16:1-25:18 ABRAMU NA MRITHI ALIYEAHIDIWA Kuzaliwa kwa Ishmaeli (16:1-16) Hapo awali kidogo Abramu alipodokeza kwamba angempokea mtumwa wake kuwa mrithi wake, Mungu alimhakikishia upya kwamba mrithi wake angekuwa mwanawe mwenyewe (taz. 15:2-4). Lakini baada ya kuishi miaka kumi katika nchi ya Kanaani, Sarai alikuwa bado tasa. Imani yake ilipokuwa dhaifu, Sarai alimshauri Abramu ajaribu kumpata mwanawe kwa njia ya mjakazi wao, Hajiri. Hh haikuwa njia ya Mungu, bali ilikuwa desturi iliyokubaliwa na watu wa eneo lile. Haki zote juu ya mtoto aliyezaliwa kwa njia hii zilikuwa juu ya mke wala si juu ya mjakazi, ila mke hakuwa na haki ya kumfukuza mjakazi. Lakini wivu ulipotokea baina ya Sarai na Hajiri, Sarai alitekeleza haki yake kwa nguvu mno, hata Hajiri akatoroka (16:1 -6). Labda Hajiri alikuwa akielekea nyumbani kwao Misri malaika wa Bwana alipomtokea. Kwa njia ya malaika yule Mungu alimwambia Hajiri arudi na kumtii Sarai, akiongeza kumwambia, Mwanao ambaye atazaliwa, yeye mwenyewe atakuwa baba wa taifa kubwa. Jina lake litakuwa Ishmaeli, naye atakuwa kijana mwenye nguvu, mkali na mtu apendaye uhuru wa nyikani (7-12; taz. 17:20; 21:13). Hajiri alistaajabu mno kwamba alimwona Mungu naye aliendelea kuishi, hata akatoa jina la pekee kwa Mungu kwa kulikumbuka tukio lake la pekee (13-16). (Katika vitabu vya kwanza vya Agano la Kale Malaika wa Bwana anaonekana akifanana sana na Mungu mwenyewe. Habari hii labda ilikuwa hivi, kwa sababu malaika huyo alifananishwa na Mungu akiwa mjumbe wake, hata alipokuwa akisema, ilikuwa sawa kama Mungu mwenyewe alisema. Ni kama malaika aliyefanana na maumbile ya binadamu kwa muda, alikuwa kana kwamba Mungu alichukua maumbile ya binadamu kwa muda; taz.pia 21:17-18; 22:15-17; Kut 3:2-6.) Kufanywa agano na kuthibitishwa (17:1-27) Abramu na Sarai walipoendelea kuwa wazee, Mungu aliwaambia tena kwamba Yeye Mungu angekuwa mwaminifu kutimiza ahadi zake. Alijidhihirisha kwao katika jina jipya lenye uwezo (Mungu Mwenyezi), naye aliwapa majina mapya (Ibrahimu na Sara), ili kusisitiza kwamba Yeye angewafanya kuwa wazazi wa watu wengi sana (17:1-6,15-16). Mwenyezi Mungu alikuwa amefanya agano kwamba, Yeye angekuwa Mungu wa Ibrahimu na wazao wake, naye angewapa Kanaani kuwa nchi maalumu ya makao yao (7-8). Ili kumhakikishia Ibrahimu upya kwamba angetimiza ahadi za agano lake, Mungu alimwambia Ibrahimu aweke ishara ya daima katika mwili wake. Ishara hiyo, yaani tohara, ilikuwa mfano maalumu wa uaminifu wa Mungu kwa agano lake, pia ilikuwa ishara kwamba Ibrahimu aliamini ahadi za Mungu na kutii amri zake. Tohara ilithibitisha imani ya Ibrahimu na utii wake (Rum 4:9-12; Mdo 7:8). Wanaume wengine katika nyumba ya Ibrahimu, sawasawa na wazao wake wote katika vizazi vya baadaye, walipaswa kutahiriwa hivyo, iwapo walitaka kuwa watu wa Mungu wa agano. Asili ya agano ilikuwa katika neema ya Mungu, lakini watu walipaswa kuitikia neema hiyo kwa njia ya uaminifu na utii, iwapo walitaka kuona baraka za agano hilo (9-14). Mungu alipomwahidi Ibrahimu kwamba Sara angemzaa mwana, Ibrahimu alitazama umri wake na ule wa mkewe, akahisi kwamba habari hii ingekuwa ya ajabu zaidi, hata asiweze kuitazamia. Alifjkiria kuwa ingekuwa jambo rahisi zaidi kama Mungu angempokea Ishmaeli (aliyekuwa mvulana mzuri wa miaka 13 wakati huo; taz. 16:16; 17:1), awe mrithi wa ahadi za agano. Mungu akamwambia Ibrahimu kwamba Ishmaeli bila shaka angekuwa na mbari ya maana sana ya wazao, lakini watu wa agano la Mungu wangejengwa katika mwana ambaye angezaliwa, yaani Isaka (15-22). Ibrahimu aliamini ahadi ya agano la Mungu, na hivyo alitimiza amri ya Mungu ya agano lake (23-27). Wajumbe waliotoka kwa Mungu (18:1-33) Muda mfupi baada ya hayo, watu watatu walimtembelea Ibrahimu. (Wakati huo Ibrahimu alikuwa bado anakaa Hebroni; taz. 13:18; 14:13; 18:1). Ibrahimu aliwakaribisha, ingawa hapo mwanzo hakutambua kwamba walikuwa wajumbe wa pekee waliotoka kwa Mungu. Ilikuwa namna nyingine ya kutokea kwa Malaika wa Bwana (18:1-8; taz.mst. 22 na 19:1; Ebr 13:2). Inaonekana kama Ibrahimu hakuweza kumsadikisha Sara kwamba angemzaa mtoto, kwa hiyo Mungu alimtuma mjumbe wake kwa Sara moja kwa moja. Yeye pia alitakiwa kuwa mshiriki wa imani ya Ibrahimu (9-15). Ibrahimu alikuwa mtu wa maana sana katika mipango ya Mungu, si kwa habari za taifa la Israeli tu, bali pia kwa ulimwengu wote. Kwa hiyo Mungu aliamua kumwambia makusudi yake kuhusu mji mwovu wa Sodoma (16-21). Kwa sababu hiyo, wajumbe wawili walipoendelea kwenda Sodoma, mmojawao, yaani mtu wa tatu, alibaki na Ibrahimu. Maombi ya Ibrahimu kwa Mungu kwamba asiangamize mji wa Sodoma yalionyesha ufahamu mkubwa wa haki na neema ya Mungu, lakini yalionyesha pia kwamba Ibrahimu hakujua ubaya wote uliokuwepo Sodoma (22-33). Sodoma na Gomora (19:1-38) Wajumbe wale wawili walipofika Sodoma, Lutu aliyejua hatari ya kutembea barabarani usiku, aliwakaribisha wageni wale nyumbani mwake (19:1-3). Ingawa Lutu hakukubaliana na tabia chafu zilizotawala Sodoma (2Pet 2:7-8), bila shaka hakuwa na ujasiri wa kutosha kupinga mambo hayo. Alikuwa tayari hata kuwapa watu wale binti zake ili wawanajisi kwa nguvu, kusudi awalinde wageni wake wasije wakachukuliwa nao. Katika hukumu ya kupofusha, Mungu alionyesha hasira yake juu ya uchafuulewakimwili(4-ll;taz.Law 18:22; 20:13; Rum 1:26-27; IKor 6:9-10; Him 1:10). Baadaye wajumbe waliwaambia Lutu na familia yake wakimbie, kwa sababu mji wote wa Sodoma ungeangamizwa (12-14). Lakini Lutu alikuwa amezoea sana maisha ya Sodoma na kuufanya mji huo kuwa maskani yake hasa, hata ilikuwa kazi sana kumtoa huko. Karibu ingaliwapasa wageni wake kumvuta kwa nguvu. Na hata hapo aliomba kibali cha pekee kwa Mungu ambacho kingemruhusu kuendelea na maisha yake ya zamani katika mji mwingine (15-22). Katika eneo lile la Bahari ya Chumvi, karibu na miji ya Sodoma na Gomora kulikuwa na mashimo ya lami, ya dawa fulani iitwayo baruti (yaani kiberiti) na ya gesi ya ardhi (taz.l4:10). Maunganiko ya matetemeko ya nchi na umeme wa radi yaliweza kusababisha mlipuko mkubwa kama kupasuka kwa baruti, sawa sawa na kupasuka kwa mlima wa volkano, na kwa matetemeko yake baruti iliyowaka ilinyesha kama mvua juu ya miji ile (na juu ya mkewe Lutu). Hii ilikuwa hukumu ya Mungu ya moja kwa moja ambayo Mungu alisema habari zake hapo awali kidogo (23-29). Uharibifu ule ulitisha mno, hata Lutu akaamua kwamba hakuweza kuishi kwa usalama tena katika mji wo wote. Hivyo aliwachukua binti zake na kukaa katika pango la mlimani. Binti zake wawili, walimlazimisha baba yao kushirikiana nao kimwili isivyo halali. Watoto wawili waliozaliwa kutokana na hayo, baadaye walikuwa mababa wakuu wa Wamoabi na Waamoni, makabila ambayo baadaye mara kwa mara yalisababisha matatizo kwa Waisraeli (30:38). Ibrahimu amdanganya Abimeleki (20:1-18) Kutoka Hebroni Ibrahimu alihamia nchi ya Wafilisti iliyokuwa chini ya mfalme Abimeleki. Kutokana na udanganyifu wa Ibrahimu kuhusu Sara, Abimeleki alimchukua Sara awe mkewe, na hivyo alijiletea kitisho cha Mungu cha kuuawa (20:1-7). Baada ya kugundua ukweli, Abimeleki alichukua hatua ya heshima upesi sana. Alimrudishia Sara heshima yake machoni pa watu wake, akampa Ibrahimu zawadi na kumkaribisha kufanya makao katika nchi yake (8-16). Hali amenyenyekezwa na matukio hayo, Ibrahimu alimrudia Mungu tena kwa imani akamwombea Abimeleki na watu wake baraka za Mungu (17-18). Kosa la Ibrahimu na Sara wakati walipokuwa karibu sana na kuzaliwa kwake Isaka, lilithibitisha tena kwamba utimizaji wa ahadi za agano kuhusu mrithi ulitegemea neema ya Mungu peke yake, wala si matendo mema ya Ibrahimu. Kuzaliwa kwa Isaka (21:1-21) Baada ya kuzaliwa kwa Isaka, Ibrahimu alimtahiri kama alivyoagizwa, akionyesha kwamba mtoto huyu alikuwa mrithi wa ahadi ya agano la Mungu (21:1-7; taz.l7:9-14). Ishmaeli alidhihaki familia ya agano kama Sara alivyokuwa ameogopa. Ishmaeli alikuwa mwana wa mjakazi, kwa hiyo alikuwa na haki ya kurithi sehemu ya mali ya Ibrahimu, lakini badala ya kupata urithi huo, aliweza kuchagua uhuru wake mwenyewe na wa mama yake. Sara aliamua kwamba mwanawe Isaka awe mrithi wa pekee, na hivyo alijaribu kumshawishi Ibrahimu awape Hajiri na Ishmaeli uhuru wao wa lazima kwa njia ya kuwafukuza. Ibrahimu alisita kufanya hivyo, kwa sababu kijana na mama yake walikuwa na haki kamili kuishi katika nyumba yake, lakini Mungu alitia mkazo katika pendekezo la Sara. Bila mashaka yo yote Mungu angewaangalia Hajiri na Ishmaeli, naye angemfanya Ishmaeli kuwa taifa kubwa, lakini agano lake lilikuwa na Isaka (8-21). Mkataba wa Ibrahimu na Abimeleki (21:22-34) Ibrahimu alikuwa amefanya maskani yake sehemu za kusini mwa Kanaani katika nchi ya Abimeleki, kwa sababu Abimeleki alimkaribisha kufanya hivyo (taz.20:15). Lakini Abimeleki alikuwa bado akijihadhari na Ibrahimu, naye alimwogopa Mungu wa Ibrahimu. Alipendekeza kwamba yeye na Ibrahimu wafanye mkataba wa kuhakikishia amani na uhusiano wa kirafiki baina yao (22-24). Ibrahimu aliyakubali hayo, lakini wakati ule ule alimhamasisha Abimeleki akubali kwamba kisima fulani ambacho watu wa Abimeleki walikidai kuwa chao, kwa kweli kilikuwa mali ya Ibrahimu. Abimeleki alikubali neon hilo, na kwa ishara yake aliwapokea kondoo sab a kutoka kwa Ibrahimu kuwa ushahidi wake (25-34). Kisima kile kilipata jina la Beer-sheba, na baadaye Ibrahimu alifanya makao yake huko (taz.22:19). Kumtoa Isaka kuwa sadaka (22:1-19) Ingawa Ibrahimu alijua kwamba baadhi ya watu wa mataifa ya kale waliwatoa watoto wao kuwa sadaka kwa miungu katika matukio fulani ya maana sana, bila shaka alishangaa mno Mungu alipomwambia amtoe Isaka kuwa sadaka. Kwa njia hii si utii wake tu ulijaribiwa sana, bali pia imani yake, kwa sababu kama Isaka angekufa, Mungu angewezaje kutimiza ahadi zake za agano za kumfanya Isaka kuwa baba wa taifa kubwa? Kulitokea mashindano ya mawazo kati ya utii kwa Mungu na imani katika ahadi zake. Lakini Ibrahimu alitii, akiamini kwamba Mungu angeweza kutatua tatizo hilo, hata kama ingempasa kumrudisha mwanawe baada ya kutolewa sadaka kutoka kwa wafu (22:1-8; taz.Ebr 11:17-19). Ibrahimu alifuzu mtihani wake: utii wake ulithibitisha imani yake. Kwa kweli, alimtoa Isaka kuwa sadaka ingawa hakumwua. Mungu alimweka mnyama asiyekosa awe badala ya Isaka, na hivyo maisha ya Isaka yalirudishwa kutoka mautini (9-14; taz.Ebr 11:19; Yak 2:21-24). Mungu alionyesha jinsi matukio yale yalivyothibitisha kwamba utii ulikuwa njia ya kubarikiwa. Alimhakikishia Ibrahimu upya habari za wingi wa wazao kwa njia ya Isaka (15-19). Alama nyingine za imani (22:20-23:20) Wakati wote Ibrahimu alipokuwa akijaribu kuimarisha familia yake huko Kanaani, pia familia ya ndugu yake Nahori ilikuwa imeongezeka katika nchi ya Mesopotamia. Mwandishi anaeleza habari hizi kama utangulizi wa habari za Rebeka, aliyekuwa mke wa Isaka baadaye (20-24). Huko Kanaani Ibrahimu alikuwa amehama Beer-sheba na kuhamia Hebroni tena, na hapo ndipo alipokufa Sara (23:1-2). Ingawa Mungu alikuwa amemwahidia Ibrahimu na wazao wake nchi yote ya Kanaani, Ibrahimu alikuwa bado hajawa na sehemu ya nchi iliyokuwa mali yake. Kifo cha Sara kilimpa nafasi ya kununua sehemu ya nchi ambayo, pamoja na kuwa uwanja wa mazishi, ilikuwa mfano wa habari kwamba siku moja nchi ile yote ingekuwa mali yake (3-18). Kwa njia ya kuzikwa Kanaani, Ibrahimu na familia yake walionyesha imani yao kwamba Kanaani ilikuwa nchi yao ambayo siku moja wazao wao wote wangeishi (19-20; taz.25:8-10; 49:29-32; 50:13,25; Ebr 11:13,22). Mke kwa Isaka (24:1-67) Isaka angemfuata Ibrahimu kuwa mrithi wa nchi ya Kanaani na kuwa baba mkuu wa taifa lililoahidiwa, kwa hiyo Ibrahimu alitaka mambo mawili kuhusu Isaka. Kwanza, asihame Kanaani; na pili, asimwoe mwanamke wa Wakanaani, kwa sababu wao walikuwa chini ya laana ya Mungu. Kwa hiyo Ibrahimu alimtuma mtumishi wake mkuu (labda Eliezeri, taz. 15:2), aende kaskazini mpaka Mesopotamia, ili amtafutie Isaka mke katika jamaa zake (24:1-9). Mtumishi huyo alimwomba Mungu amwongoze katika kazi hiyo ya pekee (10-14), na baada ya kuhakikisha kwamba Mungu alimwongoza kwa mjukuu wa ndugu yake Ibrahimu, alimtukuza Mungu kwa kujibu maombi yake. Jina la msichana aliitwa Rebeka (15-27). Hatimaye mtumishi alimweleza baba yake Rebeka, Bethueli na kaka yake Labani kwa nini aliamini kwamba Rebeka alikuwa mke ambaye Mungu alimchagulia Isaka (28-49). Walikubali kwa furaha kwamba Rebeka aende akaolewe na Isaka, na hapo mtumishi wa Ibrahimu alitoa zawadi kwa familia ya Rebeka, kama mfano wa mahari, na jamaa wa Rebeka walimpa vijakazi kama zawadi za arusi (50-61). Kisha kundi kubwa lilisafiri kwenda Kanaani, Rebeka alipokutana na Isaka na kuolewa naye (62-67). Wazao wengine wa Ibrahimu (25:1-18) Kabla ya kuendelea na habari za Isaka, mwandishi anamaliza kwanza habari za Ibrahimu, akijumlisha habari za watoto wake wengine. Licha ya Hajiri, Ibrahimu alikuwa amemtwaa mke mdogo mwingine aliyeitwa Ketura (lNya 1:28,32). Lakini kwa sababu Isaka alikuwa mrithi aliyeahidiwa, yeye peke yake aliweza kubaki Kanaani na kupokea urithi kwa Ibrahimu. Kwa hiyo Ibrahimu alitoa zawadi kwa masuria wake na watoto wao akawapeleka mbali, ili wakajenge maisha yao katika uhuru wao mahali pengine. Watoto wale walikuwa mababu wa makabila kadhaa ya Kiarabu (25:1-6). Kulikuwa na ushirikiano mfupi wa Ishmaeli na Isaka wakati wa mazishi ya Ibrahimu (7-11), lakini kwa jumla Ishmaeli na wazao wake waliishi nje ya Kanaani. Ahadi alizopewa Ishmaeli hapo awali zilitimizwa katika ukubwa na uhuru wa makabila makubwa mengi ya Kiarabu yaliyokuwa wazao wake (12-18).