71. Huduma katika Dekapoli (Mt 15:29-39; Mk 7:31-8:10)

Kutoka miji ya kando ya Bahari ya Kati ya Foiniki, Yesu alifika tena katika maeneo ya Ziwa Galilaya akaendelea mpaka Dekapoli, ambapo wenyeji wake zaidi walikuwa Wapagani. Inaonekana kama kwa muda huduma yake ilikuwa zaidi miongoni mwa Wapagani, na wengi wao wakamwamini Mungu wa Israeli (Mt 15:29-31; Mk 7:31). Mtu mmoja aliyemponya hakuona wala kusikia. Kwa sababu ya uziwi wake, Yesu alitumia matendo badala ya maneno, ili kuhakikisha kwamba imani yake ilikuwa kamili, na alielewa matendo ya Yesu (Mk 7:32-37).


Hapo tena Yesu alishikwa na huruma alipoona umati wa watu waliokuwa na njaa akaamua kuwalisha. Katika tukio la awali lililofanana, watu wake walikuwa Wayahudi (taz.Yn 6:14-15), lakini wakati huo wengi zaidi walikuwa Wapagani. Labda kwa sababu hii wanafunzi walitia shaka kama angetumia uwezo wake wa kuwalisha (Mt 15:32-33; Mk 8:1-4). Lakini aliwalisha kwa njia ya mwujiza kama alivyofanya kwa Wayahudi (Mt 15:34-39; Mk 8:5-10).


72. Tahadhari ya Mafarisayo na Masadukayo (Mt 16:1-12; Mk 8:11-21; Lk 12:1-3; 12:54-56)

Ingawa Yesu alikuwa amefanya mambo yale yote, Mafarisayo na Masadukayo bado walidai afanye ishara ya pekee, ili awaridhishe wao. Yesu alikataa. Waliweza kutazama angani na kutabiri hali ya hewa ya kesho yake, lakini walipotazama ishara za Yesu walikataa kuamini ishara zile ziliwaonyesha nini, yaani kwamba alikuwa Mwana wa Mungu. Ishara ya pekee ambayo Yesu angewapa ingekuwa ile ya ufufuo wake. Yona alirudia katika uzima baada ya siku tatu alipoonekana kama alikufa, lakini Yesu alisema angerudia katika uzima baada ya siku tatu za mauti hasa. Kwa ishara hiyo isiyoweza kuelezwa vibaya, Baba angethibitisha kwa watu wote kwamba Yesu ni Mwana wake (Mt 16:1-4; Lk 12:54-56).


Dhambi inafananishwa na chachu au hamira inayoumua na kuharibu kila kitu inachokigusa. Mafarisayo, Masadukayo na Herode walikuwa ushawishi mbaya ulioenea katika Israeli yote, kama vile chachu inavyoenea katika donge zima. Yesu aliwaonya wanafunzi wake kujihadhari na ushawishi huo wa kufanana na chachu ya watu hao. Labda maana ya maneno ya Yesu ilikuwa kwamba, wanafunzi wasishawishiwe na mafundisho ya kinyume na yenye unafiki wa Mafarisayo na Masadukayo, au na njia zilizo kinyume cha Mungu, kama zile za Herode (Mt 16:5-6; Mk 8:14-15; Lk 12:1).


Mitume walikosa kuelewa maana ya mafundisho ya Yesu ya kimfano. Wao walifikiri kwamba alitaka mkate (ila siyo ule uliookwa kwa chachu ya aina fulani), wakahangaika kwa sababu hawakuwa na mkate. Hayo yalionyesha kwamba, ingawa walimwona mara mbili akilisha umati wa watu, bado walikuwa hawajaamini kwamba angeweza kuwapatia. Zaidi ya hayo, hawakuwa na ufahamu wa kiroho wa kuelewa maana ya mfano wa Yesu mpaka awaeleze vizuri zaidi (Mt 16:7-12; Mk 8:16-21; Lk 12:2-3).


73. Ushuhuda wa Petro kuhusu Masihi (Mt 16:13-23; Mk 8:27-33; Lk 9:18-22)

Yesu na Mitume walisafiri kwenda Kaisaria Filipi, kaskazini mwa Palestina. Huko Yesu aliwauliza Mitume kwamba walifikiri Yeye ni nani. Petro, labda akisema kwa niaba ya wote, alijibu kwamba Yeye ndiye Masihi aliyeahidiwa, yaani Mwana wa Mungu (Mt 16:13-16).


Yesu alifurahia utambuzi huo, akawafahamisha wanafunzi (kwa maneno aliyomwambia msemaji wao Petro) kwamba utambuzi hiki ilikuwa msingi ambao juu yake angelijenga kanisa lake lisiloweza kushindwa na nguvu yo yote. (Mt 16:17-18; Efe 2:20). Kwa njia ya kuihubiri Injili, wangeufungua ufalme kwa watu wote ambao wangetaka kuingia. Wangechukua mamlaka ya Yesu, ili kwamba yo yote ambayo wangetenda kwa Jina lake na kwa kulitii Neno lake hapa duniani, yangethibitishwa hata mbinguni (Mt 16:19; taz.Mdo 2:32; 3:6,19). Lakini mambo hayo yangekuwa wakati wa usoni. Kwa wakati huo wamsaidie kwanza katika huduma yake, ila wasitangaze Umasihi wake hadharani mpaka wakati wake utimie (Mt l6:20).


Kisha Yesu aliweka wazi kwamba, kwa kusudi la kutimiza huduma yake ya Umasihi, ingempasa kuteswa, kuuawa na kufufuliwa tena. Petro aliyakataa mambo hayo. Ilionekana kwamba wanafunzi walikuwa bado hawajaelewa hali ya kazi ya Masihi. Ushauri kwamba Yesu asiende msalabani, ulikuwa jaribu lingine. Alijaribu kumshawishi ajipatie ufalme wake kwa njia nyingine kuliko kwa mauti yake, na hivyo angemsababisha kukosa jambo lenyewe alilolijia (Mt 16:21-23; taz.4:8-10).


74. Jaribio la uwanafunzi wa kweli

(Mt 16:24-28; Mk 8:34-9:1; Lk 9:23-27) Mara baada ya kuwaambia wanafunzi wake habari za mateso na kifo kilichomkabili, Yesu aliwaambia kwamba wao wawe tayari kutendewa hayo hayo. Wanafunzi wa Yesu ni wale waliotoa maisha yao kwa Yesu, nao watamtii Bwana wao hata ikiwa na maana ya ugumu, mateso na mauti. Hawataendelea kutawala maisha yao wenyewe, bali watayashinda mapenzi yao ya binafsi, ili wampendeze Yesu. Kwa njia ya kujikana namna hiyo, watapata maana ya kweli ya uzima. Kwa upande mwingine, watu wanaoishi kwa ajili ya binafsi yao tu, wanaweza kujipatia wanachokitaka katika dunia hii, lakini watapoteza uzima wa pekee wenye thamani ya kudumu, yaani uzima wa milele (Mt 16:24-27).


Yesu aliwaahidi wanafunzi wake kwamba wale walioshirikiana naye katika huduma yake, katika maisha yao ya sasa wangeona sehemu ya ushindi wa ufalme mtukufu wa Mwana wa Adamu. Kwa maana ya jina la 'Mwana wa Adamu', taz. kipengele kilichotangulia cha 'Yesu na Ufalme'.)


75. Kugeuka kwa sura ya Yesu (Mt 17:1-13; Mk 9:2-13; Lk 9:28-36)

Kugeuka kwa sura yake Yesu kulitokea juu ya mlima mrefu, labda Mlima Hermoni, usiokuwa mbali na Kaisaria Filipi. Tukio lenyewe lilikuwa ufunuo wa utukufu wa Kristo, nao ulishuhudiwa na Mitume wateule watatu tu. Hilo lilikuwa dokezo la utukufu ambao angeupata baada ya kumaliza kazi yake aliyoijia (Mt 17:1-2; Lk 9:28-29).


Musa na Eliya walimtokea Yesu wakati wa kugeuka kwa sura yake, labda kwa kutoa mfano kwamba sheria na unabii wa Agano la Kale vilipata utimizaji wake katika Yeye. Yeye alikuwa ndiye ambaye Agano la Kale lote lilimwonyesha. Walizungumza na Yesu kuhusu kifo chake kilichomkabili, wakithibitisha maneno yale ambayo Yesu aliwaambia Mitume kabla ya muda mfupi, yaani Masihi angepaswa kufa kabla ya kuingia katika utukufu wake (Mt 17:3; Lk 9:30-31).


Mitume walichanganyikiwa katika yale yaliyotokea, lakini sauti ya Baba kutoka mbinguni iliwaambia kwamba, hivyo ilionyeshwa kwamba aliridhika na huduma yote ya Yesu. Kwa kuunganisha maneno ya Zaburi ya Daudi na maneno ya 'Wimbo wa Mtumishi wa Mungu' wa Isaya, Mungu alieleza kwamba Mfalme Masihi angetoa maisha yake kama 'Mtumishi ateswaye'. Masihi huyo pia alikuwa nabii wa Mungu, na watu walipaswa kusikiliza ujumbe wake (Mt 17:4-5; Lk 9:32-35; taz.Zab 2:7; Isa42:l; Kum 18:15,18; Mdo 3:22).


Tukio Hie la kugeuka sura lilipopita na sura ya Yesu kuwa kama kawaida, aliwaambia Mitume tena wasidhihirishe mambo waliyoyaona kwa wakati huo (Mt 17:6-9; Lk 9:36). Maono ya Eliya yaliwasababisha Mitume waulize kama Eliya angekuja kabla ya Masihi. Kama Yesu ni Masihi, mbona Eliya hakuja? Yesu akajibu kwamba Yohana Mbatizaji alikuwa 'Eliya' aliyeahidiwa, lakini kama vile watu walivyomkataa mtangulizi wa Masihi, ndivyo ambavyo wangemkataa Masihi mwenyewe (Mt 17:10-13).