Kitabu cha Mambo ya Walawi
UTANGULIZI
Kufuatana na ahadi yake kwa Ibrahimu, Mungu aliwatoa watu Israeli Misri na kuwaweka katika njia ya kuelekea Kanaani. Baada ya miezi mitatu walifika katika Mlima Sinai, walipokaa karibu mwaka mzima. Katika muda ule walijiandaa kwa maisha yao mapya yaliyowakabili (Kut 19:1; Hes 10:11). Kitabu cha Walawi kina baadhi ya mafundisho ambayo Mungu aliwapa watu wake wakati ule wa mwaka mmoja waliokaa karibu na Mlima Sinai.
Mipango ya dini kwa watu wa agano
Waisraeli walijua kwamba Mungu aliwachagua kuwa watu wake, na neema yake iliwapa uhuru kutoka utumwa wa Misri. Kwa hiyo waliitikia tendo hilo vizuri kwa kuahidi kufanya yote aliyowaagiza (Mwa 12:2; 15:7-21; Kut 2:24; 4:22; 6:6-8; 19:4-9; 20:2). Mungu mwenyewe alijunga na Waisraeli katika sherehe ya agano ambamo alipanga kanuni fulani za msingi na amri maalumu, nao waliitikia wakiahidi kutii amri zote bila masharti yo yote (Kut 20:1-24:18).
Mungu akaendelea kuwaeleza watu wake mipango yake aliyoyakusudia kwa maisha ya dini ya taifa. Angewapa mahali maalumu kwa ajili ya ibada, ukuhani kwa kusudi la kuendesha mambo yote ya kidini na utaratibu maalumu wa sadaka mbalimbali ambao kwa njia yake wangeweza kumwonyesha imani yao (Kut 25-Law 7). Zaidi ya hayo, aliongeza sheria maalumu ili kuhakikisha kwamba makuhani na watu wa kawaida wawe watakatifu na safi katika uhusiano wao na Mungu, pia baina yao wenyewe (Law 8:1-27:34).
Muhtasari huu mfupi wa vitabu vya Kutoka na Walawi unaonyesha kwamba hakuna pengo kati ya vitabu hivyo viwili (taz. Kut 40:17; Law 1:1; 27:34). Unaonyesha pia kwamba wasomaji wanapaswa kujua habari za hema la kukutania na ukuhani katika nusu ya pili ya kitabu cha Kutoka, ili waweze kuelewa mipango ya sadaka katika mafungu ya kwanza ya kitabu cha Walawi. (Kuhusu mgawanyiko uliosababisha vitabu vitano vya kwanza katika Biblia, tazama maelezo katika utangulizi wa kitabu cha Mwanzo, kipengele cha 'Pentatuki'.)
Ingawa kitabu kinaitwa cha Walawi, kwa jumla hakisemi mengi kuhusu maagizo kwa Walawi. (Maagizo hayo yalitolewa baadaye katika kitabu cha Hesabu). Karibu maagizo yote katika kitabu cha Walawi yanawahusu makuhani waliokuwa wa ukoo mmoja tu (yaani wa ukoo wa Haruni) katika kabila la Lawi (Kut 29:9; Hes 3:9-10). Lakini utaratibu wote wa dini ya Israeli uliitwa utaratibu wa Kilawi, na ukuhani wa Haruni ulijulikana kama ukuhani wa Kilawi.
Ukristo siyo sehemu ya mipango ya dini ya Israeli, wala Wakristo hawapo chini ya sheria ya Israeli (Rum 6:14; Gal 5:1-4). Lakini Wakristo wanaweza kujifunza mengi kutoka kitabu cha Walawi. Hivyo wataelewa kanuni zile za ulimwengu wote zisizokuwa na wakati maalumu na msingi wa sheria za pekee zilizotolewa kwa taifa moja kwa muda maalumu (Rum 8:3-4; Gal 5:14, 18). Vile vile, kwa kuwa Biblia mara nyingi inataja sadaka, sikukuu na sherehe za mipango ya Kilawi, ufahamu wa kitabu cha Walawi utamsaidia msomaji kuelewa Biblia yote vizuri zaidi.
MUHTASARI
1:1-7:38 Sadaka mbalimbali
8:1-10:20 Kuthibitishwa kwa Ukuhani
11:1-15:33 Usafi na unajisi
16:1-17:16 Damu ya upatanisho
18:1-22:33 Utakatifu katika maisha ya kila siku
23:1-27:34 Matukio maalumu