15:22-18:27 SAFARI YA KWENDA SINAI Malalamiko kuhusu maji (15:22-27) Baada ya kuzoea maisha ya Misri kwa muda wote wa maisha yao, Waisraeli hawakujua hali ngumu ya jangwani. Hali ya furaha kubwa ya imani katika Mungu waliyokuwa nayo wakati wa wimbo wao wa ushindi na matumaini katika Bahari ya Shamu, haikuendelea muda mrefu. Baada ya safari ya siku tatu walipoona kiu, na maji ya pekee waliyoyaona yalikuwa machungu, hata yasifae kwa kunywa, walinung'unika vibaya sana (22-24). Mungu alipaswa kuwafundisha kwamba, kuwepo kwake kati yao haikuwa na maana kwamba wangeishi bila matatizo ya maisha ya kila siku. Hata hivyo, kama wangeishi katika imani na utii kwa Mungu, Yeye angehakikisha kuwahifadhi katika jangwa pamoja na ugumu na shida zake. Yeye angeweza kuwafundisha jinsi ya kuishi katika hali hiyo, hata maji machungu yangeweza kutibiwa ili yafae; au angeweza kuongoza safari yao ili wafike mahali penye maji safi (25-27). Manung'uniko kuhusu chakula (16:1-36) Wema wa Mungu kwa watu wake wa kuwapa maji ulisahauliwa upesi sana, nao walilalamika tena, wakati huo kwa sababu hawakuwa na chakula (16:1-3).Hapo tena kwa upendo wake mkubwa, Mungu aliwapa walichohitaji. Kuanzia wakati huo, mpaka walipoingia nchi ya Kanaani, chakula chao kilikuwa cha vipande vidogo kama magamba vilivyoitwa mana, maana yake 'Kitu gani hiki?', kwa sababu hawakujua jina lingine kwa chakula hicho (4; taz.mst. 15). Mungu aliwapa mana kila asubuhi, na watu walitakiwa waile siku ile ile. Hali ya pekee ilikuwa siku ya Sabato, siku ya mapumziko yao. Haikuwepo mana asubuhi ya Jumamosi (ambayo ni Sabato yao), lakini siku ya Ijumaa kiasi chake kilikuwa maradufu, na nusu yake ilitunzwa kwa Jumamosi. Kwa kawaida mana ilioza haraka sana, kwa hiyo kiasi kile walichokitunza kwa Jumamosi walikihifadhi kwa njia ya kuoka au kuchemsha mapema (5-7; taz.mst.23). Ugawaji wa mana ulitawaliwa, asiwepo mtu aliyekuwa na nyingi zaidi au aliyekosa kiasi chake. Tafrija ya kuongezea katika hali hiyo ilikuwa katika wingi wa ndege ambao, bila shaka walichoka kutokana na kuruka kwa muda mrefu wakatua karibu nao. Watu waliweza kuwashika na kuwapika kwa chakula cha jioni (8-13). Kuhusu ukusanyaji na ugawaji wa mana kila asubuhi, Musa alitoa maagizo ili kuhakikisha kwamba asiwepo mtu apataye zaidi au akosaye (14-18). Amri ya Mungu iliyokataza kutunza mana mpaka siku ya pili, na ahadi iliyohakikisha mapumziko kamili ya Sabato kwa njia ya kiasi cha maradufu siku ya Ijumaa, iliwapa watu nafasi ya kuonyesha utii wao kwa Mungu. Lakini katika mambo yote walikosa (19-30). Musa aliagiza kuweka sehemu ya mana katika chombo na kuitunza kama kumbukumbu, jinsi Mungu alivyowalisha watu wake jangwani. Chombo kile baadaye kiliwekwa katika sanduku la agano, pamoja na fimbo ya Haruni na mbao za mawe zilizoandikwa sheria (31-36; Ebr 9:4). Mambo yaliyotokea Refidimu (17:1-16) Watu walipofika Refidimu na kugundua kwamba hapakuwepo na maji, walimnung'unikia Mungu na Musa tena. Na hapo tena Musa aliwaombea, na mara nyingine Mungu aliitikia kwa mwujiza. Majina yaliyotolewa kwa eneo lile, yaani Masa na Meriba, yaliwakumbusha watu jinsi walivyokuwa 'wamemjaribu' Mungu (Masa), na 'walivyoshindana' na Musa (Meriba) (17:1-7). Waamaleki, kabila la wachungaji washenzi walioishi jangwani, na waliotokana na uzao wa Esau (Mwa 36:12,16), waliona msafara wa Waisraeli ukikaribia maeneo yao kuwa jambo lililohatarisha usalama wao. Waliwashambulia Waisraeli, lakini kutokana na maombi ya Musa, Mungu aliwapa Waisraeli ushindi wa ajabu (8-13). Waisraeli wangepata matatizo zaidi kutoka kwa Waamaleki baadaye. Iliandikwa kwa ajili ya viongozi wa baadaye kwamba Mungu angepigana vita kwa ajili ya Waisraeli mpaka Waamaleki wangefutiliwa mbali (14-16; taz.Kum 25:17-19; 1Sam 15:2-33; lNya 4:41-43). Kwa kutazama nyuma katika majuma machache tangu Waisraeli walipoondoka katika Bahari ya Shamu, inaonekana wazi jinsi Mungu alivyothibitisha uwezo wake wa kutoa kila kitu ambacho watu wake walikihitaji, na kuwahifadhi katika hatari zao zote na katika magumu yao, ikiwa kwa habari ya kiu, magonjwa, njaa au vita. Mikakati ya utawala katika Israeli (18:1-27) Waisraeli walipokaribia Mlima Sinai, Musa alikutana na mkewe na watoto wake tena waliokuwa wamerudishwa Midiani kwa ajili ya usalama wao wakati Musa aliposhindana na Farao. Mkwewe Musa, Yethro, alikuja pamoja nao, naye wakati huo alikuwa mwamini wa kweli wa Mungu wa Israeli (18:1-12). Musa alikuwa na kazi kubwa ya madaraka ya kuongoza watu na kutatua matatizo yao, na Yethro aliona mapema kwamba kazi hiyo ingemchosha Musa vibaya. Mpaka wakati huo mashauri yote yaliyotaka uamuzi au jibu la haki yaliletwa mbele ya Musa, na uamuzi wake ulikubaliwa na watu kama sheria ya Mungu. Yethro alitoa ushauri kwamba, kwa muda huo wakati ulifika wa kufanya mikakati maalumu kwa utawala wa madaraka, yaani watu wachaguliwe na kupewa madaraka ili wamsaidie Musa. Watu wale wakabidhiwe mashauri ya kila siku ili wayaamue, ila mashauri magumu zaidi yaletwe kwa Musa. Mpango huo, licha ya kuwa nafuu kwa Musa, ulikuwa faida kwa watu pia, kwa sababu wao nao walichoka kungoja, ili wapate nafasi ya kusikilizwa na Musa (13-23). Musa aliona thamani ya ushauri wa mkwewe akaingiza mpango huo katika Israeli yote. Yethro akarudi nyumbani kwao (24-27). Wakati huo watu wengine walipomsaidia Musa katika utawala, haja ya kanuni ya mwongozo ilitakiwa ili ikubaliwe na watu wote, yaani mpango maalumu wa sheria, ili viongozi waweze kuamua kwa kadiri yake. Kwa hiyo Mungu aliwapa amri kumi (taz.fungu la 20), ili ziwe msingi wa kanuni zilizowekwa juu ya sheria yote. Labda zilifanana na kanuni alizozitumia Musa katika kuamua kwake mpaka wakati huo. Nyongeza za sheria zilizofuata (mafungu ya 21-23, zinazojulikana kuwa kitabu cha agano), ziliwekwa juu ya msingi wa kanuni hizo. Inawezekana kwamba kanuni hizo zilichukuliwa katika mashauri ambayo Musa alikuwa amekwisha kuyashughulikia mpaka wakati huo, na hapo zilithibitishwa kuwa sheria kwa wakati wa usoni.