9:1-14:21 USHINDI WA MASIHI

Siku zote Waisraeli walitazamia siku ile ya utukufu na mamlaka makuu ya Masihi. Watu walikuwa na hamu ya kuona siku hiyo ambapo maadui wote wangeangamizwa, na haki ingeimarishwa katika nchi yao chini ya utawala wa Masihi. Kurudi katika nchi yao chini ya uongozi wa Zerubabeli na Yoshua kulikuwa kionjo cha siku ile kubwa. Waisraeli waliweza kutumaini kuwaona maadui zao wa zamani wakishindwa, na uhuru kamili ungerudishwa katika nchi yao.


Mambo hayo yalitokea kweli. Katika miaka ya 334-326 k.K. Iskanda (au Alexander) Mkuu wa Uyunani alieneza utawala wake katika nchi zile zote ambazo awali ziliwashambulia Waisraeli. Ingawa ushindi wa Iskanda Mkuu uliingiza hata nchi ya Is­raeli, wakati ulikuja Waisraeli walipojipatia uhuru kamili chini ya uongozi wa Wamakabayo (143 k.K.). Kwa kweli, wakati ulipowadia, Masihi alikuja katika mtu Yesu Kristo, lakini wakati ule Wayahudi, kwa sababu ya dhambi zao, walipoteza uhuru wao. Vibaya zaidi, walimkataa Masihi.


Unabii wa Zekaria kwa sehemu umetimizwa, lakini bado unangojea utimizwaji wake mkuu zaidi. Utimizaji huo utatokea wakati wa kurudi kwake Yesu Kristo, atakapowashinda maadui wote na kusimamisha ufalme wake ili atawale ulimwengu wote katika amani na furaha. Kwa hiyo katika kitabu cha Zekaria habari za wakati wenyewe hazina uzito zaidi. Matukio yanayochukua muda wa miaka mingi, au yanayotenganishwa na karne kadhaa, yanaweza kuingizwa katika mstari mmoja. Nyakati nyingine zilizo fupi zaidi, zinaweza kuelezwa kirefu sana.


Unabii wa Zekaria siyo maelezo ya matukio ya historia aliyoyaandika kabla ya wakati wake kama takwimu. Ni ufunuo wa makusudi ya Mungu yaliyotolewa ili kufundisha, kuonya, kutia moyo, kuongoza na kuelimisha watu wake. Matimizo yake yanaweza kutokea kwa namna na kwa nyakati tofauti. Mara nyingine utimizaji wake uliweza kuhusu matukio ya wakati wa Iskanda Mkuu hadi Wamakabayo, au katika matukio makubwa zaidi katika maisha na huduma ya Yesu Kristo, au hata katika matukio ya siku ile kubwa ya mwisho ya BWANA ambapo Yesu Kristo atatawala.


Kuadhibiwa maadui na uhuru kurudishwa (9:1-17)

Katika fungu hili Zekaria anaonyesha jinsi Waisraeli watakavyoendelea kutoka hali yao ya wakati ule (yaani kuwa katika nchi yao, lakini bado chini ya utawala wa Uajemi) hadi uhuru kamili, na baadaye hata katika wakati wa utawala wa Masihi. Anaona jeshi linaloshambulia likisogea kutoka kaskazini na kuteka miji ya Shamu (Syria), yaani Hadraki, Dameski na Hamathi, kisha miji ya Foinike, yaani Tiro na Sidoni (9:1-4). Kutoka huko linaendelea kusini kufuatia pwani ya Bahari ya Kati ili kuteka miji ya Ufilisti ya Ashkeloni, Gaza, Ekroni na Ashdodi. Desturi ya Wafilisti ya kula nyama iliyo haramu itakomeshwa, nao watakuwa sehemu ya Is­raeli, kama vile Wayebusi walivyokuwa wakati wa Daudi (5-7; taz.2Sam 5:6-10). Lakini jiji la Yerusalemu litahifadhiwa. Ingawa litakuwa chini ya utawala mkuu wa maadui, halitabomolewa (8).


(Mambo yote yaliyotajwa hapa juu yalitokea wakati majeshi ya Iskanda Mkuu yalipopita katika maeneo yale, yakiteka nchi za maadui wa zamani wa Israeli, pamoja na mfalme wao mkubwa wa wakati huo, yaani Uajemi. Ingawa Iskanda alichukua utawala mkuu wa Yerusalemu, hakubomoa jiji.)


Utawala wa Wayunani utaweza kuenea katika Palestina yote, lakini baada ya muda utapinduliwa. Kisha mfalme wa Mungu atatawala Yerusalemu, ijapokuwa hatakuwa kama mshindi mkali wa kijeshi. Ataingia jijini katika unyenyekevu na utulivu, lakini kwa hali ya heshima ya kifalme, naye ataimarisha utawala wa amani wa dunia yote (9-10).


Baada ya kudokeza kilele cha utukufu wa Israeli kwa njia ya utawala wa Masihi, nabii anarudia tena wakati wa Iskanda Mkuu. Anaonyesha kwamba Mungu atawapa watu wake uhuru kamili kadiri ya agano lake alilofanya nao katika Mlima Sinai (11-12). Taifa la Israeli litakuwa silaha mkononi mwa Mungu ili kuwaangamiza maadui zake, na hivyo kutimiza hukumu ya Mungu juu ya mataifa (13-15). Baada ya kujipatia uhuru wake, taifa litatulia katika maisha ya usalama, furaha na mafanikio (16-17).


Matatizo ya uongozi (10:1-11:3)

Wakati unabii huu ulipotolewa, hekalu lilikuwa limemalizika tangu muda mrefu na maisha jijini Yerusalemu hayakuwa kama yalivyokuwa wakati wa kwanza. Zerubabeli na Yoshua walikwisha kufa, na kwa kukosa uongozi thabiti, Waisraeli walirudi nyuma na kuiga mambo ya dhambi tena waliyoyaona katika mataifa ya jirani. Baadhi yao walitumia vinyago vya uchawi kwa matumaini ya kupata mvua nzuri na mavuno ya kuridhisha. Zekaria anawaambia waache desturi hizo na wamtegemee Mungu peke yake (10:1-2).


Mungu anakasirikia viongozi wa Israeli wasiowajali watu wanaowatawala. Mungu atawaondoa, na mahali pao ataweka viongozi thabiti wenye nguvu watakaoaminika, na kwa nguvu ya Mungu watapindua utawala wa wakati huo (3-5). Wayahudi ambao bado wametawanyika katika nchi za kigeni, watarudi katika nchi yao watakapoishi kwa amani na furaha chini ya ulinzi wa Mungu (6-7). Kutakuwa na misafara mikubwa itakayoelekea nchi ya ahadi, kama ilivyokuwa wakati watu walipotoka Misri chini ya uongozi wa Musa (8-11). Kwa kuitikia neema ya Mungu, watu watamwabudu na kumtii (12).


Kuhusu viongozi wabaya, hukumu yao ni jambo la hakika, haidhuru wenyewe wanajiona kuwa wakubwa sana na wenye mamlaka. Wanaongeza mamlaka na mali yao kwa njia ya kuwanyanyasa watu bila huruma, kwa hiyo hata Mungu naye atawaadhibu bila huruma. Hukumu yake itakuwa kama moto mkubwa unaopita katika misitu yenye miti mikubwa ambapo hata wanyama wakali na wenye nguvu watashindwa kutoroka (11:1-3).


Maigizo mawili mafupi kuhusu uongozi (11:4-17)

Baada ya kutangaza hukumu ya Mungu juu ya uongozi mbaya wa Israeli (11:1-3), Zekaria anaonyesha hukumu hiyo katika maigizo mawili. Katika maigizo hayo anamwigiza mchungaji kama mfano wa viongozi wa watu wa Mungu. Katika igizo la kwanza Mungu alimwambia Zekaria aonyeshe mfano wa mchungaji mwema. Zekaria anaagizwa aangalie watu walionyanyaswa na kunyonywa na wachungaji wabaya waliokuwa na nia ya kujitajirisha tu. Hawakujali shida za kundi lao. Lakini Mungu alimwonyesha Zekaria kwamba bidii yake haikuwa na matumaini ya kufanikiwa. Viongozi pamoja na watu wa kawaida walielekea adhabu inayowafaa (4-6).


Hata hivyo Zekaria anamaliza kucheza igizo lake fupi. Kwa fimbo ya mchungaji iitwayo 'Neema' (au 'Kibali') alijaribu kuwapa kondoo uongozi ule wa neema ambao Mungu aliwatakia. Kwa fimbo nyingine iitwayo 'Umoja' alijaribu kuwaunganisha katika amani na mapatano ya kitaifa. Aliwaondoa hata wachungaji watatu waovu. Matokeo yake, watu walimkasirikia nabii. Walikuwa mbali sana na njia za" Mungu kiasi kwamba waliwapenda wachungaji waovu kuliko mchungaji mwema (7-8).


Kwa hiyo Zekaria alivunja fimbo zake mbili ili kuwaonyesha watu kwamba hakupenda kuendelea kuwa mchungaji wao (9-11; taz. mst.14). Alipowaomba wampe mshahara wake, walimpa kiwango kidogo mno, hata ikawa kiasi cha kumchukiza. Alichukizwa kweli, kwa sababu alijua kwamba mshahara ule ulikuwa mali ya Mungu aliyemtumikia (12-13). Alijua kwamba watu walipendelea aina ya jumuia ambapo wenye uchoyo wangeweza kupata kitu cho chote kwa njia ya kuwanyanyasa wengine. Mwishowe jumuia ya namna hiyo ingejiangamiza yenyewe (14).


Katika igizo la pili Zekaria alicheza sehemu ya mchungaji mbaya aliyekuwa na tabia ile ambayo Waisraeli waliipenda. Uongozi ule wa ukatili na ubinafsi watu waliupenda, naye Mungu angewaadhibu kwa njia hiyo (15-17).


Inawezekana kwamba wakati wa Zekaria au muda mfupi baada yake yalikuwepo matukio yaliyolingana na maigizo yake mawili. Kwa kweli, ulikuwepo mlingano wa ajabu miongoni mwa Wayahudi wakati wa Bwana Yesu. Watu walimkataa Yesu wakapendelea uongozi mbaya wa mafarisayo, masadukayo, waandishi, makuhani na wazee (taz.Yn 10:7-13;26-31). Walimsulibisha Yeye ambaye Mungu alimtoa kwa neema yake ili awaokoe. Walishindana wenyewe kwa wenyewe na mamlaka ya Warumi waliowatawala, na mwisho walijipatia mauaji na uangamizi kwa mikono ya Warumi (mwaka wa 70 b.K.).


Ushindi, lakini pamoja na maombolezo (12:1-13:1)

Mara nyingine Mungu alitumia mataifa ya kipagani ili kuadhibu watu wa Israeli, lakini alipoamua kupiga vita kwa ajili ya Israeli, hakuna adui aliyefaulu kuwashambulia. Katika tukio lililotajwa na Zekaria katika fungu la 12 Mungu anawapa watu wake nguvu, ili waweze kupindua majeshi yaliyozingira Yerusalemu kivita (12:1-3). Mungu anapoingilia kati na kuwasaidia watu wake, mafarasi wa maadui wanavurugwa akili wasifae tena. Viongozi wa Wayahudi wanatambua kwamba, zaidi ya yote, ni Mungu anayesababisha ushindi wa Yerusalemu (4-5).


Askari wa Kiyahudi wanaoongoza mashambulio dhidi ya maadui siyo wenyeji wa Yerusalemu, bali ni watu wa miji na vijiji vya karibu. Kwa njia hii wenyeji wa Yerusalemu hawana nafasi ya kujisifu kwamba wao ndio waliowaangamiza maadui. Sifa ya haki wanapewa ndugu zao wa nchini kwa sababu ya ushujaa wao (6-7). Lakini wote wanatambua kwamba alikuwa Mungu aliyeokoa Yerusalemu (8-9).


Watu wa Mungu walipata ushindi mkubwa, lakini ushindi wao ulikuwa na gharama kubwa. Wanapowaombolezea ndugu zao waliokufa vitani, watu wanajinyenyekeza na kupata tabia mpya ya huzuni kuhusu makosa yao, nao wanamlilia Mungu awahurumie. Sababu kuu kwa maombolezo yao ni kwamba, wanamtambua mtu waliyemwua kabla ya muda mfupi kuwa ndiye aliyetumwa na Mungu ili awaokoe. Inawezekana kwamba walikataa maagizo na maelezo yake kuhusu vita vile, lakini wakati huo wanatambua kwamba wangalipaswa kumheshimu (10). Maombolezo yanaenea katika nchi yote, lakini yanazidi miongoni mwa wale waliohusika na uongozi wa kiraia na kidini jijini Yerusalemu (11-14). Lakini msamaha wa Mungu unapatikana kwa wote wanaohuzunika kweli kwa sababu ya uasi na usaliti wao (13:1).


Manabii wa uongo na mchungaji mwema (13:2-9)

Baada ya kutaja habari za msamaha na utakaso, Zekaria anaendelea na kushughulika na maovu yale yaliyopaswa kuondolewa nchini. Dhambi mojawapo kubwa ya Israeli ilikuwa ibada ya sanamu, na hiyo ilishawishiwa na manabii wa uongo. Kwa hiyo manabii wa uongo wote lazima wauawe (2-3).


Kama nabii wa uongo mmoja anapata nafasi ya kutoroka, anaweza kujaribu kusalimisha maisha yake akitupa nguo zake za unabii asije akaonekana kuwa nabii akajionyesha kana kwamba ni mkulima. Lakini atashindwa kuondoa makovu katika mgongo wake. (Makovu kama hayo yalikuwa alama za wachawi na manabii wa uongo. Yalitokana na kukata alama za 'kichawi' katika ngozi zao; taz.Law 19:28; lFal 18:28.) Kama mtu angeona makovu hayo, nabii wa uongo angesema uongo ili kujilinda, akisema kwamba hayo makovu yalitokana na mapigano au ajali katika nyumba ya rafiki yake (4-6).


Zekaria anarudia habari za uongozi, akitumia mfano wa mchungaji tena. (Kiongozi anayetajwa hapa anaweza kuwa mtu wa 12:10 aliyeuawa na wananchi wenzake.) Kiongozi mteule wa Mungu ni mtu aliye karibu sana na Mungu naye anawaangalia watu wa Mungu kweli. Lakini watu wanamwua na kuwaudhi wafuasi wake. Matokeo ya kifo cha mchungaji huyo ni kwamba, watu wengi zaidi wa wananchi wake watakuwa chini ya hukumu ya Mungu. Wachache wanaopona wanapata mateso makali, lakini kwa njia hiyo watakuwa watu bora na kuingizwa katika ushirikiano wa karibu na Mungu waliyekuwa wamemtegemea. Hao ndio watu wa Mungu kweli kweli (7-9).


Bila shaka mchungaji mwema huyo ni Yesu aliye Masihi (Mt 26:31; Yn 19:37). Watu wake mwenyewe walimwua, na kwa sababu ya kifo chake Waisraeli wengi sana walikuwa chini ya hukumu ya Mungu. Lakini wachache waliokolewa. Hao walikuwa watu wa Mungu kweli, ingawa walipata mateso makali kutoka kwa waasi (Rum 9:6-8; 11:5-7; Gal 4:28-29).


Ufalme wa Masihi (14:1-21) Katika sehemu ya mwisho wa kitabu chake, Zekaria anatoa muhtasari wa ushindi wa Masihi wa dunia yote. Wasomaji wake wanajua maeneo ya karibu na Palestina tu, kwa hiyo nabii anataja mambo ya jiografia ya maeneo yale tu. Mifano mingine pia imetolewa katika desturi za maisha yaliyojulikana kwa Wayahudi.


Habari zinaanza kwa kuwaonyesha maadui wa Mungu wanaodhania kwamba hatimaye waliwashinda watu wake (wa Yerusalemu). Wakitulia na kufurahi kwamba wamepata ushindi, wanakaa katikati ya jiji ili wagawanye mateka yao, ambapo Wayahudi wengine wanapelekwa kifungoni na wengine wamefungwa jijini (14:1-2). Ghafla Mungu anashughulika katika hukumu ya mwujiza. Kama vile hapo kale alivyogawanya Bahari ya Shamu ili kufanya njia ya kuokoka kwa watu wake kutoka Misri, ndivyo alivyopasua milima mashariki mwa Yerusalemu ili kuweka njia kwa watu wake waweze kuokoka kutoka jiji lililoshikwa na maadui (3-5).


Mungu anawaridhisha watu wake na kuwapa mahitaji yao kwa njia ya kubadili utaratibu wa ulimwengu kwa ajili ya manufaa yao. Hawana shida yo yote (6-8). Wakati huo Mungu anaweka kiti chake cha enzi katika jiji la Yerusalemu lililojengwa upya na kukaliwa na watu, na kutoka huko anatawala ulimwengu. Milima ya karibu na Yerusalemu inasawazishwa, ili jiji lionekane limeinuliwa machoni pa mataifa yote, na Mungu wa Israeli anaabudiwa koteduniani (9-11).


Maadui wanaangamizwa katika hukumu ya kutisha, na Israeli inafidiwa hasara zote iliyopata na majeshi yaliyoteka nyara kwao (12-15). Watu waliosalia katika mataifa wanatakiwa kufika Yerusalemu ili kumwabudu Mungu. Mkutano huo mkubwa wa mataifa unafananishwa na mavuno ya Israeli wakati wa sikukuu ya Vibanda katika mwisho wa msimu wa ukulima na mavuno (16-19).


Hakutaendelea kuwa tofauti baina ya vitu vitakatifu na visivyo vitakatifu. Kila kitu ni kitakatifu nacho kinafaa kwa huduma ya Mungu, hata vyombo vya nyumbani na vikengele katika mashingo ya mafarasi. Vitu vyote ni vitakatifu, kwa hiyo wafanya biashara hawahitajiki tena hekaluni ili kubadilisha vitu visivyo vitakatifu kwa vitakatifu. Utakatifu wa kweli utadumu na kuimarishwa katika dunia yote (20-21).