MAELEZO KUHUSU INJILI YA MATHAYO


Mwandishi na wasomaji wake

Injili ya Mathayo haitaji jina la mwandishi wake wala makusudi yake ya kuandika kitabu. Jina lake la 'Mathayo' lilitolewa katika karne ya pili, nalo linaonyesha imani ya Ekklesia la kale kwamba mwandishi wake alikuwa Mtume Mathayo. Lakini ilichukua muda na maendeleo fulani mpaka kitabu chenyewe kilipotokea sawa sawa. Haidhuru kama Mathayo mwenyewe aliandika kila neno mpaka mwisho wake, lakini ni wazi kwamba maandiko yake (yalivyokubaliwa katika karne ya pili) yalichukua nafasi kubwa zaidi ya kitabu chake.


Sawa sawa na vitabu vingine vya Agano Jipya, Injili ya Mathayo iliandikwa katika lugha ya Kiyunani (Kigiriki). Inaonekana kama iliandikwa kwa ajili ya Wakristo wa Kiyahudi waliosema Kiyunani katika maeneo ya Shamu (Siria) na Palestina, ili kuwapa uhakika kabisa kwamba Yesu alikuwa Masihi aliyeahidiwa katika Agano la Kale, naye alitimiza makusudi ya Mungu ya kuchagua Israeli. Wakristo wa Kiyahudi, wakiwa watu wa Masihi, walikusudiwa kupeleka Injili kwa Mataifa. Waisraeli wa Agano la Kale walikosa kutimiza makusudi hayo, lakini Wakristo hao walitakiwa wafanye bidii kueneza Injili hiyo katika Mataifa yote (Mt 28:19-20; taz.8:l 1-12; 11:20-24; 24:14).


Kitabu hiki huenda kiliandikwa katika maeneo ya Antiokia ya Shamu. Antiokia ilikuwa na uhusiano mzuri na maEkklesia ya Kiyahudi katika maeneo yake, pia ilihusika na uenezaji wa Injili katika Mataifa ya mbali (Mdo 11:19-22,27-29; 13:1-4; 15:1-3,22).


Mathayo mtoza ushuru

Kuna thibitisho katika Injili linaloonyesha kwamba mwandishi wake alikuwa Mathayo mtoza Ushuru, ambaye baadaye alikuwa mmojawao wa Mitume 12. Marko na Luka walipoorodhesha Mitume, walimtaja Mathayo, lakini hawakutaja kazi yake ya awali (Mk 3:18; Lk 6:15). Walipomtaja mtoza ushuru aliyekuwa mfuasi wa Yesu, hawakumwita Mathayo bali Lawi, lililokuwa jina lake la pili (Mk 2:14-17; Lk 5:27-32). Inaonekana kama kwa sababu ya kumpenda Mathayo hawakuonyesha wazi kwamba hapo awali alikuwa mtoza ushuru, kwa sababu Wayahudi waliwadharau watu wa taifa lao waliotoza ushuru kwa ajili ya wanyanyasi wa Kirumi.


Mathayo hakuficha kazi yake ya awali ya kuwa mtoza ushuru, bali aliitaja bila kuficha. Alitumia jina la Mathayo, siyo Lawi, aliposhuhudia kuitikia kwake kwa wito wa Yesu (Mt 9:9-13), na alipoorodhesha Mitume 12, alitaja kazi yake ya awali (Mt 10:3). Kitabu chake kinaonyesha shukrani moyoni mwa mtoza ushuru aliyechaguliwa na Yesu kuwa mmojawao wa Mitume wake. Masimulizi yake yanayodokeza hatari ya tamaa ya fedha, yanaonyeshwa katika mafunzo aliyopata mtu ambaye awali maisha yake yalitawaliwa na uchoyo (Mt 18:23-35; 20:1-16; 27:3-10; 28:12-13).


Mathayo alikuwa amefanya kazi yake ya kutoza ushuru mjini Kapernaumu, pwani ya Ziwa Galilaya (Mk 2:13-14). Alikuwa na mapato mazuri na nyumba kubwa ya kutosha kualika watu wengi (Lk 5:29). Inaonekana kama alifurahia maisha yenye usalama na ya hali ya juu, lakini aliacha hayo yote na kuchagua maisha yasiyokuwa na uhakika ya kumfuata Yesu na kueneza habari njema ya ufalme wake (Mt 10:5-23). Alisaidia katika kuimarisha Ekklesia la kwanza (Mdo 1:13), lakini Biblia haisemi neno kuhusu huduma yake ya baadaye.


Mipango ya habari za Injili ya Mathayo

Katika Injili ya Mathayo kuna habari nyingi ambazo pia ziko katika Injili za Marko na Luka, lakini jinsi Mathayo alivyozitumia na kuzipanga ni tofauti. Kwa mfano, Luka alipanga pamoja habari zilizo katika Injili yake tu, akaweka zile zilizopo katika Marko mahali pake. Lakini Mathayo alipanga habari zote kadiri ya utaratibu wake bila kujali kama zilikuwepo pia katika Injili nyingine. Alipanga kila jambo kadiri ya makusudi ya kitabu chake, ili habari zote zipate uhusiano maalumu. Alisimulia'mafundisho mengi zaidi kuliko matendo ya Bwana, Injili yake ikilinganishwa na zile za Marko na Luka, na habari zake mara nyingine hazifuati mfululizo wa wakati wa matukio yake.


Kwa Mathayo habari zimepangwa zaidi kadiri ya mambo muhimu kuliko mfululizo wa wakati. Habari zake zimepangwa ili zihusiane na sehemu tano maalumu za mafundisho ya Yesu, anapowafundisha wafuasi wake mambo yanayotakiwa kwa wale wanaoingia katika ufalme wake. Kila sehemu ya zile tano inamalizika kwa maneno kama haya, 'Yesu alipomaliza maneno hayo...'(Mt7:28; 11:1; 13:53; 19:1; 26:1). Sehemu zile tano zinahusu tabia ya binafsi ya watu waliomo katika ufalme wa Kristo (mafungu ya 5-7), uenezaji wa ujumbe wa ufalme (fungu la 10), mifano kuhusu ufalme (fungu la 13), tabia ya kushirikiana na wengine waliomo katika ufalme (fungu la 18) na kilele cha ufalme wakati wa kurudi kwake Yesu Kristo (mafungu ya 24 na 25).


Makusudi ya mafundisho

Alama moja ya pekee katika Injili ya Mathayo inaonekana zaidi katika habari zinazoonekana katika Injili yake tu. Katika habari hizi kuna dondoo nyingi za Agano la Kale. Mara nyingi Mathayo anaingiza dondoo hizo kwa maneno yanayoonyesha jinsi Agano la Kale lilivyotimizwa katika Yesu (Mt 1:22; 4:14; 8:17; 13:35; 21:4; 27:9).


Zaidi sana Mathayo anaonyesha kwamba Yesu alikuwa Masihi aliyeahidiwa, mwana wa Daudi na utimizaji wa makusudi ya Mungu kwa Israeli (Mt 1:1,17; 2:6; 9:27; 11:2-6; 16:16; 21:9; 26:63-64). Ufalme wa Mungu ulikuwa utawala wa Mungu, na katika Yesu ufalme huo uliingia ulimwenguni (Mt 4:17,23; 5:3; 12:28; 18:1-4; 24:14). Yesu alikuwa mfalme, ingawa hakuwa mfalme wa aina ile ambayo watu wengi zaidi walitazamia (Mt 4:8-10; 21:5,9-11; 25:31,34; 26:52-53; 27:11).


Wakristo wa Kiyahudi mara nyingi waliudhiwa na Wayahudi wasioamini, kwa sababu ya kuacha dini ya mababu zao. Mathayo aliwapa Wakristo hao uhakika mpya akiwaonyesha kwamba wao hawakuwa watu walioacha dini ya Agano la Kale. Wao hasa waliuona utimizaji wa kweli wa dini hiyo. Yesu hakupinga sheria ya Musa, bali alionyesha ukamilifu wa maana yake (Mt 5:17).


Licha ya kuwafundisha Wakristo wa Kiyahudi hali ya juu ya tabia bora iliyotakiwa kwao, Mathayo pia aliwahamasisha wawe na bidii ya kueneza Habari Njema ya ufalme kwa watu wengine (Mt 5:13-16; 10:5-8; 24:14; 28:19-20). Wayahudi wasioamini, lakini walitekeleza mapokeo kwa bidii, daima walilaumiwa (Mt 15:1-9; 23:1-36). Walikosa kupata ufalme ulioahidiwa kwa matokeo ya kwamba, Injili ilipelekwa kwa Mataifa, na wengi wao waliamini (Mt 3:7-9; 8:11-12; 12:21,38-42; 21:43). Yesu aliweka msingi wa Ekklesia. Hakuna upinzani wa Kiyahudi au wa Kirumi ambao ungeweza kushinda Ekklesia hilo (Mt 16:18).