1:1-10:10 MAANDALIZI YA SAFARI


Sensa ya watu waliofaa kwa jeshi (1:1-54)

Kabla ya kuondoka katika Mlima Sinai, Musa alifanya sensa ya wanaume wote waliofaa kwa kazi ya jeshi, kama mipango ya maandalizi ya vita vilivyowakabili. Alisaidiwa kazi hiyo na viongozi 12 waliochaguliwa kutoka makabila 12 ya Israeli (1:1-16). Sensa hiyo bila shaka ilichukua muda wa miezi kadhaa, nayo ilikwisha siku 20 kabla ya watu kuondoka Sinai (17-46; 10:11).


Walawi hawakuhesabiwa katika sensa hiyo, kwa sababu wao hawakuhitajiwa kwa huduma ya jeshi. Huduma yao ilikuwa kuchukua, kusimamisha na kutunza hema la kukutania. Iwapo Waisraeli waliweka marago yao mahali na kufanya kambi, Walawi nao waliweka mahema yao karibu na hema la kukutania, ambapo makabila mengine yaliweka marago yao mbali zaidi, kwa kadiri ya mpango unaoelezwa katika mafungu yafuatayo (47-54).


Mipango kwa marago na safari (2:1-34)

Marago yalipopangwa, makabila 12 yalipangwa katika makundi manne, kila kundi likiwa na makabila matatu. Kila upande wa hema la kukutania kulikuwa na kundi moja. Tena kila kundi katika yale manne lilikuwa na bendera yake iliyochukua jina la kabila ambalo mkuu wake aliwazidi wenziwe kwa utaratibu wa kuzaliwa kwa wana wa Israeli. Kundi lililokuwa mashariki mwa hema la kukutania lilikuwa chini ya bendera ya Yuda, na kila mara watu waliposafiri, kundi hilo lilitangulia (2:1-9). Kundi lililopanga marago yake kusini mwa hema la kukutania, lilikuwa chini ya bendera ya Rubeni, na kundi hilo lilichukua sehemu ya pili katika msafara wa watu wote (10-16). Kundi lililofuata katika msafara lilikuwa la Walawi waliochukua hema la kukutania. Kwa njia hiyo hema la kukutania na kabila lililolihudumia lilikuwa katikati ya maandamano, kama lilivyokuwa katikati ya marago yote, na hivyo habari muhimu ya kwamba Mungu alikuwa katikati ya watu wake daima ilithibitishwa (17). Kundi la chini ya bendera ya Efraimu lililopanga marago yake magharibi mwa hema la kukutania, lilikwenda nyuma ya hema katika msafara (18-24); na kundi la bendera ya Dani lililopanga marago kaskazini mwa hema la kukutania, lilikuwa katika mwisho wa msafara (25-31). Walawi walikuwa na mipango yao ya pekee (32-34; taz.3:14-39).


Maana kubwa ya Walawi (3:1-51)


Maelezo yanatolewa kuhusu hali ya Walawi katika jamii yote ya Israeli na huduma zao walizopewa. Ingawa Walawi wote walikuwa watumishi wa Mungu wa namna ya pekee, wale walioweza kuwa makuhani walikuwa wazao wa Haruni tu. Kwa hiyo mwandishi anatoa maelezo zaidi kuhusu ukoo wa Haruni (3:1-4). Kazi ya Walawi ilikuwa kumsaidia Haruni na makuhani katika kazi ya huduma na utunzaji wa hema la kukutania, na shughuli za kidini za watu, lakini kazi yenyewe ya ukuhani iliweza kufanywa na Haruni na wanawe tu (5-10; taz.lNya 23:3-5,24-32).


Mungu alikuwa amewahifadhi wazaliwa wa kwanza wa Israeli wakati wa hukumu ya Pasaka huko Misri, kwa hiyo wazaliwa wale wa kwanza walikuwa mali ya Mungu. Lakini kwa ajili ya huduma ya hema la kukutania, Mungu aliona ingefaa zaidi kuteua kabila lote la Lawi kuwa mali yake kwa namna ya pekee kuliko wale waliohifadhiwa katika hukumu ya Pasaka (11-13).


Kisha Walawi walihesabiwa na kugawanywa katika makundi matatu, kufuatana na koo tatu zilizotokana na wana watatu wa Lawi (14-20; taz.Kut 6:16). Walawi walipanga marago yao kati ya hema la kukutania na marago ya makabila mengine yaliyokuwa nje zaidi (taz.l:53).


Kundi la ukoo wa Gershoni lilipanga marago yake magharibi mwa hema la kukutania, nalo liliangalia mapazia mbalimbali ya hema na yale ya uani (21-26). Kundi la Kohathi lilipanga marago yake kusini mwa hema la kukutania, nalo lilikuwa na wajibu wa kuangalia vitu vitakatifu sana vya hemani, kama vile meza, madhabahu, kinara, sanduku la agano, vyombo vingine vya hemani na pazia lililokuwa kati ya Mahali Patakatifu na Patakatifu pa Patakatifu (27-32). Kundi la Merari lilipanga marago yake kaskazini mwa hema la kukutania, na wajibu wake ulikuwa kuangalia mbao, nguzo na vifaa vya chuma na shaba vya hema la kukutania na vya uani (33-37). Musa, Haruni na makuhani walipanga marago yao mashariki mwa hema, mbele ya mlango wake, nao walikuwa na wajibu wa kuziangalia na kuziendesha sherehe zote za dini (38-39).


Sensa ilionyesha kwamba walikuwepo wazaliwa wa kwanza 22.273, lakini Walawi walikuwa 22.000 tu. Wazaliwa wa kwanza walibadilishwa na Walawi, yaani kwa kila mzaliwa wa kwanza Mlawi mmoja aliingia. Kwa njia hii wazaliwa wa kwanza 273 walibaki bila ya kubadilishwa. Hao bado waliendelea kuwa mali ya Mungu. Kwa hiyo ilibidi wakombolewe kutoka kwa Mungu kwa njia ya kulipa pesa kwa wajumbe wa Mungu, yaani kwa makuhani (40-51).


Huduma mbalimbali za Walawi (4:1-49)

Wakati huo sensa nyingine ya Walawi ilichukuliwa, lakini walihesabiwa wale tu waliokuwa na umri wa kati ya miaka 30 na 50, kwa sababu watu wenye umri huo ndio waliotumika katika huduma ya Walawi (4:1-3). Kazi iliyoelezwa hapa ilihusu usimamishaji wa hema la kukutania na kufungia vifaa vyake kwa ajili ya uchukuzi (maelezo zaidi yametolewa 7:1-11).


Makuhani wenyewe walifungisha vyombo na vifaa vitakatifu vingine, kwa sababu hata Wakohathi waliochukua vyombo vile, hawakuruhusiwa kuviona wala kuvigusa. Vitambaa laini sana vilitumiwa kuhifadhi vyombo vile visipate mikwaruzo, na kifuniko kingine cha ngozi ya wanyama kilikinga madhara yatokanayo na hali ya hewa. Vyombo na vifaa vyote vilichukuliwa katika miti ya kuchukulia au mbao. Sanduku la agano lilikuwa na kitambaa cha pekee cha nje chenye rangi ya samawi, ili watu wote wajue chombo hicho chenye heshima katika maandamano yao (4-20).


Baada ya kuondoa vifaa vya ndani na vyombo vyote katika hema, mapazia yote na vifuniko vilitelemshwa. Mapazia hayo yalichukuliwa na Wagershoni (21-28). Kisha mbao, mataruma na nguzo vilifunguliwa na kufungiwa vifurushi kwa ajili ya kuchukuliwa na watu wa Merari (29-33).


Mwana mkubwa wa Haruni aliyebaki, Eleazari, aliyekuwa mkuu wa Walawi wote, aliangalia kazi zile zote. Aliwaangalia hasa Wakohathi, kwa sababu wao walichukua vyombo vitakatifu zaidi, ambapo ndugu yake, Ithamari, aliwaangalia na kuwaongoza Wagershoni na Wamerari (3:32; 4:16,28,33). Kisha mwandishi aliandika idadi ya watu waliofanya kazi katika makundi matatu ya Walawi (34-49).


Sheria kuhusu unajisi na kulipa fidia 5:1-10)

Sheria zilizojumlishwa katika fungu la tano zinahusu matatizo yanayoweza kutokea mahali watu wengi wanapoishi pamoja katika jumuia, kama walivyoishi Waisraeli. Watu waliokuwa najisi kidini, ama kutokana na ugonjwa au kwa sababu nyingine, walipaswa kuishi nje ya marago, ili kuonyesha kwamba uovu haukuweza kudumu katika marago ambapo Mungu alifanya makao yake. Kutengwa kwa watu hao pia kulizuia magonjwa yasiwaambukize wengine (5:1-4; taz.maelezo yaLaw 13:1-15:33).


Iwapo mtu, kwa sababu ya kutoangalia, alimdhuru mwenziwe au kumtia hasara, alipaswa kukiri kosa lake, atoe sadaka ya hatia, naye afidie hasara yake pamoja na kulipa faini ya sehemu moja ya tano (asilimia 20) ya thamani yake. Iwapo mtu aliyekosewa hakupatikana wala jamaa yake wa karibu, fidia pamoja na faini yake zililipwa kwa makuhani (5-10; taz.Law 5:14-6:7).


Wasiwasi wa zinaa (5:11-31)

Iwapo mtu alikuwa na wasiwasi kwamba mke wake alimdanganya kwa kutembea na mwanamme mwingine, lakini hakuwa na uthibitisho, aliweza kumpeleka mkewe kwa kuhani pamoja na sadaka ndogo ya dhambi, ili kuhakikisha kama alikuwa na hatia au sivyo (11-15; Law 5:11). Kipimo cha kuhani kiliitwa hukumu ya majaribu.


Kuhani alinena kiapo cha laana iliyokaa juu ya mwanamke asiyekuwa mwaminifu, akaandika laana ile kwa wino, kisha akaoshea wino ule katika chombo chenye maji matakatifu na chenye mavumbi yaliyookotwa chini katika hema la kukutania. Mwanamke akakubali laana ile juu ya dhambi kama hiyo kwa njia ya kushika sadaka ya dhambi mkononi mwake na kuapa kiapo. Kisha kuhani akasogeza sadaka madhabahuni, naye mwanamke akany wa maji yale (16-26).


Sherehe ile bila shaka ilikuwa na maana sana kwa roho ya mtu, kwa sababu kwa njia ya kunywa maji yale, mwanamke aliingiza ndani ya mwili wake mifano ya utakatifu wa Mungu (mavumbi ya hemani) na laana yake juu ya dhambi (wino ule). Lakini kama hakukosa, hakuwa na wasiwasi wo wote, kwa sababu maji yale yalikuwa yenye vumbi kidogo tu, wala yasingesababisha ugonjwa. Lakini kama mwanamke alipatwa na maumivu makali ya ghafla, ilionyesha wazi kwamba alikuwa na hatia (27-31).


Kanuni kama hizo zilijulikana kuwa majaribio kwa njia ya kiapo, nazo zilitumiwa sehemu mbalimbali na mataifa ya kale, na bila shaka hata katika Israeli. Zilitumiwa kwa kuhakikisha kama mtu alikuwa na hatia au sivyo katika hali mbalimbali za mashaka ya makosa. Mungu alitumia desturi ile iliyojulikana sana akaitakasa na kuiondolea hali ya upagani na kila kitu kilichofuatana nayo kwa kawaida, ili kuingiza mioyoni mwa watu wake usafi na uaminifu aliotaka katika maisha ya ndoa. Majaribio ya kipagani kwa njia ya kiapo, kwa kawaida yalikuwa ya ukatili sana, nayo yalimfanya mtu kuwa na hatia tu, hata kama hakukosa, isipokuwa jambo la ajabu lilitokea lililoweza kuondoa wasiwasi. Majaribio ya Kiebrania yaliyoelezwa hapa, kwa kawaida hayakuwa na dawa ya kumdhuru mtu, wala hayakukusudiwa kumwonea mtuhumiwa.


Kiapo cha unadhiri (6:1-21)

Tusichanganye majina ya Nadhiri na Mnazareti (yaani mwenyeji wa mji wa Nazareti). Jina la Nadhiri linatokana na neno la Kiebrania 'nazir'. Maana yake inadokeza kwamba kiapo cha unadhiri kilikuwa cha kujitenga au kujiweka wakfu. Mtu aliweza kuapa kiapo cha namna hiyo, kama alitaka kueleza wazi kwamba alijitenga au alijiweka wakfu kwa ajili ya Mungu kwa muda fulani, ili atimize ahadi au kazi fulani ya pekee (6:1-2).


Wanadhiri walionyesha heshima ya kiapo chao kwa mambo matatu maalumu. Kwanza, walikataa kutumia divai na kitu cho chote kilichoweza kufaa kwa kutengenezea divai, wakionyesha kwamba kwa muda huo walikataa furaha yo yote ya maisha, na wakati huo huo walihakikisha kwamba haikuwezekana kujisahau au kuacha kujitawala kwa sababu ya ulevi. Pili, waliacha nywele zao zikue bila ya kukatwa, wakiwaonyesha watu wote kwamba waliishi katika masharti ya pekee waliyokuwa wameyakubali kwa sababu ya kiapo chao. Tatu, hawakukaribia maiti au mzoga, wakisisitiza jinsi ahadi zao kwa Mungu zilivyodai utakatifu kabisa (3-8).


Hapakuwa na njia ya msaada, kama mtu alivunja kiapo chake kwa makusudi, lakini kama aligusa maiti kwa ajali, aliweza kuomba msamaha kwa njia ya sherehe ya kutoa sadaka ya ndege wawili (sadaka ya kawaida ya sherehe ya unajisi; taz.Law 15:13-15), na mwana-kondoo (sadaka ya hatia ya kuongezea; taz.Law 5:6). Lakini muda wote alioshika kiapo chake ulipotea, naye alipaswa kuanza upya tena (9-12).


Katika mwisho wa muda wa kiapo chao, wanadhiri walitoa sadaka na kunyoa nywele zao. Hivyo masharti yao matatu ya unadhiri yalifikia mwisho wake (13-20). Kuhusu jambo waliloapia, ilikuwa lazima wawe wametimiza lile walilokuwa wameliahidi katika kiapo chao. Uaminifu wao ungeonyeshwa kama wangetoa sadaka ya hiari kadiri ya uwezo wao licha ya sadaka zile za lazima (21).


Baraka ya makuhani (6:22-27) Makuhani walipowabariki watu, baraka iliyotangazwa ilikuwa kumbukumbu lingine kwamba Mungu peke yake alikuwa Ndiye aliyewapa Waisraeli afya, mafanikio, ulinzi na usalama. Katika neema na huruma yake angevumilia udhaifu wao, angerekebisha makosa yao na kuwapa furaha tele katika baraka zake zisizo na kikomo. Wao walikuwa watu wa Mungu Mwenyewe (22-27).


Sadaka za viongozi wa Israeli (7:1-88)

Masimulizi ya habari yanarudia tena kwa kifupi sherehe ya kuwekwa wakfu kwa hema la kukutania iliyokuwa imepita kama mwezi mmoja hivi (7:1; taz.Kut 40:17; Hes 1:1). Katika sherehe hiyo viongozi wa makabila 12 walileta sadaka zao madhabahuni na kuzitoa kwa Mungu. Tukio hilo linaelezwa hapa, labda kwa kusudi la kutoa maelezo kuhusu magari na ng'ombe ambao wangetumiwa kwa uchukuzi wa hema la kukutania. Wagershoni waliochukua mapazia walipewa magari mawili na ng'ombe wanne. Wamerari walipewa magari manne na ng'ombe wanane, ili kuchukua mizigo mizito zaidi, kama vile mataruma, mbao, nguzo na vitako vyake. Wakohathi waliokuwa na wajibu wa kuchukua vifaa na vyombo vitakatifu, hawakupewa magari wala ng'ombe, kwa sababu wao walipaswa kuchukua vitu vile kwa kutumia miti ya uchukuzi waliyojitwisha mabegani mwao (2-11).


Viongozi wote wa makabila 12 walitoa kiwango sawa. Walishiriki pia kulipa bei ya magari na ng'ombe sawa, nao walitoa sadaka, vyombo na wanyama sawa, kama mahitaji yalivyokuwa kwa sherehe ya sadaka za hema la kukutania (12-88).


Habari zaidi kuhusu hema la kukutania (7:89-8:4)

Maneno machache yanaeleza jinsi Musa alivyopokea maneno na maagizo ya Mungu katika Patakatifu pa Patakatifu. Kwa kawaida hakuna mtu isipokuwa kuhani mkuu aliweza kuingia Patakatifu pa Patakatifu, Lakini hali ya Musa ilikuwa ya pekee (89; taz.l2:7-8; Kum 34:10-12). Musa alimkabidhi Haruni maagizo, ili kuhakikisha kwamba taa zilizowekwa juu ya kinara chake, ziliwekwa katika hali sahihi, ili mwanga wake umulike hata kiambaza kilichozikabili, na hivyo zitoe mwanga wa kutosha ndani ya Patakatifu (8:1-4).


Kutakaswa kwa Walawi (8:5-26)

Sherehe inayoelezwa hapa inafanana na ile ya kutakaswa kwa makuhani, ilivyokwisha elezwa katika Law 8:1-36. Kuoga, kunyoa nakutoa sadaka ya dhambi kulionyesha kuoshwa dhambi, na kutoa sadaka ya kuteketezwa kulionyesha kuwekwa wakfu kwa watumishi wa Mungu. Tendo la viongozi wa makabila 12 (walilofanya kwa niaba ya taifa lote), yaani kuweka mikono yao juu ya vichwa vya Walawi, lilionyesha kwamba watu wote waliwakubali Walawi kuwa wajumbe wao. Kwa njia ya tendo la kimfano la kuinua na kushusha mikono yake, Haruni aliwasogeza Walawi mbele ya Mungu kuwa sadaka ya kutikiswa, yaani wawe katika utumishi wa Mungu (5-13). Kisha Mungu aliwarudisha Walawi kwa Haruni, ili wamsaidie yeye na makuhani wengine katika kazi zao (14-19). Mambo yote yalitimizwa kadiri ya maagizo ya Mungu (20-22).


Umri wa miaka 25 unatajwa hapa kuwa umri wa lazima au umri mdogo wa kuanzia huduma ya Kilawi, ingawa katika 4:3 umri mdogo ulitajwa kuwa miaka 30. Inawezekana kwamba kulikuwa na muda wa mamndisho yaliyochukua miaka mitano. Walawi walistaafu huduma yao maalumu walipotimiza miaka 50, lakini bado waliweza kusaidia kwa njia mbalimbali (23-26).


Sikukuu ya Pasaka (9:1-14)

Kabla ya kuondoka Sinai, Waisraeli walisherehekea Pasaka wakiadhimisha kuokolewa kwao kutoka Misri. (Kwa habari za sikukuu ya Pasaka taz.maelezo ya Kut 12:1-36). Waisraeli wote walipaswa kusherehekea Pasaka, lakini tatizo lilitokea, yaani baadhi ya watu walijiona kuwa hawakuweza, kwa sababu walikuwa najisi kwa ajili ya kushika maiti. Walimwuliza Musa wafanye nini, naye akamwuliza Mungu (9:1-8).


Maagizo ya Mungu yalikuwa kwamba, sikukuu ya pili ipangwe mwezi mmoja baada ya sikukuu ya asili kwa ajili ya watu wale na kwa wengine waliokuwa safarini wakati huo. Lakini watu wengine wote walipaswa kusherehekea katika tarehe ya kawaida, na kama mtu alivunja sheria hiyo, alikatiliwa mbali na watu wake, yaani aliuawa. Hata watu wasiokuwa Waisraeli kwa asili yao, lakini waliishi kati yao, walitakiwa washerehekee Pasaka, lakini lazima kwanza wawe wametahiriwa (9-14; taz.Kut 12:43-49).


Wakristo wa Agano Jipya wanaona sikukuu ya Pasaka kuwa mfano wa ushirika wa Meza ya Bwana (Lk 22:15; IKor 5:7-8). Wameokolewa kwa damu ya Yesu Kristo, naye Bwana amewaweka hum mbali na utumwa wa Shetani, pia aliwaambia, Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu (Lk 22:15,19; IKor 5:7-8; 11:24-25). Vile vile inafaa mtu ajihoji na kuondoa kizuizi cho chote kabla ya kushiriki (IKor 11:28). Lakini ndugu akiweza kushiriki, lakini hafanyi hivyo bila sababu, hangepaswa kujihoji mbele ya Bwana? - kifungu hiki kimeongezwa na mtafsiri.)


Uongozi wa Mungu (9:15-10:10)

Kutoka Bahari ya Shamu mpaka Sinai, wingu lilikuwa limewaongoza Waisraeli kama ishara ya kwamba Mungu alikuwa katikati ya watu wake naye aliwaongoza (Kut 13:21-22). Wingu hilo lilifunika hema la kukutania lilipokuwa limemalizika, likiwaonyesha watu kwamba Mungu aliridhika na kazi hiyo na kuikubali. Mungu alikuwa katikati ya maisha ya watu, naye alikuwa jambo kuu la ibada yao (Kut 40:34-38). Wingu lile lingeendeleakuwaongoza, tena lingesisitiza kwamba safari zao, na huduma zao zote zingetimizwa sawa sawa na amri ya Mungu (15-23).


Musa alipotaka kuwaeleza watu maagizo ya Mungu, aliitisha mkutano kwa njia ya kupiga tarumbeta mbili. Kama alipiga tarumbeta moja tu, maana yake ilikuwa kuitwa viongozi wa makabila. Iwapo wingu lilianza kusogea, na hivyo lilionyesha kwamba wakati wa kuendelea na safari uliwadia, mfululizo wa sauti ya kugutushwa (sawa na ya kujitayarisha) ilipigwa, nayo iliwaambia makabila ya Israeli kwamba walipaswa kuanza safari yao (10:1-8). Wakati Waisraeli wangeishi Kanaani, tarumbeta zingepigwa wakati wa vita na katika sikukuu kubwa za kila mwaka kama mfano wa ombi kwa Mungu, ili kumwomba awakumbuke watu wake (9-10).