Kitabu cha Maombolezo ya Yeremia MAZINGIRA Neno 'maombolezo' linadokeza maelezo ya huzuni, sikitiko au maumivu ya rohoni. Kitabu cha Biblia cha Maombolezo ni mkusanyo wa mashairi matano yanayoonyesha huzuni za mwandishi juu ya kuangukakwa Yerusalemu chini ya majeshi ya Babeli katika mwaka wa 587 k.K. na mateso ya watu yaliyotokana na maafa hayo. (Kwa maelezo zaidi kuhusu matukio ya wakati ule, tazama sehemu inayoitwa 'Mazingira ya Historia' katika maelezo yanayoangulia maelezo ya kitabu cha Yeremia.) Mtunzi na utunzi wake Ingawa watu wengi sana hufikiri kwamba Yeremia alikuwa mwandishi wa Maombolezo, kitabu chenyewe hakithibitishi jambo hili mahali po pote. Kwa hali yo yote, mwandishi wake aliishi Yerusalemu wakati ule wa kuzingirwa jiji kwa vita vikuu vya mwisho ambapo mwisho wake jiji lilitekwa na kubomolewa. Alishuhudia vitisho vya siku zile, naye aliona uchungu na ugumu wa maisha ya watu wale waliosalia katika Yuda. Ni wazi kwamba mwandishi wake alikuwa na uwezo wa utunzi naye aliona hali ya kiroho ya wakati wake. Mashairi yake yanasababisha mawazo ya huruma na upole moyoni mwa msomaji, lakini pia yanaonyesha imani thabiti ya mtunzi. Aliandika katika hali ya kukatisha tamaa, lakini hata hivyo alipeleka shida zake kwa Mungu. Kila shairi kati ya mashairi hayo matano ni fungu moja katika Biblia ya Kiswahili. Katika mipango ya mashairi yake, mwandishi alitofautisha sawa sawa kati ya hali ya kukatisha tamaa na matumaini. Shairi la katikati lililo na ay a 66, linashughulika na baadhi ya mambo ya kimsingi ya uhusiano baina ya mwanadamu na Mungu, kama vile adhabu na wokovu, haki na neema, toba na msamaha. Mashairi mengine manne ambayo kila moja lina aya 22, yanashughulika na mateso ya watu walioishi Yerusalemu na katika vijiji vya karibu, nayo yamepangwa sawa sawa katika kila upande wa shairi kuu la katikati. Jambo jingine la ajabu katika mashairi hayo linahusika na lugha ya asili ya Kiebrania, na hivyo halionekani katika lugha ya Kiswahili. Katika Kiebrania, mashairi ya mafungu ya 1,2 na 4, kila aya inaanza kwa herufi nyingine ya zile 22 zilizopo katika alfabeti ya Kiebrania, kufuatana na mfululizo wa herufi ya kwanza hadi ya mwisho. Katika shairi la fungu la tatu lenye aya 66, kuna vifungu 22 vya aya tatu tatu. Aya zote tatu katika kila kifungu zinaanza kwa herufi moja, na herufi za kwanza za kila kifungu pia zinafuata utaratibu wa herufi 22 za alfabeti ya Kiebrania. Ingawa shairi la fungu la tano lina aya 22, halifuati utaratibu huo wa herufi.