Kitabu cha Nabii Ezekieli MAZINGIRA Wakati wa Ezekieli ulikuwa wa mabadiliko makubwa katika maeneo ya Palestina. Ulikuwa wakati wa kuinuka kwa mamlaka ya Babeli, kubomolewa kwa Yerusalemu na kifungo cha watu wa Mungu katika nchi ya kigeni. Matukio hayo yote yaligusa maisha ya Ezekieli, nayo yaliingiliana na kazi ambayo Mungu alimwitia ili aifanye. Kwa hiyo inafaa wasomaji wawe na ujuzi wa historia ya wakati ule, ili waweze kumfahamu mtu yule aliyeitwa Ezekieli, na kuelewa ujumbe aliotupatia katika kitabu chake. Nchi ya Yuda yashindwa na Wababeli Zaidi ya miaka 100 kabla ya wakati wa Ezekieli, Waashuri walikuwa wameshinda na kuharibu ufalme wa kaskazini wa Israeli na kutawanya watu wake katika nchi za kigeni. Siku za utoto wa Ezekieli zilikuwa katika wakati wa mwisho wa ufalme huo wa Uashuru. Katika mwaka wa 612 k.K. Waashuri walishindwa na Wababeli walioendelea na kushambulia na kuwashinda Wamisri katika vita vikuu vya Karkemishi mwaka wa 605 k.K. (Karkemishi au Charchemish ilikuwa karibu na Mto Frati). Baada ya ushindi huo, Wababeli walikuwa watawala wakuu wa nchi zote katika maeneo yale kutoka Misri hadi Babeli, pamoja na nchi ya Yuda (2Fal 24: la,7; Yer 46:2). (Ramani ya maeneo hayo iko katika maelezo ya kutangulia kitabu cha Yeremia. Kuhusu maelezo ya majina yaliyotumiwa kwa mataifa mbalimbali, tazama maelezo ya kutangulia kitabu cha Isaya.) Washindi Wababeli walimruhusu mfalme Yehoyakimu wa Yuda aendelee kutawala Yerusalemu, lakini walidai kodi nyingi kwa Wayuda. Pia walichukua kikundi cha vijana wenye akili na elimu kutoka ukoo wa mfalme na nyumba za watu wenye sifa wa Yerusalemu na kuwapeleka kifungoni Babeli. Mmojawao alikuwa Danieli (Dan 1:1-6). Baada ya kutii utawala wa Babeli kwa miaka michache, Wayuda waliasi (2Fal 24:1b). Wababeli hawakuchukua hatua dhidi ya Wayuda mara moja, bali walingoja mpaka wakati ulipowafaa. Halafu, katika mwaka wa 597 k.K., majeshi yao yalirudi na kushambulia Yerusalemu. Wakati huo mfalme Yehoyakimu asiyefaa alikufa, na Yehoyakini (au Yekonia au Konia) alikuwa mfalme alipokuwa na umri wa miaka 18 tu. Kisha, baada ya kutawala miezi mitatu tu, aliona kwamba haikuwezekana kujitetea dhidi ya Wababeli kwa muda mrefu akajisalimisha kwao. Watu wote wa taifa la Yuda waliokuwa na hali nzuri na heshima walipelekwa kifungoni Babeli, na miongoni mwao alikuwemo kijana aliyeitwa Ezekieli. Watu wale tu ambao Wababeli hawakuwataka waliachwa Yerusalemu, na juu yao Wababeli walimweka Sedekia, baba mdogo wa Yehoyakini, awe mfalme (2Fal 24:8-17). Baada ya watu wote wenye uwezo katika Yuda kupelekwa Babeli, serikali ya Sedekia ilikuwa na ukosefu mkubwa wa washauri wenye uzoefu. Wachache tu walikomaa katika mambo ya siasa au ya dini, nao walimshawishi mfalme dhaifu atafute msaada wa Misri ili waweze kuwaasi Wababeli. Nabii Yeremia daima alipinga siasa hiyo bila kuchoka, kwa sababu aliona wazi kwamba ingesababisha vitisho vya kuzingirwa na Wababeli ambao wangebomoa jiji. Aliwasihi Wayuda wakubali hali yao kuwa ni mapenzi ya Mungu nao wawatii Wababeli (2Fal 24:18-20; Yer 21:1-10; 27:12-22; 37:6-10). Sedekia alidharau ushauri wa Yeremia akawaasi Wababeli. Majeshi ya Nebukadreza, mfalme wao, yakarudi tena yakazingira Yerusalemu kivita kwa ukatili sana, na mwisho walibomoa jiji lile lililoasi. Huu ulikuwa mwisho wa Yerusalemu (mwaka wa 587 k.K.). Jiji lilibomolewa kabisa pamoja na hekalu lake, na wenyeji wake wengi zaidi walipelekwa kifungoni. Watu wa hali ya chini kabisa na maskini tu waliotawanyika nchini waliachwa (2Fal 25:1-12). Ezekieli akiwa Babeli Watu wengi waliopelekwa kifungoni Babeli mwaka wa 597 k.K., walitumaini kwamba baada ya muda mfupi wangerudi Yerusalemu. Ezekieli aliyekuwa mmojawao, bila shaka alishiriki matumaini hayo. Alikuwa kuhani kijana (Eze 1:3), na hivyo bila shaka alitazamia siku ambayo angeweza kuanza huduma yake katika hekalu la Yerusalemu. Lakini matumaini ya namna hiyo yaliharibika aliposikia habari za barua ya Yeremia kwa wafungwa iliyosema kwamba wangekuwepo Babeli maisha yao yote (Yer 29:1-10). Mungu alimwambia Ezekieli kwamba kazi yake ingekuwa ya unabii huko Babeli wala siyo ya ukuhani Yerusalemu. Ezekieli alianza huduma yake ya unabii miaka mitano baada ya kufika Babeli, naye aliendelea nayo kwa muda wa miaka 22 au zaidi (Eze 1:2; 29:17). Katika siku za kwanza za mahubiri yake, Ezekieli alilaumu dhambi za Yerusalemu na kutangaza kubomolewa kwa jiji hilo. Aliweka wazi kwamba mateso ya Wayuda ya wakati huo, ikiwa ni yale ya watu walioishi Yerusalemu au Babeli, ni hukumu ya haki kutoka kwa Mungu. Alionya kwamba watu waliobaki Yerusalemu wamekabiliwa na mateso makali zaidi, kwa sababu jiji lingebomolewa na hekalu lingeteketezwa kwa moto wakati ambapo Wababeli wangeshambulia jiji kwa mara ya tatu na mara ya mwisho (Eze 4:1-2: 5:12; 6:1-7; 7:5-9). Wasikilizaji wa Ezekieli hapo mwanzo walikataa ujumbe wake, wakidai kwamba unabii wake kuhusu kubomolewa kwa Yerusalemu ungehusu kizazi cha wakati ujao wala si kizazi chao (Eze 12:27-28). Baada ya miaka michache, habari zilipowapata wafungwa kwamba Yerusalemu ilianguka kadiri ya utabiri wa Ezekieli, watu walitambua kwamba yeye alikuwa nabii wa kweli aliyejua mawazo ya Mungu. Walianza kusikiliza mafundisho yake, ingawa watu wachache tu walibadili maisha yao kweli (Eze 33:21,30-33). Hata hivyo, Ezekieli alitiwa moyo kuendelea na kazi yake kuu ya kuwaandaa watu wa Mungu kiroho kwa ajili ya wakati mpya ambao Mungu aliwaahidi. Alitazamia siku ambayo watu wa Mungu, baada ya kusafishwa mioyo yao dhambi zao, wangemwabudu Mungu kwa kweli na kwa moyo na kumtumikia katika upendo na utii. Maisha ya kifungoni Watu wa Yuda walipopelekwa Babeli hawakufungwa katika magereza, bali waliwekwa mahali mbalimbali katika nchi na kulazimishwa kufanya kazi kwa serikali ya Babeli (Eze 3:15). Ingawa bila shaka walitawaliwa kwa ukali na wasimamizi wao wa Babeli, walikuwa na uhuru fulani wa kuishi maisha yao ya kifamilia na kijumuia katika makao yao kwa kadiri ya mapenzi yao (Yer. 29:4-7). Alama kuu za unabii wa Ezekieli Ingawa Ezekieli aliishi katika nchi ya kigeni bila nafasi ya kutoa huduma katika hekalu la Mungu, hakusahau mvuto wake katika maendeleo safi ya mipango ya dini ya Israeli. Alikuwa amejifunza huduma ya ukuhani, na kitabu chake kinaonyesha mawazo ya kuhani juu ya mambo yote yanayohusu hekalu, huduma yake na ibada yake. Uangalifu na umakini wa kuhani pia unaonekana katika desturi ya Ezekieli ya kutaja tarehe kamili katika kila ujumbe aliotoa. Kwa kawaida alitoa tarehe yake kadiri ya mwaka wa kifungo cha mfalme Yehoyakini (au Yekonia) ambao pia ulikuwa mwaka wa kifungo chake. MUHTASARI 1:1-3:27 Wito wa Ezekieli 4:1-7:27 Hukumu juu ya Yerusalemu 8:1-24:27 Dhambi za Yerusalemu 25:1-32:32 Hukumu juu ya mataifa ya kigeni 33:1-39:29 Kurudi katika nchi ya Israeli 40:1-48:35 Wakati mpya