1:1-2:3 HABARI ZA UUMBAJI Biblia na sayansi Kutokana na uchunguzi wa kisayansi imeonekana kuwa mambo mengi kuhusu maajabu na ukubwa wa ulimwengu yanayoonekana, binadamu anaweza kujiona kuwa ni kiumbe kidogo sana. Lakini Biblia inatazama mambo hayo kwa namna nyingine. Kuhusu mwanadamu Biblia inaeleza kwamba ni kiumbe cha pekee kilichoumbwa kwa mfano wa Mungu. Hii ni habari kuu ya Biblia. Habari za uumbaji ni kama utangulizi tu wa habari za mwanadamu. Inawezekana kwamba kusudi la kusisitiza utaratibu huu ulio muhimu, kuwa Mungu alipanga habari za uumbaji zifae katika muda wa juma moja tu katika ukurasa wa kwanza wa kufungua kitabu cha Biblia chenye kurasa elfu moja. Kamwe Biblia haikukusudiwa kuwa kitabu cha mafundisho ya sayansi. Haishughuliki na aina ya uchunguzi ambao sayansi ya kisasa inatumia. Kama lugha yake ingefaa kwa sayansi ya kisasa, watu wa karne za kale wasingalielewa, na watu wa vizazi vitakavyokuja wangeiona kuwa ya zamani isiyofaa. Kusudi la maelezo ya kitabu cha Mwanzo kuhusu uumbaji haikuwa kufundisha mambo ya sayansi, bali ni kutoa habari fupi na rahisi kuhusu chanzo cha vitu vyote na uhusiano wake na mwanadamu, na katika lugha ambayo watu wa wakati wo wote wanaweza kuelewa. Lugha ya Biblia Kama ilivyokuwa katika Biblia nzima, kitabu cha Mwanzo kiliandikwa katika lugha ya kawaida ya kila siku kama ilivyotumiwa na watu wa wakati ule. Kwa mfano, Biblia inasema habari za ncha nne za dunia (Isa 11:12), na za nguzo, msingi na jiwe la pembeni la dunia (Ayu 9:6; 38:4-6); lakini kutumia maneno hayo kwa kukanusha kwamba dunia ni sayari kungekuwa kutumia Biblia vibaya. Kungeonyesha kueleweka vibaya kwa lugha ya Biblia. Lakini kuelewa vibaya namna hiyo kunatokea. Karne chache zilizopita watu waliamini kwamba jua linazunguka dunia, lakini mtaalamu mmoja wa sayansi aliposema dunia inazunguka jua, alilaumiwa kwamba hakuiamini Biblia. Neno ambalo washtaki wake walilitumia kwa kumshtaki lilikuwa kwamba,' Biblia inasema kuwa dunia inakaa bila kutikisika, na jua linachomoza na kushuka (1 Nya 16:30; MhU 1:5). Biblia inasema habari za mbingu na nchi kama zinavyoonekana kwa watu wakaao duniani. Mtaalamu wa sayansi anaweza kusema habari za jua kama sehemu ya katikati ya anga lote lenye majua mengi, ambapo dunia ni sayari ndogo karibu na jua, na mwezi kuwa sayari ndogo zaidi ifuatayo dunia. Lakini kwa watu wa nyakati za kale, na hata kwetu siku hizi, dunia wanapoishi wanadamu ni sehemu ya katikati ya ulimwengu wao; jua likiwa 'mwanga mkubwa utawalao mchana', na mwezi ukiwa 'mwanga mdogo utawalao usiku'. Tukisoma Biblia, jambo muhimu zaidi si kuelewa yale tu yasemwayo katika Biblia, bali pia kuelewa Biblia ina maana gani katika maandiko yake. Biblia ikisema kwamba Mungu anaketi juu ya duara ya dunia (Isa 40:22), haina maana kwamba Mungu amekaa mahali fulani angani mbele ya upeo wa macho, bali inataka kusema kwamba, Yeye ni Mwenye Enzi yote katika ulimwengu wote pamoja na anga zote. Vile vile kama inasema kwamba Mungu alimtengeneza mwanadamu kutoka katika mavumbi ya ardhi (Mwa 2:7), haina maana kwamba Mungu alishika donge la udongo wa mfmyanzi mkononi mwake akaukanda-kanda mpaka ukatokea kuwa sanamu ya mwanadamu, bali ina maana kwamba Mungu alimwumba mwanadamu kwa vifaa vya kidunia. Hata sisi tuliozaliwa kwa njia ya kawaida tunasema kwamba tumeumbwa kwa udongo na kwa mavumbi ya dunia hii (Ayu 10:9; Mhu 3:20). Mungu katika kazi yake Inafaa watu wachunguze na kutafakari kazi ya Mungu ya kuumba, ili wajifunze maajabu yake (Zab 111:2). Biblia inatuambia kwamba Mungu ni Mwumbaji, nayo inatuonyesha sehemu ya makusudi ya kazi ya kuumba, lakini watu wakitaka kugundua jinsi uumbaji ulivyofanya kazi kwa namna ya sayansi ya fizikia (physics), kazi hiyo itakuwa ngumu, kama Mungu alivyopanga (Mwa 3:19), hatoi ujuzi huo kwa njia ya ufunuo. Kwa mfano, jinsi viungo mbalimbali vya mwili wa binadamu vinavyofanya kazi, ni kazi ya wataalamu wa dawa (Baiolojia) kuchunguza na kueleza, si kazi ya Biblia. Sheria hii inahusika pia katika mambo yote ya sayansi. Sayansi inaweza kutuambia mambo mengi kuhusu uumbaji, lakini inatazama mambo hayo kwa namna nyingine kuliko Biblia. Biblia inatuambia kwamba Mungu ndiye aliyefanya vitu hivi, na sayansi labda inaweza kutuambia jinsi alivyovifanya. Biblia ikituambia kwamba 'Mungu alikifanya hiki' au 'Mungu alikiumba kile', haina maana kwamba alifanya kila kitu katika nukta moja au kwa namna ya kimuujiza. Tunaomba, 'Utupe leo riziki yetu' (Mt 6:11), lakini hatutazamii kwamba Mungu afanye kazi kwa nukta ile ile na kutuwekea chakula kutoka mbinguni katika sahani zetu. Tunamtazamia Mungu atulishe kwa njia za kawaida ya ulimwengu, yaani kuotesha chakula katika nafaka zipatikanazo kwa kazi ngumu. Lakini hata hivyo tunamshukuru Mungu, kwa sababu tunajua kwamba Yeye ndiye atoaye vitu vyote. Mwamini sawa sawa na mtu asiyeamini, anajua kabisa jinsi tunavyopata chakula chetu, lakini mwamini anaongeza neno ambalo mtu asiyeamini hawezi, kwa sababu mwamini anatambua kwamba Mungu anafanya kazi katika hali ya viumbe vyote. 'Sheria za viumbe' ni sheria na kanuni za Mungu. Sayansi inaweza kuhisi jinsi kitu Fulani kilivyofanyika, lakini haiwezi kusema nani aliyekifanya. Mwamini anaweza, kwa sababu 'kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa Neno la Mungu' (Ebr 11:3). Kwa hiyo si jambo la busara kwa mwamini kupinga maneno ya sayansi kila mara akisema, 'Lakini mimi naamini kwamba Mungu alifanya haya', kwa sababu maneno ya sayansi pengine yalionyesha jinsi Mungu alivyofanya jambo fulani. Kama mtaalamu wa sayansi anatuambia jinsi mvua inavyonyesha au jinsi nyasi zinavyokua, hatumpingi tukisema, 'Lakini Biblia inasema kwamba Mungu analeta mvua, Mungu anafanya nyasi zikue' (Mt 5:45; 6:30). Tunakubali kwamba yote mawili ni kweli. Mpango wa maelezo ya kitabu cha Mwanzo Maelezo ya kitabu cha Mwanzo kuhusu uumbaji ni jinsi ambavyo mtu alivyoweza kuona mambo hayo, na kueleza habari za uumbaji kama mtu aliyeishi hapa duniani. Dunia ni sehemu ndogo sana tu ya viumbe vyote vya Mungu, lakini maelezo ya hapa yanahusika hasa na dunia, na hivyo vitu vya nje yake vinatajwa kwa uhusiano wake na dunia tu. Masimulizi ya kitabu cha Mwanzo yanaonyesha kwamba Mungu alifanya vitu vyote bila kuwa na vifaa vya asili, yaani alifanya kazi ya kuumba kuanzia kitu kisichokuwa na sura na hata kukifanya kipendeze, kutoka katika kitu kidogo na hata kukifanya kiwe kikubwa. Yanaonyesha kwa jumla jinsi alivyoleta ulimwengu kutoka katika hali . mbalimbali ya ukiwa na utupu mpaka alipomwumba mwanadamu. Mpango wake wa kimsingi ni kugawa habari za uumbaji katika mafungu mawili ya siku tatu tatu. Siku tatu za kwanza zinaonyesha kwamba Mungu aliumba vitu vya msingi kwa kazi yake, kama vile nuru na giza; bahari na anga; nchi iwezayo kuotesha mimea. Siku tatu zilizofuata zinaonyesha kwamba aliumba nuru ya usiku na mchana; viumbe vya baharini na angani na viumbe vya nchi kavu. Habari hii rahisi ya uumbaji, ingawa haikukusudiwa kuwa ripoti ya kisayansi, lakini bado haipingani na habari hizo. Maelezo yafuatayo yanapendekeza njia moja ambayo kwa namna yake ujuzi wa sayansi ya watu ulioongezeka, ili utusaidie na kutupanulia mawazo kuhusu uumbaji huo, badala ya kututia mashaka katika habari za uumbaji. Uumbaji (1:1-2:3) Kabla ya miaka isiyohesabika, Mungu aliumba mbingu na nchi (ulimwengu wote) kwa kutumia mamlaka na mapenzi ya enzi yake mwenyewe. Hapo mwanzo dunia ilikuwa na ukiwa na utupu, bila kitu cho chote kilichoweza kuvutia macho. Mawingu mazito yenye ukungu na mvuke yalitanda juu ya uso wa nchi na kutia giza katika dunia yote. Lakini mawingu yale mazito ya ukungu na mvuke yalipoanza kupungua, nuru iliweza kupenya kidogo kidogo katika mchana wa jua (1:1-5; siku ya kwanza).Uzito wa mawingu hayo ulipopungua zaidi, mawingu yenye ukungu na mvuke yaliyotanda juu ya nchi yalipanda pole pole kutoka nchini, yakaweka mgawanyiko wazi, chini kukawa bahari, na juu dari ya mawingu mazito (6-8; siku ya pili). Wakati huo dunia ilikauka na nchi ilionekana wazi. Aina fulani za viumbe hai vidogo vidogo vilianza kuonekana. Kwa hiyo hapo ndipo uhai wa hali ya chini ulianza. Aina mbalimbali za udongo na hali ya hewa zilisaidia kuotesha mimea ya aina mbalimbali. Matunda na mbegu zilizopukutika ziliota, na mimea mingi ya kila aina ikaongezeka (9-13; siku ya tatu). Mawingu mazito sana yalipopunguka zaidi na zaidi mwishowe yalikatika. Jua, mwezi na nyota zilizokuwa zimefichwa mpaka hapo, wakati huo zilionekana wazi. Matokeo yake, katika dunia yalisaidia kuleta hali mbalimbali za hewa na kanuni ya misimu ya mwaka (14-19; siku ya nne). Kazi ya Mungu ya uumbaji ilipoendelea, wanyama wa kila aina walitokea, waliokuta mazingira yaliyowafaa, hasa viumbe vilivyokwisha kuwepo katika bahari na anga (20-23; siku ya tano). Nchi iliendelea kujaa kila aina ya viumbe. Mwishowe mwanadamu aliumbwa, akiwa kilele cha viumbe vyote. Kama vile wanyama wote, hata mwanadamu aliumbwa ili aweze kula katika yale yaliyoota katika nchi, naye aweze kuzaa watoto wa aina yake. Lakini mwanadamu alitofautiana na wanyama, naye alipewa mamlaka juu yao, kwa sababu yeye peke yake, kuliko viumbe vingine vyote vya Mungu, aliumbwa kwa sura ya Mungu (24-31; siku ya sita. Tazama maelezo ya 'sura ya Mungu' chini zaidi). Kupumzika kwa Mungu baada ya kumwumba mwanadamu hakuonyeshi kwamba alichoka, au hakufanya kazi yo yote baada ya kazi hiyo (kwa sababu anaendelea kutunza viumbe vyake); bali kunaonyesha kwamba alifikisha kazi yake ya uumbaji katika lengo lake. Baada ya kumwandalia mwanadamu mahali kwa njia ya uumbaji, Mungu wakati huo alimtazamia mwanadamu avifurahie viumbe hivyo vyote pamoja na Mwumbaji wake (2:1-3; siku ya saba). Sura ya Mungu Mwanadamu ameumbwa kwa sura ya Mungu, na kwa hiyo ni kiumbe cha pekee katika viumbe vyote. Kwa namna fulani amefanana na Mungu kwa jinsi isivyowezekana kwa viumbe vingine. Maana ya neno hili kwamba 'sehemu' fulani tu za mwanadamu zinaonyesha hali ya Mungu, kama vile hali ya pekee ya kiakili, ya uwezo na ya kiadili tu. Mwanadamu mzima ni sura ya Mungu. Kwa sababu ya hali hiyo ya Mungu wa milele ndani yake, kwa namna fulani mwanadamu ni mjumbe wa Mungu hapa duniani, na hivyo tunaelewa kwamba Mungu alimchagua mwanadamu awe mtawala wake wa dunia juu ya viumbe vyake (taz. 1:27-28). Bila sura hiyo ya Mungu mwanadamu asingekuwa mwanadamu (kufuatana na maelezo ya Biblia). Angeweza kuonekana sawa na mwanadamu kwa maumbile ya nje, lakini asingemzidi mnyama. 'Unyama' wa mnyama urao katika hali na tabia yake m'wenyewe; ubinadamu wa mwanadamu sivyo. Unamtegemea Mungu katika roho na uwezo wake wa kuishi. Kwa hiyo, ingawa Mungu alimpa heshima sana, mwanadamu hawezi kuishi akitengwa na Mungu. Anaweza kutaka kuishi bila Mungu, lakini kwa hali hii analeta balaa na uharibifu juu ya nafsi yake tu (kama inavyoonekana katika habari za uasi wake wa kwanza, taz. maelezo ya Mwa 2:8-17 na 3:1-24), lakini hawezi kuharibu hali yake ya kuwa sura ya Mungu. Ni sura ya Mungu ndani ya nafsi yake inayomfanya awe mwanadamu.