35:1-40:38 HEMA LA KUKUTANIA

Sehemu hii ya kitabu kwa jumla ni marudio ya maagizo yaliyotolewa mlimani, kama yalivyoandikwa katika mafungu ya 25-31. Inasisitiza kwamba kazi ya Mungu lazima ifanywe kadiri ya maagizo yake kufuatana na agano. Kwa hiyo ilikuwa lazima kuheshimu siku ya Sabato (35:1-3; taz.31:16). Ili sadaka zikubaliwe na Mungu, ilikuwa lazima zitolewe kwa furaha na kwa moyo (35:4-29). Ingawa watu wote waliweza kutoa sadaka, kazi yenyewe ilitakiwa ifanywe na wale tu waliopewa uwezo na Mungu, na waliopenda kufanya hivyo (35:30-36:1). Kiasi cha vifaa vilivyotolewa kwa hiari ya watu kilikuwa kikubwa mno, hata watu waliagizwa wasilete zaidi (36:2-7).



Kisha mafundi walifanya hema hilo la kukutania pamoja na mapazia yake mawili ya kulifunika upande wa nje (36:8-19), mbao zake za miti, mataruma yake na nguzo zake, mapazia yake ya kutenganisha vyumba na milango yake (36:20-32), sanduku la agano (au la ushuhuda), kiti cha rehema (37:1-9), meza, kinara cha taa na madhabahu ya kufukizia uvumba (37:10-29). Pia vyombo vya uani vilifanywa, yaani madhabahu kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa (38:1-7), birika ya shaba (38:8) na wigo (fensi) uliozingira eneo lote la ua (38:9-20). Vifuatavyo ni orodha ya sadaka mbalimbali (38:21-31) na hesabu ya nguo za makuhani (39:1-31).



Kisha Musa alikagua na kuridhika na vifaa vyote vya hema vilivyokuwa tayari akawashukuru mafundi. Lakini hema lenyewe lilikuwa halijaunganishwa bado (39:32-43). Musa mwenyewe akasimamia kazi yote ya kulisimamisha, akatakasa hema la kukutania, akiwa pamoja na makuhani wake kama alivyokuwa ameagizwa (40:1-33).



Ilikuwa mwaka mmoja kamili baada ya kuondoka Misri, au miezi tisa baada ya kufika katika Mlima Sinai, hema la kukutania lilipomalizika na kutakaswa (taz.l2:2; 19:1; 40:17). Hapo wingu lilitulia au lilisimama juu ya hema la kukutania kama alama ya kuonekana wazi kwamba Mungu alikaa kati ya taifa la Israeli, akiwa sehemu ya katikati ya maisha ya watu, na mkuu wa ibada yao. Wingu hilo liliwaongoza katika safari yao ya kupitia jangwani na mpaka Kanaani. Kama walisafiri au kupumzika katika marago yao, YAHWEH (BWANA), Mkombozi wao wa agano, alikuwa pamoja nao na kati yao (40:34-38).