120. Yesu asafisha hekalu (Mt 21:12-17; Mk 11:15-19; Lk 19:45-48)
Katika mwanzo wa huduma yake ya hadhara, Yesu alisafisha hekalu (Yn 2:13-25), lakini desturi zile mbaya zilirudia tena. Wakati huo alipofika katika jiji lake la Umasihi, alisafisha hekalu tena. Kwa tendo lake alionyesha hukumu ya Mungu juu ya wale waliosahau makusudi ya kweli ya sherehe za kidini wakazitumia ili kuchuma fedha (Mt 21:12-13).
Mungu alipendezwa zaidi na matendo ya Yesu ya kuponya vipofu na viwete kuliko na sadaka zote na desturi za kidini zilizoendeshwa na Wayahudi. Hata watoto waliona thamani ya matendo yake wakamsifu kwa kadiri yao. Wenye mamlaka ya hekalu walichukia vitendo vya sifa ya watoto hekaluni, lakini Yesu alijibu kwamba watoto waliyaona mambo ambayo viongozi wa dini walishindwa kuyaona, yaani habari ya Yesu kuwa Masihi (Mt 21:14-16). Jioni ile Yesu alirudi Bethania tena (Mt 21:17).
121. Yesu aulaani mtini (Mt 21:18-22; Mk 11:12-14,20-26)
Asubuhi yake, Yesu na wanafunzi wake walipoondoka Bathania kuelekea Yerusalemu, walipitia mtini naye Yesu aliuona mti huo kama mfano wa taifa la Kiyahudi. Aliuendea mtini huo na kutafuta matunda asiyaone. Hali kadhalika alifika katika taifa la Wayahudi akitafuta matunda ya kiroho, lakini ingawa aliona alama nyingi za desturi za kidini. kwa kiroho taifa hilo halikufaa wala halikumtolea Mungu matunda. Kwa kuulaani mtini ukauke, Yesu alionyesha mfano wa hukumu ambayo taifa la Kiyahudi lingepata baada ya kumkataa Masihi wake (Mt 21:18-20; Mk 11:12-14,20-21).
Tukio lile pia lilikuwa funzo juu ya nguvu na matokeo ya maombi. Watu wakimwomba Mungu jambo maalumu, ni lazima wawe na imani isiyo na mashaka juu ya Mungu pamoja na tabia ya kuwasamehe watu wengine (Mt 21:21-22; Mk 11:22-26).
122. Mamlaka ya Yesu yahojiwa (Mt 21:23-32; Mk 11:27-33; Lk 20:1-8)
Yesu aliporudi hekaluni, viongozi wa dini walifika ili kumtega kwa njia ya swali. Walitumaini kwamba wangeweza kupata neno katika jibu lake ambalo lingewawezesha kumshtaki, ikiwa kiraia au kidini. Walimwuliza ni kwa mamlaka gani alifanya mambo yake, na hasa tendo lile la kupindua desturi za Kiyahudi katika hekalu lao (Mt 21:23).
Badala ya kuwajibu moja kwa moja, aliwauliza wao swali, ili wao wapate shida ya kujibu. Katika kufanya hivyo, Yesu hakuogopa kuwaambia ukweli, bali alitaka kuwawezesha wao wauone ukweli. Kama wangejibu swali la Bwana vizuri, wangekuwa na jibu sahihi kwa swali lao. Swali la Yesu lilihusu mamlaka ya Yohana Mbatizaji. Kama wangekubali kwamba Yohana alitumwa na Mungu, pia wangekubali kwamba Yesu alitumwa na Mungu, kwa sababu ujumbe wa Yohana ulikuwa kutangaza kuja kwake Yesu kama Masihi aliyeteuliwa na Mungu. Lakini kama wangekanusha kwamba Yohana alitumwa na Mungu, wangeweza kutazamia matata kutoka kwa umati wa watu ambao bado walimheshimu Yohana sana (Mt 21:24-27).
Walipokataa kujibu, Yesu aliwasimulia habari ili kuwalaumu tena kwa kukataa kwao kutubu. Aliwafananisha wenye dhambi kama vile watoza ushuru na wamalaya na mwana ambaye mwanzo alikataa kumtii baba yake, lakini baadaye alibadili mawazo yake. Wenye dhambi walitubu makosa yao na kuingia katika ufalme wa Mungu. Aliwafananisha Mafarisayo na mwana mwingine aliyemdanganya baba yake kuwa angemtii, lakini kwa kweli alikataa kumtii. Mafarisayo walijidai kumtii Mungu, lakini walikataa wito wa Yohana Mbatizaji wa toba (Mt 21:28-32).
123. Wakulima wahalifu wa shamba la mizabibu (Mt 21:33-46; Mk 12:1-12; Lk 20:9-18)
Mfano huu unachora picha ya Israeli kuwa shamba la mizabibu, Mungu akiwa mwenye shamba na viongozi wa Wayahudi kama wapangaji au wakulima walioliangalia shamba hilo. Kama vile wapangaji wale walivyowapiga na kuwaua watumishi waliotumwa na mwenye shamba, vivyo hivyo viongozi wa Israeli waliwaudhi na kuwaua wajumbe wa Mungu, kuanzia kwa manabii wa Agano la Kale mpaka kwa Yohana Mbatizaji. Wakati huo walikuwa tayari kumkataa hata Mwana wa Mungu mwenyewe (Mt 21:23-39). Kwa kumkataa Yeye, Wayahudi wangejipatia adhabu kali. Mungu angewaondolea mapendeleo ya baraka zake na kuwapa Mataifa (Mt 21:40-41).
Mfano mwingine unaonyesha ukweli huu. Yesu alifananishwa na jiwe la pembeni. Katika majengo ya kale jengo lote lilitegemea jiwe la pembeni kuhusu vipimo na kuimarishwa kwake. Katika kumkataa Yesu, Wayahudi walikuwa sawa na waashi waliotupa jiwe kuu la pembeni. Kisha Mungu alilitwaa jiwe lile lile lililokataliwa na kulitumia kwa kujenga nyumba mpya, yaani Kanisa la Kikristo. Jumuia hiyo mpya zaidi sana ingetokana na Mataifa, na wote wangejengwa juu yake na ndani yake Yesu Kristo (Mt 21:42-43). Uamuzi wa watu kuhusu Yesu ungeamua majaliwa yao wanakoelekea, kama wangemkataa wangeangamizwa. Viongozi wa Wayahudi walijua kwamba alisema habari zao wakataka kumfunga, lakini walikuwa na wasiwasi juu ya uamuzi wa umati wa watu (Mt 21:44-46).
124. Arusi ya mfalme (Mt 22:1-14)
Tangu wakati wa Agano la Kale mpaka wakati wa Agano Jipya Mungu alituma wajumbe wake kwa Waisraeli, lakini watu walidharau ujumbe wake. Mungu alifanana na mfalme aliyewaalika watu wengi katika sherehe ya arusi ya Mwanawe. Lakini wakati wa karamu ulipowadia, watu walikataa kufika (Mt 22:1-5). Habari hii ilikuwa mfano wa Wayahudi waliokataa kupokea ujumbe wa Yesu na kuingia katika ufalme wa Mungu. Kwa kumkataa Yesu wangejipatia hukumu na kusababisha kubomolewa kwa Yerusalemu (Mt 22:6-7). Wakati huo mwaliko uliokataliwa na Wayahudi ulikwenda kwa Mataifa, na watu hao waliupokea kwa furaha kubwa (Mt 22:8-10).
Lakini si watu wote waliokubali mwaliko huo walikuwa na imani thabiti. Baadhi yao walifanana na mtu aliyetaka kwenda katika sherehe, lakini alikuwa mvivu au alishughulika zaidi na mambo yake binafsi asiweze kujiandaa vizuri. Mfalme alikuwa amewaalika watu wote, lakini aliwakataa wale waliotaka kunufaika karamu yake bila ya kubadili njia zao za ubinafsi. Yesu aliwaalika watu wote waingia katika ufalme wake, lakini hakuna nafasi kwa wale wasemao wanaamini, lakini hawaonyeshi mabadiliko ya tabia na maisha yao (Mt 22:11-14; taz.7:21-23; 11:29; 13:20-21; 16:24).
125. Swali kuhusu kulipa kodi (Mt 22:15-22; Mk 12:13-17; Lk 20:19-26)
Maherodi walikuwa kundi la Wayahudi ambao, kinyume cha Wayahudi wengi walipendelea utawala wa Herode, na hivyo kwa namna fulani walipendeiea utawala wa Warumi. Kwa kawaida hawakupatana na Mafarisayo, lakini makundi yale mawili yalishirikiana katika kumtega Yesu kwa maswali. Walimwuliza kama ilikuwa halali kwa Wayahudi kulipa kodi kwa Warumi (Mt 22:15-17; Lk 20:19-22).
Kama Yesu angesema 'Ndiyo', Mafarisayo wangemshtaki mbele ya Wayahudi kuwa msaliti. Kama angesema 'Siyo', Maherode wangemshtaki mbele ya serikali ya Warumi kwa hatia ya uasi. Yesu akajibu kwamba wajibu kwa serikali ya kiraia na wajibu kwa Mungu havikupingana. Watu wanawiwa na kila upande kwa ajili ya huduma na fadhili wanazozipokea. Inawapasa kutoa kwa mamlaka ya kiraia yale wanayodaiwa, na hapo hapo wamtolee Mungu yote wanayotakiwa kumpa Yeye (Mt 22:18-22; Lk 19:23-26).