Jiji la Yerusalemu ambalo awali lilijaa shughuli za biashara, sasa lina ukiwa. Limefanana na mwanamke aliyefiwa na mumewe, au binti wa mfalme aliyelazimishwa kuwa mjakazi. Mataifa ('Wapenzi' wake) ambayo jiji lilifikiri kwamba yangelisaidia yameonekana kuwa hayafai, na baadhi yake yamegeuka kuwa maadui zake (1:1-3).
Viongozi wake wametoroka saa ya taabu ilipokuja, wakiwaacha watu wake washambuliwe tu, wanyang'anywe mali yao na kupelekwa kifungoni. Sasa, shughuli zote za kawaida ya kila siku zilipokwisha, zimebaki kumbukumbu tu za maisha ya kupendeza na starehe zilizofurahiwa zamani, na kumbukumbu za jinsi maadui zake walivyowacheka watu wakati wa kuanguka kwa jiji lao (4-7).
Sababu ya ukiwa wa Yerusalemu ni dhambi zake. Katika ibada zake za sanamu na uovu wake, watu wake waliishi kama mwanamke aitwaye malaya, na sasa wametendewa kama mwanamke wa namna hiyo anavyotendewa (8-9). Askari wa Babeli hawakuingia hekaluni tu (jambo ambalo ni marufuku kwa mtu wa mataifa), bali pia walichukua vitu vyake vya thamani vilivyo vitakatifu. Watu waliopata njaa kali sana katika jiji lililozingirwa kivita walibadilisha hata vitu vyao vya thamani kwa askari wa maadui kwa kusudi la kupata chakula kidogo (10-11).
Jiji linalosema kama mwanadamu, katika shida yake linawauliza wapita njia kama hawana huruma nalo, kwa sababu ya shida yake kubwa ambayo Mungu ameliletea. Limeshambuliwa na kuteketezwa kwa moto nalo limeachwa katika hali ya magofu pasipo matumaini (12-13). Dhambi zake zililigandamiza chini kama vile kongwa nzito shingoni mwa mnyama afany aye kazi. Mungu alipoliletea askari wa maadui, jiji halikuweza kujitetea dhidi yao (14-16).
Ingawa jiji halipati huruma linayoililia, halina uchungu juu ya Mungu. Linajua kwamba Mungu ameliadhibu kwa haki kwa sababu ya dhambi zake. Linawaonya wengine wajifunze kutokana na mambo yaliyotokea kwake (17-18). Lilipolilia msaada haukuwepo msaada. Baadhi ya watu wake wamekufa njaa wakati wa kuzingirwa kivita, wengine waliuawa au kupelekwa kifungoni wakati jiji lilipotekwa na maadui (19-20).
Huzuni za Yerusalemu zinazidishwa na dhihaka za majirani zake. Wao wanafurahi juu ya kuanguka kwa Yerusalemu, lakini wao wenyewe ni waovu. Jiji linaomba kwamba haki ya Mungu itendeke kwa mataifa hayo ya jirani kama ilivyotimizwa juu ya Yuda (21-22).
Wazo kuu la shairi hili la pili ni kwamba, maafa yaliyokuja juu ya Yuda ni kazi ya Mungu. Yeye alinyenyekeza taifa lililotukuzwa, aligeuza utukufu wake kuwa giza (2:1). Jiji na mashamba, hekalu na ngome, vyote vimebomolewa naye. Mungu ambaye awali alikuwa mlinzi wa Israeli, amegeuka kuwa mshambulizi wake. Mbali na kuwahurumia amewakasirikia (2-5).
Mungu amebomoa hekalu akaliacha kama kibanda cha zamani kilichobomoka katika bustani iliyoachwa bila ya kutumiwa. Sherehe za dini zimekoma. Katika nyumba ya Mungu ambayo awali ilikuwa takatifu, askari wa kipagani wamepiga kelele wakati wa kuibomoa na kuiba vitu vyake vya thamani (6-7). Kama vile waashi wanavyopima kwa uangalifu wanapojenga ukuta, ndivyo Mungu alivyobomoa ukuta wa Yerusalemu kwa uangalifu. Aliwaruhusu maadui wavamie jiji, na wakati huo viongozi wa Yerusalemu wameondoka (8-9).
Mwandishi analia anapoeleza hali ya Yerusalemu katika kilele cha kuzingirwa na maadui. Njaa kali ilienea kila mahali, wala viongozi wa jiji hawakuweza kufanya jambo lo lote ili kubadilisha hali hiyo. Watoto waliopita mitaani wakitafuta kitu cho chote cha kuliwa wanaanguka na kufa njaa (10-13).
Baada ya kuanguka kwa jiji, watu wanaweza kuona wazi jinsi utabiri wa manabii wa uongo ulivyowapoteza walipowatabiria wokovu. Afadhali wangalisema sawa sawa na manabii wa kweli waliolaumu dhambi za watu na kuwaonya kuhusu hukumu ya Mungu, ambayo ingekuja kama wasingetubu (14; taz.Yer 14:13-16; 23:14-17). Sasa unabii wa manabii wa kweli umetimia. Maadui wa Yerusalemu wanadhihaki jiji lililoanguka (15-17; taz.Yer 24:8-10; 27:12-15).
Tena mtunzi anatoa mfano wa hali ya kusikitisha moyo iliyokuwepo Yerusalemu iliyozingirwa watu wanapomlilia Mungu awahurumie kisha wanakufa njaa. Wengine huwachinja hata watoto wao na kuwala (18-20). Kama vile awali wasafiri walivyofika Yerusalemu katika makundi makubwa kwa ajili ya ibada za sikukuu, ndivyo askari wa maadui wanavyoingia jijini kwa makundi makubwa, lakini kwa kusudi la kuwaua wenyeji wake tu (21-22).
Shairi hili ni tofauti katika utunzi wake likilinganishwa na mashairi mawili yaliyotangulia. Mtunzi anasema kana kwamba yeye ni mjumbe wa taifa lote la Yuda, akieleza mateso ya Yuda kana kwamba ni mateso yake binafsi, na mateso yale ni hukumu ya haki ya Mungu (3:1-3). Anafanana na mtu aliye karibu na kufa kwa sababu ya njaa kali. Kwa kweli, hujisikia kana kwamba amekwisha fika katika wafu (4-6). Amefanana na mtu aliyefungwa minyororo na kuwekwa katika magereza ya mawe pasipo njia ya kutoka (7-9).
Mungu anaonekana kwake kama mnyama mkali wa porini anayerarua mawindo yake vipande vipande, au kama mwindaji aliyeua mawindo yake kwa mshale (10-12). Hali amedhihakiwa na kuonewa, mtunzi hujisikia kama mtu aliyeadhibiwa kwa kulishwa na kunyweshwa vitu vinavyomdhuru (13-15). Amefanana na mtu ambaye uso wake umechubuliwa katika nchi na furaha yake ya maisha imekwisha (16-18). Anajisikia kuwa ameumizwa na kuhuzunishwa, lakini katika giza lote la mateso yake anaanza kuona kidokezi kidogo cha matumaini (19-21).
Mungu anaweza kuadhibu, lakini mwandishi bado anamtegemea Yeye. Anajua kwamba upendo wake haubadiliki. Upendo huo ni imara nao ni jambo la kuaminika (22-24). Mungu anafundisha nidhamu, lakini watu wale wanaovumilia watafurahia ukamilifu wa wokovu wake (25-27). Ni muhimu kujinyenyekeza, hata mbele ya adui ambaye Mungu anamtuma ili kuwaadhibu watu wake (28-30).
Watu wa Mungu wawe na uhakika kwamba hatawatupa watu wake mpaka milele wala hapendezwi kuwaadhibu. Hata hivyo, adhabu ni jambo la lazima (31-33). Lakini Mungu hapendi adhabu yenye ukatili isiyokuwa lazima, inayodharau haki ya mtu au kugeuza sheria (34-36).
Watu wakijua kwamba Mungu anatawala mambo yote, nao wakikiri kwamba hukumu zake ni haki, wataweza kuvumilia adhabu yake (37-39). Kwa hiyo mtunzi anawahamasisha watu wake wajihoji, ili watambue dhambi zao na kukubali kwamba walipata adhabu ya haki, na hivyo wamgeukie Mungu na kutafuta msamaha wake (40-42).
Mwandishi akisema kana kwamba yeye ni taifa lote la Yuda, anakubali dhambi zake. Anakiri kwamba dhambi hizo zilikuwa kizuizi au wingu kati yake na Mungu, zikimzuia Mungu asiweze kusikia maombi yake ya kutafuta rehema. Matokeo yake, ameharibiwa na kuaibishwa (43-45). Amejaa huzuni kwa sababu ya ukatili na aibu aliyopata kutoka kwa maadui zake (46-48). Analia kwa sababu ya mateso makali yaliyoletwa juu ya watu wa Yerusalemu (49-51).
Mwandishi anajisikia kama ndege aliyewindwa au kama mtu aliyetupwa katika shimo la maji ili afe (52-54). Lakini sasa baada ya kutubu kwake, Mungu anasikia kilio chake kwa msaada naye anamhakikishia kwamba hana haja ya kuogopa (55-57). Hatimaye anajua kwamba Mungu amemwokoa. Wakati huo huo anamkumbusha Mungu kuhusu ukatili wa wale waliomtesa (58-60), kwa sababu wao, kwa moyo mgumu, walimtukana na kumdhihaki mtu mwenye shida kali (61-63). Anakabidhi hukumu juu ya watu wale mkononi mwa Mungu (64-66).
Utukufu wa zamani wa Yerusalemu unalinganishwa na shida yake ya wakati huo. Hekalu lililopendeza sana kwa utukufu wake hapo awali, sasa limechafuliwa na kubomolewa, ni mfano wa utukufu wa zamani wa watu ambao sasa wameaibishwa na kuvunjwa mioyo. Maiti za wenyeji wa Yerusalemu zimelala mitaani kama vigae vya vyombo vya udongo (4:1-2). Mtunzi anakumbuka tena hali ya kutisha wakati jiji lilipozingirwa na maadui. Hata wanyama wakali wa porini hutoa chakula kwa watoto wao, lakini jijini Yerusalemu akina mama hawawezi kuwalisha watoto wao. Matajiri na wenye heshima wanakufa mitaani kama waombaji (3-5).
Adhabu ya Sodoma ilikuwa kali, lakini ile ya Yerusalemu imezidi, kwa sababu Sodoma iliangamizwa ghafla siku moja tu, lakini Yerusalemu inaangamizwa katika maumivu makuu ya muda mrefu (6). Hata watu wa hali ya juu waliotumia muda mrefu na fedha nyingi ili waonekane wazuri, sasa wanaonekana vibaya nao wanachukiza kutokana na magonjwa na njaa kali (7-8). Ingekuwa afadhali kuuawa vitani kuliko kufa kwa njaa au kulazimishwa kula watoto wake mwenyewe (9-10). Wenyeji wa Yerusalemu walifikiri kwamba, kwa kuwa BWANA alikuwa Mungu wao, maadui wasingeweza kuingia katika jiji lao, lakini sasa Mungu mwenyewe amelibomoa (11-12).
Lawama kuu kwa kuangamizwa Yerusalemu inawapata viongozi wake wabaya, na hasa manabii na makuhani. Wao, kuliko mtu mwingine, wanastahili lawama kwa kusababisha machafuko ya maisha yaliyoleta hukumu ya Mungu juu ya jiji (13). Watu wakitambua jambo hili, wanawafukuza viongozi wao wa zamani watoke jijini, wakiwatendea kama wakoma. Wakimbizi hao wakijaribu kuishi sehemu nyingine, wenyeji wa sehemu hiyo wanakataa kuwapokea (14-16).
Mtunzi anakumbusha jinsi Yerusalemu ilivyotazamia msaada kutoka Misri, lakini msaada wao haukupatikana. Badala yake Wababeli walifika, wakiwafanya wenyeji wa Yerusalemu kuwa wafungwa katika mji wao wenyewe (17-18; taz.Yer 37:6-10). Watu waliojaribu kukimbilia milimani walikamatwa, pamoja na mfalme Sedekia ambaye watu walimtumaini bure (19-20; taz.Yer 39:3-5).
Waedomu walifurahi walipowaona maadui zao wa zamani, yaani Wayuda, wakipinduliwa, lakini Waedomu pia watapinduliwa, ila kinyume cha Wayuda, wao hawatainuka tena. Kubomolewa kwa Yerusalemu ni jambo la muda, lakini Edomu haitainuka tena (21-22; taz.Zab 137:7; Obad 10-14).
Inaonekana kama shairi hili liliandikwa katika nchi ya Yuda muda fulani baada ya kuanguka kwa Yerusalemu. Watu wale tu wasiofaa kabisa kwa Wababeli waliachwa nchini, na shairi hili linaonyesha baadhi ya matatizo yaliyowapata (taz.Yer52:16).
Watu wanapomsihi Mungu awahurumie, wanamkumbusha shida kali walizo nazo (5:1). Mauti iliharibu familia zao, na washambulizi walitwaa nyumba zao na mashamba yao (2-3). Wanapaswa kuishi na kufanya kazi kama watumwa katika nchi yao wenyewe, wakipaswa kununua hata maji ya kunywa kwa mabwana wao wa kigeni (4-5). Wazazi wao walijaribu kuokoa taifa lao kwa njia ya kutafuta msaada kwa Wamisri na Waashuri, lakini kwa kweli walileta uharibifu juu ya nchi. Sasa watu wanapaswa kujinyenyekeza kwa walinzi wa Babeli ambao wenyewe ni watumwa tu (6-8).
Hali ya nchini Yuda ni ya tabu sana. Watu wanapaswa kutafuta chakula katika sehemu za nyika, na wakifanya hivyo wako katika hatari ya kuuawa na wezi wajifichao porini (9-10). Wanawake wa Yuda wanafanyiwa jeuri, wakuu wa zamani wanateswa na watoto wanalazimishwa kufanya kazi kama watumwa (11-13). Desturi za zamani zimepita, na pamoja nazo furaha imeondoka nchini (14-15). Watu kila mahali wanasikitika tu, wanakata tamaa na kuona aibu. Lakini wanakubali kwamba ni dhambi zao wenyewe zilizowaletea matatizo hayo yote (16-18).
Katika ombi la mwisho lenye dhiki kubwa, watu wanamlilia mtawala mkuu wa ulimwengu, ili asiwakatae, bali awarudishe kwake tena. Wanaomba ajenge taifa lao upya na kuwapa furaha ile tena waliyokuwa nayo hapo zamani. Mungu ni wa milele wala habadiliki, nao ni watu wake. Kwa kweli, hatawasahau watu wake (19-22).