41. Kutoa, kusali na kufunga (Mt 6:1-18; Lk 11:1-4)
Kama wafuasi wa Yesu wanatoa msaada kwa wenye dhiki kwa kusudi la kupata sifa ya watu, kutoa kwao hakuna thamani machoni pa Mungu. Watapata thawabu yao katika sifa wanayoitafuta, lakini watakosa thawabu kutoka kwa Mungu. Afadhali mambo ya kutoa au ya kufadhili yawe ya siri, hata marafiki au majirani wasijue (Mt 6:1-4).
Sala au maombi pia yawe mambo ya binafsi. Waamini hawana haja ya kufanya maonyesho ya bidii ya maombi, kana kwamba Baba yao wa mbinguni anahitaji maombi marefu yenye mtindo wa kupendeza, ili aguswe na kushughulika. Yeye hafanani na miungu ya kipagani isiyokuwa na uhai, bali ni Baba wa upendo anayeelewa shida za watoto wake (Mt 6:5-8).
Ili kuwatia moyo waamini waombe kwa ujasiri, Yesu aiiwapa mfano wa kufuata wakati wa kuomba kwao. Ingawa wanaweza kusema na Mungu kwa uhuru wa watoto wasemao na baba yao, wafanye hivyo kwa heshima wakikumbuka kwamba Yeye ni Mtakatifu. Neno la ibada linahakikisha kwamba utukufu wake uwepo kabla ya mahitaji yao (Mt 6:9). Waamini waombe ili utawala wa Mungu uonekane katika maisha yao na katika maisha ya watu wengine, wakiwa ni watu binafsi au jumuia yote. Maombi yanaweza kuhusu mambo makubwa kama vile utimizaji wa mipango mikubwa na ya milele ya Mungu, au mambo madogo kama vile mahitaji ya kila siku (Mt 6:10-11). Waamini pia watubu dhambi zao wakikumbuka kwamba Mungu anawasamehe wale tu wanaowasamehe wengine. Pia wamwombe Mungu atawale mambo ya maisha yao, matatizo yao yasije yakawasababisha kuanguka katika dhambi (Mt 6:12-15).
Kama wakati wo wote waamini wanaunganisha maombi yao na kufunga, wasijaribu kuvuta mawazo ya watu wengine juu yao kwa njia ya kuonekana kama wanahuzunika. Kufunga kwao hakuna maana yo yote machoni pa Mungu kama wanatumia kufunga kwao ili wasifiwe na watu. Wakifunga wafanye shughuli zao na wavae kama kawaida (Mt 6:16-18).
42. Masumbufu kuhusu vitu vya dunia (Mt 6:19-34; Lk 12:22-34)
Watu wataingia katika ufalme wa Mungu, wasiendelee kuona vitu vya kawaida ya maisha kama watu wengine wanavyoviona. Wao wayape mambo ya Mungu kipao mbele na wawe wakarimu kwa kuwapa watu wengine. Watu wanaokaza mioyo yao juu ya vitu vya dunia, siyo waaminifu kwa Mungu, na kwa kweli watakatishwa tamaa wakati wa mwisho (Mt 6:19-21).
Ili kutoa mfano wa matokeo ya tabia nzuri na mbaya kuhusu vitu vya dunia, Yesu alitaja imani ya maeneo yale kuhusu matokeo ya kuweza kuona vizuri au vibaya. Watu waliamini kwamba macho yalikuwa kama madirisha yanayoingiza nuru mwilini mwa mtu na kumfanya mtu awe na afya nzuri. Macho yenye afya yangekuwa dalili ya mwili wenye afya nuru), na macho magonjwa yangekuwa na maaa ya ugonjwa wa mwili (giza). Kuona mambo ya vitu vya dunia vizuri, matokeo yake ni uzima wa kiroho wenye afya, lakini kuona mambo hayo vibaya, maana yake giza la asili ya kiroho lililokuwemo moyoni tangu awali litakuwa giza zaidi (Mt 6:22-23). Mtu anaweza kuwa mtumwa wa bwana mmoja tu kwa wakati mmoja. Watu wanaoshughulika na mambo ya kuongeza mali na utajiri wao tu, watakuwa watumwa wa vitu vile. Hawawezi kujidai kuwa waaminifu kwa Mungu (Mt 6:24).
Wapo wengine wanaoingia katika utumwa wa vitu vya kidunia, si kwa sababu ni wenye ubahili au tamaa ya vitu, bali kwa sababu wanajisumbua zaidi kwa kuogopa, huenda fedha zao hazitawatosha kwa mahitaji yao. Afadhali wangetambua kwamba Mungu yule aliyewapa uzima, pia anaweza kuwapa mahitaji yao kwa kuhifadhi uzima huo (Mt 6:25-27). Kama Mungu anashughulikia mambo tunayoyaona madogo au hayana maana zaidi, kama vile ndege, maua na nyasi, kwa hakika anaweza kuwaangalia watu wake. Wakristo wasijisumbue sana kwa vitu vya dunia. Watu wasiomjua Mungu wanaweza kuhangaika, lakini waamini wamtegemee Mungu na kuupa ufalme wake kipao mbele. Wamruhusu Mungu atawale mioyo na maisha yao, wakiamini kwamba kadiri matatizo yanavyotokea, ndivyo Mungu atakavyotoa jibu lake (Mt 6:28-34).
43.Kuwahukumu wengine (Mt 7:1-6; Lk 6:37-42)
Watu wanaoona makosa ya wengine daima, wanavuta hukumu juu yao wenyewe kutoka kwa wenzao na kutoka kwa Mungu. Wanapoonyesha makosa ya wengine wanavuta mawazo ya watu juu yao wenyewe. Wao pia wana makosa, ingawa labda wao wenyewe hawayaoni, ila watu wengine wanayaona wazi(Mt 7:1-5).
Hata hivyo kuna namna ya hukumu inayotakiwa sana. Wale wanaohubiri Injili lazima waweze kutofautisha baina ya watu walio na nia ya kumjua Mungu kweli na wale wanaotaka kudhihaki na kutukana tu. Nyama nzuri haitupwi mbele ya mbwa wachafu, wala lulu hazitupwi mbele ya nguruwe (Mt 7:6).
Wafuasi wa Yesu wajifunze kuhukumu mambo hayo vizuri, kama wanataka kuwasaidia wengine. Wakiwa walimu, wao ni vielelezo kwa wengine, na Mungu atawapa thawabu kwa kadiri wanavyokuwa vielelezo, kama ni vizuri au vibaya. Ni lazima wakumbuke kwamba hawawezi kuwaongoza vipofu, kama wao wenyewe ni vipofu. Zaidi ya yote, wajihadhari wasije wakawapoteza wengine kwa njia ya kutaja makosa yao tu (Lk 6:37-42).
44.Kuomba kwa kusihi (Mt 7:7-12; Lk 11:5-13)
Yesu alitoa mifano miwili ili kuwaonyesha wafuasi wake kwamba wanaweza kupeleka maombi yao kwa Mungu kwa ujasiri. Hata kama jirani aliyechoka hataki kusaidia, lakini anabembelezwa na mtu anayemwomba sana kisha akampa mahitaji yake. Zaidi sana Mungu aliye Baba wa upendo, atawapa watoto wake mahitaji yao (Lk 11:5-10). Wakristo hawana haja ya kumwomba au kumsihi Mungu kana kwamba hataki kutoa. Wanamwendea Mungu kama vile watoto wanavyomwendea baba yao, wakiwa na ujasiri kwamba hatawakatisha tamaa kwa kuwanyima kitu wanachohitaji (Mt 7:7-12; Lk 11:11-13).
45.Njia mbili (Mt 7:13-29; Lk 6:43-49)
Katika maisha ya watu kuna njia mbili: Njia mojani rahisi ipendezayo ubinafsi, nayo inachaguliwa na watu wengi, lakini inawapeleka katika uharibifu. Pia kuna njia nyembamba ya kujikana kwa ajili ya Bwana Yesu, inayowapeleka watu wake uzimani (Mt 7:13-14).
Sababu moja inayowasababisha watu wengi wasifuate njia nyembamba ni kwamba, hudanganywa na wale wafundishao mawazo yao binafsi kuhusu jinsi ambavyo watu wangeweza kupata maana ya kweli ya maisha. Mafundisho yao mwanzo yanaonekana kama ni sawa, lakini mwisho wake inathibishwa kuwa ni njia ya uharibifu. Walimu wake wanaonekana wema kama kondoo, lakini kwa kweli ni watu wa hatari kama mbwa-mwitu. Mti mwovu hutoa matunda maovu, na mafundisho mabaya huleta tabia mbaya (Mt 7:15-20).
Sababu nyingine inayowasababisha watu wasiifuate njia nyembamba ni kwamba hujidanganya wenyewe. Wanafikiri kwamba, kwa kuwa wanaambatana na wafuasi wa Yesu, wanaweza kuingia katika ufalme wa Yesu. Wanaweza hata kuhubiri katika jina la Yesu, lakini kama hawakukutana na Mungu kwa njia ya toba na imani hata siku moja, wao pia watakwenda mahali pa uharibifu (Mt 7:21-23). Watu wanaposikia mafundisho ya Yesu, lakini hawafanyi uamizi wo wote, hujidanganya na huelekea kuangamizwa. Wanafanana na mtu ajengaye nyumba inayoonekana kama ni imara, lakini haina msingi, nayo itabomoka itakapojaribiwa na mvua na upepo mkali wa majaribu (Mt 7:24-27).
Tofauti baina ya mafundisho ya Yesu na yale ya waandishi ni wazi kwa watu wote. Waandishi waliwataja walimu walioheshimiwa wakati uliopita ili mafundisho yao yapate mamlaka, lakini Yesu alihubiri kutokana na mamlaka yake mwenyewe. Waandishi waliweza kukariri kanuni za Kiyahudi tu, lakini Yesu alieleza sheria katika mamlaka yaliyotoka kwa Mungu (Mt 7:28-29).
YESU YUKO YERUS ALEMU TENA
46. Uponyaji katika Bethzatha na matokeo yake (Yn 5:1-29)
Yesu alifika Yerusalemu kutoka Galilaya kwa ajili ya sikukuu ya dini ya Kiyahudi. Wakati huo alitembelea birika ambapo walemavu wengi na wasioona walitegemea kupona (Yn 5:1-5). Mmojawao alimwomba Yesu amsaidie. Hakumwomba amponye (kwa sababu hakumjua), bali amsaidie kuingia katika birika. Yesu aliitikia akamponya pale pale (Yn 5:6-8a). Uponyaji huo ulitokea siku ya Sabato, kwa hiyo viongozi wa Wayahudi walifanya bidii sana kumfahamu aliyesababisha jambo hilo. Bila shaka Yesu alijua kwamba shida ya mtu aliyepona kwa sehemu ilisababishwa na makosa yake, kwa hiyo alimhamasisha atubu. Lakini badala yake alitoa taarifa juu ya Yesu kwa wale waliomtafuta (Yn 8b-15).
Viongozi wa Wayahudi walipomlaumu Yesu kwa kuvunja sheria ya Sabato, alijibu kwamba hata Baba yake anafanya kazi siku ya Sabato. Kila siku anahifadhi ulimwengu na kutunza viumbe vyake. Akisababisha jua liche, mvua inyeshe na nyasi zikue siku ya Sabato, havunji sheria. Yesu ameunganika na Baba yake, naye hafanyi dhambi akifanya tendo la huruma siku ya Sabato (Yn 5:16-17).
Wayahudi walikasirika zaidi walipomsikia Yesu akimwita Mungu Baba yake. Yesu akajibu kwamba katika kazi yao yote Baba na Mwana wameunganika. Wako wawili katika nafsi, lakini akili mmoja. Katika kuponya siku ya Sabato, hakufanya jambo kinyume cha mapenzi ya Baba, bali alitimiza mapenzi yake (Yn 5:18-20a).
Yesu mwenye adhama ya Mungu, kwa hiyo angefanya mambo makubwa zaidi kuliko Hie, atawafufua wafu na kuleta hukumu ya mwisho juu ya watu wote. Watu wanaomkataa Mwana wanamdharau Mungu, lakini wale wanaompokea Mwana, mara moja wanatoka katika mauti ya kiroho na kuingia katika uzima wa kiroho (Yn 5:20b-24). Wafu watakapofufuliwa kwa hukumu ya mwisho, hukumu hiyo itaendeshwa na Mwana. Lakini haitakuwepo hukumu kwa wale wapokeao uzima ule anaoutoa (Yn 5:2-29).
47. KumshuhudiaYesu(Yn 5:30-47)
Yesu alifanya kazi kwa mamlaka ya Mungu, lakini hakutaka kutoa ushuhuda juu ya nafsi yake, ili kuwaridhisha Wayahudi. Mungu alikuwa shahidi wake, naye alikubali ushuhuda wake, hata kama Wayahudi hawakuukubali (Yn 5:30-32). Kama Mungu alikuwa shahidi wake, Yesu hakuhitaji ushuhuda mwingine. Lakini kama Wayahudi walitaka mashahidi wa kidunia, wangepatikana. Yesu aliwapa mashahidi watatu, ili kuwaridhisha wale waliotaka kumhukumu kufuatana na matakwa ya mashahidi kadiri ya sheria ya Kiyahudi (taz.Kum 19:15). Wa kwanza alikuwa Yohana Mbatizaji. Matangazo yake kuhusu Masihi ajaye yalikuwa sawa na kuwasha taa katika sehemu ya giza. Kwanza watu walimpenda, lakini waliacha kuifurahia huduma yake walipomwona akiwaita watoke katika njia zao za dhambi (Yn 5:33-35).
Ushahidi wa pili ulikuwa kazi za Yesu. Miujiza yake ilithibitisha uwepo wa nguvu za Mungu asiyeonekana. Hata hivyo Wayahudi hawakuamini (Yn 5:36-38). Ushahidi wa tatu ni Maandiko ya Agano la Kale ambayo Wayahudi waliyachunguza kwabidii sana,wakifikiri kwamba kama wangetimiza sheria mbalimbali wangepata uzima wa milele. Lakini uchunguzi wao haukuwaongoza kumpokea Yesu ambaye Maandiko hayo yanamwonyesha kuwa ndiye atoaye uzima wa milele (Yn 5:39-40)
Kinyume cha Wayahudi, Yesu hakutafuta sifa za wanadamu. Wao waliwakubali wale waliojidai kuwa walimu, lakini walimkataa yule aliyewekwa na Mungu (Yn 5:41-44). Kama wangalielewa maana ya kweli ya sheria ya Musa, kuliko kushindana juu ya kanuni ndogo ndogo na mipango, wangempokea Yesu, nao wangeona kwamba Yeye ndiye aliyetajwa katika mafundisho ya Musa. Katika kumkataa Yesu walimkataa Musa, na hivyo walihukumiwa na maneno yale alioyaandika Musa (Yn 5:45-47).
YESU KATIKA GALILAYA TENA
48.Mtumishi wa akida, mwana wa mjane (Mt 8:5-13 Lk 7:1-17)
Baada ya kurudi Kapernaumu, akida wa Kirumi alimwomba Yesu amponye mmojawao wa watumishi wake aliyekuwa mgonjwa mahututi, lakini hakumwomba aingie katika nyumba yake. Yeye akiwa mkuu wa jeshi, alifanya kazi yake katika sheria ya mamlaka. Kama alitoa amri, mapenzi yake yalifanyika. Aliamini kwamba Yesu alikuwa na mamlaka ya Mungu, naye alihitaji kusema neno tu, na mtumishi wake angepona (Mt 8:5-9; Lk 7:1-8).
Yesu aliona kwamba yule Mrumi alikuwa na imani zaidi kuliko Wayahudi. Alitumia tukio hilo ili kuwaonya Wayahudi kwamba wengi wao wangeachwa nje ya ufalme wa Mungu, lakini Mataifa kutoka nchi za mbali na karibu wangeingia kwa sababu ya imani yao (Mt 8:10-13; Lk 7:9-10).
Katika kijiji kingine cha kaskazini, Naini, Yesu alimfufua mwana wa mjane kutoka kwa wafu. Inaonekana kama katika tukio hilo hakuombwa kufanya jambo lo lote, bali alimhurumia mama yule. Baada ya kufiwa na mumewe, na wakati huo hata na mwanawe wa pekee, yule mama angekabiliwa na umaskini na ugumu sana mpaka mwisho wa maisha yake. Kwa hiyo Yesu alisimamisha msafara wa mazishi na kumrudisha kijana kwa mama yake (Lk 7:11-17).
49.Wajumbe kutoka kwa Yohana Mbatizaji (Mt 11:1-19; Lk 7:18-35)
Yohana Mbatizaji alipofungwa gerezani, alipata habari kwa nadra tu kuhusu kazi na mafundisho ya Bwana Yesu, na labda habari nyingine hazikuwa sawa. Ripoti kama hizo bila shaka zilimsababisha kutia shaka kama Yesu kweli alikuwa Masihi jinsi alivyokuwa ametabiri. Yesu akamrudishia Yohana ujumbe kwamba alitekeleza huduma ya kuwasaidia walioonewa, iliyokuwa huduma ya Masihi sawa sawa na unabii wa Agano la Kale (Mt 11:1-5; Isa 35:5-6; 61:1). Watu wengi hawakufurahi kwamba Yesu hakuleta ushindi wa kisiasa walioutazamia kwa Masihi, lakini Yesu aliahidi baraka ya pekee kwa wale walioelewa huduma yake bila ya kukata tamaa (Mt 11:6).
Watu wengine wasije wakaacha kumheshimu Yohana, kwa sababu ya kuuliza maswali hayo, Yesu alieleza jinsi alivyokuwa mtu mkubwa. Yohana hakuwa mtu wa tabia ya wasiwasi, aliyekuwa na mashaka juu ya kazi yake wala hakupeperushwa na maneno ya watu. Wala hakupenda maisha makubwa yenye sifa na starehe. Alikuwa nabii, na sawa sawa na manabii wengi, alivumilia maisha magumu (Mt 11:7-10).
Yohana alikuwa nabii mkuu na wa mwisho kabla ya wakati wa Masihi, lakini kwa sababu alikuwa mtu wa wakati ule, baraka alizozipata zilikuwa ndogo kuliko zile za mwamini mdogo kabisa aingiaye ufalme wa Masihi. Ingawa watu wengine walipinga ukweli huo kwa nguvu, wengine walifanya bidii yote ili waingie (Mt 11:11-12). Katika kuandaa njia kwa ufalme na kumtambulisha Masihi, Yohana alikuwa ndiye 'Eliya' ambaye nabii Malaki alisema habari zake (Mtl 1:13-15; taz.Mal 4:5).
Watu walioamini na kuyatii mahubiri ya Yohana walifurahi kusikia maneno yenye sifa aliyoyasema Yesu juu yake. Lakini viongozi wa dini waliomchukia Yohana walikasirika (Lk 7:29-30).
Yesu alifananisha watu wa siku zake na kundi la watoto watundu wachezao mitaani. Hawakukubaliana kucheza maigizo ya arusi wala yale ya maombolezo ya mazishi. Hakuna kinachowaridhisha. Wayahudi walifanana na watoto wale. Walimlaumu Yohana kwa sababu alijipangia sheria kali kuhusu vyakula na vinywaji vyake, asichangamane na watu, kama vile mkaaji wa pekee au mtawa wa jangwani. Lakini pia walimlaumu Yesu kwa sababu hakuwa na kanuni kali namna hiyo kuhusu chakula na vinywaji, naye alichangamana na watu wasioheshimiwa na jumuia. Lakini Mungu alikuwa na makusudi yake ya kuwatuma Yohana na Yesu wakiwa na ujumbe tofauti, na hekima yake ilithibitishwa na maisha ya watu yaliyobadilishwa baada ya kuamini ujumbe wao (Mt 11:16-19).
50.Ghadhabu na neema ya Mungu (Mt 11:20-30)
Wenyeji wa Bethsaida, Korazini na Kapernaumu ya Galilaya ambapo Bwana alifanya kazi nyingi, hawakuwa wabaya sana, wakilinganishwa na watu waovu wa baadhi ya miji ya wapagani wakati wa Agano la Kale kama vile Tiro, Sidoni na Sodoma. Lakini kwa kuwa watu wa miji ya Galilaya waliona huduma ya Yesu kisha wakamkataa kwa makusudi, wangepata hukumu kali kuliko miji ya Kitaifa isiyosikia wala kuona habari za Yesu. Upendeleo na nafasi zaidi waliyopata, iliweka juu yao madaraka na wajibu mkubwa zaidi, na hivyo wangepata hukumu kali zaidi, kama wangekosa kutubu na kuamini (Mt 11:20-24).
Watu wachache sana wenye hali ya juu na wenye elimu walimpokea Yesu, kwa sababu waliridhika na hali nzuri waliyqjipatia maishani mwao. Lakini wengi waliojisikia kuwa walihitaji msaada, walimgeukia Yesu kwa shida za mioyo yao, na kwa njia hiyo walipata uhusiano mpya na Mungu. Walipata kiburudisho cha roho kwa njia ya kujifunza kwa Yesu na kutii mafundisho yake. Walipomkubali Yeye kuwa Bwana wao, walipata uzima wa kweli (Mt 11:25-30).