5:1-32 VIZAZIVYA ADAMU MPAKA NUHU Jamii ya wanadamu ilipozidi duniani, inaonekana kama wale waliokuwa waaminifu kwa Mungu walipungua zaidi na zaidi. Kusudi la orodha ya vizazi iliyoandikwa katika fungu hili lilikuwa kuonyesha mstari mwembamba sana wa waamini kutoka kwa Adamu mpaka kwa Nuhu waliotunza na kukabidhiana ujuzi wa Mungu. Orodha hiyo haiwataji wazao wote kuanzia Adamu mpaka Nuhu, bali inateua majina kumi yaliyokuwa muhimu, ili kuonyesha vizazi vile kwa jumla. (Orodha za vizazi zilizofupishwa au kurahisishwa zilitumika mara nyingi nyakati za kale, ili ziwe rahisi kukumbukwa. Katika Mwa 11:10-26 kuna orodha nyingine yenye majina kumi inayounganika na hiyo ya kwanza, ikitaja majina kutoka kwa Nuhu mpaka kwa Abramu. Hali kadhalika orodha ya vizazi ya Bwana Yesu katika Mt 1:1-17 iliacha nje majina kadhaa, ili iweze kuonyesha mpango rahisi wa vikundi vitatu vya majina 14). Neno 'mwana' linaweza kutumiwa kwa kuonyesha uzao tu, na neno 'baba' linaweza kutumiwa kuonyesha kuwa mtu yule alikuwa mmojawao wa mababu (taz. Mt 1:1,8). Watu kumi waliotajwa kwa majina katika orodha ya fungu letu walikuwa wale tu waliojulikana zaidi katika wakati ule wote. Orodha hiyo pia inataja umri wa kila mwanamume alipomzaa mwana aliyekuwa kiungo cha kwanza katika mstari uliomwunganisha yeye na mtu aliyefuata kutajwa kwa jina. Mauti, kama kawaida, ilionyesha matokeo ya dhambi (5:1-20), ingawa habari ya pekee ya Henoko ilidokeza kwamba mauti haikuwa na nguvu siku zote juu ya wale waliompendeza Mungu (21-24; taz. Ebr 11:5). Baba wa Nuhu alionyesha matumaini kwamba nchi na mashamba vingeondolewa laana ya Mungu (25-32). Hali tofauti ya hewa na ya maisha na vyakula labda iliweza kuwa sababu ya maisha marefu sana ya watu wa wakati ule. (Hata ripoti za nje ya Biblia zinaeleza habari za maisha marefu sana ya watu wa wakati ule katika nchi za Mesopotamia.) Kwa hali yo yote, tunaweza kusema kwamba huo ulikuwa mpango wa neema ya Mungu kwa kuona umuhimu wa wanadamu kujaza dunia na kutiisha nchi chini ya mamlaka yao (1:28). Kazi hiyo haikuwa rahisi watu walipokuwa wachache tu, na wale waliokuwepo hawakuwa na maarifa mengi ya ufundi. 6:1-9:29 UOVU WA WANADAMU NA HUKUMU YA MUNGU Uovu wa wanadamu (6:1-8) Watu walipoongezeka na jamii mbalimbali zilipopata maendeleo yake, watu katika uasi wao tena walionyesha tamaa yao ya kutaka kuwa sawa na Mungu na kuishi milele (taz. 3:5,22). Mungu alimwadhibu mwanadamu kwa kupunguza umri wake wa kuishi uwe miaka 120 tu badala ya kuishi maisha marefu kama awali (6:1-4). Lakini watu hawakujali maonyo ya Mungu. Uovu wao ulizidi kuongezeka, mpaka Mungu alipoamua kwamba jambo la pekee la kutenda lilikuwa kuwaangamiza (5-8). Gharika (6:9-8:19) Katikati ya machafuko ya wakati ule alikuwepo mtu mmoja aliyekuwa mwaminifu kwa Mungu. Mungu alitaka kumhifadhi Nuhu pamoja na familia yake, kusudi baada ya kuangamizwa kwa wanadamu wote wa wakati ule, aweze kumtumia yeye na familia yake kwa kujenga jamii mpya (9-12; taz. Ebr 11:7). Chombo cha Mungu cha kuangamiza kilikuwa gharika kubwa. Kama vile Mungu alivyomhifadhi Nuhu na familia yake, alihifadhi pia dume na jike mmoja mmoja wa kila aina ya wanyama, na hivyo alitunza usawa kati ya wanadamu na wanyama. Watu na wanyama wote waliohifadhiwa walikuwa katika jengo kubwa la miti lililofanana na sanduku kubwa mno. Sanduku hilo liliitwa safina nalo lilibuniwa na kujengwa ili liweze kuelea juu ya maji ya gharika. Urefu wake ulikuwa meta 133, upana wake meta 22, na kimo chake meta 13. Lilikuwa na mlango ubavuni, na sehemu ya wazi ya sentimeta 44 kwa ajili ya hewa na mwanga iliyozunguka kote juu, yaani chini ya matokezo ya paa. Maunganiko ya dari tatu na viambaza vya vyumba vyake vyote vilisaidia mambo mawili, yaani wanyama walitengwa katika vyumba, pia jengo la safina lilikuwa imara sana (13-22). Katika wanyama safi Nuhu aliwaingiza wengi zaidi katika safina, ili baadaye waweze kutumiwa kwa ajili ya dhabihu na chakula (7:1-10; taz. 8:20; 9:2-3). Inaonekana kama licha ya mvua kali mno ya siku 40, pia kulikuwa na mabadiliko hata katika nchi. Maji ya kutoka chini na ya baharini yalifura juu ya nchi kwa nguvu sana (11-16). Hata baada ya kuacha kunyesha mvua na hali ya nchi na bahari kutulia tena, ilichukua miezi mingi mpaka maji ya mafuriko yalipotoka tena katika nchi (17-24). Karibu miezi minne baada ya kuacha kunyesha mvua, safina ilitua katika nyanda za milima ya Ararati (8:1-4). Ilikuwa vigumu kwa Ntihu kuona kitu cho chote nje ya safina, lakini aliweza kuona vilele vingine vya milima vilivyoonekana baada ya muda (5). Kwa njia ya kumtuma kunguru kwanza na baadaye njiwa, alichunguza jinsi nchi ilivyoendelea kukauka hata katika sehemu za chini zaidi asizoweza kuziona (6-12). Mwishowe alipoondoa paa la safina aliona wazi kwamba nchi ilikauka sawa sawa, lakini hata hivyo ilimpasa kungojea zaidi mpaka nyasi na mimea mingine vilipoota kiasi cha kutosha, ili wanyama wapate chakula chao. Mwishowe, baada ya miezi saba tangu safina ilipotua, Nuhu, familia yake na wanyama wote walitoka katika safina (13-19). Mwanzo mpya (8:20-9:7) Wakati wa kurudi tena katika dunia iliyosafishwa mbali na dhambi, Nuhu alianza kutoa sadaka kwa Mungu. Ahadi ya Mungu kwamba asingeangamiza dunia tena kwa njia hiyo haikuwa kwa sababu aliwatazamia wanadamu kuwa wema zaidi. Alijua kwa hakika kwamba watu wangekuwa na dhambi kama siku zote. Kama Mungu angetaka kumlipiza mwanadamu kadiri alivyostahili, angepaswa kuleta gharika mara kwa mar a; lakini katika neema yake, Mungu angewaruhusu watu wenye dhambi waendelee kuishi katika dunia yake (20-22). Katika mwanzo huo mpya, Mungu alimpa Nuhu amri zilizofanana na zile alizompa Adamu hapo awali. Mwanadamu bado aliendelea kuwa mjumbe wa Mungu duniani, lakini hata wakati huo hakupewa uhuru kufanya mambo bila ruhusa ya Mungu. Hata katika kumchinja mnyama kwa ajili ya chakula alipaswa kutambua kwamba hakuwa na uhuru na haki ya kutoa uhai wake. Pale alipoambiwa asitumie damu ya mnyama (iliyokuwa kiini cha uhai wake) kwa ajili ya faida yake, alipaswa kutambua kwamba Mungu ndiye aliyekuwa akiumiliki uhai wake. Uhai wa mwanadamu ulikuwa na thamani zaidi kwa Mungu kuliko ule wa wanyama. Kwa hiyo, mtu ye yote aliyemwua mtu mwenziwe bila idhini ya Mungu, hakustahili kuendelea kukifurahia kipawa cha Mungu cha uhai, naye alipaswa kuuawa pia (9:1-7). Agano la Mungu na Nuhu (9:8-17) Agano lilikuwa mapatano baina ya makundi mawili yaliyokuwa na wajibu na uwezekano wa faida au adhabu, kwa kadiri ambavyo mtu alilitimiza au kulivunja agano hilo. Lakini maagano baina ya Mungu na wanadamu yalitofautiana na maagano ya baina ya watu, yaani maagano ya Mungu na wanadamu hayakuwa kama mapatano baina ya makundi mawili yaliyokuwa sawa. Mungu siku zote ni mtoaji, na wanadamu siku zote ni wapokeaji. Ahadi za agano zilitokana na neema ya Mungu, nazo zilithibitishwa na Yeye mwenyewe. Hapo awali Mungu alikuwa ametoa ahadi ya agano kwa Nuhu, ili amwokoe yeye na familia yake (taz. 6:18). Baada ya gharika alitoa ahadi nyingine ya agano ambayo, kama ile ya kwanza, ilitokana na neema yake tu. Agano hilo halikufanywa na Nuhu binafsi tu, bali lilikuwa baina ya Mungu na uhai wote wa duniani ambao ungepatikana katika Nuhu. Mungu asingeangamiza uhai wa duniani kwa njia ya gharika tena (8-11). Alimwonyesha Nuhu upinde wa mvua kuwa ishara yake kwa vizazi vyote, kwamba agano lake lingemtegemea Mungu peke yake, Yeye angelitimiza (12-17). Nuhu na wanawe (9:18-29) Siku moja Nuhu alileta aibu juu ya nafsi yake alipolewa divai, lakini hukumu ya Mungu ilimpata mwanawe, Hamu, na hasa mjukuu wake Kanaani, kwa sababu Hamu alijaribu kuzidisha aibu yake (18-23). Kwa hiyo Mungu alitangaza laana juu ya wazao wa Hamu katika ukoo wa Kanaani, si kwa watoto wengine wa Hamu. Wazao wa Kanaani wangenyang' any wa nchi yao na wazao wa Shemu (taifa la Israeli), na wenyewe wangefanywa watumwa kwa Waisraeli (24-26; taz. Yos 9:23; Amu 1:28; lFal 9:21). Wazao wa Yafethi, walioenea katika sehemu za kaskazini na magharibi katika nchi za Asia Ndogo na Uyunani (Ugiriki), waliahidiwa kushiriki baraka za Shemu. Kwa sehemu fulani hayo yalitimizwa wakati Ekklesia la Agano Jipya lilipoenea kwanza katika maeneo yale, na mataifa mengi zaidi yalifurahia baraka za watu wa Mungu ambazo zamani zilikuwa kwa ajili ya watu wa Israeli tu (27-29; taz. Gal 3:14; Efe 3:6).