11:27-15:21 ABRAMU AINGIA NCHI YAAHADI Abramu atii wito wa Mungu (11:27-12:9) Mungu alimchagua mtu mmoja kati ya mataifa yote duniani, ili aanzishe taifa jipya kuwa chombo cha kupeleka baraka zake kwa mataifa yote (taz. 12:2-3). Mtu huyo alikuwa mteule wa Mungu, Abramu (aliyeitwa Ibrahimu baadaye). Hapo awali Abramu aliishi katika mji wa Uru wa Wakaldayo (au Babeli ya kale) ambako watu waliabudu miungu. Ingawa jamaa wengine wa ukoo wake waliabudu miungu (Yos 24:2), Abramu alimwabudu Mungu mmoja wa kweli, naye alimtii alipoambiwa ahame Uru. Alihama pamoja na mkewe Sarai (aliyeitwa Sara baadaye), baba yake Tera na Lutu, mtoto wa ndugu yake. Walisafiri kuelekea kaskazini-magharibi katika bonde la Mesopotamia, mpaka walipofika katika mji wa Harani walipoishi kwa muda (11:27-32; Mdo 7:2-4). Baada ya muda, Abramu na Sarai, pamoja na Lutu walihama Harani kwenda kusini kadiri ya agizo la Mungu, mpaka walipofika Kanaani. Abramu aliamini kwamba Mungu angempa nchi bora ya kuishi, ingawa hakujua sawa sawa aende wapi. Aliamini pia kwamba Mungu angemfanya kuwa baba wa taifa kubwa, ingawa mke wake alikuwa tasa, yaani hajaweza kuzaa watoto (12:15; Ebr 11:8-12). Wakati ule Wakanaani waliishi katika nchi ile, lakini Abramu aliamini kwa hakika kwamba siku moja wazao wake wangeishi huko badala yao. Alionyesha wazi imani yake katika ahadi ya Mungu alipojenga madhabahu katikati ya makao ya Wakanaani (6-9). Safari ya kwenda Misri na kurudi (12:10-13:18) Muda mrefu wa ukame bila shaka ulimsababisha Abramu kutia shaka kama nchi ile ya ahadi iliaminika kweli. Mwishowe alisafiri kwenda Misri kutafuta malisho bora kwa wanyama wake (10). Alipoogopa kwamba huenda Wamisri wangeweza kumwua, ili wamtwae mkewe aliyekuwa mzuri sana, alijikinga akisema kwamba alikuwa dada yake. Habari hii ilikuwa kweli, lakini nusu tu, kwa sababu Sarai alikuwa binti wa Tera kwa mke mwingine (taz. 20:12), lakini ilikuwa vibaya kusema nusu ya ukweli tu kwa kusudi la kuficha ukweli wote (11-16). Hata mfalme wa Misri ambaye Abramu alikuwa amemdanganya, alikuwa mkweli zaidi kuliko Abramu. Bila kukawia alimfukuza kutoka Misri kwa kumwaibisha (17-20). Abramu pamoja na nyumba yake yote walirudi Kanaani (13:1). Katika muda wote wa mambo hayo yeye na Lutu walikuwa wamehifadhi makundi yao, nao waliweza hata kuzidisha mali yao (taz. 12:5,16). Kwa kweli, walikuwa na wanyama wengi sana, hata eneo walilohamia, yaani sehemu za kaskazini-magharibi ya Bahari ya Chumvi, halikuweza kutosha kwa makundi yao wote wawili, hata matata yakatokea kati yao (2-7). Kinyume cha tabia yake aliyoonyesha Misri, hapa Abramu aliamua kwa roho ya ukarimu na imani. Alimruhusu Lutu ajichagulie kwanza eneo la malisho ya wanyama, yeye mwenyewe akikubali kuchukua lo lote lililobaki kwa makundi yake. Bila shaka alimtegemea Mungu amwangalie katika nchi aliyomwahidia. Lutu alichagua nchi yote yenye rutuba upande wa mashariki ya Bahari ya Chumvi (8-13). Mungu alijibu imani ya Abramu akirudia ahadi yake kwamba angewafanya wazao wake kuwa taifa kubwa na kuwapa nchi ya Kanaani kuwa nchi yao hasa ya kitaifa. Baada ya hayo, Abramu alikwenda katika maeneo ya malisho yaliyokuwa upande wa magharibi ya Bahari ya Chumvi akafanya makao yake karibu na mji wa Hebroni (14-18). Abramu akutana na Melkisedeki (14:1-24) Ubinafsi wa Lutu katika uchaguzi wake ulimletea matatizo ambayo hakuyatazamia. Kundi fulani la wafalme wa miji midogo ya karibu na Bahari ya Chumvi alipoishi Lutu, walikuwa wamewaasi wafalme wao wakubwa wa Mesopotamia wakachokoza vita. Lutu alitekwa na mali yake yote alinyang'anywa (14:1-12). Abramu hakuwa katika hatari yo yote, lakini alihangaika kwa ajili ya Lutu. Akakusanya jeshi la watu 300 wa watu wake mwenyewe, pamoja na majeshi ya majirani zake akawafuata wachokozi walioanzisha vita vile. Akawastusha maadui kwa mashambulio ya usiku yaliyopangwa vizuri, akawashinda, akamwokoa Lutu na kurudisha mateka yote (13-16). Abramu aliporudi alilakiwa na mfalme wa Sodoma, ambaye Abramu alimrudishia mali yake. Alilakiwa pia na Melkisedeki, mfalme wa mji wa Kikanaani wa Salemu (baadaye uliitwa Yerusalemu) ambaye, kama vile Abramu, alimwabudu Mungu Aliye Juu Sana. Zaidi ya hayo, Melkisedeki alikuwa kuhani wa Mungu. Kwa hiyo alimbariki Abramu, akimkumbusha kwamba, Mungu huyo wala si mwingine, alikuwa mkuu wa mbingu na nchi. Alikuwa ndiye aliyempa Abramu ushindi ule mkubwa. Abramu alikubali hayo, kwanza, kwa njia ya kutoa sadaka kubwa kwa kuhani wa Mungu, na pili, kwa kukataa kupokea thawabu yo yote kutoka kwa mfalme wa Sodoma. Mungu peke yake alitawala mambo ya Abramu katika nchi ya Kanaani. Lakini Abramu alikubali kwa furaha kwamba majirani zake wapate thawabu kutokana na vita vile (17-24; taz. Ebr7:l-10). Agano la Mungu na Abramu (15:1-21) Hapo awali Mungu alikuwa amemwahidi Abramu kuwa taifa na kupata nchi (taz. 12:2; 13:15). Imani ya Abramu kuhusu nchi ya ahadi ilijaribiwa kwa njia ya ukame na matatizo, na imani yake kuhusu taifa lililoahidiwa ilijaribiwa daima kwa njia ya utasa wa mke wake, yaani Sarai kumpata mtoto. Ilikuwa desturi kwa mume na mkewe wasiopata watoto kumpokea mtoto mwingine na kumfanya awe mwana wao. Kwa hiyo Abramu alifikiria habari ya kumpokea mtumwa wake aliyemwamini sana, Eliezeri wa Misri, na kumfanya mrithi. Mungu alimhakikishia Abramu kwamba angempata mtoto wake mwenyewe, na katika yeye angepata wazao wasiohesabika. Abramu akamwamini Mungu, na juu ya msingi wa imani hiyo Mungu alimpokea kuwa mwenye haki (15:1-6; taz. Rum 4:1-5, 13-22). Baadaye Mungu alithibitisha ahadi yake kwa Abramu kuhusu taifa na nchi kwa njia ya kufanya naye agano kama ilivyokuwa desturi ya nchi ile. Kwa kawaida katika maagano ya namna hiyo wanyama wa sadaka walikatwa katikati kuwa nusu mbili, kisha watu wa makundi mawili ya agano walipita katikati ya vipande vile, wakikubali kwamba kifo kilichowapata wanyama wale kiwapate wao wenyewe, kama wangevunja ahadi ya agano lao. Kwa hiyo Mungu alimwagiza Abramu awaandae wanyama (7-11; taz. Yer 34:18). Lakini katika habari hiyo, Mungu peke yake (kwa namna ya mfano wa tanuru ya moshi na mwenge uliowaka) alipita katikati ya vipande vya wanyama waliochinjwa, kwa sababu Yeye peke yake alichukua madaraka ya kutimiza ahadi za agano hilo. Yote yalitegemea neema ya Mungu, nayo yalipokelewa na Abramu kwa imani. Lakini hata hivyo Abramu alitishwa na giza kubwa lililomwangukia, kwa sababu agano lingetimizwa katikati ya upinzani, utumwa, hukumu na kunyanyaswa kwa muda wa karne kadhaa. Mungu angeonyesha uvumilivu kwa watu wa Kanaani na kuwapa nafasi ya kutosha ili watubu, na baada ya uovu wao kuzidi kabisa, angewaruhusu Waisraeli kuwaangamiza na kuteka nchi yao (12-21). Kusudi la Mungu la kuwajenga wazao wa Abramu kuwa taifa la Israeli, zaidi lilikuwa kulitumia taifa hilo ili limlete Yesu Mwokozi. Ahadi ya Mungu kwa Abramu kwamba katika yeye watu wa ulimwenguni kote wabarikiwe, ilitimizwa katika Yesu Kristo ambaye, kwa Yeye watu wa mataifa yote wanaweza kupokea wokovu wa Mungu. Katika hali ya pekee, Yesu Kristo alikuwa mzao wa Abramu aliyeahidiwa (taz. 12:3; Lk 1:54-55,72-73; Gal 3:16). Watu wanaompokea Kristo kwa imani, katika Yeye huyo wanakuwa wazao wa Abramu, na hivyo wanazishiriki baraka alizoahidiwa Abramu (Rum 4:16-17; Gal 3:6-9,29; Efe 3:6). Raha na amani (ya sabato) wanayopewa na Mungu ni zaidi kuliko makao katika nchi ya Kanaani; ni wokovu ulio katika Yesu Kristo (Ebr 4:6-10).