2:4-4:26 SIKU ZA KWANZA ZA MWANADAMU Maisha katika bustani ya Edeni (2:4-25) Kuanzia sehemu hii mwanadamu ni mhusika mkuu katika habari za uumbaji. Fungu hili linaeleza tena kwamba dunia haikuwa siku zote kama ilivyo sasa, bali ilitengenezwa hatua kwa hatua mpaka ilipofaa kwa kuishi mwanadamu. Mwanadamu hakuumbwa bila kuwepo kifaa cho chote, bali aliumbwa kutokana na vifaa ambavyo Mungu aliviumba tangu hapo awali. Kama ilivyo kwa wanyama, hata mwanadamu ana asili yake katika vitu vya kawaida vya dunia, kama vile vitamini na dawa nyingine, lakini maisha yake hasa yanategemea uhusiano wake na Mungu ambao hakuna mnyama awezaye kuushiriki (2:4-7). Hali na cheo cha mwanadamu viliumbwa kwa sura ya Mungu, na hivyo mwanadamu alipewa madaraka ili atimize makusudi yake. Kwa hiyo Mungu alimweka katika bustani iliyopendeza sana, ili amfundishe na kumjaribu. Bustani hiyo ilikuwa sehemu ya eneo fulani lililoitwa Edeni, katika nchi ya Mesopotamia (8-14). Vyakula vya aina nyingi vilipatikana huko, na kazi mbalimbali alizotakiwa azifanye pamoja na kulinda bustani hiyo, zilimpa mwanadamu nafasi tele ya kujiendeleza kiakili na hata kwa mwili wake. Aliweza kukomaa kwa njia ya kuamua mambo na kwa kujifunza maarifa mapya. Mungu alitaka mwanadamu aufurahie ukamilifu wa maisha yake ya pekee aliyopewa naye (hata kula matunda ya mti wa uzima), lakini mwanadamu alipaswa kufanya hivyo katika hali ya kumtii Mungu. Kwa kuwa aliumbwa kwa sura ya Mungu, hakuweza kujitenga naye. Hakuwa na uhuru na haki pasipo mipaka kwa kufanya lo lote alilolitaka, yaani kuchagua peke yake kilichokuwa chema au kibaya (kula katika mti wa ujuzi wa mema na mabaya)(15-17). Mkazo katika habari yetu si kwamba miti yenyewe ilikuwa yenye dawa fulani ya mwujiza, bali ilimweka mtu katika uchaguzi, yaani kumtii Mungu katika kila neno, au kujitenga naye na kuamua mwenyewe. Kukua katika hali ya kumtii Mungu kunaleta hali ya kujikana (Ebr 5:8). Hali ya kukomaa huja kwa njia ya kuchagua mema na kukataa mabaya (5:14), na kila ushindi Juu ya majaribu ungalimsaidia mwanadamu kukua kutoka hali ya kutojua, kama ya mtoto, na kufikia hali ya kukomaa ya mtu mzima. Uhusiano wake na Mungu ungalikomaa zaidi, na ujuzi wake wa makusudi ya Mungu ungaliongezeka. Mwanadamu peke yake aliumbwa kwa sura ya Mungu, kwa hiyo hakuna kiumbe kingine duniani kiiichoweza kushiriki naye kimaisha kwa njia ya kumridhisha. Hivyo Mungu alimpa mwenziwe wa aina yake, lakini kwa hali ya kimwili mwanamke, ili awe mwenzi wake. Huyo aliumbwa kwa hali na cheo kile kile, yaani kwa sura ya Mungu (1:27). Mwanamume na mwanamke waliunganishwa kwa hali ya amani na kupatana, kwa jinsi isivyowezekana kwa viumbe vingine vyote (18-25). Mwanamke baadaye alipewa jina la Hawa, maana yake 'maisha' au 'kuishi', kwa sababu kwa njia yake baadaye uhai (taz. 3:20) Kutotii kwa mwanadamu (3:1-24) Mwanadamu aliumbwa kwa sura ya Mungu, naye Mungu alikuwa hana kikomo katika uwezo na ujuzi. Kwa hiyo kulikuwa na mvuto katika wanadamu wa kutaka kuwa bila kikomo pia. Lakini walipaswa kukumbuka kwamba hawakuwa Mungu, bali waliumbwa kwa sura au mfano wa Mungu tu. Hawakuweza kuishi katika hali ya kutengwa na Mungu, kama mfano wa kitu katika kioo, au mfano wa mwezi katika maji usivyoweza kuendelea bila kitu cha asili yake. Ilikuwa kwa sababu ya hali hiyo ya kutegemea au ya kikomo, katika uhusiano wa wanadamu kwa Mungu kwamba Mungu aliweka kikomo katika uhuru wao: Aliwaambia wasile matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya. Kazi ya nyoka ilikuwa kuwajaribu wavuke mpaka uliowekwa na Mungu, wasimtegemee Mungu, bali wajiweke mahali pa Mungu, waamue wenyewe, watawale maisha yao wenyewe, wawe waamuzi wa pekee wa mema na mabaya. Dhambi ya asili ilikuwa kiburi, yaani tamaa ya wanadamu wenyewe kuwa Mungu, na kwa njia hii nyoka alifaulu kuwajaribu wanadamu wamwasi mwumbaji wao (3:1-7). Kwa namna fulani mwanamume na mwanamke walipata ujuzi wa mema na mabaya, lakini kutoka kwa upande wa wenye dhambi waliokuwa na hatia kwa Mungu, si kutoka kwa upande wa Mungu Mtakatifu. Walijua mabaya kwa njia ya kuyatenda, na matokeo yake yalikuwa dhamiri mbaya yenye aibu nahaya(8-13). Tangu wakati huo wanadamu wote, yaani wazao wa Hawa, siku zote walikuwa na uadui na vita dhidi ya dhambi. Lakini hata hivyo ushindi juu ya dhambi uliahidiwa. Nyoka anaweza kumwuma mtu katika kisigino (Kifu ya Yesu), lakini mtu anaweza kumwua nyoka kwa kumponda kichwa (Kifu ya kifu, 1 Kor. 15:54). Mwanadamu alishindwa na dhambi, lakini katika Yesu Kristo, mwanadamu mwishowe angemshinda dhambi, ingawa ushindi huo ungekuwa na mateso (14-15). Machafuko yaliyoletwa na dhambi ya mwanadamu yalileta mateso kwa wanadamu wote. shida tu. Ugomvi uliingia katika uhusiano wa wanadamu, na hata mapatano baina ya mume na mke yaliharibika, kwa sababu ya kutaka kutawala kwa nguvu (16-21). Mwanadamu hakuweza kuendelea kushirikiana na Mungu kwa amani. Alikuwa amekataa uzima wa milele, kwa hiyo Mungu alimnyima uzima huo. Alitaka uhuru kuwa mbali na Mungu, kwa hiyo Mungu alimfukuza mbele yake. Alitaka kuamua mwenyewe yaliyokuwa mema na mabaya, kwa hiyo Mungu alimfukuza na kumpeleka katika ulimwengu ambako angejifunza mema na mabaya kwa njia ya shida na masumbufu yaliyotokana na makosa yake mwenyewe (22-24). Dhambi na mauti ya mwanadamu Kufuatana na Biblia, mauti ya kimwili ya mwanadamu ni matokeo ya dhambi yake (Rum 5:12). Je, kuna jibu kwa swala hili? Adamu alionywa kwamba siku ambayo angefanya dhambi angekufa (taz. 2:17). Alipofanya dhambi, alitoka katika hali ambayo uzima ulitawala, akaingia katika hali ambayo mauti ilitawala. Nafsi yake yote iliingizwa katika hali hiyo, hata kwa kiroho alitengwa na uzima wa milele, na kwa kimwili alijua hakika kwamba siku moja angekufa (Rum 5:12-17). Kazi ya wokovu wa Kristo inageuza matokeo ya dhambi, ikileta ushindi juu ya mauti, yaani mauti ya kiroho na ya kimwili pia (Rum 6:23; 1 Kor 15:21-22). Kristo anamfanya mwanadamu awe kiumbe kipya katika utu wake wote, akimwingiza katika uzima unaomfaa mwanadamu, yaani uzima wa milele. Mwanadamu ni kiumbe cha hali ya dunia hii, na uzima wake unatawaliwa na sheria za hali ya dunia hii, kwa hiyo hana budi kufa, kama vile viumbe vingine vyote vinavyokufa. (Mit.3:19-20). Ilidokezwa kwamba kabla mwanadamu hajatenda dhambi, uzima wa kiroho uliokuwa ndani yake ulikuwa na nguvu sana, hata ukazuia kanuni ya kawaida ya uharibifu au upungufu wa kimwili kama tunavyoweza kufikiri kuwa hali ya viumbe vyote. Dhambi ilibadilisha hali hiyo kabisa, hata upungufu wa nguvu za kimwili haukuweza kuzuiwa tena, na hivyo mauti ilikuwa tokeo la lazima. Hivyo mauti ya kimwili ilikuwa kanuni ya kawaida kama ilivyo kwa viumbe vyote, lakini hapo hapo ilikuwa matokeo ya dhambi. Matokeo ya dhambi katika ulimwengu wote Kuhusu mauti ya viumbe vingine kabla ya kuingia dhambi kwa njia ya Adamu, hatuna haja ya kuufikiria ulimwengu ambamo mauti haikutokea kamwe. Ni mauti ya 'mwanadamu' iliyokuwa matokeo ya dhambi. Viumbe vya mwituni viliishi kabla mwanadamu hajatenda dhambi (taz. 3:1). Simba na chui, papa na wadudu ambao chakula chao cha pekee ni vidudu vingine, bila shaka waliishi huku wakila wanyama wengine, na hivyo walisaidia wanyama wengine wasizidi kujaa duniani, kama wanavyofanya siku hizi. Mungu hakuumba ulimwengu kuwa Paradiso kubwa sana, wala hakumkusudia mwanadamu apoteze wakati wake katika uvivu tu. Kwa kweli, inaonekana kama sehemu kubwa zaidi ya ulimwengu ilikuwa katika hali ya kimwitu, nayo ilimngojea mwanadamu aje na kuleta utukufu wake kamili (Rum 8:19-23). Kazi ya mwanadamu ilikuwa kuitiisha dunia (1:28), yaani kuleta dunia yote chini ya utawala wake. Jambo hili angeweza kujipatia pole pole kwa kadiri ambavyo watu wangeongezeka na kupanua bustani ile kila siku (1:28). Lakini badala yake mwanadamu mwenyewe alianguka katika machafuko. Hali ya juu na ya ustaarabu wa Paradiso ilikuwa katika bustani ya Edeni tu, mahali mwanadamu alipowekwa kwa ajili ya kufundishwa na kujaribiwa. Alipotenda dhambi alifukuzwa kutoka bustani na kupelekwa nje katika ulimwengu wa hali ya kimwitu. Lakini kwa sababu alikuwa amepoteza uzima ule wa kiroho aliopewa na Mungu, hali yake ya kimwili iliyokusudiwa kwanza kwa maendeleo yake, iligeuka kuwa njia ya uchungu na masumbufu yake. Bidii ya kimwili na uwezo wake vilivyokusudiwa kumletea furaha, badala yake vilileta maumivu na ugumu (3:16-19). Kaini na Habili (4:1-16) Wana wawili wa Adamu na Hawa, Kaini na Habili, walitunza imani yao kwa Mungu wakamtolea sadaka. Habili alitoa katika wanyama bora wa kundi lake, akiwa na hali ya unyenyekevu na imani, naye Mungu alimpokea. Tabia ya Kaini ilikuwa ya kiburi na bila ya kumcha Mungu, kwa hiyo Mungu alimkataa (4:1-5; taz. Ebr 11:4; 1 Yoh 3:12). Tabia na maisha ya watoaji wa sadaka vilikuwa na maana zaidi kuliko vitu walivyovitoa, kwa hiyo Mungu alimwambia Kaini kwamba, kama alitaka Mungu ampokee, angepaswa kushinda dhambi iliyokuwa ikitaka kumwangamiza. Dhambi hiyo ilikuwa kama mnyama wa mwitu ajikunjaye na kuotea mlangoni, ili aweze kumshambulia mtu akitoka nje (6-7). Kaini hakuweza kushinda dhambi yake, na katika hasira ya wivu alimwua Habili. Tendo lake la kutwaa uzima wa ndugu yake lilidai kisasi kwa Mungu aliyetoa uhai ule. Kwa hiyo Mungu alimfukuza Kaini aende katika nchi isiyotoa mazao, mbali na mahali walipoishi watu wengine, ambao ingawa walikuwa wenye dhambi, walimwabudu Mungu. Lakini Kaini alidumu katika hali ya kutotubu, na hata hivyo Mungu katika huruma yake kubwa alimlinda asiuawe kwa hali ya kisasi (8-16). Wafuasi wa Kaini na wafuasi wa Sethi (4:17-26) Mwanzo wa kuishi katika sehemu maalumu ulikuwa ni alama za wema na ubaya pia. Kulikuwa na maendeleo ya ufugaji wa kondoo na ng'ombe, pia kulikuwa na maendeleo ya ufundi na utamaduni, lakini kwa upande wa maadili watu walizidi kuwa waovu. Lameki, licha ya kumwua kijana kwa ajili ya kumwumiza kidogo, alitunga wimbo uliotukuza ukatili wake. Kaini alikuwa afadhali kidogo. Alitafuta na alipata kinga fulani ya Mungu, asije akauawa kwa kisasi, lakini Lameki hakujali jambo lo lote, akatisha sana, mtu asije akathubutu kumdhuru (19-24). Baada ya mambo hayo, wazao wa Kaini hawaonekani tena katika habari za Biblia. Kuanzia hapo masimulizi yanaendelea na habari za wazao wa mwana mwingine wa Adamu, Sethi, kwa sababu walikuwa wale walioendelea kumwabudu Mungu (25-26). Adamu na Hawa walizaa watoto wengi, wa kiume na wa kike (taz. 5:4), kwa sababu sehemu ya wajibu wao ilikuwa kusaidia kujaza dunia (taz. 1:28). Katika muda wa miaka mingi makabila mbali mbali ya watu yalipatikana, na watu wale walifanya makao yao mahali tofauti. Lakini Biblia inashughulika na historia inayoendelea na sehemu ndogo tu ya wanadamu wote, yaani wale waliotokana na watoto wa Shemu, ambao Waebrania walikuwa wametokana nao. Katika uzao huo wa Sethi wanadamu walitunza imani yao katika Mungu mmoja wa kweli (Rum 1:20-23).