Kitabu cha Hesabu


MAZINGIRA YA KITABU

Kitabu cha Hesabu kinapoanza, watu wa Israeli walikuwa wameishi karibu na Mlima Sinai kwa muda wa karibu mwaka mmoja. Katika muda huo Mungu aliwaandaa kwa maisha yaliyowakabili, akiwafundisha aina ya dini, kanuni za uadilifu na utamaduni alivyotaka wawe navyo kama watu wake wa agano. (Kwa habari zaidi taz. maelezo katika utangulizi wa kitabu cha Walawi.) Wakati huo muda umewadia kwa Waisraeli waondoke katika Mlima Sinai na wasafiri kuelekea nchi ya ahadi, yaani Kanaani. Kitabu cha Hesabu kinasimulia habari za maandalio kwa safari hiyo, kinaeleza kwa kifupi maagizo mengine yaliyobidi kutimizwa, pia kinasimulia matukio mengine ya maana sana yaliyotokea njiani.


Taifa jangwani

Katika matukio mawili kati ya muda wa Waisraeli kutoka Misri na kuingia kwao Kanaani, Musa alihesabu watu kwa sensa maalumu ya kitaifa. Sensa hizo mbili zimeandikwa katika kitabu cha Hesabu, na kutokana na sensa hizo kitabu kilipata jina lake.


Sensa ya kwanza ya mwanzo wa kitabu iliwasaidia watu kuandaa jeshi kwa kuteka nchi ya Kanaani. Ingawa safari ya kwenda Kanaani ingeweza kuchukua majuma machache tu, kwa kweli ilichukua karibu miaka 40. Sababu yake ilikuwa kwamba, watu walimwasi Mungu wakikataa kumtegemea kuwa angewapa ushindi. Matokeo yake, Mungu aliwaacha jangwani mpaka kizazi kile kilipokufa na kizazi kipya kilipokua wawe watu wazima. Sensa ya pili iliandikwa karibu na mwisho wa kitabu, hivyo ilikuwa karibu miaka 40 baada ya ile ya kwanza, na makusudi yake yalikuwa kuwapanga watu wa kizazi kipya ili wateke nchi ya Kanaani.


Sensa hizo mbili zilichukua sehemu ndogo tu ya kitabu kizima, kwa hiyo jina la Kiswahili la kitabu hiki 'Hesabu' halionyeshi hasa yaliyomo katika kitabu. Jina la Kiebrania, 'Jangwani', linafaa zaidi, kwa sababu kitabu kinasimulia habari za safari yao kutoka Mlima Sinai hadi mpakani mwa nchi ya Kanaani, na sehemu nyingi zaidi ya safari hiyo ilikuwa jangwani. Habari nyingi zilizosimuliwa katika kitabu cha Hesabu zinahusu safari hiyo. Kitabu kinatoa habari chache sana kuhusu miaka yote 40, Waisraeli waliposafiri na kutangatanga jangwani (Hes 32:13).


MUHTASARI

1:1-10:10 Maandalizi ya safari

10:11-14:45 Kutoka Sinai hadi Kadeshi

15:1-19:22 Mafundisho ya Kadeshi

20:1-22:1 Kutoka Kadeshi hadi jangwa la Moabu

22:2-32:42 Matukio katika nchi tambarare ya Moabu

33:1-36:13 Maandalizi ya kuingia Kanaani