Kitabu cha Kutoka UTANGULIZI Kama ilivyokuwa katika kitabu cha Mwanzo, hata kitabu cha Kutoka kilipewa jina lake Exodus na watafsiri wa Agano la Kale katika lugha ya Kiyunani, yaani Septuaginta. Maana yake ni 'kutoka nje' au 'kuhama', nalo linaeleza habari za kutoka au kuhama Misri. Habari za kitabu cha Mwanzo zilimalizika kwa familia ya Yakobo (Israeli) ilivyoishi katika nchi ya Misri. Kitabu cha Kutoka kinaanza habari zake muda wa miaka kama 400 hivi baada ya hayo (Mwa 15:13; Kut 12:41). Wakati huo wazao wa Israeli walikuwa wameongezeka sana, hata walikuwa taifa la maana, ingawa bado waliishi Misri. Kitabu hiki kinaonyesha jinsi Mungu alivyowaokoa watu wake katika utumwa wa Misri, akawapeleka mpaka karibu na Mlima Sinai, na huko alithibitisha rasmi agano alilolifanya na Ibrahimu, ili Israeli liwe taifa la kweli na mali ya Mungu, nalo liishi kwa ajili yake. Kisha Mungu, kwa njia ya Musa, aliwapa watu hao kanuni zile ambazo kwa njia yake wangeweza kuishi, pia aliwapa sheria za dini walizotakiwa kuzitimiza, iwapo wangetaka kuzifurahia na kufaidi baraka za agano. Ufunuo wa tabia ya Mungu Licha ya thamani yake ya kutoa masimulizi ya matukio ya historia ambayo maisha ya Israeli ya kidini na ya kitaifa yalijengwa juu yake, kitabu cha Kutoka pia kina thamani katika kudhihirisha sehemu kubwa ya tabia ya Yule aliyekuwa Mungu wa Israeli. Zaidi ya yote, alidhihirishwa kuwa Mungu aokoaye. Waisraeli walitakiwa wamkumbuke daima kuwa Ndiye aliyewaokoa na kuwatoa 'katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa' (Kut 6:3-8; 20:2). Waisraeli walitakiwa watambue historia yao siyo kama kusanyiko la masimulizi ya matukio, bali kama ufunuo wa tabia ya Mungu. Yeye kwao alikuwa nani, aliwafanyia nini, naye aliwatazamia wafanye mambo gani? Mungu alishughulika na kila sehemu ya maisha wa Waisraeli. Matendo yake ya kuokoa yalikuwa yenye ushindi, na hukumu zake ziliangamiza. Kuhifadhiwa kwa taifa na kukua kwake kulikuwa kazi yake (1:21; 14:21-22:31; 32:35). Mungu wa Israeli pia alikuwa Mtakatifu, maana yake ilikuwa kwamba watu pia wawe watakatifu. Walitakiwa wawekwe wakfu kwa Mungu, wakifuata kwa uangalifu sana matakwa yake kuhusu maisha ya maadili yaliyopangwa wazi naye (Kut 19:5). Hata hivyo, Mungu huyo aliyetofautiana kabisa na wanadamu wenye dhambi (19:12-13), pia alitaka kuishi kati ya watu (25:8; 33:14). Yule ambaye utakatifu na haki yake vilidai adhabu na hukumu kwa wenye dhambi (32:33), alikuwa Yule Yule ambaye kwa huruma na neema yake aliandaa njia kwa wenye dhambi ili waweze kumkaribia tena, wasamehewe dhambi zao na kurudishwa tena katika ushirika hai na Mungu Mtakatifu (Kut 29:10-14; 34:6-7). MUHTASARI 1:1-4:31 Maandalizi ya Musa 5:1-15:21 Kuokolewa kutoka Misri 15:22-18:27 Safari ya kwenda Sinai 19:1-24:18 Kutolewa kwa agano 25:1-31:18 Hema la kukutania na ukuhani 32:1-34:35 Kuvunjwa kwa agano na matengenezo yake 35:1-40:38 Kuandaliwa na kujengwa kwa hema la kukutania