166. Katika mlima wa Galilaya (Mt 28:16-20; Mk 16:15-18)
Mitume walikuwa na dokezi la sababu ya Yesu kuwaambia waende Galilaya alipowapeleka juu ya mlima mmojawapo. Kutoka huko waliweza kuona hatua ya kufuata katika ujumbe wa ufalme, yaani mataifa ya Kipagani yaliyokuwa katika upeo wa macho yao, Katika muda wake wa miaka mitatu na nusu huduma yake ya hadhara hapa duniani ilikoma katika Israeli tu (Mt 10:5-6; 15:24; Rum 15:8), lakini huduma ya Kristo aliyefufuka waliyopewa wanafunzi wake wakati huo, iliongezeka kwa watu wote bila tofauti. Uwezo wake ungekuwa ndani ya wanafunzi wake, ukiwahifadhi katika hatari zote na kuwawezesha kufanya kazi ya ajabu (Mt 28:16-17; Mk 16:15-18).
Makusudi ya Yesu katika kazi hiyo yalikuwa kuanzisha na kueneza kanisa lake (taz.Mt 16:18), wafuasi wake walipohubiri Injili, walipowabatiza wale walioamini na kuwafundisha wanafunzi wapya wafuate njia na mafundisho ya Yesu. Na hivyo wanafunzi wapya wangepeleka ujumbe kwa wengine, na kanisa lingeendelea kuenea kote ulimwenguni, wakiwa na uhakika kwamba mshindi Yesu angefanya kazi kwa njia hii ya watu wake (Mt 28:18-20).
167. Kupaa kwa Yesu (Mk 16:19-20; Lk 24:50-53)
Kuanzia wakati wa kufufuka kwa Yesu mpaka kupaa kwake ulikuwa muda wa majuma sita au siku 40, na wakati huo aliwapa wanafunzi wake mafundisho zaidi kuhusu ufalme wa Mungu (Mdo 1:3). Muhtasari wa mafundisho hayo labda unaonekana katika muhtasari uliounganishwa na habari ya Jumapili ile ya kwanza alipowatokea wanafunzi wake. Aliwaonyesha jinsi huduma yake ya hapa duniani ilivyokuwa kilele cha makusudi ya Mungu ya Agano la Kale na chanzo cha uenezi wake wa duniani kote kwa njia ya wafuasi wake. Ufahamu kamili wa makusudi ya Mungu, pamoja na ushahidi wao wa maelezo ya kufa na kufufuka kwa Yesu vingewapa ujasiri wa kupeleka Injili kwa watu wengine (taz.Lk 24:44-49; Mdo 1:8).
Wakati ulipowadia kwa Yesu kuwaacha wanafunzi wake na kuabiri kwa Baba yake, wanafunzi wake hawakuhangaika, bali walikuwa na ujasiri. Hapo tena Yesu aliondolewa kutoka kwao, lakini wakati huo, badala ya kukimbia kwa hofu na kukata tamaa, walifuatana naye mpaka mahali alipochagua kupaa. Kutoka karibu na kijiji cha Bethania kwenye miteremko ya Mlima wa Mizeituni nje ya Yerusalemu, Yesu aliwaacha wanafunzi wake, wakiwa na ahadi kwamba siku moja angerudi (Mk 16:19; Lk 24:50-51; taz.Mdo 1:9-12).
Wanafunzi walirudi Yerusalemu wakimsifu Mungu, na baada ya siku chache walimpokea Roho Mtakatifu. Hapo walianza kazi yao ya kuihubiri Habari Njema ya Yesu, na watu wengi sana waliamini. Bwana wao aliyefufuka alifanya kazi pamoja nao (Mk 16:20; Lk 24:52-53; taz.Mdo 2:10-12).