24:1-28:31 PAULO AONDOKA MASHARIKI NA KWENDA RUMI
Kufungwa Kaisaria kwa miaka miwili (24:1-27)
Mahakamani mbele ya Feliki Wayahudi walimtumia mwanasheria mwenye uwezo ili aendeshe mashtaka dhidi ya Paulo (24:1-4). Walimshtaki Paulo kuwa na hatia tatu. Kwanza, alisababisha ghasia miongoni mwa Wayahudi, na hasa washtaki walijaribu kumsukumia maneno ya kuwa Paulo alichochea uasi wa kupinga Rumi. Pili, alikuwa kiongozi mmojawapo wa Wanazorayo, kikundi cha dhehebu lililoendelea kushiriki bila kibali cha serikaii, na hivyo lingeweza kuasi Rumi. Tatu, Paulo alinajisi hekalu la Yerusalemu (5-9).
Paulo alianza kujitetea akikanusha kwamba hakusababisha ghasia miongoni mwa watu wa Yerusalemu. Hata washtaki wake wasingeweza kuthibitisha tuhuma hiyo (10-13). Pili, alikubali kwamba alikuwa mshiriki wa 'njia He', lakini imani hiyo siyo uzushi, bali ni maendeleo na matimizo hasa ya dini ya Agano la Kale. Njia hiyo haikuwa dhehebu jipya, wala mafundisho yake hayakuwa kinyume. Paulo aliamini habari ya ufufuo wa wafu, kama walivyoamini Wayahudi wengi zaidi, naye alimwabudu Mungu yule yule kama wao (14-16). Mwishowe, hakunajisi hekalu, bali kwa kweli alitimiza kawaida ya dini yake ya utakaso. Na zaidi, alileta pesa za michango, ili kuwasaidia Wayahudi wenziwe katika dhiki zao. Jambo la pekee ambalo Wayahudi wangeweza kumshtakia lingekuwa imani yake ya ufufuo, na hata shtaka hilo lingekubaliwa na kundi moja tu la Wayahudi (17-21).
Feliki aliwajua Wayahudi vizuri, naye alijua kabisa kwamba Paulo hakukosa, lakini kwa sababu ya kuwaogopa Wayahudi hakutaka kumfungua. Hivyo Paulo aliachwa gerezani bila kuhukumiwa kwa miaka miwili, ingawa aliruhusiwa kupokea wageni (22-23,27). Feliki alitaka sana kujua zaidi juu ya imani ya Kikristo, lakini Paulo alipoeleza habari za maisha safi ya haki na hukumu ya baadaye, Feliki aliamua kwamba amesikia vya kutosha. Paulo angeweza kufunguliwa, kama angekubali kulipa rushwa aliyoitafuta Feliki, lakini Paulo alikataa. Kwa hiyo Feliki alimwacha gerezani mpaka Liwali mpya alipofika. Yeye angeweza kuamua kesi hiyo kadiri ya mapenzi yake (24-27).
Hakuna matumaini ya kupata haki katika Uyahudi (25:1-12)
Liwali mpya, Festo, alipofika Palestina, Wayahudi walifanya haraka sana kumshtaki Paulo upya. Bila shaka walidhani kwamba ukosefu wa uzoefu wa Liwali mpya katika mambo ya Kiyahudi ungewasaidia, ili Paulo ahukumiwe (25:1-5).
Kesi ya Paulo mbele ya Festo ilifanana sana na ile ya mbele ya Feliki, lakini Festo alihangaika kwa jinsi ya kuamua. Hakuona sababu ya Paulo kuwa gerezani, lakini pia alitafuta kujipendekeza kwa Wayahudi tangu siku za kwanza za utawala wake. Kwa hiyo alishauri kwamba Paulo aende Yerusalemu kwa hukumu, na Festo mwenyewe awe hakimu wake huko (6-9). Paulo hakuweza kuvumilia zaidi kuvunjiwa haki yake daima. Si Lisia wala Feliki wala Festo hawakuweza kuona kosa kwake, lakini hata hivyo alitunzwa kuwa mfungwa wa Rumi kwa miaka miwili kwa kusudi la kuwaridhisha Wayahudi tu. Paulo aliona wazi kwamba hangepata haki yake kwa Festo wala kwa Sanherdin. Hivyo akaamua kutumia haki ya mwisho ya raia wa Kirumi akakata rufaa kwa Kaisari (10-12).
Paulo aelezewa tena kuwa hana kosa (25:13-26:32)
Kati ya wakuu waliofika Kaisaria ili kumtembelea Liwali mpya na kumwonyesha heshima yake alikuwa Herode Agripa II. Mtu huyo alikuwa mwana wa Herode Agripa I (Liwali aliyetajwa katika 12:1-4, 20-23) na kaka yao Bernisi na Drusila (13; taz.24:24; taz.pia 'Ulimwengu wa Agano Jipya'). Herode Agripa II alikuwa mtawala aliyewekwa na Warumi juu ya maeneo ya kaskazini mwa Palestina, lakini hakuwa na mamlaka katika eneo lililotawaliwa na Festo. Alikuwa mtaalamu katika mambo ya Kiyahudi (taz.26:3,27,31), na Festo alifurahi kumwuliza ushauri katika kesi ya Paulo (14-22).
Tatizo la Festo lilikuwa kwamba alipaswa kumtuma Paulo Rumi ili ahukumiwe na Kaisari, lakini hakujua neno la kumwandikia Kaisari kuhusu kesi yake. Hakujua mashtaka ambayo Wayahudi waliyaleta dhidi ya Paulo au kwa sababu gani walitaka ahukumiwe kifo (23-27).
Paulo alifurahi sana, baada ya siku nyingi za kufungwa bila sababu, kupata nafasi ya kujieleza mbele ya mtawala aliyejua mambo ya dini ya Kiyahudi vizuri (26:1-3). Maelezo yake ya matukio yalifanana na yale aliyoyatoa mbele ya umati wa Yerusalemu kabla ya miaka miwili, ila alibadili mikazo yake kidogo, yaani sehemu alipodhani kwamba ingesaidia zaidi kwa wasikilizaji wake. Kama vile Wayahudi wengi, Paulo aliamini habari ya kufufuka kwa wafu, lakini aliudhiwa na Wayahudi kwa sababu alihubiri kwamba kwa njia ya ufufuo wa Yesu tumaini lote la kale la Kiyahudi lilitimizwa (4-8).
Kwa sehemu Paulo alielewa mawazo ya Wayahudi, kwa sababu yeye mwenyewe awali aliwaudhi wafuasi wa Yesu (9-11). Lakini Bwana Yesu aliyefufuka alimtokea na kumtuma ili ahubiri habari ya msamaha wa dhambi kwa watu wote, Wayahudi na Mataifa bila tofauti (12-18). Agizo hilo alilitimiza kwa furaha, kwa sababu wakati huo alijua kwamba wokovu ulioletwa na Yesu aliye Masihi ulikuwa matimizo ya maneno yote yaliyonenwa na torati na manabii (19-23).
Festo hakuweza kufuata maelezo hayo akafikiri Paulo alichanganyikiwa (24). Lakini Agripa aliyejua habari za Maandiko ya Agano la Kale alielewa maneno ya Paulo. Kwa hiyo Paulo alimsihi amsaidie (25-27). Bila kutaka kuonyesha kwa mtu ye yote kama alikubali au alikataa maneno hayo, Agripa alijibu (ama kwa dhihaka au kwa moyo wa kutojali zaidi) kwamba bidii ya Paulo ya kusema ilizidi, wala asidhani kwamba angeweza kumfanya Agripa kuwa Mkristo kwa maneno hayo machache (28-29). Hata hivyo, Agripa alikubali kwamba Paulo hakutenda neno lo lote liliosababisha kifungo chake (30-32).
Kwa njia ya mifano mbalimbali Luka alimwonyesha Theofilo kwamba Wakristo hawakuwa waasi waliovunja sheria. Licha ya hao waliokwisha tajwa na wasioona hatia kwa Paulo (yaani Jemedari wa jeshi la Yerusalemu, Sanhedrin ya Kiyahudi na Maliwali wawili wa Kirumi), hata mtaalamu wa mambo ya Kiyahudi asiyehusika alimwona Paulo kuwa hana hatia.
Kutoka Kaisaria hadi Rumi (27:1-28:15)
Festo aliwaagiza jemadari na kikosi cha askari wa Kirumi kuwapeleka Paulo pamoja na wafungwa wengine Rumi. Pia Wakristo wawili walifuatana na Paulo, yaani rafiki yake mwaminifu, Luka na kiongozi mmoja wa kanisa la Thesalonike aliyeitwa Aristarko (27:1-2; taz.l9:29; 20:4). Walianza safari yao ya kuelekea Rumi katika meli iliyowapeleka kwanza mpaka Mira ya Asia Ndogo. Huko walibadili na kupanda meli kubwa ya nafaka iliyosafiri kati ya Iskanderia na Italia. Baada ya siku kadhaa wakafika katika kisiwa cha Krete (3-8).
Katika mahali palipoitwa Bandari Nzuri (au Bandari Salama) Paulo aliwashauri wakuu wa meli wakae huko mpaka msimu wa baridi na upepo mkali upite kwanza. Walikataa ushauri wa Paulo wakaamua kuendelea na safari yao wakitumaini kufika Foinike, bandari nyingine ya Krete ambapo walifikiri pangefaa zaidi kukaa kwa muda wa baridi (9-12).
Baada ya muda mfupi tu wote walisikitika kwa kutojali onyo la Paulo. Dhoruba kali ilipiga ikaonekana wazi kwamba meli ingezama na abiria wote wangeangamia (13-20). Paulo hakuamini hayo. Mungu alimhakikishia kwamba, ingawa meli ingepotea, watu wote wangenusurika, na Paulo mwenyewe angefika Rumi (21-26).
Hapa tunaona wazi kipawa cha Paulo cha kuwa kiongozi. Ingawa alikuwa mfungwa, habari yote ilikuwa mkononi mwake. Meli ilipoanza kugusa mchanga na miamba chini, na baadhi ya mabaharia walitaka kutoroka, mlinzi wa Kirumi alifuata agizo la Paulo na kuwazuia (27-32). Paulo alipoonya kwamba watu walikuwa katika hatari ya kufa njaa, mkuu wa meli pia alisikiliza maneno yake (33-38). Heshimaya jemadari wa Kirumi kwa Paulo iliwazuia askari wasiwaue wafungwa meli ilipoharibika. Mwisho watu wote 276 waliokuwa melini walifika pwani salama (39-44).
Kisiwa walichofikia kilikuwa Melita (Malta). Wenyeji wa kisiwa walikuwa wakarimu wakawasaidia wageni, lakini Paulo tena alivutia macho ya watu wote (28:1-6). Ingawa kisheria alikuwa mfungwa tu, yeye na watu wake walikuwa wageni wa heshima wa mkuu wa kisiwa kwa muda wa siku tatu. Kama kwa shukrani kwa fadhili walizopokea kutoka kwa wenyeji wa kisiwa, Paulo na Luka waliweza kutibu wenyeji wengi katika shida zao za kimwili (7-10).
Miezi mitatu baada ya kufika Melita (Malta), msimu wa baridi ulipopita na bahari kutulia tena, Paulo na wengine waliabiri meli nyingine ya nafaka kutoka Iskanderia wakafika bandari ya Puteoli ya Italia. Kutoka huko walisafiri barabarani hadi Rumi huku wakilakiwa na Wakristo wa Rumi sehemu mbalimbali barabarani (11-15).
Paulo jijini Rumi (28:16-31)
Jijini Rumi Paulo alifurahia uhuru wa kiasi. Aliweza kuishi katika nyumba ya mtu binafsi, na watu waliweza kumtembelea bila wasiwasi, ingawa alilindwa daima na askari wa Kirumi (16; taz.mst.30).
Muda mfupi baada ya kufika, Paulo aliwakaribisha viongozi wa Kiyahudi walioishi Rumi waje kumwona. Alijumlisha matukio yaliyomleta Rumi akisisitiza kwamba hakutenda neno lo lote kinyume cha sheria ya Kiyahudi. Aliweka wazi kwamba hakuwa na shtaka lo lote dhidi ya watu wa Kiyahudi. Alikata rufani kwa Kaisari kwa kusudi la kuonyesha kwamba hana hatia yo yote (17-20).
Paulo alishangaa juu ya jibu la viongozi wa Kiyahudi kwamba hawakupata habari yo yote kuhusu tuhuma za Paulo, ingawa walijua kwamba watu walipinga Ukristo kila mahali (21-22). Inaonekana kama Wayahudi wa Yerusalemu walidhani kwamba baada ya Paulo kutoka Palestina, walifaulu katika makusudi yao. Haionekani kwamba walipeleka shtaka lo lote Rumi, kwa sababu kama walikosa kuwapata Feliki na Festo upande wao katika nchi yao wenyewe, hawakuwa na matumaini tena kupata kibali kwa Kaisari huko Rumi ambako Wayahudi kwa jumla hawakupendwa. Zaidi ya hayo, kama Festo alituma barua rasmi, bila shaka iliangamia pamoja na meli ile.
Kama ilivyokuwa desturi yake, Paulo alihubiri ujumbe wake kwa Wayahudi kwanza, akionyesha kutoka Maandiko ya Agano la Kale kwamba Injili aliyoihubiri ni matimizo kamili ya dini ya Israeli. Lakini kama kawaida, Wayahudi wengi walikataa ujumbe wake. Hayo pia, alisema Paulo, yalitabiriwa na Maandiko ya Agano la Kale. Kwa hiyo aligeuka na kupeleka ujumbe wa wokovu wa Mungu kwa Mataifa nao wakaamini (23-29).
Kifungo cha Paulo cha miaka miwili huko Rumi katika nyumba fulani labda kilikuwa na muda wa miezi 18 iliyokuwa nafasi ya sheria kwa washtaki kupeleka mashtaka yao mahakamani. Ilivyoonekana huko Rumi hakuwepo mtu aliyeleta shtaka, kwa hiyo hatua nyingine haikuweza kuchukuliwa. Miezi sita zaidi ya muda ule labda ilitakiwa kwa shughuli za kiofisi kati ya Rumi na Yerusalemu kuhusu kesi hiyo.
Mkazo wa Luka kuhusu miaka miwili ya Paulo jijini Rumi ni wa manufaa, yaani mjumbe kiongozi wa Ukristo aliruhusiwa kuhubiri Injili bila kizuizi jijini Rumi, na maafisa wa Kirumi walipata ujuzi kamili wa kazi yake. Ni wazi kwamba mamlaka ya Kirumi hayakuona Ukristo kuwa dini ya kinyume cha sheria au ya hatari kisiasa. Paulo alitangaza habari ya ufalme wa Mungu katika 'moyo wa ufalme' wa Kirumi sawa sawa na alivyofanya kila mahali. Na kwa habari hiyo ya ushindi Luka alimaliza masimulizi yake (30-31).
Wakati wa baada ya Matendo ya Mitume
PAULO JUINI RUMI
Katika muda wa miaka miwili ya kifungo cha Paulo jijini Rumi watu mbalimbali kutoka nchi za mbali walifika kumtembelea. Habari ambazo Paulo alizipata kutoka kwa wageni hao zilimhamasisha kuandika barua kadhaa, ambazo baadhi yake zimeingizwa katika Agano Jipya.
Barua kwa kanisa la Kolosai
Mtu mmoja aliyemtembelea Paulo Rumi alikuwa Epafra (au Epafrodito), Mkristo kutoka Kolosai ya Asia Ndogo. Kanisa la Kolosai labda lilianzishwa wakati Paulo alipoishi Efeso kwa muda wa miaka mitatu. Wakati ule wanafunzi wa Paulo walipeleka Injili katika miji yote iliyokuwa karibu na Efeso (Mdo 19:9-10). Inawezekana kwamba Epafra alikuwa mtu maalumu aliyesaidia kuanzisha kanisa la Kolosai (Kol 1:6-7; 4:12). Wakati huo tatizo lilitokea katika kanisa na Epafra alishindwa kulitatua. Kwa hiyo alikwenda Rumi kutafuta ushauri kwa Paulo.
Mafundisho ya kigeni na ya kinyume yaliingizwa katika kanisa la Kolosai. Mafundisho hayo yalikuwa aina ya Unostiki katika mwanzo wake, yaani ni falsafa ya kidini iliyounganisha imani ya Kikristo na mithiolojia (=elimu ya visasili) ya Kipagani. Pia ilikuwa na mambo mengine ya Kiyahudi, hasa kuhusu sheria za biashara na sherehe fulani za siri (Kol 2:16,20-21).
Walimu wale wa uongo walijaribu kuunganisha mambo tofauti kabisa ili yaweze kukaa pamoja, kama vile mambo mema na mabaya, roho na mwili au vitu, Mungu na mwanadamu. Waliamini kwamba vitu na viumbe ni vibaya, kwa hiyo walisema kwamba Mungu aliye mtakatifu hakuweza kukutana na wanadamu wenye dhambi. Walifundisha kwamba kuna viumbe vingi sana vya kati, yaani nusu roho na nusu mwili waliosaidia kuziba pengo baina ya Mungu na wanadamu, na Kristo alikuwa mmojawao. Watu walitakiwa kuwaabudu viumbe vile kama walitaka ushindi juu ya uovu, na mwisho wamfikie Mungu (Kol 2:8-10,18).
Paulo alipinga mafundisho hayo ya kinyume akionyesha kwamba Yesu Kristo ni mpatanishi wa pekee baina ya Mungu na wanadamu, naye ni wa pekee awezaye kuwaokoa wanadamu. Yeye ni mwanadamu kamili ambaye kwa njia ya mauti yake aliushinda uovu na kuwafanya wenye dhambi watubuo waunganike na Mungu (Kol 1:15-22; 2:9,15). Umoja huo unamaana kwamba, upande mmoja waamini wanaweza kuwa na ushindi juu ya uovu, na upande mwingine uhai wa Kristo unaweza kuwa ndani yao (Kol 3:3-5,10).
Barua kwa Filemoni
Wakati Epafra alipokuwa kwa Paulo, mtu mwingine kutoka Kolosai alifika Rumi. Mtu yule, Onesimo, alikuwa mtumwa wa Filemoni, Mkristo ambaye kanisa la Kolosai lilikutana nyumbani kwake (Flm 1-2,10).
Onesimo alikuwa amemtoroka Bwana wake akaenda Rumi ili kutafuta maisha mapya ya uhuru. Lakini huko Rumi alikutana na Paulo akaokoka. Alijua kwamba baada ya kuwa Mkristo, ilimpasa kurekebisha makosa yake na kurudi kwa Bwana wake. Lakini aliogopa adhabu ya kawaida aliyopata mtumwa aliyetoroka. Paulo alimjua Filemoni vizuri sana, na hivyo alimwandikia barua akimwomba amsamehe Onesimo na kumpokea tena kama ndugu katika Kristo. Si Filemoni binafsi tu aliyeombwa kumkaribisha upya Onesimo katika nyumba yake, bali pia kanisa limpokee ndugu mpya aliyefaa sana katika ushirika wake (Flm 10-20; Kol 4:9).
Barua kwa kanisa la Efeso
Labda Paulo alisikia kutoka kwa Epafra kwamba mafundisho yale ya kinyume hayakuwepo Kolosai tu. Kwa hiyo aliandika barua nyingine ili ipelekwe katika maeneo yale, kama mafundisho kwa makanisa yote. Barua hiyo, tunayoijua kama Waraka kwa Waefeso, ilikuwa barua kwa waamini wote, wala siyo kwa kanisa moja. Haikutaja habari za watu binafsi wala matukio maalumu ya kanisa fulani, bali ilishughulika zaidi na mambo makuu ya imani na maisha ya Kikristo kwa jumla. Ilitoa mafundisho mengine kuhusu mambo yaliyojadiliwa katika barua kwa Wakolosai, kama vile upekee wa Kristo, ushindi wake juu ya mamlaka, umoja wake na watu wake na matokeo ambayo umoja huo unatakiwa kujenga katika maisha ya Wakristo (Efe 1:20-23; 2:2-6; 4:1,17; 6:12).
Inaonekana kama Waraka kwa Waefeso ilikuwa barua mojawapo ya barua kadhaa zilizofanana ambazo Paulo alizituma kwa makanisa ya maeneo yale. Labda jina la kanisa lililopokea barua liliandikwa katika utangulizi wa kila barua ilivyotolewa. Ikiwa hivyo, tunaelewa kwa nini baadhi ya maandiko (manuscripts) ya kale yana neno 'Waefeso' katika utangulizi wake na mengine hayana neno hilo (Efe 1:1). Inawezekana kwamba barua ya Paulo kwa kanisa la Laodikia ilikuwa nakala nyingine ya barua hiyo (Kol 4:16). Mtu aliyepeleka barua hizo, yaani Tikiko, pia alichukua habari za hali ya Paulo huko Rumi (Efe 6:21-22; Kol 4:7-9).
Ingawa Paulo alikuwa mfungwa jijini Rumi, hakuwa peke yake. Luka na Aristarko waliokuja naye kutoka Kaisaria, bado walikuwepo (Kol 4:10,14; Flm 24). Hata Marko na Timotheo waliokuwa wamesafiri pamoja naye katika safari yake ya kueneza Injili walikuwepo (Kol 1:1; 4:10; Flm 24). Pia alikuwepo Myahudi aliyeitwa Yesu Yusto (Kol 4:11) na rafiki mwingine, Dema (Kol 4:14; Flm 24). Bila shaka marafiki zake miongoni mwa Wakristo wa Rumi walimtembelea mara nyingi (Rum 16:1-15).
Barua kwa kanisa la Filipi
Labda ilikuwa wakati wa miaka ile miwili jijini Rumi Paulo alipoandika barua kwa Wafilipi. Barua hiyo inasema kwamba Paulo alikuwa mfungwa wakati wa kuandika barua hiyo (Flp 1:13), lakini haielezi mahali alipofungwa. Habari za maisha yake zinaonyesha kwamba alifungwa mara nyingi na katika hali tofauti (Mdo 16:23; 22:23-30; 24:23-27; 28:16,30; 2Kor 11:13), lakini kifungo cha wakati huo huko Rumi kinaonekana kuwa kinafaa zaidi kwa kuwaandikia Wafilipi.
Kanisa la Filipi lilionyesha lilivyomfikiria sana Paulo lilipomtuma mshiriki wake, Epafrodito (au Epafra), ili amsaidie na kumpelekea msaada kutoka kanisa. Paulo aliandika ili kuwashukuru Wafilipi kwa msaada wao (Flp 1:5; 4:18) na kurekebisha tabia mbaya zilizotokea katika kanisa (Flp 2:1-4,14; 4:2-4). Wafilipi wasikate tamaa kwa sababu ya kufungwa kwake, kwa sababu alipata nafasi nyingi ya kuhubiri na kufundisha (Flp 1:12-14). Wakristo wa Rumi waliweza kumsaidia, miongoni mwao walikuwa wengine waliofanya kazi serikalini (Flp 4:21-22).
PAULO ATEMBELEA MAKANISA TENA
Huru tena
Ingawa matokeo ya kesi yake yalikuwa na mashaka kwa muda mrefu, Paulo aliendelea kuwa na matumaini kwamba angefunguliwa. Aliwaandikia Wafilipi kwamba alitazamia kuwatembelea baada ya muda mfupi (Flp 1:25,27; 2:24), na kabla yake alimwandikia Filemoni kuhusu mipango yake ya kutembelea Kolosai (Flm 22). Kuna dalili za uhakika kwamba baada ya kifungo cha miaka miwili Paulo alifunguliwa tena. Matukio ya baada ya kufunguliwa huko hayana uhakika, lakini kutokana na madokezi mengine aliyofanya katika barua zake kwa Timotheo na Tito, tunaweza kuhisi juu ya safari zake ambazo labda aliweza kuzifanya.
Kuwasaidia Timotheo na Tito
Sehemu moja Paulo alipotembelea baada ya kufunguliwa Rumi, ilikuwa kisiwa cha Krete. Inaonekana kama miongoni mwa watu waliofuatana naye katika safari hiyo walikuwa Timotheo na Tito waliokuwa pamoja naye hata katika safari za zamani. Paulo alitambua kwamba makanisa ya Krete yalikuwa katika hali ya machafuko, hasa kwa sababu ya kazi ya walimu wa uongo. Kwa hiyo walikaa huko kwa muda fulani, ili awasaidie kurekebisha matatizo yao, lakini alipopaswa kwenda sehemu nyingine, alimwacha Tito Krete, ili aendelee na kazi ya huko na kuimarisha uongozi katika makanisa (Tit 1:5).
Paulo alipofika Efeso, alikuta matatizo mengine ya mafundisho yale maovu. Hapo awali alikuwa amewaonya wazee wa kanisa la Efeso kwamba walimu wa uongo wangesababisha machafuko katika kanisa (Mdo 20:29-30), na wakati huo mambo hayo yalionekana. 'Wataalamu' waliokuwa wamejiweka wenyewe walikuwa wakiharibu kanisa kwa njia ya mafundisho yasiyofaa na yaliyojengwa juu ya msingi wa hadithi za kale, sheria mbalimbali na orodha za vizazi (1Tim 1:4-7; 4:1-3; 6:3-5). Baadhi ya mafundisho yalikuwa yenye uharibifu zaidi, kiasi kwamba Paulo aliamini kwamba njia ya pekee ya kushughulika na wachokozi wasiotubu ilikuwa kuwafukuza kutoka kanisa (ITim 1:19-20).
Baada ya muda Paulo aliondoka Efeso kwenda Makedonia, lakini alimwacha Timotheo ili aendelee na kulisaidia kanisa (ITim 1:3). Huko Makedonia Paulo bila shaka alitimiza hamu yake ya kulitembelea kanisa la Filipi tena (taz.Flp 2:24; 4:1). Lakini alihangaika kuhusu watu wawili aliokuwa amewaacha Krete na Efeso, akaamua kuwaandikia barua. Barua hizo mbili, yaani ya Tito na ya kwanza kwa Timotheo, zinafanana kwa njia nyingi, ingawa ile kwa Timotheo ni ndefu na ya binafsi zaidi.
Katika barua zote mbili Paulo anawatia moyo wafanyakazi wenzake wawe na ujasiri kwa kutekeleza kazi waliyokabidhiwa (ITim 1:3,18; 4:6,11-12; Tit 1:5; 2:15), kupanga utaratibu fulani kuhusu uongozi katika makanisa (ITim 2:1,8; 3:1-13; 5:17; Titl:6-9; 2:2-8), kuwafundisha watu katika ukweli wa Kikristo (ITim 3:14-15; 4:13-14; 6:20; Tit 2:1; 3:8) wala wasipoteze wakati kwa kuhojiana juu ya mambo yasiyo ya maana (ITim 4:7; 6:20; Tit 3:9).
Kufungwa tena
Muda fulani baada ya kuandika barua za 1 Timotheo na Tito, Paulo aliondoka Makedonia. Hatuna uhakika kuhusu njia aliyoshika, lakini baadhi ya makanisa aiiyoyatembelea yalikuwa ya Korintho kusini mwa Ugiriki na Mileto katika pwani ya magharibi mwa Asia Ndogo (2Tim 4:20). Pia alitembelea Troa kaskazini zaidi. Habari ya kuwa huko Troa aliacha baadhi ya vitu vyake vya thamani inadokeza kwamba, inawezekana alifungwa huko na kulazimishwa kuondoka kwa haraka (2Tim 4:13). Kutoka mahali po pote alipofungwa, alipelekwa Rumi tena, na kutoka gerezani aliandika barua yake ya mwisho, yaani 2Timotheo (2Tim 1:8; 2:9).
Wakuu wa Rumi walipomshtaki Paulo, baadhi ya marafiki zake walimwacha, lakini Mungu aliyekuwa naye siku zote, alimwokoa kutoka hatari zaidi na kumwezesha kushuhudia Injili mbele ya maafisa wakuu wa Kirumi (2Tim 4:16-17). Hata hivyo, hakuwa na matumaini aliyokuwa nayo wakati wa kifungo chake cha kwanza. Badala ya kutazamia kufunguliwa, aliona angekabiliwa na kuuawa (2Tim 4:6-8).
Akijua kwamba amebakiwa na muda mfupi tu, Paulo alimwandikia Timotheo, ili kumtia moyo na kumwomba mambo mengine ya umuhimu. Kanisa la Efeso bado lilikuwa na shida ya walimu wa uongo, na Paulo alitaka Timotheo asimame imara na kufundisha ukweli wa Kikristo (2Tim 1:6-8,14; 2:3; 15; 3:14-17; 4:2,5). Wakati huo huo asipoteze wakati kwa kuhojiana na watu ambao nia yao hasa ilikuwa kufanya matata (2Tim 2:14,16,23; 3:5).
Watu wawili ambao bila shaka wangemsaidia sana Timotheo katika kazi yake ngumu walikuwa Akila na Prisila. Wao wawili wakati huo walikuwa Efeso baada ya kuishi Rumi mara ya pili kwa muda (2Tim 4:19; Mdo 18:2,18-19,24-26; Rum 16:3). Familia ya Onesiforo waliomsaidia Paulo huko Rumi, pia walirudi Efeso, nao pia walikuwa watu wa kutegemewa kuwa msaada kwa Timotheo (2Tim 1:16-18; 4:19).
Kuuawa kwa ajili ya Bwana jijini Rumi
Maombi kadhaa ya haraka ambayo Paulo alimtumia Timotheo yanadokeza hali ya kukata tamaa ya kifungo chake cha mwisho. Hali akifungwa katika chumba cha baridi na kuhatarisha afya, aliona baridi na kutamani kusoma vitabu vyake (2Tim 4:13,21). Dema aliyekuwa naye kwa uaminifu wakati wa kifungo cha kwanza, wakati huo alikuwa amemwacha (Kol 4:14; 2 Tim 4:10). Wengine walikwenda sehemu mbalimbali katika kazi ya kumtumikia Mungu (2Tim 4:10-12). Baadhi ya Wakristo wenyeji wa Rumi walimtembelea (2Tim 4:11).
Watu wawili aliowataka sana waje na wawe pamoja naye katika siku zake za mwisho walikuwa Timotheo na Marko, yaani ndugu wale wawili ambao kama vijana wakati wa safari za kwanza za kueneza Injili walitembea pamoja na Paulo. Marko labda alikuwa Kolosai, mji wa karibu na Efeso. Kwa hiyo Timotheo hangekuwa na shida kumchukua huko (2Tim 4:9,11; taz.Kol 4:10). Kama walifika Rumi mapema ya kutosha na kumkuta Paulo hatujui. Mtume mkuu wa Mataifa ambaye katika huduma yake yote ya miaka mingi alikuwa akikabiliwa na hatari ya kifo katika mikono ya Wayahudi, mwisho aliuawa kwa kukatwa kichwa na mamlaka ya Rumi (kama mwaka wa 62 b.K.).
KAZI ZA PETRO ZILIZOENEA SANA
Kuwatia moyo walioudhiwa
Wakati ule adha dhidi ya Wakristo ilizidi katika nchi zote za madola ya Kirumi. Katika muda wote Ukristo ulipotazamiwa kuwa tawi la dini ya Kiyahudi ulilindwa na sheria, kwa sababu dini ya Kiyahudi ilikubaliwa na serikali. Lakini tofauti baina ya Uyahudi na Ukristo zilionekana wazi machoni pa watu kwa jumla. Wayahudi wa Yerusalemu walipomwua Yakobo, ndugu wa Bwana (kama wakati ule ule Paulo alipouawa Rumi), kila mtu aliweza kuona wazi kwamba Ukristo haukuwa dhehebu au tawi la Uyahudi, bali ulihesabiwa rasmi kuwa dini tofauti isiyokuwa na kibali cha serikali.
Zaidi ya hayo, Wakristo walichukiwa kwa sababu hawakuweza kuchangamana na wenyeji wengi ambao katika maisha na tabia zao walitafuta ibada ya miungu na anasa za zinaa. Kaisari Nero, aliyeanza utawala wake wa ukatili miaka kumi ya awali, wakati huo alianza kupata wazimu wake, tena alikuwa adui mkali wa Wakristo. Aliwasukumia Wakristo hatia kwamba wao ndio waliowasha moto mkubwa jijini Rumi (mwaka wa 64 b.K.). Matokeo yake, adha kali sana dhidi ya Wakristo ilianza. Wakati kama huo Mtume Petro aliandika barua tunayoijua kuwa Waraka wa kwanza wa Petro. Makusudi yake yalikuwa kuwatia moyo Wakristo ili wavumilie adha kwa imani thabiti, hata kama ingekuwa na maana ya kufa kwa ajili ya Bwana (IPet 2:20-23; 3:14-15; 4:12-19), na kuwahakikishia matumaini yao hai na wakati wa utukufu hapo baadaye (IPet 1:3-9).
Lakini Petro alikuwa wapi miaka hiyo yote? Mara ya mwisho tunasoma habari zake katika Matendo ya Mitume alipokuwa katika mkutano ule mkubwa pamoja na Paulo na wengine jijini Yerusalemu. Tangu wakati huo miaka 13 au 14 ilipita (Mdo 15:6-7; 12-13). Kwa hiyo turudi katika wakati wa baada ya mkutano huo, ili tujaribu kujaza baadhi ya mapengo katika ujuzi wetu kuhusu historia ya Petro.
Petro na Marko
Barnaba alipoachana na Paulo kabla ya safari kubwa ya pili ya kueneza Injili, alikwenda Kipro akimchukua Yohana Marko, ambapo Paulo na Sila walipitia Asia Ndogo mpaka Ulaya (Mdo 15:36-41). Kutokana na ripoti za historia ya wakati ule, tunajua kwamba, baada ya Barnaba na Marko kumaliza kazi zao huko Kipro, Marko aliambatana na Petro. Kisha watu hao wawili walifanya kazi pamoja kwa miaka kadhaa wakihubiri na kufundisha katika maeneo ya kaskazini mwa Asia Ndogo ambapo Paulo alikatazwa na Roho Mtakatifu asiende (Mdo 16:7-8; IPet 1:1). Kuna thibitisho la kudokeza kwamba baada ya kazi ile, Petro na Marko walikwenda Rumi kwa muda na kuwafundisha Wakristo wa huko. Petro alipoondoka, Marko alibaki. Wakristo wa Rumi wakamwomba Marko aandike historia ya Bwana Yesu, kama walivyokuwa wameisikia kwa Petro. Marko akafanya hivyo, na matokeo yake ni Injili ya Marko.
Marko na Luka
Wakati kama huo Paulo alifika Rumi akiwa mfungwa katika kifungo chake cha kwanza, akiwa pamoja na Aristarko na Luka (Mdo 28:16,30; taz.27:2). Kwa hiyo Marko na Luka walikuwa Rumi Paulo alipoandika barua za kifungo chake cha kwanza, na bila shaka walijuana vizuri sana (Kol 4:10,14; Flm 24). Kwa muda wa miaka kadhaa Luka alikuwa akikusanya na kuandaa habari kwa ajili ya kitabu alichotaka kukiandika, na alipofika Rumi alifurahi kukuta masimulizi ya Marko yamemalizika. Aliweza kutumia baadhi ya habari za Marko na kuziingiza katika kitabu chake ambacho baadaye kilitokea kuwa juzuu mbili, yaani Injili ya Luka na Matendo ya Mitume.
Katika Injili yake na katika Matendo ya Mitume Luka alitaka kuonyesha kwamba Yesu Kristo alikuwa Mwokozi wa Mungu kwa watu wa kila mahali bila ya kujali ukabila (Lk 2:32; 3:6-8; 4:25-27; 7:9), na wafuasi wake walikuwa na wajibu wa kueneza ujumbe wa wokovu huo kote duniani (Lk 4:18; 19:10; 24:47). Habari ya kuwa wafuasi wa Yesu waliwasaidia maskini, wagonjwa, watu walioonewa na wengine wenye shida ilionyesha kwamba walijifunza kutoka kwa Bwana wao (Lk 6:20; 7:12,22; 13:11; 17:16).
Petro na Sila
Baada ya Paulo kufunguliwa kifungo cha kwanza, Marko pia alitoka Rumi. Baadaye Paulo alifungwa Rumi tena, na alipofikiri kwamba alikuwa karibu na kuuawa, alituma ujumbe kwa Marko na Timotheo waje kwake (2Tim 4:9,11). Kama walifika Rumi kabla ya kuuawa kwa Paulo au sivyo hatujui, lakini inaonekana kama Marko aliendelea kuishi Rumi naye bado alikuwepo Petro alipotembelea jiji hilo tena (IPet 5:13). (Wakristo wa wakati ule waliita Rumi kwa jina la mfano, yaani Babeli, maana yake makao makuu ya upinzani dhidi ya Mungu uliopangwa rasmi.) Wakati huo Sila alitembea pamoja na Petro (ni mtu yule yule aliyetembea na Paulo katika safari yake ya pili). Petro akimtumia Sila kuwa mwandishi wake, aliandika barua iliyotajwa hapo juu (yaani Waraka wa kwanza wa Petro), akaituma katika makanisa ya sehemu za kaskazini mwa Asia Ndogo, yaani katika sehemu zile Petro aliposaidia kuhubiri Injili na kuanzisha makanisa (1 Pet 1:1; 5:12).
Petro na Yuda
Baada ya mwaka mmoja hivi, Petro alipokuwepo Rumi, alisikia habari za bidii ya walimu wa uongo katika makanisa yale aliyokuwa ameyaandikia barua yake. Hivyo aliyaandikia barua ya pili inayojulikana kuwa Waraka wa pili wa Petro (2Pet 3:1). Katika barua hiyo Petro aliwapinga walimu wa uongo, waliodai kwamba hakuna uhusiano baina ya imani na tabia, na hivyo maisha ya zinaa n.k. hayakuwa kosa kwa wale waliokuwa na ujuzi wa hali ya juu kuhusu mambo ya kiroho (2Pet 1:5-7; 2:1-3). Petro pia aliwapinga wale waliodhihaki imani ya Wakristo kuhusu kurudi kwake Kristo. Aliwahamasisha watubu kabla ya kuchelewa, kwa sababu kurudi kwake Kristo pia kungeleta hukumu ya mwisho (2Pet 3:3-4,9-10).
Wakati wa kuandika barua hiyo, labda Petro alikabiliwa na kuuawa (2Pet 1:14; taz.Yn 21:18-19). Kufuatana na mapokeo ya karne ya kwanza, Petro alisulibiwa Rumi katika nusu ya pili ya mwongo wa 6b.K.
Aina ya mafundisho ya kinyume yaliyoshughulikiwa katika 2Petro yalisababisha wasiwasi zaidi na zaidi katika makanisa. Barua nyingine ya Agano Jipya iliyoandikwa kwa kusudi la kupinga kwa ukali mafundisho hayo ni ile ya Yuda (Yud 4,19). Mwandishi wa barua hiyo huaminiwa kuwa ndugu yake Bwana, naye sawa sawa na kaka yake Yakobo, alimwamini Yesu baada ya kufufuka kwake (Mk 6:3; Yn 7:3-5; Mdo 1:14). Kufanana kwa barua yake na ile ya 2Petro kunadokeza kwamba waandishi hao wawili walitumia aina ya mafundisho ya kuwapinga walimu wa uongo iliyotumiwa sehemu mbalimbali. Mafundisho yale ya mchanganyiko wa uharibifu wa falsafa na dini yalikuwa aina nyingine ya Unostiki uliotaabisha makanisa ya karne ya kwanza.
MWISHO WA WAKATI WA KWANZA WA UKRISTO
Wakristo wa Kiebrania wanakufa moyo
Adha dhidi ya Wakristo ilipozidi chini ya utawala wa Kaisari Nero, baadhi ya Wakristo wa Kiyahudi walianza kujiuliza kama walifanya vizuri walipoacha Uyahudi na kupokea Ukristo. Walikuwa wameamini kwamba dini ya Agano la Kale imepata utimilifu wa makusudi yake katika Kristo, na hekalu la Yerusalemu libomolewe. Lakini miaka 30 baada ya kifo cha Yesu hekalu bado halijabomolewa na desturi za dini ya Kiyahudi ziliendelea kama kawaida.
Kwa Wakristo wengine wa Kiyahudi ilionekana kama dini ya Kiyahudi ilikuwa na nguvu yake daima ambapo Ukristo ulizidi kupata shida. Wengi wao walikata tamaa wakaacha kuhudhuria mikutano ya kanisa, na wengine waliacha kabisa imani yao ya Kikristo na kurudia Uyahudi. Waraka kwa Waebrania uliandikwa kwa makusudi ya kurekebisha mawazo yale na kuzuia ukengeufu (Ebr 6:4-6,9-12; 10:23-25,35-39).
Mwandishi wa barua hiyo hakutaja jina lake, ingawa bila shaka alijulikana sana kuwa mwalimu mwenye kipawa katika wakati wake. Labda alikuwa Myahudi (Ebr 1:1), na yeye mwenyewe pamojana wasomaji wake walipata Injili kwa njia ya Mitume au wengine waliokuwa wamemwona na kumsikia Yesu (Ebr 2:3). Barua haisemi Wakristo wale wa Kiyahudi waliokata tamaa waliishi sehemu gani, lakini mwandishi alitegemea kuwaona baada ya muda mfupi (Ebr 13:19).
Kwa njia ya mifano mbalimbali mwandishi alilinganisha upungufu wa mipango ya dini ya Kiyahudi na ukamilifu wa Kristo. Kila jambo la wakati wa kale lilikuwa la muda tu, halikukamilika wala halikutosha, lakini lilipata utimizaji katika Yesu. Kristo ni Mkuu na wa juu kabisa kuliko manabii, malaika, viongozi na makuhani, na sadaka yake moja ilifanya yale ambayo sadaka zote za mpango wa torati zilishindwa kufanya (Ebr 9:11-14; 10:11-18). Kama iliwapasa Wakristo wa Kiyahudi kuteswa kwa ajili ya imani yao katika Injili hiyo, waliyapata yale yale tu ambayo waaminifu wote wa Mungu waliyapata. Lakini waaminifu walivumilia (Ebr 11:36-40; 12:1-2; 13:23). Hata Yesu Kristo aliteswa, lakini Yeye naye alivumilia, na wakati wa Mungu ulipotimia, alipata ushindi wa utukufu (Ebr 12:2-4).
Mwisho wa ushirika na Uyahudi
Wakati wa mwongo wa sita wa karne ya kwanza kulikuwa na hisia ya kutotulia na wasiwasi kati ya wenyeji wa Kiyahudi wa nchi ile. Hasira yao haikuwa zaidi dhidi ya Wakristo, bali walichukia serikali ya Rumi. Wayahudi wengi siku zote waliwachukia Warumi, lakini hasira yao ilizidi kwa kadiri Maliwali wao wa Uyahudi walivyotawala mambo ya Kiyahudi vibaya. Wayahudi wenye mawazo ya siasa kali wakati huo waliandaa uasi mkubwa wa kupigana vita na Warumi.
Vita vilipoanza, Wayahudi walitiwa moyo kwa ushindi wa sehemu mbalimbali, lakini hawakuweza kushindana na nguvu kubwa ya jeshi la Rumi kwa muda mrefu. Mwisho mambo yakageuka yakawa mabaya zaidi. Majeshi ya Rumi yakaja, na baada ya kuteka nchi za Galilaya, Perea na Uyahudi, walizingira jiji la Yerusalemu. Kwanza Wayahudi walijitetea, lakini mwaka wa 70 b.K. jiji lilitekwa, na sehemu kubwa ya jiji pamoja na hekalu lilibomolewa kabisa. Ingawa mambo hayo yalidhoofisha nguvu ya Kiyahudi, yalitokea kuwa wema kwa Wakristo, kwa sababu kwa njia hii kamba zote za zamani zilizowaunganisha Wakristo na Uyahudi na hekalu zilikatwa kabisa.
Kuhifadhi masimulizi ya Injili
Mpaka wakati huo ilikuwa miaka kama 40 hivi tangu kufa na kufufuka kwake Yesu Kristo. Wengi wao waliokuwa mashahidi wa maneno na matendo ya Yesu, walihama kwenda nchi nyingine na wengine walikufa. Wakristo walitaka kuhifadhi mafundisho ya Yesu yaliyoenezwa na kuelezwa na watu wale, kwa hiyo maandiko mbalimbali na masimulizi ya maneno maalumu kuhusu mafundisho na matendo ya Bwana Yesu yalianza kukusany wa (Lk 1:1-2).
Tumekwisha ona jinsi Marko alivyoandika muhtasari wa mafundisho aliyoyasikia kwa Petro kwa ajili ya Wakristo wa Rumi, na muda ulipoendelea maandiko yale yalitumiwa katika makanisa mengi. Luka naye aliandaa na kuandika habari zile, na ingawa kitabu chake kwanza kilikusudiwa kwa mtu binafsi (labda mkuu fulani wa serikali), kilienea sana. Wakati huo mtu mwingine, yaani Mathayo, aliandika Injili yake. Alisaidiwa katika kazi yake kwa kutumia baadhi ya yale yaliyoandikwa na Marko na maandiko mengine, akaongeza yale aliyoyashuhudia mwenyewe katika maisha ya Bwana. Kusudi na lengo lake lilikuwa kuandika mafundisho na matukio ya maisha ya Yesu yalivyojulikana zaidi katika maeneo ya Wayahudi walioishi Palestina. Kwa sababu hii kitabu chake kina maneno mengi yanayolingana na imani ya Wayahudi.
Mathayo alitaka kuonyesha kwamba Yesu alikuwa Masihi aliyeahidiwa (Mt 9:27; 11:2-6), yaani yule aliyeonyeshwa katika Agano la Kale (Mt 2:5-6; 12:17-21), utimizaji wa makusudi ya Mungu kwa ajili ya Israeli (Mt 1:17; 5:17) na mfalme ambaye kwa njia yake ufalme wa Mungu ulikuja ulimwenguni (Mt 4:17; 12:28; 27:11). Wale waliotubu na kuiamini Injili walikuwa watu wa ufalme wa Kristo, bila kujali ukabila wao, ambapo wale walioshikamana na mapokeo ya dini ya Kiyahudi hawakuwemo (Mt 3:7-10; 8:11-12; 21:43; 23:23-28).
Kwa hiyo Wakristo wa Kiyahudi walionywa wasije wakaanguka katika makosa ya Wayahudi wasioamini. Walipaswa kujenga tabia iliyokuwa zaidi kuliko kutimiza sheria mbalimbali tu (Mt 5:22,28,42; 20:26), nao walipaswa kueneza Habari Njema ya ufalme kwa watu wote bila kujali ukabila au utaifa wao (Mt 5:13-16; 12:21; 24:14; 28:19-20).
Injili ya nne
Karibu na mwisho wa karne ya kwanza masimulizi mengine ya huduma ya Kristo yalitokea, wakati huo mjini Efeso. Mwandishi wake alikuwa mtu wa mwisho aliyebaki hai katika kundi la Mitume, yaani Yohana, 'mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda' (Yn 21:20,24). Wakati ule Injili nyingine tatu zilijulikana sehemu nyingi. Kwa hiyo Yohana hakuandika masimulizi mengine kuhusu huduma ya Yesu, bali alichagua matukio kadhaa na kuonyesha makusudi ya ujumbe wake. Matukio yale mengi yalionyesha miujiza (au ishara) iliyoonyesha kwamba Yesu alikuwa Masihi na Mwana wa Mungu (Yn 20:30-31). Kwa kawaida majadiliano marefu baina ya Yesu na Wayahudi yalifuata matukio hayo (k.mf. Yn 5:1-15 ilifuatwa na Yn 5:16-47; Yn 9:1 -12 ilifuatwa na Yn 9:13-10:39).
Mafundisho ya aina ya Unostiki wakati ule yalisababisha matatizo makubwa kuliko wakati wo wote, hasa zaidi katika maeneo ya karibu na Efeso. Baadhi ya walimu wale walikanusha kwamba Yesu alikuwa Mungu kamili na wengine walikanusha kwamba alikuwa mwanadamu kamili. Yohana alipinga makosa yote mawili kwa nguvu sana (Yn 1:1,14,18; 3:13; 19:28,34). Lakini alitaka zaidi kuliko kupinga mafundisho ya kinyume tu. Alitaka kuongoza watu wamwamini Kristo, ili wapate uzima wa kweli na wa milele ambao Yesu Kristo aliutoa (Yn 1:4; 3:15; 6:27; 10:10; 14:6; 20:31).
Nyaraka za Yohana
Muda mfupi baada ya kuandika Injili yake, Yohana aliandika barua ya kusambazwa katika makanisa ya maeneo ya Efeso. Wakristo walichanganyikiwa kutokana na mafundisho ya aina ya Unostiki. Yohana alisema kwamba walimu hao wa uongo walikuwa maadui wa Kristo. Ukanushaji wao wa Uungu na ubinadamu wa Kristo ulishambulia kwa ukali msingi wa imani ya Kikristo (lYoh 2:18-19,22,26; 4:1-3). Yohana alitaka waamini wawe na uhakika wa wokovu wao katika Kristo (lYoh 5:13), nao wawapinge wale walioshawishi dhambi kwa njia ya kufundisha kwamba tabia ya mwili haikuwa na uhusiano na usafi wa roho (lYoh 2:4; 3:6,8). Wakristo wanapaswa kujitawala nao wawe na upendo (lYoh 2:6; 3:3,17; 5:3).
Alitaka wasomaji wake wawe na uhakika kwamba uzima mpya ule alioandika habari zake katika Injili yake, ni uzima wao hasa. Wengi wao hawakuwa na uhakika huo, kwa sababu ya mtu mmoja aliyeishi Efeso, jina lake Kerintho. Yule mtu alijaa mawazo ya Unostiki naye alieneza mafundisho yake ya uovu sana. (Kabla ya miaka mingi Paulo aliwaonya wazee wa Efeso kwamba walimu wa upotovu wangesababisha shida na matata katika kanisa lao, Mdo 20:29-30.)
Mafundisho ya uongo yalienezwa katika makanisa na walimu waliotembea tembea. Yohana aliandika barua fupi inayojulikana kuwa Waraka wa pili wa Yohana, ili kuonya kanisa moja la pekee lisije likawaruhusu walimu wa uongo hata kuhudhuria mikutanoyao (2Yoh 10-11).
Kwa upande mwingine walikuwepo walimu wengine waliotembelea makanisa na kuhubiri Injili ya kweli. Lakini katika kanisa moja alikuwepo mtu, jina lake Diotrefe, aliyejisogeza mbele katika hali ya mamlaka kanisani akakataa kuwapokea wale walimu wa kweli. Alidai kwamba walikuwa wajumbe wa Mtume Yohana ambaye yeye Diotrefe alimpinga. Kwa hiyo Yohana aliandika barua fupi ya binafsi (3 Yohana) kwa mmojawao wa viongozi wema katika kanisa, rafiki yake Gayo, ili amsaidie na kumtia moyo(3Yoh 1,5,9-10).
Ushindi au kushindwa?
Tangu mwanzo wa adha dhidi ya Wakristo chini ya Kaisari Nero (iliyosababisha kifo cha Paulo na Petro), kanisa liliudhiwa na kuteswa daima. Ingawa adha hiyo ilipungua kidogo kwa muda fulani, ilizidi sana katika enzi ya Kaisari Domitian (81-96 b.K.). Wakati ule Wakristo waliuawa kwa maelfu, waliteswa sana na kufanywa watumwa katika sehemu mbalimbali za madola ya Rumi. Dhuluma ya kila namna ilizidi. Watu waovu walifanikiwa, watu kwa jumla walipinga Ukristo, na serikali ililazimisha ibada ya Kaisari kama sheria rasmi. Zaidi ya hayo, makanisa yalisumbuliwa na walimu wa uongo waliowashawishi Wakristo washiriki mambo ya kipagani na dhambi. Katika hali hiyo ya hatari Yohana alipokea mfululizo wa ujumbe kutoka kwa Mungu ulioandikwa katika kitabu cha Ufunuo (Ufu 1:1; 2:10,13-14; 6:9-11; 22:6).
Yohana alijua ukali wa mateso waliyoyapata Wakristo, kwa sababu yeye mwenyewe alifungwa kwa ajili ya imani yake. Alikuwa mfungwa katika kisiwa cha Patmo, si mbali kutoka pwani ya Efeso. Alituma kitabu chake kwa makanisa saba yaliyojulikana sana katika mkoa wa Asia, na kutoka huko ujumbe wake ungeenea katika makanisa madogo ya karibu. Mtu aliyepeleka kitabu hicho labda alikipeleka kwanza Efeso, kisha akatembelea makanisa mengine na kurudi Efeso tena, na kutoka huko alirudi Patmo (Ufu 1:9-11).
Kwa sababu ya matatizo yaliyokuwepo katika makanisa, baadhi ya Wakristo waliacha imani yao na wengine walikata tamaa. Wengi wao walichanganyikiwa, kwa sababu ilionekana kama Yesu Kristo, mfalme wa utukufu waliyemtazamia arudi katika mamlaka makuu hakuweza au hakutaka kuwaokoa kutoka mamlaka ya Warumi.
Kwa njia ya Yohana, Yesu aliwahakikishia watu wake kwamba Yeye bado alitawala mambo yote, ingawa hakuwapa matumaini ya kinyume kwa kuwaahidi nafuu ya haraka. Kinyume chake, aliwaandaa kwa kuvumilia mambo makali zaidi kwa njia ya kuwadhihirishia matatizo yaliyowakabili na ushindi mkuu wa mwisho unaowangojea wale waliosimama imara upande wake. Yeye bado alikuwa mtawala wa ulimwengu naye anaangalia mambo yote. Katika muda unaomfaa Mungu angerudi kuwaadhibu maadui, kuwaokoa watu wake na kuanzisha wakati mpya wa amani na furaha ya milele (Ufu 1:5; 12:10-11; 19:15.16; 21:1-4).
UTARATIBU WA MIAKA NA MATUKIO WAKATI WA AGANO JIPYA
|
M akaisari wa Rumi |
Mwaka |
Matukio ya Agano Jipya |
|
|
(tarehe za takriban) |
|
|
Kaisari Augusto |
6k.K. |
Kuzaliwa kwa Yesu |
|
(27k.K.-14b.K.)(Lk2:l) |
|
|
|
Tiberio (14-37 b.K.) (Lk 3:1) |
28 b.K. |
Ubatizo wa Yesu |
|
|
31 b.K. |
Kusulibiwa kwa Yesu |
|
|
32 b.K. |
Kuokoka kwa Paulo |
|
Caligula (37-41 b.K.) |
35 b.K. |
Ziara ya 1 ya PauloYerusalemu (Mdo 9:26) |
|
Klaudio (41-54 b.K.) |
46 b.K. |
Ziara ya 2 ya PauloYerusalemu (Mdo 11:30) |
|
(Mdo 18:2) |
46 b.K. |
Paulo aanza safari ya kwanza ya Injili |
|
|
49 b.K. |
Mkutano mkuu Yerusalemu (Mdo 15) |
|
|
49 b.K. |
Paulo aanza safari ya pili ya Injili |
|
|
53 b.K. |
Paulo aanza safari ya tatu ya Injili |
|
Nero (54-68 b.K.) |
57 b.K. |
Paulo apeleka mchangoYerusalemu (Mdo |
|
|
|
21:17) |
|
|
60 b.K. |
Paulo afika Rumi (Mdo 28:16) |
|
|
62-68 b.K. |
Vifo vya Yakobo mwenye haki, Paulo na Petro |
|
Galba (68- 69 b.K.) |
|
|
|
Otho; Vitelio (69 b.K.) |
|
|
|
Vespasian (69-79 b.K.) |
70 b.K. |
Kubomolewa kwa Yerusalemu |
|
Tito (79-81 b.K.) |
|
|
|
Domitian (81-96 b.K.) |
98 b.K. |
Kifo cha Mtume Yohana |