliyokuwa kaskazini mwa eneo lililopangwa kwa njia ya pekee kuwa katikati (taz. 45:1-8), iligawanyika katika maeneo saba yaliyokuwa sawa kwa njia ya kupiga mistari iliyonyooka kutoka Bahari ya Kati hadi mpaka wa mashariki. Ingawa hali ya nchi yenye milima, mabonde na mito ingefanya ugawaji wa namna hiyo usiwezekane kabisa, ugawaji huo ulikuwa na maana yake. Ulidokeza kwamba kulikuwa na usawa fulani katika makabila yote (kwa sababu maeneo yao yote yalikuwa na ukubwa sawa; taz.47:14), lakini kulikuwa na tofauti katika madaraka, kwa sababu makabila yenye maana zaidi yalikuwa karibu zaidi na Yerusalemu na hekalu (48:1-7). Katikati ya nchi kulikuwa na eneo maalumu kwa ajili ya hekalu, makuhani, Walawi, jiji na mfalme (8; taz.maelezo ya 45:1-8). Sehemu ya katikati ya eneo hilo ilikuwa na uwanja wa hekalu. Sehemu hiyo walipewa makuhani (9-12). Sehemu iliyopakana na eneo hilo upande wa kaskazini ilikuwa ya Walawi (13-14). Sehemu iliyopakana na eneo la makuhani upande wa kusini ilikuwa kwa ajili ya jiji kuu na wenyeji wake. Jiji maalumu lilijengwa kwa mraba uliozungukwa na mstari wa nchi wazi. Eneo lake lilikaliwa na watu wa makabila yote 12. Upande wa magharibi na mashariki ya jiji kulikuwa na maeneo ya mashamba ambayo nafaka zake zilifaa kuwa riziki ya wenyeji wa Yerusalemu (15-19). Sehemu yote iliyokuwa kwa ajili ya makuhani, Walawi, na jiji kuu la taifa ilikuwa ya mchoro wa mraba (20). Kila upande wa mraba huo wa katikati kulikuwa na eneo la mfalme (21-22; taz.45:7-8). Upande wa kusini mwa sehemu ile ya katikati kulikuwa na maeneo ya makabila matano yaliyobaki, yakigawanywa tena kwa mistari sawa ya ardhi. Hapo vile vile makabila ya maana zaidi yalikuwa karibu zaidi na Yerusalemu na hekalu (23-29). Malango ya Yerusalemu (48:30-35) Ezekieli anapomaliza kueleza maono yake, anasema tena habari za Yerusalemu. Anasisitiza kwamba jiji Una malango 12, matatu kila upande, yakiwa mfano wa makabila yote ya watu wa Mungu (30-34; taz.Ufu 21:12-14). Baada ya kuwarudisha watu wake katika nchi yao na kutengeneza upya maisha yao ya kiraia na ya kidini kadiri ya makusudi yake maalumu, wakati huo Mungu anakaa pamoja nao milele (35; taz.Ufu 21:23).