MAELEZO KUHUSU INJILI YA LUKA


Luka na Theofilo

Katika maneno ya kwanza ya Injili ya Luka na kitabu cha Matendo ya Mitume inadokezwa kwamba vitabu hivyo viwili vimeandikwa na mtu mmoja. Kwa pamoja ni masimulizi ya mfululizo kuhusu asili ya Ukristo, kuanzia kuzaliwa kwa mwanzilishi wake mpaka kufika kwa mmisionari wake mkuu jijini Rumi.


Vitabu vyote viwili viliandikwa kwa ajili ya mtu aliyeitwa Theofilo ambaye kutokana na cheo chake alichoitiwa, alikuwa mtu wa maana sana, labda afisa mkuu katika serikali ya Kirumi (Lk 1:1-4; Mdo 1:1-2). Vitabu vyake havitaji jina la mwandishi wake, lakini imani ya kawaida ya wakati wa kwanza wa Ekklezia ni kwamba viliandikwa na Luka.


Mwandishi wa historia aliye mtu wa Mataifa

Inaonekana kuwa jambo la uhakika kwamba Luka alikuwa Myunani (yaani mtu wa Mataifa), na hivyo alikuwa mwandishi wa pekee wa Agano Jipya asiyekuwa Myahudi. Maandiko ya kale yanadokeza kwamba alizaliwa Antiokia ya Shamu, ingawa wakati wa safari za Paulo za kueneza Injili inaonekana kama aliishi Filipi, kaskazini mwa Ugiriki wa siku hizi.


Kwa taaluma yake Luka alikuwa mganga (Kol 4:14), lakini pia alikuwa mtaalamu wa mambo ya historia. Kwa uangalifu sana aliandika tarehe za mwanzo wa habari zake kadiri ya matukio ya historia yaliyojulikana wazi (Lk 2:1-2; 3:1-2), na vitu vilivyochimbuliwa au kuchunguzwa na wataalamu wa akiolojia vinathibitisha uhalisi wa maneno ya kitaalamu aliyoyatumia kwa mahali pamoja na maafisa mbalimbali (Mdo 13:7; 16:12,35; 18:12,16; 19:31,35).


Luka anaonekana mara ya kwanza katika maandiko ya Bibiia alipojiunga na kikundi cha Paulo kaskazini-magharibi mwa Asia Ndogo, akafuatana naye katika safari ya kwanza ya kupeleka Injili Ulaya. Safari za Luka, kwa namna fulani zinaweza kufuatiwa kwa jinsi yeye mwenyewe alivyotumia neno 'sisi', alipokuwa katika kikundi cha wamisionari na neno 'wao' asipokuwa pamoja nao. Mji wa kwanza ambapo Paulo alieneza Injili Ulaya ulikuwa Filipi (Mdo 16:10-12), na Luka alibaki huko Paulo alipoondoka kwenda sehemu nyingine za Ugiriki (Mdo 17:1). Alijiunga na kikundi cha Paulo tena katika safari iliyofanana Paulo alipopitia Filipi katika safari ya kuelekea Yerusalemu (Mdo 20:5-6).


Inaonekana kama tangu wakati huo Luka aliendelea kuwa pamoja na Paulo kama mmojawao wa wajoli wake wa maana sana. Paulo alipokamatwa Yerusalemu na kufungwa Kaisaria baadaye, Luka aliendelea kuwa karibu naye. Bila shaka alitumia wakati huo kwa kukusanya habari za Yesu kutoka kwa mashahidi waliokuwa wameona maisha yake, yaani habari alizotaka kuziandika katika Injili yake (Lk 1:2-3). Baada ya kifungo cha miaka miwili, Paulo alipelekwa Rumi na Luka alifuatana naye (Mdo 27:1; 28:16). Alikuwa pamoja na Paulo katika kifungo kingine cha miaka miwili huko Rumi, na wakati huo alimaliza kuandika Injili yake na Matendo ya Mitume (Mdo 28:30; Kol 4:14; Flm 24).


Luka alimaliza masimulizi yake ya sehemu mbili pale alipochagua kuyamaliza. Mjumbe mkuu wa Ukristo alikuwa akitangaza Injili wazi na bila kuzuiwa katika makao makuu ya ufalme wa Rumi (Mdo 28:31). Lakini mwisho wa kitabu cha Luka haukuwa mwisho wa maisha ya Paulo. Ilivyokuwa mara nyingi kabla, Paulo alifunguliwa kutoka gerezani akaweza kusafiri tena. Baada ya kutembelea maEkklezia ya sehemu mbalimbali, alifungwa tena, akapelekwa Rumi ambapo wakati huo alihukumiwa kifo. Luka bado alikuwa pamoja naye, na kwa kweli alikuwa mtu wa pekee aliyekuwa naye siku zile alipongojea kutimiziwa hukumu ya kifo (2Tim 4:6,11).


Masimulizi yenye makusudi

Katika Injili zote nne, ile ya Luka ilipangwa kwa utaratibu mzuri nayo ni ndefu zaidi. Inasimulia mengi zaidi kuhusu maisha ya Yesu kuliko Injili nyingine, ingawa, sawa sawa na zile, haikutaka kusimulia habari za maisha ya Yesu tu. Mwandishi alipanga habari zake akiwa na makusudi maalumu, na kwa hekima nyingi aliandika kitabu chenye habari nyingi zaidi zinazojulikana kuhusu maisha ya Yesu kuliko vingine.


Luka alipoandika maelezo yake, alilenga zaidi kuliko kumpatia Theofilo masimulizi ya kinaga naga ya historia. Alichagua na kusimulia habari zake kwa namna ya kutetea na kukuza Ukristo. Alitaka kuonyesha kwamba Mungu katika upendo wake alifanya mikakati ya wokovu kwa watu wenye dhambi, na kufuatana na mikakati hiyo Yesu Kristo

alikuja kuwa Mwokozi. Watu waliomwamini Yesu walipokea wokovu ulioahidiwa, kisha walieneza ujumbe wa wokovu huo duniani kote (Lk 1:17, 68-73:2:11; 3:4-6; 4:18,21; 19:10; 24:44-48; taz.Mdo 1:8). (Maneno mengi ya kutetea Ukristo yaliyotajwa hapo juu, yanaonekana katika Injili ya Luka tu.)


Mwokozi kwa wote

Luka alionyesha kwamba, ingawa Yesu kwa kabila lake alikuwa Myahudi na kulelewa katika dini ya Kiyahudi, wokovu aliouleta, haukuwa kwa ajili ya Wayahudi tu. Watu hawakuwa na haja ya kupokea dini ya Kiyahudi wala mila za Kiyahudi ili kuokolewa. Ni kweli kwamba dini ya Israeli iliandaa njia kwa Yesu, lakini sasa, baada ya kuja kwake, dini hiyo ilitimiza makusudi yake. Wokovu aliouleta ulikuwa kwa watu wa kila mahali, bila kujali kabila au taifa lao. Wayahudi hawakupendelewa wala watu wa Mataifa hawakuonewa (Lk 2:32; 3:6-8; taz.Mdo 15:6-11). Kwa kweli, Yesu mara nyingi aliheshimiwa na watu wa Mataifa kuliko na Wayahudi, kwa matokeo ya kwamba watu hao walipokea wokovu wake, lakini Wayahudi waliukosa (Lk 4:25-27; 7:11; 11:31-32; 17:11-18).


Kama vile kusivyokuwa na ubaguzi kuhusu kabila au dini, vivyo hivyo haukuwepo ubaguzi kuhusu hali ya mtu katika jumuia. Wokovu unapatikana kwa watu wote. Luka alitoa mifano hai ya jambo hilo (na hivyo alitoa onyo kwa Theofilo) akionyesha kwamba, mara nyingi watu wa hali ya juu katika jumuia walikataa wokovu, lakini wale waliodharauliwa waliupokea (Lk 7:29-30; 10:30-37; 16:19-31; 18:9-14; 19:1-9).


Luka akitia mkazo katika mambo hayo, anasimulia matukio mbalimbali ambapo watu wasiokuwa na nafuu katika jumuia walipokea baraka za Mungu. Miongoni mwao walikuwa watumwa (Lk 7:2-7; 12:37), wageni (Lk 10:30-37; 17:16), maskini (Lk 1:53; 2:7; 6:20; 7:22) na wanawake (Lk 1:28; 2:36-38; 7:37-48; 8:2; 13:11-13), na hasa zaidi wajane(Lk 4:25; 7:12-15; 18:1-7; 21:1-4).