23:1-27:34 MATUKIO MAALUMU

Siku takatifu za Mungu (23:1-3) Kulikuwa na sikukuu kubwa tatu katika mwaka wa Kiisraeli: Pasaka au sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, Pentekoste au sikukuu ya Malimbuko ya Mavuno katika mwanzo wa mwaka na sikukuu ya Upatanisho au ya Vibanda, mavuno yalipoingizwa katikati ya mwaka. Katika matukio hayo matatu, wanaume wote wa Israeli walitakiwa wajionyeshe mbele ya BWANA katika uwanja mkuu wa ibada (Kut 23:14-17). Watu walishiriki sikukuu hizo katika hali ya mchanganyiko wa heshima na furaha. Walijinyenyekeza mbele ya Mungu, lakini hata hivyo walimshukuru kwa wokovu na neema yake, na kwa kuwapa mahitaji yao bila kukoma (23:1-2).


Kabla Mungu hajawapa maelezo zaidi kuhusu sikukuu hizo, aliwakumbusha tena kwamba msingi wa sikukuu zote za dini ilikuwa siku takatifu ya Sabato ya kila juma. Katika harakati za sikukuu za mwaka watu wasisahau wajibu wao wa kila juma (3).


Sikukuu za mwanzo wa mwaka (23:4-22)

Mwaka wa Kiisraeli ulianza na mwezi ule ambamo sikukuu ya Pasaka iliadhimisha wokovu wao kutoka Misri (Kut 12:2). Sikukuu hiyo ilikuwa katika miezi ya Machi au Aprili ya kalenda yetu. (Inaonekana kama katika Israeli kulikuwa na kalenda za aina mbili, moja ya kidini na moja ya kawaida, nazo zilitofautiana kwa miezi sita. Hivyo mwezi wa kwanza katika kalenda ya kidini ulikuwa mwezi wa saba katika kalenda ya kawaida, na mwanzo wa mwezi wa saba katika kalenda ya kidini ulikuwa mwanzo wa mwaka mpya katika kalenda ya kawaida.)


Katika siku ya 14 ya mwezi wa kwanza, sikukuu ya Pasaka iliadhimishwa, ikiwa kumbukumbu kwa tendo kuu la Mungu la 'kupita' (pass over) katika nyumba za Waisraeli, wakati alipowaua wazaliwa wa kwanza wa Misri (4-5). (Kwa habari zaidi ya sikukuu hiyo taz.maelezo ya Kut 12:1-14.) Mara baada ya sikukuu ya Pasaka, ilifuata sikukuu ya siku saba, yaani sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu. Sikukuu hiyo ilikuwa kumbukumbu la Waisraeli kuondoka Misri kwa haraka, wakati wasipokuwa na nafasi ya kupika mikate iliyotiwa chachu, bali walichukua donge na vyombo vyake pamoja nao, wakipika mikate yao wakati waliposafiri (6-8). (Kwa habari zaidi ya sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu taz.maelezo ya Kut 12:15-36.)


Wakati ule shayiri ingekuwa imekomaa mashambani na kuwa tayari kwa mavuno. (Ngano isingekomaa mpaka baada ya majuma kadhaa.) Kwa hiyo, katika siku ya pili ya sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, mganda wa malimbuko ya shayiri uliletwa kwa makuhani, nao waliutikisa juu na chini mbele ya BWANA, kama sadaka kwa Mungu. Kwa njia hii walikiri kwa Mungu kwamba Yeye ndiye aliyewapa mavuno yote waliyokuwa wakitaka kuyatoa mashambani (9-11).


Siku ile ile walipotoa sadaka ya mganda, watu pia walitoa sadaka ya wanyama. Walitafuta msamaha kwa dhambi zao kwa njia ya sadaka ya dhambi, na kama shukrani kwa Mungu kwa ajili ya kuwapatia mahitaji yao, walijitoa kwake upya kwa njia ya kumtolea sadaka ya kuteketezwa. Pia walitambua utunzaji wa Mungu na kuwapa chakula cha kila siku walipotoa sadaka ya unga na ya divai, yaani vitu walivyotoa katika chakula chao cha kila siku nyumbani kwao (12-13; Hes 28:16-25). Baada ya kukiri tu kwamba mavuno yote yalikuwa mali ya Mungu, waliruhusiwa kufaidi wao wenyewe katika mavuno yao (14).


Katika muda wa majuma sita yaliyofuata, watu wangeshughulika kuingiza mavuno yao, kwanza shayiri na baadaye ngano. Mwishoni mwa mavuno ya ngano walitoa sadaka ya mikate miwili kwa Mungu, yaani walitoa mikate ya kawaida, kama walivyokula kila siku, na hivyo walionyesha shukrani kwake kwa ajili ya chakula chao cha kila siku. Pia wakati huo walitoa sadaka ya dhambi na sadaka ya kuteketezwa, kama walivyotoa wakati wa malimbuko ya mavuno ya shayiri, na zaidi ya hayo, walitoa sadaka ya amani. Ilikuwa sikukuu ya Mavuno, kwa hiyo ulikuwa wakati wa furaha kubwa (15-21; Hes 28:26-31).


Sikukuu hiyo ilikuwa na majina tofauti. Ilikuwa siku 50 baada ya Pasaka, na hivyo iliitwa Pentekoste (maana ya pentekoste ni hamsini). Pia iliitwa sikukuu ya Majuma (kwa sababu majuma saba yalihesabiwa baada ya sadaka ya malimbuko ya shayiri), au sikukuu ya Malimbuko, au sikukuu ya Mavuno.


Ilionyesha mwisho wa msimu wa mavuno, na hivyo watu walionywa kuacha mabaki fulani ya nafaka mashambani kwa ajili ya maskini na wageni (22;Kum 16:9-12).

Sikukuu ya katikati ya mwaka (23:23-44)

Katika siku ya kwanza ya mwezi wa saba (Septemba-Oktoba), kulikuwa na sikukuu ya Baragumu. Katika siku hiyo watu waliitwa kwa mabaragumu, ili wakutane kwa sherehe ya dini, na kusudi lasherehe hiyo lilikuwa kuwaandaa watu wajitakase na dhambi zao, ili wawe tayari kwa sikukuu ya Upatanisho iliyoadhimishwa baada ya siku kumi (23-32). (Kwa habari zaidi ya sikukuu ya Upatanisho taz.maelezo ya 16:1-34.)


Baada ya siku nyingine tano, yaani siku ya 15 ya mwezi, sikukuu ya juma zima ilifuata, yaani sikukuu ya Vibanda. Wakati wote wa sikukuu hiyo watu waliishi katika vibanda vilivyotengenezwa kwa matawi ya miti na makuti, kwa kumbukumbu ya wakati wa kuishi kwao jangwani. Sikukuu ile iliitwa pia sikukuu ya Kuingiza Mavuno, kwa sababu ilikuwa alama ya mwisho wa msimu wa kilimo, wakati ambao mapato yote ya mashambani,- kama vile zabibu, zeituni, tende, tini n.k. yalikuwa yamevunwa, na Waisraeli walifurahi na kumshukuru Mungu (33-44; Kum 16:13-15). (Kwa habari ya sadaka zilizotolewa katika sikukuu ya Vibanda taz.Hes 29:12-38.)


Wakati huo watu walikuwa wamejaza ghala zao chakula cha kutosha kwa msimu wa baridi uliokuwa unawakabili. Baada ya msimu huo wa baridi, watu wangeanza tena muhula mpya.


Heshima kwa Mungu (24:1-23)

Maagizo mengine yalitolewa ili kuwakumbusha Waisraeli kazi za kila siku na za kila juma katika Mahali Patakatifu. Mwanzo watu walipaswa kutoa mafuta, ili makuhani waweze kuhudumia taa katika kinara zilizotakiwa ziwake daima (24:1-4). Makuhani pia walipaswa kuhakikisha kwamba mikate 12 kwa ajili ya 'Mikate ya Wonyesho' iliyohitaji kubadilishwa kila juma ilikuwepo katika meza yake mbele ya Bwana. Jambo hili labda lilitaka kuonyesha kwa mfano kwamba, taifa la Israeli katika makabila yake yote 12, liliishi mbele ya Mungu wake daima. Pia Mungu alikuwa mtoaji wa mahitaji yao, na ilifaa kwa Waisraeli kukiri jambo hili siku zote mbele yake (5-9; Kut 25:23-30).


Ugomvi uliotokea katika marago ulimsababisha mtu mmoja aliyehusika kulikufuru Jina Takatifu la Mungu. Habari hiyo haikuwa 'lugha mbaya' tu, bali ilionyesha tabia ya dharau iliyokataa mamlaka ya Mungu. Musa hakuchukua hatua ya haraka kwa kumwadhibu mkosaji, bali alimngojea Mungu ili amwonyeshe jambo la kufanya (10-12).


Hukumu ya Mungu ilikuwa kwamba, mtu awaye yote, akiwa Mwisraeli au mgeni, aliyesikiwa akikufuru Jina lake, auawe kwa mawe. Habari ya kuwa washtaki wenyewe walipaswa kushiriki katika uuaji wa hadharani, ingewaonyesha watu wote kwamba wasifanye mashtaka ya namna hiyo kwa urahisi. Ilitakiwa kuwa na uhakika kabisa kwamba mshtakiwa alikuwa na hatia (13-16).


Kanuni iliyopangwa kuwa msingi wa hukumu ya makosa ya kidini na hata ya kiraia, ilikuwa kwamba adhabu siku zote ilingane na makosa. Isichukue kamwe namna ya kisasi, wala isizidi kiasi cha kosa lililotendeka (17-23; taz.pia maelezo ya Kut 21:22-27).


Miaka ya Sabato na miaka ya Yubile (25:1-34)

Waisraeli walipoteka Kanaani na kugawa nchi hiyo kati ya makabila na jamaa zao, waliambiwa wasiwe na ubinafsi au ubahili katika matumizi ya ardhi yake. Kama vile watu na wanyama wao wa kazi walivyotakiwa kupumzika kila siku ya saba, hata mashamba yao yapate nafasi ya kupumzishwa mwaka mmoja baada ya kulimwa miaka sita. Haikuruhusiwa kulima wakati ule wa mwaka wa Sabato. Kutolima huku kwa mwaka mmoja kuliwapa wanadamu nafasi ya kukumbuka kwa njia ya pekee kwamba Mungu alikuwa mwenye nchi yote. Wakati huo huo ardhi ilipata nafasi ya kukusanya nguvu na rutuba mpya kwa ajili ya kulimwa tena (25:1 -7; Kut 23:10-11).


Baada ya kupita miaka saba mara saba, yaani baada ya miaka 49, kulikuwa na mwaka wa Sabato wa pekee ulioitwa Yubile, au mwaka wa Hamsini. Katika mwaka huo sehemu yo yote ya nchi, ikiwa ni mashamba au viwanja vingine, vilivyokuwa vimeuzwa au kubadilishwa kwa namna nyingine, vilipaswa virudishwe kwa wenyewe wa awali. Kwa njia hiyo ilihakikishwa kwamba ugawaji wa haki wa nchi yote katika familia zote za Israeli baada ya kuteka nchi ya Kanaani uliendelea bila kubadilika. Jambo hili liliwasaidia maskini wasipoteze mali ya urithi wa familia zao bila ya kuipata tena. Pia matajiri walizuiwa wasijipatie nchi yote pole pole (8-12).


Nchi yote ilipaswa kurudishwa kwa wenyewe wa awali katika mwaka wa 50 au wa Yubile, kwa hiyo bei ya mashamba au viwanja lazima ipangwe kadiri ya miaka iliyobaki mpaka kutimiza mwaka huo wa 50. Watu walitakiwa wawe waaminifu katika kununua au kuuza ardhi bila ya kudanganyana (13-17).


Watu wasingekuwa na haja ya kuogopa kwamba labda chakula chao kisingetosha kwa miaka ya Sabato au ya Yubile. Cho chote kilichoota chenyewe katika miaka hiyo ya 'kupumzika' kingetosha kwa maskini na kwa mifugo (taz.mist.6-7,12; Kut 23:10-11). Zaidi ya hayo, Mungu angeubariki kila mwaka wa sita, kiasi kwamba mashamba yangetoa nafaka maradufu, na katika mwaka wa 48 mashamba yangetoa kiasi cha mara tatu kuliko kawaida ya miaka mingine. Habari hiyo ingehakikisha kwamba chakula kingetosha kwa miaka ya Sabato na hata kwa miaka ya Yubile (18-22). Watu waliagizwa wasifanye kana kwamba nchi ilikuwa mali yao, nao waliweza kuimiliki kadiri ya mapenzi yao. Mungu ni Mwenyewe, na wao walikuwa wapangaji au wadhamini tu (23-24).


Iwapo mtu angehitaji fedha angeweza kuuza mashamba na milki yake, lakini baada ya muda mfupi ingewezekana yeye mwenyewe au jamaa yake wa karibu akomboe milki hiyo tena. Hapo bei yake pia ingetegemea idadi ya miaka ambayo ingebaki mpaka kutimiza mwaka wa Yubile, wakati ambao kwa vyo vyote angerudishiwa milki yake bila malipo (25-28).


Sheria hizo za kurudisha milki katika mwaka wa Yubile zilihusika kwa aina yo yote ya ardhi katika mikoa ya nchi, kama vile ardhi ya kulimwa mashamba au ya malisho ya mifugo, na hata kwa vijiji na wilaya ambapo Walawi wangeishi na kufuga wanyama wao. Mahali pekee ambapo sheria hii isingehusika, pangekuwa katika miji iliyokuwa na kuta maalumu zilizozunguka miji hiyo, ambapo nyumba zilijengwa karibu karibu wala hazikuwa na haja ya kiwanja kikubwa. Malengo ya watu walioishi katika miji hiyo yalikuwa kufanya biashara, wala hawakushughulika na ukulima au miaka ya Sabato na ya mapumziko ya nchi (29-34; taz.15-16).


Uhusiano wa huruma kwa watu wengine (25:35-55)

Taifa lote la Israeli liliishi kwa uhusiano wa pekee na Mungu wake, kwa hiyo ilikuwa marufuku kwa Mwisraeli kunufaika kutokana na umaskini wa ndugu yake wa Kiisraeli. Alipaswa kumkopesha ndugu yake aliyekuwa na dhiki, lakini asimdai faida ya hisa au riba (35-38). Aliweza kumwajiri mwenye deni aliyetaka kulipa deni yake kwa njia ya kufanya kazi, lakini hakuweza kumfanya mtumwa wa kudumu, kama alivyoweza kufanya kwa mgeni asiyekuwa Mwisraeli (39-46).


Iwapo Mwisraeli alijiuza kuwa mtumwa kwa mgeni aliyeishi katika nchi ya Israeli kwa kulipa deni yake, jamaa zake yule Mwisraeli walipaswa kufanya bidii ili kumkomboa tena. Walipaswa kufanya hivyo kwa njia ya kulipa kiwango cha haki cha mshahara wa mfanyakazi kwa muda wote tangu alipojiuza mpaka kutimiza mwaka wa Yubile ambapo kwa kawaida mtumwa angepewa uhuru wake. Watumwa siku zote wafikiriwe vizuri, wala wasitendewe ukatili au dhuluma (47-55).


Ahadi na maonyo (26:1-46)

Mungu aliwakumbusha watu wajitahidi kutimiza mambo yote waliyofundishwa kuhusu Mungu, Sabato na Mahali Patakatifu (26:1-2). Utii ungeleta mafanikio katika ukulima na ufugaji, amani kati ya watu, ushindi juu ya maadui na faraja kwamba Mungu angeishi kati yao (3-13). Lakini kama wangeasi, matokeo yake yangekuwa magonjwa ya kila aina, maadui wangewashinda na ukame na maafa vingewatesa, ili watu watambue dhambi zao na kumrudia Mungu wao tena (14-20).


Kama watu wasingeitikia na kutubu, Mungu angezidisha sana maafa, angewaletea maadui wakali ambao wangewanyang'anya vyakula vyao hata wafe njaa, wangewaua kwa upanga na kubomoa miji yao, na mabaki yao wangewapeleka katika nchi za kigeni kuwa mateka (21-33). Kama watu wangekataa kupumzisha nchi kila mwaka wa saba, Mungu angewalazimisha kuipumzisha kwa njia ya kuruhusu maadui wawapeleke kuwa mateka katika nchi za kigeni. Wakati huo mashamba yao yangekuwa mahame na yenye ukiwa (34-39; taz.2Nya 36:20-21; Yer 34:13-22). Na mwisho, kama wangekiri na kutubu dhambi zao na kumrudia Mungu wao, Yeye angewarudisha katika nchi yao, kwa sababu ya maagano aliyokuwa ameyafanya nao (40-46).


Makadirio ya nadhiri (27:1-34) Mara nyingi watu walimwahidi Mungu kitu au jambo kwa kiapo au nadhiri, kutokana na shukrani ya neema yake kwao, au kama Mungu aliwasaidia katika dhiki kubwa. Iwapo nadhiri au ahadi waliyoapia ilikuwa mwanadamu, mtu yule hakuweza kutolewa sadaka, bali alipaswa akombolewe kwa njia ya kulipa pesa Mahali Patakatifu. Kiwango cha kulipiwa kilikadiriwa na makuhani kufuatana na uwezo na afya ya mtu aliyeahidiwa kuwa nadhiri ya Mungu. Mpango wa pekee ulifanywa kwa ajili ya maskini wasioweza kulipa kiwango kilichokadiriwa (27:1-8).


Iwapo nadhiri iliyoahidiwa ilikuwa mnyama aliyefaa kuwa sadaka, mwenye mnyama hakuweza kumkomboa. Alipaswa kumtoa sadaka au kuwapa makuhani kuwa mali yao. Wao waliweza kumfuga au hata kumwuza. Fedha zote zilizopatikana katika mauzo hayo ziliingizwa katika hazina ya Mahali Patakatifu. Iwapo mtu, baada ya kuweka wakfu kitu kimoja, alitaka kuweka kitu kingine badala yake, alikosa vyote viwili (9-10).


Mnyama asiyekuwa safi (yaani asiyefaa kuwa sadaka, kama vile ngamia au punda), alipaswa wapewe makuhani, walioweza kumtumia kwa kazi zao au kumwuza. Vile vile mtu aliyemtoa mnyama yule, aliweza kumkomboa tena kwa kiwango kilichokadiriwa, lakini alipaswa kuongeza sehemu moja ya tano (asilimia 20) ya bei ya mnyama kama faini, kwa sababu alijitwalia tena kitu alichomtolea Mungu nadhiri (11-13). Sheria zilizofanana zilihusika iwapo mtu aliweka nyumba yake wakfu kwa Bwana au nadhiri (14-15).


Mipango kwa mtu aliyeweka mashamba yake nadhiri kwa Bwana ilifanana na ile iliyotangulia. Iwapo mtu alitaka kukomboa mashamba yake tena, thamani yake ilitegemea kiasi cha miaka iliyobaki mpaka mwaka wa Yubile ambapo kwa kawaida mashamba yote yalirudishwa tena kwa mwenyewe wa awali. Kama mtu aliweka wakfu mashamba yake, naye hakutaka kuyakomboa tena, au kama ameyauza baada ya kuyaweka wakfu, hayakurudi kwake katika mwaka wa Yubile. Yalikuwa mali ya Mahali Patakatifu daima (16-21). Iwapo mashamba ambayo mtu aliyaweka nadhiri hayakuwa mali yake ya awali, nayo hayakukombolewa naye baada ya kuyaweka nadhiri, yalirudishwa kwa mwenyewe wa awali katika mwaka wa Yubile (22-25).


Wazaliwa wa kwanza katika wanyama waliofaa kuwa sadaka, hawakuweza kutolewa wakfu au nadhiri kwa Bwana, kwa sababu walikwisha kuwa mali yake (Kut 13:2). Wazaliwa wa kwanza wa wanyama wasiofaa kuwa sadaka waliweza kuwekwa wakfu kwa Bwana, na kisha waliweza kukombolewa tena na mtoaji, au makuhani waliweza kuwauza kwa njia ya kawaida (26-27). Kitu cho chote kilichowekwa wakfu kwa Mungu ili kiangamizwe, hakikuweza kuapiwa tena kuwa nadhiri, wala hakikuweza kukombolewa au kuuzwa (28-29).


Sehemu moja ya kumi (asilimia 10) ya nafaka yote na mifugo yote ilikuwa mali ya Mungu, nayo iliweza kushikwa kwa matumizi ya binafsi kwa njia moja tu, yaani kama mtu alitoa malipo ya thamani yake pamoja na faini ya kawaida (yaani asilimia 20). Malipo yote yawekwe katika hazina ya Mahali Patakatifu (30-34).