25:19-28:9 ISAKA AKABIDHIURITHI Wana wawili wa Isaka (25:19-34) Isaka na Rebeka walipaswa kungoja miaka 20 mpaka mtoto wao wa kwanza alipozaliwa. Hapo Rebeka alizaa watoto mapacha, na walipokuwa wakubwa, tabia zao zilitofautiana kabisa, kama ilivyokuwa hali katika mataifa mawili yaliyotokana nao baadaye. Mungu alipanga kwamba mkubwa wao, yaani Esau, amtumikie mdogo wake Yakobo (19-26). Lakini habari hii haikuwa udhuru au ruhusa kwa Esau kuwa mtu asiyefaa, auzaye haki yake ya kuwa mzaliwa wa kwanza (taz.Ebr 12:16-17). Wala haikuwa udhuru au ruhusa kwa Yakobo kuwa mtu asiye na huruma na kujipatia haki ya kuwa mzaliwa wa kwanza kwa hila (27-34). Haki ya kuwa mzaliwa wa kwanza ilikuwa kwamba, mtu awe mkuu wa ukoo na apokee maradufu katika sehemu ya urithi wakati ulipogawiwa kati ya watoto. Katika maana kubwa ya ahadi ya agano aliyopewa Ibrahimu, urithi ulijumlisha ukuu juu ya taifa kubwa na kuwa mkuu wa nchi ya Kanaani. Isaka na Abimeleki (26:1-33) Njaa kubwa ilipofanya maisha yawe magumu Kanaani, Isaka alionyesha imani na utii wake akikataa kutoka katika nchi. Alibaki katika maeneo ya Wafilisti, sehemu ya pwani kusini mwa nchi ya Kanaani, akiamini kwamba Mungu angeweza kumhifadhi yeye na familia yake katika nchi aliyoahidiwa na Mungu. Lakini alikosa imani ya kumtegemea Mungu kwamba amlinde kwa watu wabaya, na kama vile baba yake, alisema uongo kwa kusudi la kujikinga maisha (26:1-11; taz. 12:10-20; 20:1-18). Mungu alimbariki Isaka kama alivyoahidi, lakini mafanikio yake katika ukulima yaliamsha wivu wa Wafilisti. Yeye na watu wake walilazimishwa kuhama sehemu baada ya sehemu, kwa sababu Wafilisti waliwanyang'anya visima au walivijaza kifusi (12-22). Pole pole alisukumwa nje ya nchi ya rutuba bora ya Wafilisti, lakini Mungu alimpa moyo asiogope wala asikate tamaa (23-25). Mfalme wa Wafilisti aliyeogopa nguvu ya Mungu wa Isaka, alifikiri ingekuwa jambo la busara kuthibitisha upya mkataba uliofanywa na Ibrahimu hapo awali. Ingawa Wafilisti walikuwa wakimwonyesha uadui na hila, Isaka alikubali kuthibitisha mkataba huo (26-31; taz.21:22-24). Siku ile ile watu wa Isaka walipata maji, baada ya kuchimba upya katika kisima cha Ibrahimu ambacho Wafilisti labda walikuwa wamekifukia (32-33; taz. 21:25-34). Maelezo: Abimeleki (maana yake baba mfalme) halikuwa jina la mtu, bali jina la cheo cha mfalme wa Wafilisti (kama vile jina la cheo cha mfalme wa Misri 1 ilivyokuwa Farao). Abimeleki wa siku za Ibrahimu alikuwa mtu mwingine kuliko Abimeleki wa siku za Isaka. Abimeleki wa siku za Daudi alikuwa na jina la Akishi (linganisha utangulizi wa Zab 34 na ISam 21:10-15). Hali kadhalika Fikoli halikuwa jina la mtu, bali ni cheo cha jemadari au kamanda wa jeshi (taz.21:32; 26:26). Yakobo apokea baraka za Esau (26:34-28:9) Ilikuwa desturi katika nyakati za kale kwa baba wa nyumba kuthibitisha haki ya mzaliwa wa kwanza juu ya mwana aliyezaliwa kwanza kwa njia ya kumpa baraka za pekee karibu sana na kufa kwake. Baraka hizo zilikuwa kama ahadi pamoja na unabii wa kibali cha Mungu kwa wakati wa usoni. Isaka alijua kwamba mapenzi ya Mungu yalikuwa kwamba Yakobo, wala si Esau, apokee baraka ya mzaliwa wa kwanza (taz.25:23). Lakini hata hivyo alikusudia kumpa Esau baraka hiyo, ingawa Esau, kwa njia ya kuwatwaa wake zake kutoka kwa Wakanaani, alielekea kuthibitisha hali yake ya kuwa nje ya baraka za agano la Mungu (26:34-27:4). Rebeka na Yakobo walifanya kosa kubwa vile vile walipofanya hila ya kudanganya na walipokosa kumtegemea Mungu (27:5-24). Lakini ijapokuwa watu walikosa, Yakobo alipata baraka ambazo Mungu alikuwa amemkusudia. Yeye alitakiwa awe mkuu wa taifa lililoahidiwa na Mungu, ambalo lingeishi katika nchi yenye rutuba na kusitawi, naye angekuwa na ushindi juu ya maadui zake (25-29). Baada ya kugundua kwamba mpango wake haukufaa, Isaka alikubali kuwa mapenzi ya Mungu kwa kumbariki Yakobo yasingeweza kubadilishwa (30-37). Baraka ya pekee aliyoweza kumpa Esau ilikuwa ahadi kwamba angekuwa mzazi wa taifa kubwa (ambalo lingejulikana kuwa la Waedomu; taz.25:30). Lakini taifa hilo lingeishi katika nchi isiyo na rutuba sana, nalo daima lingekuwa na matatizo na majirani zake, na hasa na Waisraeli (38-40; Hes 24:18; ISam 14:47; 2Sam 8:13-14; lFal 11:15-16; 2Fal 8:20-22; 14:7,22). Katika uchungu wake, Esau alikusudia kumwua Yakobo, na hivyo Rebeka aliamua kumpeleka Yakobo kwa kaka yake Labani kwa usalama wake (41-45). Lakini Rebeka alijua jinsi Isaka alivyochukia mambo aliyoyafanya Yakobo. Kwa hiyo alimweleza Isaka sababu nyingine ya kumpeleka Yakobo mbali: Yakobo alimhitaji mke, na Rebeka alijua kwamba Isaka asingempenda mwanamke wa tatu aliyetoka kwa Wakanaani, baada ya kuona matatizo yaliyoletwa na wake wawili wa Esau (46; taz.26:34-35). Kwa hiyo Isaka alikubali mapendekezo ya Rebeka kwa furaha, yaani kumtuma Yakobo sehemu za kaskazini, ili atafute mke kati ya jamaa wa Rebeka. Isaka akamwaga Yakobo akimpa baraka ya agano, wakati huo akitoa baraka hiyo hali akijua na kufurahi. Kwa upande wa Rebeka, yeye alipata aliyoyataka, lakini kama tunavyojua habari zao, hakumwona tena mwanawe aliyempenda sana (28:1-5). Esau alipotambua kwamba wazazi wake hawakuridhika na wake zake wa Kikanaani alioa tena, ingawa uchaguzi wake wa kumtwaa binti wa Ishmaeli ulithibitisha upya kwamba alikuwa nje ya baraka za agano la Mungu (6-9).