19:1-24:18 KUTOLEWA KWA AGANO Waisraeli katika Mlima Sinai (19:1-25) Kufika kwa watu katika Mlima Sinai kulikuwa alama maalumu ya kutimizwa kwa ahadi ya Mungu aliyompa Musa wakati ule kichaka kilipowaka moto bila ya kuteketea (taz.3:12). Safari ya kutoka Misri ilichukua muda wa miezi mitatu nayo ilikuwa hasa kwa uwezo na utunzaji wa Mungu, kwa kadiri ya ahadi zake za agano. Hata kabla ya kuwepo kwa taifa la Israeli, Mungu alikuwa amekwisha lichagua kwa neema yake kuwa taifa lake, alipofanya agano lake na Ibrahimu na kuthibitisha mambo hayo. Baadaye alitawala historia ya wazao wa Ibrahimu na kutimiza ahadi za agano hilo (taz.Mwa 12:2; 15:7-21; Kut 2:24; 4:22; 6:6-8; 15:13. Kwa maana ya 'Agano' taz.maelezo ya Mwa 9:8-17). Baraka za uhusiano huu wa pekee wa agano zilikuwa kwamba, watu wa Israeli watengwe na mataifa mengine, ili wawe mali ya Mungu, wawe makuhani, wamwabudu na kumtumikia Yeye. Kama wateule wa Mungu, Waisraeli walitakiwa wamwakilishe Mungu wao kwa mataifa ya ulimwengu (19:1-6). Ingawa agano liliwekwa kwa neema ya Mungu tu, baraka kuu ya agano ya ushirika na Mungu iliweza kuwa kweli kwa njia moja tu, yaani kama watu wangekuwa watakatifu katika maisha yao na kujitoa kwa Mungu; na jambo hilo waliweza kulipata tu, kama walielewa maagizo yake na kuyatii. Watu walikubali mambo hayo kwa moyo wote, nao waliahidi kutimiza amri za Mungu. Kwa njia hii, ingawa asili ya agano ilikuwa katika neema ya Mungu tu, wala haikuwa na masharti ya matendo ya wanadamu (taz.Gal 3:17-18), watu walipaswa kutimiza sehemu yao ya agano, kama walitaka kuzifurahia baraka zake (7-9). Kabla ya kuambiwa maagizo ya agano moja moja, watu walionyeshwa kwa kifupi nguvu za kutisha za Mungu Yule ambaye walijikabidhi kwake. Alikuwa mkuu na mtakatifu kiasi kwamba, hata watu waliagizwa watimize matendo ya kimfano ya kujitakasa siku mbili kabla ya kuruhusiwa hata kuutazama mlima wakati Mungu alipokuwa akisema na Musa huko. Mpaka uliwekwa umbali wa kutosha kuzunguka mlima wote, ili kusisitiza umbali uliokuwa kati ya Mungu Mtakatifu na watu wake wenye dhambi (10-15). Kisha watu walipewa nafasi ya kuona kwa kifupi mamlaka ya kutisha ya Yule waliyejikabidhi kwake. Mtu ye yote asiyekaribishwa rasmi, kama angethubutu kuvuka mpaka huo, ikiwa kwa kutojali tu, au kwa kupotea kwa bidii yake, angeuawa (16-25). Kanuni kuu za agano (20:1-17) Mungu akifuata utaratibu wa kawaida kama mkuu afanyaye agano na watu walio chini yake, alijijulisha kwanza kwa Waisraeli kwa kueleza jina na hali yake ya kuwa BWANA Mwenyezi, na kwa kuwaeleza watu wake tena mambo aliyowafanyia katika neema yake. Mwanzo kabisa Waisraeli walikumbushwa kwamba Mungu wao yu hai naye anashughulika daima, pia maneno ambayo wangeyasikia kwake yangekuwa mafunuo yaliyotoka kwake moja kwa moja (20:1-2). Kisha masharti ya agano yalifuata kwa njia ya amri kumi. Amri kumi hizo hazikuwa sheria kama sheria za kawaida za serikali fulani, kwa sababu hazikuwa na faini au adhabu, bali zilikuwa kanuni ambazo taifa lilipaswa kuishi kwa kadiri yake. Amri tatu za kwanza zilihusu uhusiano wa wanadamu na Mungu. Yeye peke yake ni Mungu wa kweli, hakuna nafasi tena kwa mwingine awaye yote (3). Sanamu ya namna yo yote isitumiwe kwa ibada, si mfano wa Mungu wa kweli, wala si sanamu ya kitu kingine ambacho kingeweza kuwa mfano wa miungu isiyo Mungu wa kweli. Mungu angechukua hatua kali ya hukumu ya haki dhidi ya watu wale ambao wangeasi agizo hilo, pia dhidi ya vizazi vya baadaye ambao wangefuata mifano mibaya ya mababu zao. Dhambi za kizazi kimoja zingechukua uzito wake hata juu ya kizazi kifuatacho. Lakini kwa wale ambao wangekuwa waaminifu, Mungu angejidhihirisha kuwa mwaminifu kwao (4-6). Watu wa YAHWEH (BWANA) walikatazwa kulitumia jina lake ovyo, si katika kuapa kwa neno lisilokuwa kweli, wala si katika kiapo kisichotimizwa baadaye. Pia walipaswa kuwa waangalifu wasije wakatumia jina hilo pasipo heshima, kama vile katika hasira au kulaani (7; taz.Law 24:16). Amri ya nne ilikuwa na sehemu ya Mungu na ya wanadamu pia. Siku ya Sabato ya kila juma ilihamasisha tabia ya kumwabudu Mungu, kwa sababu siku hiyo iliwekwa wakfu kuwa takatifu kwa Mungu, pia ilisaidia kwa mahitaji ya miili ya wanadamu kupumzika (8-11). Amri sita zilizofuata zilihusu wajibu wa watu katika jumuia. Ya kwanza katika hizo iliwafundisha watu kuwa waaminifu katika wajibu wao ndani ya familia zao. Katika kutimiza amri hiyo, wangesaidia jamii yote iwe imara na yenye afya, pia wao wenyewe wangekuwa na maisha marefu yenye furaha na amani. Kila mtu ampende jirani yake kama nafsi yake, akijiepusha kabisa na mambo ya uuaji. Atunze usafi wa maisha ya ndoa na kujiepusha na zinaa na uasherati. Aheshimu haki ya kila mtu ya kuwa na mali yake mwenyewe. Akatae kabisa kufanya mashtaka ya uongo, na hata kuzuia mafikira ya ndani yawezayo kutamani kitu cho chote kilicho mali ya mtu mwingine (12-17). Tabia inayotakiwa katika ibada (20:18-26) Musa aliridhika alipoona hali ya unyenyekevu wa watu baada ya kuona matukio ya kutisha yaliyounganika na kuja kwa Mungu juu ya Mlima Sinai. Walipojitambua katika upungufu wao, waliongezewa hofu kwa Mungu (18-21). Tabia hiyo ya unyenyekevu ilitakiwa pia kama mtu angetaka kujenga madhabahu wakati wo wote na mahali po pote ambapo Mungu angejidhihirisha kwake (k.mf.l7:14-16). Waisraeli walikuwa kabila lililosafiri, na hivyo madhabahu zile hazikuweza kuwa za kudumu. Waisraeli walikuwa taifa lenye dhambi, na hivyo madhabahu hazikutakiwa kujengwa kwa umaridadi na gharama zaidi. Zilitakiwa kuwa za unyenyekevu, kama fungu la udongo au fungu la mawe yaliyopangwa tu, kwa kadiri vifaa vyake vilivyopatikana mahali walipokuwa wakipita. Madhabahu hazikutakiwa kuwa juu sana, kiasi cha kuhitaji ngazi, kwa kusudi la kuzuia aibu kama mtu angekwea na kuinua nguo zake wakati wa kupanda ngazi ya madhabahu (22-26; taz.28:42-43). Hali ya sheria ya Kiebrania Sheria za Kiebrania kwa jumla zilikuwa za namna mbili. Namna ya kwanza tumekwisha ona katika amri kumi. Amri zile zilikuwa maagizo maalumu. Zaidi zilikataza mambo, bila ya kuruhusu walakini wa aina yo yote (k.mf.'usiibe'). Namna ya pili ambayo tutaiona mara kwa mara katika mafungu matatu yafuatayo, ni sheria mbalimbali ambazo labda zilitokana na maamuzi aliyoyatoa Musa au wasaidizi wake katika mashauri yaliyotokea wakati uliopita, na wakati huo zilipokelewa kama kanuni maalumu katika mashauri yo yote ya baadaye (k.mf.'kama mtu akiazima mnyama kwa mwenziwe, naye akaumia huyo mnyama au akafa, ...lazima atalipa'). Sheria za namna ya kwanza zinaweza kuhesabiwa kuwa kanuni za msingi; zile za namna ya pili, matumizi ya kanuni hizo katika hali ya namna mbalimbali. Itaonekana kwamba sheria za Kiebrania kwa jumla zilifaa kwa hali ya utamaduni na desturi za maisha ya kawaida ya wakati ule. Zilipangwa ili kutunza amani na uamuzi wa haki baina ya watu waliokwisha tulia katika mila za maisha yao. Kwa mfano, sheria hizo hazikukataza utumwa moja kwa moja, kwa sababu katika hali ya jamii, ya biashara na ya siasa ya wakati ule taifa lingalipata shida kama utumwa ungeondolewa ghafla. Lakini sheria ya Kiebrania iliingiza msimamo mpya wa kufikiria hali nzuri kwa watu wengine isivyojulikana katika mila za mataifa mengine ya wakati wa kale, na hivyo maendeleo mapya yalianza ambayo baada ya muda mrefu yalileta mwisho kabisa wa utumwa. Kwa njia nyingine sheria za Kiebrania zilifanana na sheria nyingine za ulimwengu wa kale, lakini pia zilikuwa na tofauti za maana sana. Kwanza, adhabu au faini zilipangwa kadiri ya uzito wa makosa. Haukuwepo ukatili ulioonekana katika mataifa mengine ambapo adhabu mara nyingi iliingiza mateso makali kiasi kisichokuwa sawa na kosa (21:22-25; Kum 25:3). Pili, haki ilikuwa sawa kwa wote. Hazikuwepo sheria nyingine kwa watu wa daraja la juu, bali zilihakikisha usikilizaji wa haki kwa watu wote (23:3,6; Law 19:15). Na hasa, sheria za Kiebrania zililinda haki za wale wasioweza kujitetea au waliokuwa maskini (23:6), wageni (23:9, wajane au yatima (22:22), wenye madeni waliokuwa wamejiuza kuwa watumwa (21:1-11) na hata wale waliozaliwa katika utumwa (23:12). Sababu ya msingi iliyoleta tofauti kubwa hizo bila shaka ilitokana na sheria yao iliyotoka kwa Mungu mwenyewe, kama ilivyohakikishwa mara kwa mara. Mambo ya kiraia, ya kiadili na ya kidini hayakutengwa, kama ilivyokuwa katika jamii nyingine, kwa sababu katika jumuia ya watu wa Mungu sehemu zote za maisha zilikuwa na uhusiano. Watu waliona kila jambo katika nuru ya ujuzi wao wa Mungu na uhusiano wao naye. Sheria kuhusu utumwa (21:1-11) Katika jumuia ya Kiebrania mtumwa alikuwa na haki zake. Mwanamme au mwanamke kama alikuwa mtumwa Mwebrania, hakuweza kulazimishwa kuwa mtumwa kupita muda wa miaka sita (21:1-2; Kum 15:12). Iwapo mtu alimchukua mke wake wakati wa kuingia utumwani, alimchukua tena baada ya kupata uhuru, lakini kama alikuwa hana mke wakati alipoingia katika utumwa, na baadaye alipewa mke na bwana wake, hakuweza kumchukua mke huyo pamoja na watoto wake wakati wa kurudishiwa uhuru wake. Wao walibaki kuwa mali ya bwana wake. Lakini kama alitaka, aliweza kuendelea kufanya kazi kwa bwana wake, na hivyo kuendelea kuwa na mke na watoto wake (3-6). Iwapo mwanamke alikuwa mjakazi naye alikuwa mke au mke mdogo wa bwana wake, mambo yalitofautiana. Hakupewa uhuru baada ya miaka sita, kama ilivyokuwa sheria kwa watumwa wengine, wala hakuweza kuuzwa kwa mtu mwingine, kama bwana wake hakumtaka tena. Wazazi wake waliweza kumkomboa. Kama hakukombolewa, mume au bwana wake alipaswa kuendelea kumtunza kwa kadiri ya hali yake ya kuwa mkewe. Kama mume alikosa kufanya hivyo, ilikuwa lazima mwanamke huyo apewe uhuru bila malipo yo yote (7-11). Sheria kuhusu ujeuri na madhara (21:12-27) Hukumu ya kifo ilikuwa adhabu kwa uuaji wa makusudi, ujeuri kwa wazazi na utekaji nyara wa watu kwa ajili ya kuwafanya watumwa. Desturi iliyoenea katika nchi za maeneo yale ya kuwa mwuaji aliyeshika pembe za madhabahu na kupaza sauti akiomba neema ya kuepukana na adhabu, haikuruhusiwa katika Israeli, ingawa mtu aliyeua kwa ajali bila makusudi, aliweza kupata usalama katika mji mmojawapo wa miji ya makimbilio ambayo ingetajwa hapo baadaye (12-17; taz.Hes 35:9-15; Kum 19:1-6). Mtu alipaswa kulipa fidia kama aliwaumiza wengine, kiwango cha fidia ilitegemea hali ya kuumizwa kwenyewe na hasara au umaskini uliotokana na kuumizwa (18-19). Mtu hakuweza kumtesa mtumwa wake au kumpiga mpaka afe. Kama alifanya hivyo, aliadhibiwa. Kama haikuthibitishwa kwamba kifo kilisababishwa na kupigwa, bwana wake hakuadhibiwa wala hakuweza kutozwa fidia. Yeye mwenyewe alipata hasara ya kupotewa na mtumwa wake (20-21). Kanuni ya ljicho kwa jicho na jino kwa jino' ilikuwa msingi kwa mahakama, yaani adhabu ilitakiwa kuwa sawa na kosa, yaani adhabu kubwa kwa kosa kubwa na adhabu ndogo kwa kosa dogo. Kanuni hiyo ilitolewa ili kuzuia kisasi, kwa sababu watu huwa na tabia ya kulipiza kisasi kikubwa kuliko kosa walilotendewa (22-25). Kama mtumwa aliumizwa sana, alitakiwa alipwe fidia kwa njia ya kupewa uhuru bila masharti yo yote (26-27). Katika hotuba yake ya mlimani katika Mt 5:38-42, Yesu hakupinga kanuni ya adhabu ya haki kwa makosa, kwa sababu ni sehemu ya msingi wa sheria ya serikali ya kiraia. Yesu hakutaka kuweka msingi kwa sheria mpya ya serikali, kama ilivyokuwa kwa Musa, bali aliwaonya wanafunzi wake wasidai haki yao daima. Katika uhusiano wao wa binafsi waongozwe na roho ya kusamehe, wakijikana wenyewe na kuonyesha upendo kwa wale wanaowatendea mabaya. Roho atawalaye mioyo ya Wakristo si roho atawalaye sheria za mahakama ya serikali. Madhara yaletwayo na wanyama (21:28-36) Sheria zilipangwa ili kuwalinda au kuwaadhibu wenye wanyama walioumiza au kuua watu. Katika kukadiria ukubwa wa kosa na kupanga fidia iliyotakiwa kulipwa, ilifikiriwa zaidi kiasi ambacho mwenye mali alikosa kumtawala mnyama wake. Kama mtu aliyeuawa na mnyama alikuwa mtumwa, fidia ilipasa kulipwa kwa bwana wake, kwa sababu mtumwa alikuwa mali yake. Lakini pia mtumwa alihesabiwa kuwa mwanadamu wala siyo 'kifaa' au 'chombo' tu, na mnyama aliyeua alipaswa kuuawa, sawa sawa na ilivyokuwa kama alimwua mtu hum. Kuangamizwa kwa mnyama yule kulithibitisha utakatifu wa uzima wa binadamu (28-32). Kanuni zilizopangwa hapo juu za kukadiria jukumu kwa madhara ya wanadamu pia zilihusika kwa wanyama. Kulikuwa na haki ya ajabu kwa kila upande uliohusika (33-36). Sheria kuhusu maiipo ya fidia (22:1-17) Mwizi aliyekamatwa naye alikiri kosa lake, alipaswa kurudisha vitu alivyoiba, na juu yake alipe faini kuwa fidia kwa mwenye vitu. Kadiri kosa lilivyokuwa kubwa, ndivyo ilivyozidi faini yake. Kama hakuweza kulipa kiwango alichodaiwa, yeye mwenyewe alipaswa kujitoa kuwa maiipo kwa njia ya kuwa mtumwa wa mtu yule aliyeibiwa vitu vyake. Haikuwa halali kumwua mwizi, kama alikamatwa katika tendo hilo, isipokuwa usiku, ikiwa mtu aliyeibiwa alipaswa kujitetea maisha. Lakini kwa kawaida mwizi alitakiwa akamatwe na kupelekwa mahakamani (22:1-4). Fidia ilibidi kulipwa kwa madhara yaliyosababishwa na mifugo au moto (5-6). Mtu aliyeachiwa mali ili aitunze, hakudaiwa fidia kwa kuharibika au kupotea kwa mali hiyo, kama aliweza kuwaridhisha mahakimu, ama kwa njia ya kuapa kiapo au kwa kuthibitisha kwamba hasara ile haikuwa kosa lake. Kama yalikuwepo mashaka juu ya uaminifu wake, au kama vikundi viwili vilidai kitu fulani kuwa mali yao, mahakimu walikuwa na nafasi ya kuamua kikundi kipi kilidai kwa uongo (7-15). Mtu aliyembikiri mwanamwali alipaswa kulipa fidia kwa baba mzazi wa msichana. Fidia hiyo ilidaiwa kwa hali yo yote, haidhuru kama baba wa msichana baadaye alimruhusu mwanamme huyo kumwoa binti yake au sivyo, kwa sababu baada ya kitendo kile, baba yake hangeweza kupata mahari kamili kwa binti yake, kwa sababu alipotewa na ubikira wake (16-17). Mambo mengine (22:18-23:19) Desturi na mambo ya dini ya kipagani yaliyohatarisha imani na dini ya Israeli yalipigwa marufuku. Adhabu ya kawaida kwa makosa kama hayo ilikuwa kifo (18-20). Waisraeli waliagizwa kukumbuka mambo yaliyowapata wao wenyewe nchini Misri, na hivyo waonyeshe huruma kwa watu wasiokuwa na hali nzuri katika jumuia yao. Waliokuwa fukara au maskini wasionewe au kunyonywa na matajiri, bali wasaidiwe (21-27). (Kinachohesabiwa hapa kuwa dhuluma ni kumnyonya maskini na watu wa hali ya chini, wala siyo biashara ya halali. Yesu alilaumu dhuluma, lakini alithibitisha biashara ya halali; taz.Lk 6:34; 19:23.) Waisraeli wakiwa taifa la Mungu lililojitoa kwake, walitakiwa kumheshimu na kumtolea Yeye vitu vyao kwa ukarimu, na hapo hapo wajiepushe na uchafu wo wote (28-31). Maafisa walipaswa kuendesha huduma ya haki kila wakati. Wasiwapendelee matajiri wala maskini, wala wasikubali hukumu ishawishiwe na maoni ya watu wengi. Lakini kufuata kila agizo la sheria tu haikutosha: Kilichotakiwa zaidi ni utu mwema na huruma kwa watu wote, hata kwa maadui na wageni, na hata kwa wanyama (23:1 -9). Kila mwaka wa saba mashamba yalitakiwa yapumzike, yaani yasilimwe. Kitu cho chote kilichoota shambani hivi hivi tu kwa mwaka huo, kilipaswa kiachwe kwa ajili ya maskini. Mungu angetoa mavuno mengi zaidi katika mwaka wa sita, kusudi kusiwepo shida katika mwaka wa saba. Kila siku ya saba ilitakiwa kuwa siku ya kupumzika kwa watu wote, yaani kwa wakuu, kwa wafanyakazi na hata kwa wanyama (10-13; taz.Law 25:18-22). Sikukuu tatu ziadhimishwe kila mwaka, na angalau wanaume wazima wote wahudhurie sikukuu hizo. Sikukuu hizo zilikuwa Pasaka pamoja na Mikate Isiyotiwa Chachu, iliyowakumbusha watu walivyookolewa kutoka Misri; Pentekoste, yaani Malimbuko ya Mavuno, siku hamsini baada ya Pasaka, ya kuadhimisha mwisho wa mavuno ya ngano; na sikukuu ya Vibanda na Mavuno ya mwisho wa msimu wa ukulima (14-17. Kwa habari zaidi ya sikukuu hizo taz.Walawi 23). Desturi za ushirikina za kipagani za kusaza sehemu ya sadaka, na kumchemsha mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake, kwa matumaini ya kuongeza mafanikio katika mifugo, mambo haya yote yalipigwa marufuku (18-19). Ahadi na maagizo (23:20-33) Maandiko rasmi ya hati ya agano yaliyoanza katika fungu la 20, ambapo Mungu alijidhihirisha kwa Waisraeli, yalidai uaminifu na utii wa watu, nayo yaliweka masharti juu yao, kama walitaka kuzifurahia baraka za agano. Hata wakati huo yalimalizwa kwa kutoa ahadi na maonyo mbalimbali. Habari hii tena ilifuata mfano uliojulikana katika desturi za kale za kufunga maagano. Ahadi kuu kwa Waisraeli zilikuwa ulinzi katika safari yao ya kuelekea nchi ya ahadi, ushindi juu ya maadui zao, afya na fanaka katika Kanaani na kuongezeka kwa taifa lao mpaka lijaze nchi yote. Lakini baraka hizo zilikuwa na masharti, yaani watu wawe waaminifu katika utii wa kumfuata BWANA kabisa (20-23). Kutiwa sahihi kwa agano (24:1-18) Musa alipokariri maagizo ya agano kwa watu, wao waliahidi kuyatii yote kwa moyo mkunjufu (taz.l9:8). Katika nyakati za kale maagano mengi yalitiwa sahihi kwa damu (taz.maelezo ya Mwa 15:7- 21), na hata katika Mlima Sinai Mungu na watu wake waliunganishwa kwa njia ya sherehe ya damu. Nusu ya damu ilinyunyizwa katika madhabahu (iliyokuwa mfano wa uwepo wa Mungu), na nusu nyingine ilinyunyizwa juu ya watu. Lakini Waisraeli pia walikuwa wamejifunza kwamba damu ya sadaka ilikuwa ishara ya uzima uliotolewa ili kumkomboa mtu aliyekuwa chini ya hukumu ya kifo (k.mf.Pasaka). Kwa hiyo damu katika habari hiyo ya agano inawezekana kuwa na maana zaidi kuliko ya sherehe ya kufunga agano. Inawezekana kwamba ilikuwa na maana ya usuluhishi kwa ajili ya dhambi pia, kusudi Waisraeli waingie katika agano hali wamesafishwa dhambi zao za zamani, nao wamejitoa kwa Mungu (24:1-8. Kwa habari zaidi ya maana ya sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani, n.k. taz.Law 1:1-7:38). Ili kuonyesha kuwa karibu sana na uhusiano wa agano hilo na Mungu, wajumbe wa Israeli walikwea mlima walipoona utukufu wa Mungu (bila ya kupigwa na utukufu huo hata wafe, anavyokumbusha mwandishi), na huko walikula karamu ya sadaka ya amani pamoja (9-11). Waliporudi, Musa aliwaweka Haruni na Huri, ili wawatawale watu kwa niaba yake wakati yeye na Yoshua waliporudi mlimani. Yoshua alifuatana na Musa katika safari hiyo kwa sehemu tu, ambapo Musa, baada ya kukaribishwa, alikaribia mpaka mbele ya Mungu kabisa. Alikuwa huko kwa muda wa karibu majuma sita, alipopata maelezo yote yaliyohusu hema la kukutania na makuhani yanayoelezwa katika mafungu ya 25-31 (12-18).